Watafiti nchini Japan wamegundua jinsi seli za mfumo wa fahamu zinavyoweza kutumika kama seli mbadala zinazofaa kupandikizwa kwenye seli kongosho ili kutibu kisukari. Ripoti ya utafiti huo ambayo imechapishwa kwenye jarida la kitafiti la EMBO Molecular Medicine, inaonesha kuwa seli zinazovunwa kutoka katika mfumo wa fahamu zinaweza kupandikizwa katika tezi kongosho na hivyo kumaliza tatizo la ukosefu wa seli za beta ambazo huitajika kwa ajili ya uzalishaji wa insulin.
Kisukari ni ugonjwa unaosababishwa na ukosefu wa kichocheo cha insulin kinachozalishwa na tezi kongosho, na ambao huathiri karibu watu milioni 200 duniani. Mpaka sasa hakuna tiba yeyote ya ugonjwa huu, hali inayowafanya wagonjwa wa kisukari kutegemea zaidi matumizi ya dawa au njia nyingine mbadala kuthibiti kiwango cha sukari mwilini.
Utafiti huo ulioongozwa na Dr Tomoko Kuwabara kutoka taasisi ya tafiti za Afya ya AIST ya Tsukuba nchini Japan, ulilenga katika kuchunguza jinsi seli za binadamu zinavyokua na kijiwagawa kulingana na kazi mbalimbali za mwili, na pia kuchunguza uwezekano wa kutumia seli mbalimbali kutekeleza kazi zilizo nje ya majukumu yake ya kawaida.
Katika kufafanua, Dr. Kubawara anasema kuwa kwa vile kisukari ni ugonjwa unaosababishwa na ukosefu wa aina moja ya seli, ugonjwa huu unaweza kutibika kwa kutumia njia ya upandikizaji wa seli mpya zitakazotumika kuzalisha kichocheo cha insulin. Anasema, hata hivyo kwa vile kupandikiza seli za beta kutoka tezi kongosho za watu wengine ni ngumu kwa sababu ya ukosefu wa watoaji, njia muafaka ni kutumia seli za mfumo wa fahamu wa mgonjwa mwenyewe katika kufanikisha upandikizaji huo.
Seli za mfumo wa fahamu zinazoweza kupandikizwa kwenye tezi kongosho kwa urahisi zaidi ni zile zilizopo katika maeneo ya ubongo wa mbele yajulikanayo kitaalamu kama hippocampus na olfactory bulb.
Kwa kawaida seli za mfumo wa fahamu huzalisha kiwango kidogo sana cha insulin tofauti na seli za tezi kongosho, hata hivyo, mara tu baada ya kupandikizwa kwenye tezi kongosho, seli hizo zilianza kutoa kiwango kikubwa cha kichocheo cha insulin na kiwango cha sukari katika damu kilionekana kupungua kwa kiwango kikubwa. Na hata seli zilizopandikizwa zilipoondolewa, kiwango cha insulin kilishuka na kusababisha kupanda tena kwa kiwango cha sukari katika damu.
Utafiti huo ulifanyika kwa kutumia panya waliokuwa na ugonjwa wa kisukari.
Upandikizaji uliofanywa katika majaribio haya wa seli za mfumo wa fahamu kwenda kwenye tezi kongosho, siyo tu umeonesha uwezo wa seli za mfumo wa fahamu kuthibiti uzalishaji wa kichocheo cha insulin, bali pia ukweli kuwa seli zinazotajika kwa ajili ya upandikizaji zinaweza kutoka kwa mgonjwa mwenyewe bila kuhitaji uwepo wa mtoaji (donor).
Akihitimisha, Dr. Kubawara alisema kuwa, matokeo ya utafiti wao yameonesha uwezo mkubwa wa seli za mfumo wa fahamu katika kutibu kisukari bila kuhitaji kufanya mabadiliko ya kinasaba au mtoaji (donor), hali ambayo inaleta matumaini ya kuondokana na tatizo la ukosefu wa watoaji wa seli za upandikizaji siku za mbele.
No comments:
Post a Comment