KATIKA safari ya mapenzi kuna uwezekano mkubwa mtu akawa ameshawahi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na watu wengi kabla ya kumpata yule sahihi wa kuishi naye kama mke na mume.
Rekodi zinaweza kutofautiana kutoka kwa mtu na mtu ila kama wewe umewahi kuwa na uhusiano na zaidi ya mtu mmoja huko nyuma, unatakiwa kuwa makini katika maisha yako ya sasa ili huyo mpenzi wako wa zamani asije akakutibulia.
Tumekuwa tukishuhudia mikwaruzano ya hapa na pale kati ya wapenzi chanzo kikiwa ni mmoja kukuta aidha meseji isiyoeleweka kwenye simu ya mwenzake ikitoka kwa mpenzi wake wa zamani au unaweza kusikia mwanaume kamshushia kipigo mpenzi wake baada ya kumkuta akiwa katika mazingira tata na ‘mtu’ wake wa zamani.
Hayo yamekuwa yakitokea kila siku lakini chanzo ni wengi kutojua jinsi wanavyoweza ‘kuwahendo’ wapenzi wao wa zamani na kuhisi hata wakiwa karibu nao hawawezi kuwa na madhara.
Yawezekana ni kweli huyo mpenzi wako wa zamani hamkuachana kwa shari bali kuna mambo ya hapa na pale yalitokea hivyo mkaamua kumwagana. Katika mazingira hayo ni vigumu kumkwepa kabisa lakini sasa unatakiwa kujiuliza, mpenzi wako wa sasa atawafikiriaje? Unadhani atachukulia poa kuwaona mnaendelea kuwasiliana na kupiga stori hata kama hamuendi mbali zaidi ya hapo?
Hakuna mtu wa kuweza kuvumilia hilo na ndiyo maana siku hizi unaweza kumkuta msichana yuko na mpenzi wake na akikutana na yule wa zamani anamchunia kama hamjui, kwa nini? Kwa sababu anajua salamu tu inaweza kuleta matatizo kwa mpenzi wake!
Lakini hofu pia inatokana na usaliti ambao umekuwa ukitokea kila kukicha. Ukweli ni kwamba, kama mpenzi wako anaonesha ukaribu sana na mtu wake wa zamani kisha wewe ukachukulia poa, ipo siku utavuna mabua. Nasema hivyo kwa kuwa, watu ambao wanajuana vizuri ‘nje ndani’, wakiendelea kuwa karibu wana asilimia nyingi za kuweza kukumbushia enzi zao. Hata kama utabisha, huo ndiyo ukweli.
Uko tayari wa zamani akutibulie?
Yawezekana hamkuachana kwa shari lakini tayari hauko naye tena na umefanikiwa kumpata mwingine ambaye moyo wako umemzimia, uko tayari ‘mtu’ wako wa zamani akuharibie? Sidhani na kama uko tayari basi utakuwa huna msimamo na maisha yako.
Nini cha kufanya?
Kikubwa kama nilivyosema hapo juu ni kuwa na msimamo na maisha yako. Mpenzi wako wa zamani atabaki kuwa wa zamani tu, hata kama mliachana kwa heri hutakiwi kujenga ukaribu naye ili kuunusuru uhusiano wako wa sasa. Zaidi zingatia yafuatayo:
Usimpe namba yako
Katika kulinda uhusiano wako wa sasa, hakikisha mpenzi wako wa zamani hana namba yako ya simu. Unaweza kumpatia tu endapo mpenzi wako wa sasa atakuwa ameridhia kwa sababu maalum.
Fanya hivyo kwani watu wengine hawana akili timamu, yaani anajua kabisa kuwa una mtu wako lakini unaweza kushangaa anakutumia sms za ajabu eti tu kwa sababu mliwahi kuwa wapenzi.
Muepuke
Hata kama huna chuki naye lakini suala la wewe kukaa sehemu na mpenzi wako wa zamani hakuwezi kuleta picha nzuri kwa mpenzi wako. Kwa maana hiyo akihitaji ufaragha wa aina yoyote na wewe, muepuke, labda kama ni kwa sababu maalumu na mpenzi wako wa sasa awe na taarifa.
Usimgeuze rafiki
Kuna wale ambao walikuwa na wapenzi wao lakini baada ya kuachana eti wakakubaliana wabaki kuwa marafiki tu na kusaidiana kwa shida na raha. Sawa mnaweza kubaki marafiki lakini unadhani mpenzi wako atakuelewa?
Unadhani itaaminika kuwa nyie ni marafiki wa kawaida tu wakati mlishawahi kulala pamoja mkiwa kama mlivyozaliwa? Ni vigumu na ndiyo maana nashauri kuuepuka hata huo urafiki ili kulilinda penzi lako la sasa.
Mwisho niseme tu kwamba, unapoingia kwenye uhusiano, unaweza kumdatisha mpenzi wako kwa vitu vingi sana kiasi kwamba mkija kuachana ni vigumu kukusahau na wakati mwingine kutaka mrudiane. Unachotakiwa ni kufanya maamuzi sahihi na kuwa na msimamo na maisha yako.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment