Sunday, March 18, 2012

Kuoza kwa Kasi kwa Meno Mengi kwa Watoto Wadogo (Rampant Caries in Children)

Rampant Caries in Children-kuoza kwa meno watoto

Tafsiri za maneno “rampant caries” ni nyingi katika fani ya meno lakini la msingi ni kuoza kwa meno kunako enea kwa kasi na kuharibu vichwa (crowns) vya meno mengi au yote yaliyoota. Hii ni hali mbaya ya kuoza kwa meno ambayo hushambulia zaidi meno ya utotoni (milk teeth or primary dentition), japo wakati mwingine hata ukubwani.

Ugonjwa huu unajidhihirisha kwa kuanza na kuongezeka kwa kasi na kwa namna unavyo yashambulia meno na vyanzo vyake. Meno hushambuliwa kwa mpigo hasa kuanzia meno ya juu mbele, ingawa meno ya chini mbele ni mara chache kushambuliwa kwa vile yanakingwa na visababisha vya kuoza na ulimi.

Ugonjwa huu hushambulia hata maeneo ya meno ambayo kwa hali ya kawaida si rahisi kuoza, kama sehemu ya kukatia kwa meno ya mbele (incisal edges) na sehemu ya mbele kati na nyuma kati (facial and lingual surfaces).

Nini husababisha meno kuoza kwa kasi utotoni?

Nadharia nyingi zinaonesha kuna uhusiano mkubwa kati ya ugonjwa huu na tabia ya ulaji ya mtoto (feeding habits). Mfano kisababishi kikubwa ni watoto kunywa vinywaji vyenye sukari kwa muda mrefu na mara nyingi kwa kutumia chupa za kunyonyea (nursing bottles) ndiyo maana ugonjwa huu wakati mwingine huitwa nursing bottle caries. Hii hujitokeza hasa kwa watoto wanaochwa na yaya zao, ambao huwapa vinywaji hivyo kila wanapohitaji au wakilia.

Pamoja na kwamba ugonjwa huu hutokana zaidi na chupa za kunyonyea, japo mara chache, lakini pia yawezekana kutokana na mama kumnyonyesha mtoto mara kwa mara au tuseme kila anapo hitaji; vile vile wale akina mama ambao hawataki usumbufu usiku hivyo kutumbukiza nyonyo zao kwenye vinywa vya watoto na wao kujilalia, hapa mtoto hujinyonyea usiku kucha hali hii kitaalamu hujulikana kama at will breast feeding.

Vijino vilivyoathirika huonekana brauni au vyeusi kama mkaa

Watoto walio katika hatari ya kupata ugonjwa huu

  • Watoto wa masikini ambao hawapigi mswaki kwa kizingizio cha kwamba mtoto ni mdogo, kumbuka meno ya utotoni yana madini kidogo
  • Watoto wa wafanyakazi wanashinda maofisini wakati wa kunyonyesha na waacha watoto kutumia chupa za kufyonzea kwa muda mrefu ambao hawapo nao
  • Watoto wagonjwa sugu wanaotumia dawa zenye sukari (syrups) mara kwa mara.
  • Watoto wanaoachwa kunyonyeshwa mapema na hivyo kutumia chupa kama mbadala

Namna ya kumkinga mtoto wako

  • Punguza matumizi ya chupa za kufyonzea
  • Msipende kuwanyonyesha watoto kila wanapotaka hivyo, hasa kunyonyesha inapotumika kama njia ya kupoza mtoto anayelia
  • Jenga tabia ya kuwakagua watoto vinywani mara kwa mara na ukiona tatizo mpeleke hospitali mapema
  • Wasaidieni watoto kupiga mswaki mara baada ya meno kuanza kuota
  • Dhibiti matumizi ya vinywaji na na vitu vya sukari mara kwa mara
  • Msipende kuwapa watoto wadogo fedha kwani matumizi yake ni pipi na ice water au vinavyo fanana na hivyo

Matibabu

  • Kuziba meno yanayoweza kuzibika
  • N’goa yanayouma na hayawezi kuzibika na kutumia vitunza nafasi (space maintainers).
  • Acha yasiyoweza kuzibika lakini hayaumi yatatoka wakati wake ukifika
  • Pakaza madini ya fluorini kwa watoto walio katika hatari kubwa

No comments:

Post a Comment