Upungufu wa damu (anaemia) hutafsiriwa kama kupungua kwa kiwango cha hemoglobin katika damu damu chini ya kiwango kinachokubalika kiafya. Kiwango cha kawaida cha haemoglobin (Hb) katika mwili wa binadamu ni kati ya gramu 12 mpaka 14 kwa kila mililita ya damu. Hata hivyo shirika la afya duniani (WHO) linatambua kiwango cha mpaka 11gm/mililita kuwa cha kawaida kwa mama mjamzito. Hivyo basi mjamzito mwenye kiwango chochote cha haemoglobin chini ya 11 gm/mililita hutafsiriwa kuwa na upungufu wa damu. Hata hivyo nchi nyingi hasa zinazoendelea hutambua kiwango cha mpaka gramu 10 kwa mililita kuwa ni upungufu wa damu kwa mjamzito.
Kwa mjamzito anayehudhuria kliniki kwa mara ya kwanza, upungufu wa damu kipindi cha ujauzito humaanisha kiwango cha hemoglobin chini ya <11.0 g/dL, na mimba inapofikisha wiki 28 upungufu wa damu hutambuliwa iwapo hemoglobin itashuka na kuwa chini ya 10.5 g/dL.
Kwa kuzingatia hilo, mama mjamzito hushauriwa kupima wingi wa damu siku anapohudhuria kliniki kwa mara ya kwanza na pindi mimba inapofikisha wiki 28.
Viwango vya Anaemia
Upungufu wa damu unaweza kugawanywa katika viwango vikuu vinne, yaani upungufu wa damu wa kawaida (mild anaemia) ambao ni kati ya 9-11 gm/ml, upungufu wa damu wa kati (moderate anaemia) ambao ni kati ya 7-9 gm/ml, upungufu wa damu mkali (severe anaemia) ambao ni kati ya 4-7 gm/ml na upungufu wa damu mkali zaidi (very severe anaemia) ambao ni chini ya 4gm/ml.
Mzunguko wa madini ya chuma mwilini
Kwa kawaida mwili wa mwanamke huifadhi gramu 3.5 mpaka 4.5 za madini ya chuma. Asilimia 75 huifadhiwa kama hemoglobin katika chembe damu nyekundu, asilimia 20 kama ferritin katika mifupa na asilimia 5 inayobaki huifadhiwa katika misuli na vimeng’enyo vingine vya mwili.
Wanawake wasio wajawazito hupoteza karibu gramu 1 za madini ya chuma kutoka katika seli za mwili zinazokufa kila siku na gramu 1 zaidi kila siku wanayokuwa kwenye hedhi.
Ukubwa wa tatizo
Upungufu wa damu kipindi cha ujauzito ni tatizo linalowakumba kina mama wajawazito wengi sana, siyo tu Tanzania bali nchi nyingi zinazoendelea. Inakisikiwa kuwa karibu theluthi moja ya wajawazito katika miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito hukumbwa na tatizo hili.
Kwa mujibu wa WHO, inakadiriwa kuwa karibu asilimia 56 ya wajawazito huko kusini mashariki ya Asia hukumbwa na tatizo hili. Kwa hapa Tanzania, hakuna takwimu sahihi kuhusu tatizo hili. Sehemu nyingine duniani, inakadiriwa kuwa karibu asilimia 4-16 ya vifo vinavyotokana na ujauzito husababishwa na upungufu wa damu. Aidha upungufu wa damu wakati wa ujauzito huongeza uwezekano wa madhara kwa mtoto ikiwemo kifo.
Chanzo cha upungufu wa damu wakati wa ujauzito
Kipindi cha ujauzito huambatana na mabadiliko mbalimbali ya mwili. Moja ya mabadiliko hayo ni ongezeko la maji (plasma volume) katika mzunguko wa damu. Katika hali hii, pamoja na kwamba kiasi cha damu huonekana kuongezeka, kiwango cha hemoglobini hupungua mpaka kufikia 11.5mg/dl.
Karibu asilimia 85 ya anaemia wakati wa ujauzito husababishwa na upungufu wa madini ya chuma mwilini. Upungufu wa madini ya chuma unaweza kusababishwa na kula chakula chenye kiasi kidogo cha madini haya au mwili wa mjamzito kushindwa kutunza madini ya chuma ya kutosha kutokana na ama mimba zilizopita au kupoteza kiasi kingi wakati wa hedhi kabla ya kushika mimba.
Vyanzo vingine ni pamoja na
- Upungufu wa folic acid
- Ugonjwa wa sickle cell
- Lishe duni kabla na wakati wa ujauzito
- Kupoteza damu kwa sababu ya kuumia au kuwa na minyoo (hookworms)
- Ugonjwa wa malaria wakati wa ujauzito
- Ugonjwa wa chembe damu nyekundu ujulikanao kama beta thalassaemia. Ugonjwa huu huwapata zaidi watu wanaoishi Asia ya kusini, Ulaya ya kusini na Afrika.
- Upungufu wa vitamin B12
- Ugonjwa sugu wa kuvunjika chembe damu nyekundu (chronic haemolysis) kama vile ugonjwa kurithi wa chembe damu nyekundu (hereditary spherocytosis)
- Ugonjwa wa kupoteza hemoglobin kupitia mkojo (paroxysmal nocturnal hemoglobinuria)
- Saratani ya damu (leukemia)
- Matatizo ya kupoteza damu kwenye njia ya chakula (gastrointestinal bleeding)
- Matatizo katika utumbo hasa wakati wa ujauzito.
Vihatarishi vya tatizo hili
- Masuala ya kijamii kama vile umri wa mjamzito, kiwango chake cha elimu na uelewa kuhusu afya yake, kama ana mwenza wa kumsaidia kiuchumi, makazi anayoishi vinaweza kuchangia mjamzito kupata upungufu wa damu
- Vihatarishi vingine ni vile vinavyohusu masuala ya uzazi kama vile idadi ya mimba zilizotanguli (waliowahi kuzaa wana hatari ya kupata anaemia kuliko wanaopata mimba kwa mara ya kwanza), kuwa na mimba ya mapacha na kuwa na historia ya kuzaa mtoto njiti
- Vihatarishi vingine vinahusu tabia za mjamzito kama vile uvutaji sigara, unywaji wa pombe na kutohudhuria kliniki wakati wa ujauzito
- Pia kuwa na magonjwa kama vile kisukari, magonjwa ya figo, pamoja na shinikizo sugu la damu
Madhara ya upungufu wa damu kwa mama na mtoto
Sehemu nyingine duniani, inakadiriwa kuwa karibu asilimia 4-16 ya vifo vinavyotokana na ujauzito husababishwa na upungufu wa damu. Aidha upungufu wa damu wakati wa ujauzito huongeza uwezekano wa madhara kwa mama na mtoto ikiwemo kifo. Madhara haya ni pamoja na
- Madhara kwa mama kipindi cha ujauzito: kukonda au kuongezeka uzito kwa kiasi kidogo sana, kuhisi uchungu kabla ya muda, kondo la nyuma kutunga pasipostahili, shinikizo la damu wakati wa ujauzito, na chupa kupasuka kabla ya wakati.
- Madhara kwa mama wakati wa kujifungua: kupatwa na uchungu usioeleweka na usio wa kawaida, mtoto kuvuja damu ndani kwa ndani, kupatwa na shock, hatari ya ganzi (anesthesia risk) kwa anayefanyiwa upasuaji, na moyo kushindwa kufanya kazi.
- Madhara kwa mama baada ya kujifungua: maambukizi baada ya kujifungua, kizazi kushindwa kurudi katika hali ya kawaida au damu kuganda kwenye mishipa.
- Madhara kwa mimba na mtoto atakayezaliwa: Madhara ni pamoja na mtoto kuzaliwa njiti, mtoto kuzaliwa na uzito mdogo, mtoto kuwa na score ndogo (poor Apgar score), mtoto kuzaliwa akiwa amechoka (fetal distress), na upungufu wa damu kwa mtoto
Watoto wanaozaliwa wakiwa na upungufu wa damu hukua kwa tabu, huwa na maendeleo duni ya kiakili na kimatendo (poorer intellectual developmental milestones), uwezekano mkubwa wa kuwa na kasoro mwilini na hata kifo. Kasoro hizo ni pamoja na matatizo ya magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo (congenital heart diseases
Dalili
Mjamzito mwenye upungufu wa damu wa kawaida mara nyingi anaweza asioneshe dalili zozote. Hata hivyo iwapo upungufu ni mkubwa, dalili za awali ni pamoja na uchovu wa mara kwa mara na kupumua kwa shida, kukosa hamu ya kula, mapigo ya moyo kwenda kasi, na kuchafuka kwa tumbo.
Wakati wa uchunguzi mjamzito anaweza kuonekana mweupe kuliko kawaida hasa sehemu za viganjani, kucha za vidoleni, ulimi, au macho. Anaweza pia kuwa na dalili za kuvimba miguu.
Vipimo na uchunguzi
Uchunguzi wa upungufu wa damu hufanywa kuwa kupima kiasi cha haemoglobin pamoja kufanya kipimo kingine cha damu kijulikanacho kama peripheral smear.
Vipimo vingine vya maabara ni pamoja na kipimo cha kufahamu uwezo wa kuhifadhi madini ya chuma yaani total iron binding capacity (TIBC), kiasi cha feritin katika damu, kiasi cha folic acid. Katika mazingira mengine kipimo cha kuchukua sehemu ya supu ya mifupa na kuichunguza maabara yaani bone marrow biopsy kinaweza kufanywa. Hata hivyo hivi si vipimo vinavyofanywa mara kwa mara.
Matibabu
Mama mjamzito huitaji miligramu 2 mpaka 4.8 za madini ya chuma kila siku. Ili aweze kupata kiasi hiki, inampasa kula kati ya miligramu 20 mpaka 48 za madini ya chuma. Kwa jamii ambayo upatikanaji wa vyakula vyenye madini hayo ni wa shida, suala hili linaweza kuwa gumu sana kutekelezeka, ndiyo maana Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeweka mpango maalum wa kuwapa wajawazito wanaohudhuria kliniki madini ya chuma na folic acid ili kufidia pengo hilo.
Vidonge vya madini ya chuma ni salama, nafuu na njia makini ya kuongeza na kurekebisha upungufu wa damu mwilini. Kwa wajawazito ambao hawawezi kunywa, kwa sababu yeyote ile, njia ya sindano inaweza pia kutumika.
Wajawazito wanashauriwa kutumia miligramu 60 za madini ya chuma (ferrous sulphate) na 500mg za folic acid kila siku, ambapo utaratibu huu huendelea kwa miezi mitatu mpaka sita ili kuongeza hifadhi ya madini ya chuma mwilini, hata kama kiwango kinachotakiwa kitakuwa kimefikiwa.
Utumiaji wa vidonge vya madini ya chuma na baadhi ya vyakula: Kuna baadhi ya vyakula kama vile chai ya rangi ambavyo vikiliwa wakati mjamzito amekunywa vidonge vya madini ya chuma vinaweza kupunguza unyonyaji wake katika utumbo. Kwa upande mwingine baadhi ya vyakula vyenye vitamini C kama vile matunda ya jamii ya machungwa huongeza uwezo wa utumbo kunyonya madini ya chuma mwilini.
Vyakula vya kuongeza damu: Pamoja na mkakati huo, wajawazito hushauriwa pia kula vyakula vyenye madini ya chuma kwa wingi kama vile nyama, maini, mayai, samaki, mimea jamii ya kunde, maharage makavu, mboga za majani, matembele, na mikate iliyoongezwa madini ya chuma.
Matibabu ya upungufu wa damu mkali kwa wajawazito walio katika wiki za mwisho (baada ya wiki ya 32): Wagonjwa wa kundi hili hutibiwa hospitali. Wengi wanaweza pia kuwa na dalili za matatizo ya moyo, hivyo wanapaswa kulazwa na kupumzika kitandani, na wakati fulani kuongezewa hewa ya oksijeni. Pamoja na kutibiwa matatizo ya moyo, huongezewa pia damu (packed red cells) kwa vile vidonge vya madini ya chuma havitafaa kurekebisha tatizo hili kwa haraka kabla ya muda wa kujifungua kufika.
Matibabu ya maradhi mengine: kwa mazingira yetu, magonjwa kama malaria na minyoo huchangia kwa kiasi kikubwa kutokea kwa upungufu wa damu kwa wajawazito, hivyo basi magonjwa haya hayana budi kutibiwa kikamilifu ili yasilete madhara kwa mjamzito. Wajawazito wanaoishi maeneo yenye malaria kwa wingi hupewa dawa za SP kwa ajili ya kuwalinda wasipatwe na ugonjwa huu. Pia dawa za minyoo za Albendazole au mebendazole hutolewa kwa wajawazito baada ya miezi mitatu ya mwanzo ili kuua minyoo. Ili kuzuia kujiridia kwa minyoo, wajawazito pia hushauriwa kuvaa viatu/kandambili kila wakati, na kuhakikisha miili na mazingira yao yapo safi.
No comments:
Post a Comment