Showing posts with label magonjwa. Show all posts
Showing posts with label magonjwa. Show all posts

Sunday, March 18, 2012

Hiatus Hernia (Ngiri ya Kwenye Kifua)

Hiatus Hernia (Ngiri ya Kwenye Kifua)
Hiatus Hernia ni tundu linalotokea baada ya sehemu ya juu ya mfuko wa kuhifadhia chakula (tumbo) kuingia kwenye sehemu ya kifua kupitia uwazi unaojulikana kama esophageal hiatus. Kwa kawaida uwazi huu (esophageal hiatus) hupitisha mrija wa chakula kwenda kwenye tumbo yaani esophagus na si utumbo.
Mara nyingi, tatizo hili huonekana kwa takribani ya 60% ya watu wenye umri wa miaka 50 na kuendelea, ingawa pia linaweza kuwapata wale walio na umri wa chini ya huo.
Kuna aina mbili kuu za hiatus hernia
  • Sliding type : Kama jina lake linavyomaanisha, aina hii hutokea iwapo sehemu ya juu ya utumbo inaposukumwa juu na kuingia kwenye upenyo wa esophagus hiatus baada ya kutokea kwa ongezeko la presha katika maeneo ya tumbo (increased pressure in the abdominal cavity) na kurudi kama kawaida wakati presha inapopungua.
  • Fixing type: Aina hii hutokea iwapo sehemu ya juu ya utumbo inapokuwa kwenye maeneo ya kifua na haishuki chini.
Vihatarishi vya Ugonjwa huu
1. Ongezeko la presha tumboni kutokana na;
  • Kunyanyua vitu vizito au kuinama sana
  • Kukohoa sana au kukohoa mara kwa mara kutokana na sababu mbalimbali
  • Kutapika sana (violent vomiting)
  • Kupiga chafya sana (Hard sneezing)
  • Ujauzito -Kutokana na mfuko wa uzazi (uterus) kusukuma viungo kwenda juu kutokana na kuongezeka ukubwa wake.
  • Wakati wa kujifungua- Kutokana na kuongezeka kwa presha ndani ya tumbo wakati mama anajitahidi kusukuma mtoto. Si wanawake wote wanaopata tatizo hili.
  • Kujikamua wakati wa kwenda haja kubwa (straining during constipation)
  • Uzito uliopitiliza -Kutokana na kuongezeka uzito ambao unasukuma viungo kwenye maeneo ya kifua kwenda chini na hivyo kuongeza presha tumboni.
  • Kujisaidia haja kubwa wakati mtu amekaa - Kutokana na maendeleo ya binadamu, watu wengi sasa hivi wameanza utamaduni wa kutumia vyoo vya kukaa wakati wa kujisaidia haja kubwa, katika tafiti iliyofanywa na Dr Denis Burkitt (1), imeonekana ya kwamba kujisaidia wakati mtu amekaa hufanya mtu kujikamua zaidi na hivyo kuongeza presha ndani ya utumbo (Increased intraabdominal pressure) na hivyo kusukuma mfuko wa kuhifadhia chakula (utumbo) kupitia kwenye upenyo wa esophagus hiatus na hivyo kusababisha hiatus hernia.
2. Tatizo la kurithi (Heredity)
3. Uvutaji sigara
4. Matumizi ya madawa ya kulevya kama cocaine
5. Kuwa na kiwambo hewa (diaghram) dhaifu
6. Msongo wa mawazo (depression)
7. Matatizo ya kuzaliwa (congenital defects).
Dalili na Viashiria
  • Maumivu ya kifua
  • Kichomi (pleurisy) ambacho kinakuwa kikali sana wakati wa kuinama au mtu anapolala chini
  • Matatizo katika kumeza chakula
  • Kupumua kwa shida Kutokana na hiatus hernia kupunguza uwezo wa ufanyaji kazi wa kiwambo hewa (diaphragm).
  • Mapigo ya moyo kwenda kasi Kutokana na mkwaruzo wa neva inayojulikana kama vagus nerve.

Mara nyingi sana hiatus hernia haioneshi dalili zozote zile isipokuwa inapokuwa kubwa sana. Maumivu na kichomi hutokana na kurudishwa kwa tindikali ya kwenye tumbo (gastric acid) kwenye kifua. Pia tindikali aina ya bile acid na hewa huwa inasukumwa juu kwenye kifua.

Vipimo vya Uchunguzi
1. Barium Swallow X-ray – X-ray ya kuangalia viungo vya ndani, mgonjwa hupewa au huchomwa sindano yenye dawa maalum ambayo huonekana vizuri kwenye X-ray, na baada ya hapo hupigwa picha za X-ray akiwa amekaa au amesimama. Kawaida kipimo hiki huchukua masaa 3-6.
2. Esophagogastroduodenoscopy (OGD) - Mpira maalum wenye taa na camera kwa mbele unaoingizwa mdomoni kwenye mpira wa kupitisha chakula (esophagus) na hutazama kama kuna magonjwa yoyote kwenye esophagus hadi kwenye sehemu inayojulikana kama duodenum.
3. Electrocardiography (ECG)- Kipimo cha kuangalia kama kuna matatizo katika jinsi moyo unavyopiga
4. Chest X-ray- Kuangalia kama kuna magonjwa kama homa ya mapafu (Pneumonia), kama kuna pafu lolote ambalo halifanyi kazi, madhara kwenye moyo (injury to the heart) na pia kuangalia matatizo yoyote yale.
5. Complete Blood Count- Kipimo cha kuangalia wingi wa damu, kuangalia aina mbalimbali za chembechembe za damu kama zipo katika maumbo yao ya kawaida, wingi wao kama ni wa kawaida.
Tiba ya Hiatus Hernia
Kama ilivyoelezwa hapo awali, hiatus hernia mara nyingi haioneshi dalili zozote na hivyo mtu anaweza kuendelea na shughuli zake za kila siku bila madhara yoyote. Tiba ya hiatus hernia inahusisha dawa na upasuaji.
Tiba ya Dawa
  • Dawa za kuyeyusha tindikali mwilini (antacids) hutumika kama Gelusil, Maalox nk.
  • H2 receptor antagonist –Dawa zinazopunguza kiwango cha utolewaji wa tindikali kama cimetidine, ranitidine nk.
  • Dawa ambazo huzuia utolewaji wa tindikali na kuponya tishu za esophagus (Proton Pump Inhibitors) dawa hizi ni omeprazole, lansoprazole nk.
Tiba ya Upasuaji
Upasuaji hufanyika kwa wagonjwa wa dharura au pale ambapo mgonjwa hajapata nafuu hata baada ya kutumia dawa na hali yake inazidi kuwa mbaya. Upasuaji huu hufanywa na daktari wa upasuaji kwa kuchana (incision) kwenye kifua (thoracotomy) au tumbo (laparatomy) na kuvuta sehemu ya utumbo iliyopanda juu kwenye kifua ili kuirudisha katika sehemu yake ya kawaida na kupunguza ule uwazi uliopo kwenye diaphgram, kurekebisha sphincters (nyama zinazosaidia katika kufunga na kufungua uwazi kwenye diaphragm) za esophagus ambazo zimekuwa dhaifu. Pia daktari anaweza kufanya upasuaji huu kwa kuchana sehemu ndogo sana kwenye tumbo na kwa kutumia kifaa maalum chenye kumsaidia kurekebisha henia hii. Aina hii ya upasuaji hujulikana kama endoscopic surgery.
Madhara ya Hiatus Hernia
Madhara ya hiatus hernia hutokana na kurudishwa juu kwa tindikali aina ya gastric acid na hivyo kusababisha ugonjwa unaojulikana kama Gastroesophageal Reflux Disease (GERD).
Madhara haya ni;
  • Kichomi
  • Ugonjwa wa esophagitis
  • Barretts esophagus
  • Saratani ya kwenye mpira wa kupitisha chakula (esophageal cancer)
  • Kuoza kwa meno (dental erosion)
  • Strangulation of the stomach (kunyongwa kwa sehemu ya juu ya tumbo na hivyo kusababisha sehemu hii kukosa damu ya kutosha na hivyo tishu zake kufa na kuoza (ischemic and necrosis)
  • Kuzuia pafu kujaa hewa na hivyo kushindwa kutanuka na kusababisha mtu kupumua kwa shida sana.
Jinsi ya kujikinga
1. Kuacha kunywa pombe
2. Kuacha matumizi ya madawa ya kulevya kama cocaine
3. Kupunguza uzito uliopitiliza
4. Kula milo midogo mara nyingi kwa siku
5. Epuka vyakula vinavyoongeza kichomi kama chocolate, vitunguu, vyakula vikali, vinywaji venye limau, ndimu nk.
6. Kula chakula cha usiku masaa matatu kabla ya kwenda kulala
7. Pumzika kwa kukaa baada ya kula usilale chini.
8. Nyanyua sehemu unayoweka kichwa chako wakati wa kulala kwa angalau 15cm (6 inches)
9. Punguza msongo wa mawazo
10. Acha kuvuta sigara.
Marejeo
1. Burkitt DP (1981). "Hiatus hernia: is it preventable?". Am. J. Clin. Nutr. 34 (3): 428–31. PMID 6259926
2. Sontag S (1999). "Defining GERD". Yale J Biol Med 72 (2-3): 69–80. PMC 2579007. PMID 10780568

Maambukizi ya Fangasi katika Sehemu za Siri (v.Candidiasis)

candidiasis
Kati ya maambukizi yanayowasumbua wanawake wengi duniani ni maambukizi ya fangasi. Inakisiwa asilimia 75 ya wanawake wote duniani hupata maambukizi haya katika kipindi cha uhai wao.
Maambukizi ya fangasi katika sehemu za siri za mwanamke husababishwa na uwepo wa fangasi wanaojulikana kitaalamu kama Candida albicans. Maambukizi haya pia hujulikana kama yeast infection au thrush. Fangasi hupatikana kama vimelea vya kawaida katika mdomo, mpira wa kupitisha chakula sehemu inayojulikana kama pharynx, katika kibofu cha mkojo, uume na hata kwenye uke.
Mfumo mzuri wa kinga wa mwili pamoja aina fulani za bakteria wanaoishi pamoja na fangasi hawa husaidia sana katika kuthibiti maambukizi yanayoyosababishwa na aina hi ya fangasi.
Nini hutokea?
Kwa kawaida, Candida albicans huishi kwenye uke na sehemu nyingine (kama zilivyoelezewa hapo juu) bila kusababisha madhara yoyote yale isipokuwa pale mazingira ya eneo husika yanapobadilika kama vile mabadiliko katika hali ya pH ya eneo husika (ifahamike ya kwamba pH ya kawaida ndani ya uke ni 4.0 - 4.5) au uwiano wake na vimelea (microorganisms) wengine unapoharibiwa kutokana na sababu mbalimbali kama vile matumizi ya madawa aina ya antibiotics, kupungua kwa kinga mwilini kutokana na magonjwa mbalimbali n.k.
Maambukizi haya ya fangasi yanaweza kugawanywa katika sehemu kuu mbili;
1. Maambukizi yasiyo makali yaani uncomplicated thrush: Katika kundi hili, mgonjwa hupatwa na maambukizi mara moja hadi nne kwa mwaka na dalili zake huwa si mbaya sana na maambukizi haya husababishwa na fangasi wa jamii hii ya Candida albicans.
2. Maambukizi makali yaani complicated thrush: Katika kundi hili, mgonjwa hupatwa na maambukizi zaidi ya mara nne kwa mwaka, dalili zake kuwa mbaya zaidi au kama maambukizi yatakuwa yametokea kipindi cha ujauzito, ugonjwa wa kisukari, upungufu wa kinga mwilini. Aina hii kusababishwa na vimelea vya aina nyingine tofauti na Candida albicans.

Vihatarishi

Watu walio katika hatari ya kupata maambukizi ya fangasi hawa ni wale wenye;
• Kutumia sana dawa aina ya detergents kwenye sehemu za siri au douches (vifaa vinavyotumiwa kusafishia uke kwa kutumia maji yaliyochanganywa na siki au antiseptic yoyote ile) kwa sababu hali husababisha kuharibika kwa uwiano wa fangasi na aina nyingine ya vinyemelezi kama bakteria aina ya lactobacilli
• Kutumia sana madawa aina ya antibiotics, steroids ambayo yana tabia ya kushusha kinga ya mwili
• Mabadiliko ya mfumo wa homoni mwilini ambayo husababisha mabadiliko katika s ehemu za siri na hivyo kufanya kuwepo kwa ukuaji wa kasi wa fangasi hawa
• Ujauzito (kutokana na kubadilika kwa mfumo wa homoni mwilini na kupungua kwa kinga ya mwili). Hata hivyo ieleweke hapa kuwa si kila mjamzito hupatwa na maambukizi haya.
• Matumizi ya dawa za kupanga uzazi (vidonge vya majira)
• Upungufu wa kinga mwilini kutokana na magonjwa sugu kama kisukari, saratani aina yoyote ile, ugonjwa aina ya mononucleosis na nk.

• Ugonjwa wa ukimwi (HIV/AIDS)
• Matibabu ya homoni (hormonal replacement therapy) kutokana na sababu mbalimbali
• Matibabu ya kusaidia kushika mimba kwa wale wenye matatizo ya uzazi (infertility treatment)
• Msongo wa mawazo (stress)
• Utapia mlo (malnutrition)
• Kuvaa nguo au mavazi yanayoleta joto sana sehemu za siri kwa muda mrefu kama nguo za kuogelea (swimwear), nguo za ndani (chupi) zilizotengenezwa kwa kitambaa aina ya nylon, nguo za ndani zinazobana sana nk.
• Kujamiana kwa njia ya kawaida mara tu baada ya kujamiana kupitia njia ya haja kubwa au matumizi ya vilainishi venye glycerin wakati wa kujamiana pia yamehusishwa na maambukizi haya.
• Kuvimba kwa tezi la koo (goiter)
• Saratani ya tezi la koo (thyroid cancer)
• Wanawake wenye umri wa miaka kati ya ishirini na thelathini wapo kwenye hatari kubwa ya kupata maambukizi haya wakati wale ambao wameshaacha kupata hedhi au wale ambao hawajaanza kupata hedhi kabisa hawako kwenye hatari kubwa.

Kwa wanaume vihatarishi vya maambukizi haya ni;

• Kujamiana na mwanamke mwenye tatizo hili au maambukizi haya
• Upungufu wa kinga mwilini
• Matumizi ya madawa aina ya antibiotics kwa muda mrefu bila ushauri wa daktari
• Magonjwa sugu kama kisukari, saratani ya aina yoyote ile na nk.

Dalili na viashiria kwa wanawake;

• Kuwashwa sehemu za siri (kwenye tupu ya mwanamke)
• Kuhisi kuwaka moto sehemu za siri (burning sensation)
• Kufanya kama vidonda katika sehemu za siri (soreness)
• Maumivu wakati wa kujamiana (superficial dyspareunia)
• Maumivu au usumbufu wakati wa kujisaidia haja ndogo (wakati mtu anakojoa)
• Kuvimba na kuwa rangi nyekundu kwa mdomo wa nje wa tupu ya mwanamke (labia minora)
• Kutokwa na uchafu wa rangi nyeupe au nyeupe kijivu, unaoweza kuwa mwepesi, majimaji au mzito na ambao umefanana na jibini (cottage cheese like discharge) wenye muonekano unaojulikana pia kama curd-like appearance. Kwa kawaida, uchafu huu haumbatani na harufu yoyote isipokuwa panapokuwa na tatizo la ziada kama ugonjwa wa zinaa aina ya Bacteria vaginosis. Uchafu huu unaotoka hapa unaweza kuenea kwenye maeneo mengine yaliyokaribu na tupu ya mwanamke kama kwenye mitoki (groin area) au perineum na kusababisha kuharibika kwa ngozi katika sehemu hizo.
Dalili na viashiria hivi huwa mbaya zaidi wakati mwanamke anapokaribia kupata hedhi.

Dalili na viashiria kwa wanaume ni;

• Kuwashwa sehemu za siri
• Kuvimba na kuwa rangi nyekundu kwenye ncha ya uume
• Kuwepo kwa uchafu wa rangi nyeupe (kama nilivyoeleza hapo juu) kwenye sehemu ya juu ya uume.
• Kuwa na vidonda vidogo kwenye uume (sore on the glans)
Hata hivyo, mara nyingi wanaume hawaoneshi dalili zozote zile, ni vizuri kwa mwanamke kumueleza mwenza wake pale anapopata maambukizi haya ili naye pia apate kutibiwa.

Vipimo vya uchunguzi

Kabla ya vipimo vya uchunguzi, ni muhimu kwa daktari kuchukua historia ya mgonjwa kwa usahihi kabisa. Vipimo vitahusisha;
1. Uchunguzi wa uke (
(PV exam)
– Daktari huvaa gloves, na kuzilainisha gloves hizi kwa jelly maalum, mgonjwa hulala kwenye kitanda na kutanua miguu yake ili njia itanuke na kumrahisishia daktari kumfanyia uchunguzi, wakati akiwa tayari, daktari ataingiza vidole vyake viwili (cha shahada na cha kati) ukeni kwa dhumuni la
i. Kuhisi kama kuna uvimbe wowote ndani ya tupu ya mwanamke
ii. Kuangalia kama anapata maumivu wakati wa kujamiana
iii. Kuangalia kama kuna uchafu wowote unaotoka, wingi wake, rangi yake, harufu yake, uzito wake (mwepesi, majimaji au mzito), na aina ya uchafu unaotoka kama ni sahihi kutokana na maelezo ya mgonjwa au ni tofauti
iv. Kuangalia kama sehemu ya siri ipo kawaida
v. Kuangalia kama kuna uvimbe wowote wa tezi za sehemu ya siri (mitoki)
vi. Kuangalia nywele za sehemu za siri zilivyo na jinsi zilivyokaa
vii. Kuangalia shingo ya kizazi, bartholin glands nk.
viii. Kuangalia sehemu ya haja kubwa kama kuna skin tags, bawasiri (haemorrhoids) nk.
ix. Kuangalia kwenye kinembe
kama kuna tatizo lolote lile.
Hayo ni baadhi tu ya malengo na faida za kipimo hiki kwa vile humuwezesha daktari kugundua tatizo au maradhi mengine ya ziada ambayo hayajaanza bado kuonesha dalili zake kwa mgonjwa au mgonjwa mwenyewe hafahamu kama hali aliyo nayo ni tatizo. Hata hivyo inashauriwa sana kabla ya kufanya kipimo hiki, daktari amjulishe mgonjwa aina ya kipimo, lengo lake na jinsi kitakavyofanyika ili kumuandaa mgonjwa kisaikolojia. Aidha ni muhimu pia kumtaarifu wakati anapoanza kuingiza vidole.
2. Kuchunguza uchafu unaotoka kwa kutumia hadubini (microscope). Mara tu baada ya kuchukua sehemu ya uchafu kwa kutumia swab, kipimo hicho humwagiwa tone la 10% potassium hydroxide ambayo huyeyusha chembechembe za ngozi na kubakisha seli za Candida albicans. Kuwepo kwa pseudohyphae (mfano wa aina fulani ya mizizi au miguu ya fangasi hawa) pamoja na budding yeast cells (yaani seli za fangasi zinazojigawa kwa ajili ya kuzaliana) ni uthibitisho wa maambukizi ya fangasi aina ya Candida albicans.
3. Kuchukua kipimo na kuotesha kwenye maabara ili kuangalia aina ya uoto huo kama ni wa fangasi aina ya Candida albicans, ama la.
4. Kipimo cha mkojo (Urinalysis)
5. Vipimo vingine hufanyika kulingana na dalili zinazoashiria uwepo wa magonjwa mengine kama vile ugonjwa wa kisukari, HIV/AIDS, ugonjwa wa kuvimba tezi la koo (goiter), saratani ya tezi koo (thyroid cancer) nk.
Matibabu
Matibabu ya fangasi huusisha dawa za kutibu fangasi (antifungal drugs) kama vile dawa za kupaka za topical Clotrimazole, topical Nystatin, Fluconazole au topical Ketoconazole.
Wagonjwa wenye maambukizi yasiyo makali yaani uncomplicated va#@ginal candidiasis wanaweza kutumia dawa za kupaka (cream) kutoka dawa za fangasi za jamii ya -azole kama vile Butoconozale, Miconazole, Clotricomazole nk. Dawa hizi hutumika kwa muda wa siku 3-7 kulingana na aina ya dawa. Mgonjwa anashauriwa kupaka dawa ndani ya uke pamoja na maeneo yote yanayozunguka sehemu hiyo. Jinsi ya kupaka dawa hizi ni kuanzia mbele kuelekea nyuma.
Aidha mgonjwa anaweza kupewa dawa za kutumbukiza ukeni ambayo atatumia kwa muda wa siku 3-14 kulingana na aina ya dawa. Dawa hizo ni pamoja na Miconazole, Tiaconazole, Terconazole, Nystatin nk. Kidonge cha kumeza aina ya fluconzole pia huweza kutolewa. Dawa hizi nilizotaja hapa juu zina kawaida ya kuharibu ubora wa mipira ya kondomu zilizotengenezwa na mpira aina ya latex (latex condoms) pamoja na vifaa vya upangaji uzazi aina ya diaphragms. Ni vizuri kwa daktari kabla ya kumpa mgonjwa dawa hizi kumfahamisha kwa ufasaha jinsi ya kuzitumia na tahadhari anayotakiwa mgonjwa kuchukua. Inashauriwa kama baada ya matumizi haya bado mgonjwa ana dalili za maambukizi au mgonjwa akapata tena maambukizi haya ndani ya miezi miwili baada ya matibabu ya awali, basi anashauriwa kwenda kumuona daktari ili apate matibabu zaidi.
Kwa wale wenye maambukizi makali yaani complicated v@ginal candidiasis, kabla ya kupewa tiba, ni muhimu kwanza kufanyiwa kipimo cha kuotesha sehemu ya uchafu unaootoka ukeni ili kuwa na uhakika kama kweli fangasi wanaosababisha maambukizi haya ni Candida albicans ama la, kwani fangasi aina ya Candida glabrata pia wanaweza kusababisha aina ya maambukizi haya na huwa siyo rahisi kutibika kwa kutumia matibabu ya kawaida ya kutibu fangasi pamoja na pia si rahisi kuonekana kwa kutumia hadubini (microscope).
Matibabu ya wagonjwa wenye aina hii ya fangasi hujumuisha matumizi ya dawa za kupaka au vidonge vya kuweka ukeni kwa muda mrefu yaani kwa muda wa siku saba hadi kumi na nne (7-14) au dawa aina ya fluconazole ambayo hutumika kila baada ya siku tatu (yaani siku ya 1, siku ya 4 na siku ya 7). Mara baada ya kumaliza tiba hii, mgonjwa hutakiwa kuendelea nayo mara moja kwa wiki kwa muda wa miezi sita. Ikiwa matibabu haya hayatasaidia basi mgonjwa anaweza kushauriwa kutumia mchanganyiko wa fluconazole pamoja na dawa ya kupaka ya Clotrimazole mara mbili au moja kwa wiki kulingana na dozi ya dawa, au fluconazole na dawa nyingine za kupaka kwa wakati mmoja.
Matibabu ya wagonjwa wenye maambukizi hatari sana yaani severe v@#ginal candidiasis ambayo kwa kawaida huambatana na dalili kama uke kuwa mwekundu sana, uke kuvimba, michubuko ya ngozi ya ukeni (excoriation) na kutokea kwa mifereji kama vidonda (fissure formation) huwa ni dawa zozote za kupaka zilizotajwa hapo juu kwa muda wa siku 7 mpaka 14 au dawa ya fluconazole ambayo hutolewa mara mbili, ambapo dozi ya pili hutolewa siku ya tatu baada ya kutolewa kwa dozi ya awali (second dose 72hrs after initial dose).
Matibabu ya maambukizi ya fangasi ambayo hayasababishwi na Candida albicans kwa mfano Candida glabrata nk ni matumizi ya dawa za kupaka jamii ya nonfluconazole azole groups kama vile Posaconazole, Voriconazole nk zitolewazo kwa muda wa siku 7 mpaka 14 pamoja na kidonge cha Boric acid kwa muda wa siku 14. Mtu mwenye maambukizi haya pia anashauriwa kuonana na daktari bingwa wa magonjwa ya akina mama.
Kwa vile maambukizi ya fangasi hutokea sana kwa wanawake wajawazito, hivyo basi wanashauriwa kutibiwa kwa kutumia dawa za kupaka tu kwa muda wa siku 7. Aidha dawa aina ya Itraconazole haipaswi kutumiwa na mwanamke mjazito au anayekusudia kushika mimba. Dawa ya Ketoconazole haipaswi kutolewa bila ushauri wa daktari kwani ina madhara ya kusababisha ugonjwa hatari wa Ini (Fulminant hepatitis). Usugu wa fangasi dhidi ya dawa za jamii ya azole groups hutokea baada ya matumizi ya dawa za vidonge (vya kumeza) za kutibu fangasi kwa muda mrefu.
Maambukizi ya fangasi pia huonekana sana kwa wagonjwa wenye Ukimwi. Tiba ya maambukizi haya ni sawa na tiba ya watu ambao hawana ugonjwa wa Ukimwi. Hata hivyo, kwa wale wagonjwa wa ukimwi ambao wamepata maambukizi ya fangasi mara kwa mara wanashauriwa kunywa dawa aina ya fluconzole mara moja kwa wiki kama kinga dhidi ya maambukizi haya au kama njia ya kupunguza fangasi hawa. Kadhalika dawa za kutibu fangasi aina ya Itraconazole, Voriconazole, Posaconazole huingiliana sana katika utendaji kazi na dawa za kurefusha maisha za ugonjwa wa Ukimwi (Antiretroviral drugs, ARVs) aina ya Protease Inhibitors, PIs (rotinavir nk.) na Nonnucleoside Reverse Trancriptase Inhibitors, NNRTI (maraviroc nk).
Wakati mwingine, maambukizi ya fangasi yanaweza kuambatana na magonjwa ya zinaa (Bacterial vaginosis nk), hivyo dawa zitatolewa kulingana na dalili na historia ya mgonjwa.
Kinga ya maambukizi ya fangasi
• Kuosha sehemu ya siri kwa kutumia kitambaa kisafi kila siku na kuosha kuanzia mbele kuelekea nyuma, epuka kurudia ukishafika nyuma.
• Epuka matumizi ya sabuni zenye manukato, bubble baths, v@#ginal deodorant products, feminine hygiene, na bath powder.
• Vaa chupi ambazo hazibani sana na zilizotengenezwa kwa kutumia pamba au hariri (silk), epuka synthetic underwear.
• Epuka mavazi yoyote ya kubana kama jeans za kubana nk.
• Badilisha nguo za ndani (chupi) kila zinapopata unyevunyevu.
• Fua chupi zako kwa maji yenye nyuzi joto 90 na kuendelea.
• Tumia pad wakati tu unapozihitaji (kama umeingia kwenye mzunguko wako wa hedhi)
• Kula mlo wenye virutubisho vyote kamili (balanced diet)
• Epuka kufanya mapenzi na mpenzi wako ambaye amepata maambukizi ya fangasi.
• Epuka kuoga maji moto sana (hot baths) tumia maji ya uvuguvugu, hii kwa wale ambao wanaishi kwenye ukanda wa joto (tropical climate).
• Matumizi ya vifaa vya ngono , vifaa vya upangaji uzazi (diaphragms, cervical caps) yanaweza kuleta kujirudia kwa maambukizi ya fangasi kama havitaoshwa na kukaushwa vizuri baada ya kutumiwa.
• Baadhi ya tafiti zilizofanyika, zimethibitisha ya kwamba unywaji wa maziwa ya mtindi (yoghurt) yenye live culture, husaidia kupunguza maambukizi ya fangasi.

Kukosa Usingizi Husababisha Upungufu wa Homoni ya Testosterone

Kukosa Usingizi
Mnamo mwaka 2007, watafiti nchini Marekani walifanikiwa kutoa ripoti inayojaribu kuhusisha ukosefu wa usingizi na upungufu wa homoni ya testosterone miongoni mwa wanaume watu wazima.

Kwa kawaida kiwango cha homoni ya testosterone hupungua kadiri mwanaume anavyozidi kuwa mtu mzima, na kwa baadhi ya wanaume, kupungua huku kwa testosterone huweza kusababisha ulegevu wa mwili, kukosa hamu ya ngono na hata kuvunjika mifupa ya mwili.

Watafiti wanasema kuwa, wapo baadhi ya wanaume walio kwenye miaka 80 bado huweza kuwa na kiwango cha juu cha testosterone sawa na kile kinachopatikana kwa wanaume vijana. Hata hivyo sababu kubwa inayofanya kuwepo na utofauti katika viwango vya testosterone miongoni mwa rika hizo mbili bado hazieleweki sawasawa, ingawa watafiti wanasema kuwa ukosefu wa usingizi miongoni mwa watu wazima na wazee unaweza kuwa chanzo kimojawapo cha kuwepo kwa hali hiyo.

"Matokeo ya utafiti wetu yanaongeza uwezekano kuwa wanaume watu wazima na wazee ambao hupata muda mfupi sana wa kulala nyakati za usiku huwa na kiwango kidogo sana cha homoni ya testosterone wakati wa asubuhi," anasema mtafiti Plamen Penev, wa kutoka Chuo Kikuu cha Chicago, nchini Marekani.

Wakati wa utafiti, wataalamu waliofanya uchunguzi huo walipima kiwango cha homoni ya testosterone katika damu kila asubuhi cha wanaume watu wazima wenye umri kati ya miaka 64 na 74 waliojitolea kushiriki kwenye utafiti huo. Aidha, mtindo wao wa kulala pamoja na kupata usingizi pia vilichunguzwa kila siku kwa muda wa wiki nzima.

Matokeo ya uchunguzi huo yalionesha kuwa kiasi cha usingizi walicholala kilikuwa na uhusiano wa karibu sana na kiwango cha testosterone katika damu wakati wa asubuhi. Wale waliopata usingizi mzuri na kwa muda mrefu (walau saa nane) walikuwa na kiwango kikubwa cha testosterone wakati wale waliopata usingizi wa kubabaisha (saa nne) walikutwa na kiwango cha chini cha homoni hiyo. Wastani wa muda wa kulala ulikuwa masaa sita.

"Pamoja na kwamba matokeo ya utafiti huu yanaonesha kuwa urefu wa muda wa kulala wa mtu waweza kuwa kiashiria cha mabadiliko ya homoni katika mwili yanayohusiana na umri, matokeo ya utafiti huu yanatoa tu picha ya nini kinachotokea mwilini kama mtu asipopata usingizi wa kutosha. Hata hivyo, tafiti zaidi zinahitajika ili kuthibitisha umuhimu wa uhusiano kati ya usingizi na mabadiliko ya homoni katika mwili," anasema Dr. Penev.

Wataalamu wa masuala ya afya ya usingizi wanashauri watu wazima kupata wastani wa angalau saa saba mpaka nane za kulala kila usiku ili kuwa na afya bora. Ripoti kamili ya matokeo ya utafiti huu inapatikana katika toleo la mwezi April, 2007 la jarida la afya la Sleep.

Dawa za Usingizi Chanzo cha Saratani na Kifo

Dawa za Usingizi
Utafiti uliofanywa nchini Marekani hivi karibuni umetoa matokeo ya kushangaza kwa kusema ya kwamba matumizi ya dawa za usingizi huongeza hatari ya kupata saratani pamoja na mtu kufa mapema. Utafiti huo umesema wale wanaotumia dozi kubwa ya dawa ya usingizi wako kwenye hatari ya kupata magonjwa ya saratani.
Utafiti huo ambao ulifanywa na watafiti wa kitengo cha usingizi katika kituo cha Jackson Hole Centre for Preventive Medicine in Wyoming and the Scripps Clinic Viterbi Family Sleep Centre kilichopo jijini California nchini Marekani ili kuangalia hatima ya watu wanaotumia dawa za usingizi aina ya benzodiazepines kama temazepam, diazepam (valium), dawa mpya aina ya zolpidem, zopiclone, zaleplon, dawa za jamii ya barbiturates na zile zinazotumiwa kutibu mcharuko mwili (allergy) na ambazo huleta usingizi.
Matokeo ya utafiti huo yanasema wale wanaotumia dawa za usingizi (Hypnotics) walizoandikiwa na Daktari wako kwenye hatari ya 4.6 kufa ndani ya miaka 2 na nusu ukilinganisha na watu ambao hawatumii dawa za usingizi. Wale ambao wanatumia dozi ndogo ya dawa za usingizi yaani wanaotumia wastani wa vidonge 4-18 kwa mwaka wako kwenye hatari ya mara 3.6 zaidi kufa kulinganisha na wale ambao hawatumii dawa za usingizi.
Wale wanaotumia dozi kubwa yaani vidonge 18-132 kwa mwaka wako kwenye hatari kubwa ya mara 4.4 zaidi kufa, na wale wanaotumia zaidi ya vidonge 132 kwa mwaka wako kwenye hatari ya mara 5.3 zaidi kufa kulinganisha na wale ambao hawatumii dawa za usingizi. Asilimia 93 ya wale walioshiriki katika utafiti huu walikuwa ni wale wanaotumia dozi kubwa ya dawa za usingizi. Pia wale wanaotumia dozi kubwa ya dawa hizi wako kwenye hatari ya asilimia 35 kupata saratani kubwa. Kwa wale wanaotumia dawa aina ya zolpidem wako kwenye hatari ya mara 5.7 kufa huku wale wanaotumia dawa aina ya temazepam wako kwenye hatari ya mara 6.7 kufa kulinganisha na wale wasiotumia dawa za usingizi.
Utafiti huo umesema wale walio kwenye hatari ya madhara haya ya dawa za usingizi ni wale walio katika umri wa miaka 18-55 ingawa sababu halisi haikuelezwa katika matokeo ya utafiti huo. Wagonjwa 10,500 wanaotumia dawa za usingizi walishiriki katika utafiti huo wakilinganishwa na watu 23,500 ambao hawatumii dawa za usingizi walioshiriki katika utafiti huo.
Watafiti hao walisema tiba ya kutotumia dawa yaani ya tiba ya utambuzi wa tabia (cognitive behavior therapy) inaweza kuwa na manufaa zaidi kuliko matumizi ya dawa za usingizi na hata matumizi ya dawa za usingizi kwa muda mfupi yanapaswa kuangaliwa kwa makini. Watafiti hao wakiandika katika jarida la British Medical Journal walisema “Faida chache zinazopatikana kutokana na matumizi ya dawa za usingizi ambazo zilitafitiwa kwa kina na makundi ambayo hayana maslahi yoyote na dawa hizi haziwezi kuhalalisha madhara yatokanayo na matumizi ya dawa hizi za usingizi”.
Matokeo ya utafiti huu ni changamoto kubwa katika fani ya afya hasa ukizingatia ya kwamba watu wengi hutumia dawa za usingizi kutokana na kupatikana kiurahisi katika maduka mbalimbali ya dawa katika Afrika Mashariki. Pia ni changamoto kubwa sana kutokana na dawa hizi kutumika wakati wa upasuaji, kutibu magonjwa ya akili, kutibu mcharuko mwili, msongo wa mawazo na hata kwa wazee.
Kulingana na matokeo haya ni vizuri kuangalia upya matumizi ya dawa za usingizi na utafiti zaidi unahitajika kufanyika kabla ya kutoa msimamo kuhusu matumizi ya dawa za usingizi.

Upandikizaji wa seli za mfumo wa fahamu waweza kutibu kisukari

Watafiti nchini Japan wamegundua jinsi seli za mfumo wa fahamu zinavyoweza kutumika kama seli mbadala zinazofaa kupandikizwa kwenye seli kongosho ili kutibu kisukari. Ripoti ya utafiti huo ambayo imechapishwa kwenye jarida la kitafiti la EMBO Molecular Medicine, inaonesha kuwa seli zinazovunwa kutoka katika mfumo wa fahamu zinaweza kupandikizwa katika tezi kongosho na hivyo kumaliza tatizo la ukosefu wa seli za beta ambazo huitajika kwa ajili ya uzalishaji wa insulin.

Kisukari ni ugonjwa unaosababishwa na ukosefu wa kichocheo cha insulin kinachozalishwa na tezi kongosho, na ambao huathiri karibu watu milioni 200 duniani. Mpaka sasa hakuna tiba yeyote ya ugonjwa huu, hali inayowafanya wagonjwa wa kisukari kutegemea zaidi matumizi ya dawa au njia nyingine mbadala kuthibiti kiwango cha sukari mwilini.

Utafiti huo ulioongozwa na Dr Tomoko Kuwabara kutoka taasisi ya tafiti za Afya ya AIST ya Tsukuba nchini Japan, ulilenga katika kuchunguza jinsi seli za binadamu zinavyokua na kijiwagawa kulingana na kazi mbalimbali za mwili, na pia kuchunguza uwezekano wa kutumia seli mbalimbali kutekeleza kazi zilizo nje ya majukumu yake ya kawaida.

Katika kufafanua, Dr. Kubawara anasema kuwa kwa vile kisukari ni ugonjwa unaosababishwa na ukosefu wa aina moja ya seli, ugonjwa huu unaweza kutibika kwa kutumia njia ya upandikizaji wa seli mpya zitakazotumika kuzalisha kichocheo cha insulin. Anasema, hata hivyo kwa vile kupandikiza seli za beta kutoka tezi kongosho za watu wengine ni ngumu kwa sababu ya ukosefu wa watoaji, njia muafaka ni kutumia seli za mfumo wa fahamu wa mgonjwa mwenyewe katika kufanikisha upandikizaji huo.

Seli za mfumo wa fahamu zinazoweza kupandikizwa kwenye tezi kongosho kwa urahisi zaidi ni zile zilizopo katika maeneo ya ubongo wa mbele yajulikanayo kitaalamu kama hippocampus na olfactory bulb.

Kwa kawaida seli za mfumo wa fahamu huzalisha kiwango kidogo sana cha insulin tofauti na seli za tezi kongosho, hata hivyo, mara tu baada ya kupandikizwa kwenye tezi kongosho, seli hizo zilianza kutoa kiwango kikubwa cha kichocheo cha insulin na kiwango cha sukari katika damu kilionekana kupungua kwa kiwango kikubwa. Na hata seli zilizopandikizwa zilipoondolewa, kiwango cha insulin kilishuka na kusababisha kupanda tena kwa kiwango cha sukari katika damu.

Utafiti huo ulifanyika kwa kutumia panya waliokuwa na ugonjwa wa kisukari.

Upandikizaji uliofanywa katika majaribio haya wa seli za mfumo wa fahamu kwenda kwenye tezi kongosho, siyo tu umeonesha uwezo wa seli za mfumo wa fahamu kuthibiti uzalishaji wa kichocheo cha insulin, bali pia ukweli kuwa seli zinazotajika kwa ajili ya upandikizaji zinaweza kutoka kwa mgonjwa mwenyewe bila kuhitaji uwepo wa mtoaji (donor).

Akihitimisha, Dr. Kubawara alisema kuwa, matokeo ya utafiti wao yameonesha uwezo mkubwa wa seli za mfumo wa fahamu katika kutibu kisukari bila kuhitaji kufanya mabadiliko ya kinasaba au mtoaji (donor), hali ambayo inaleta matumaini ya kuondokana na tatizo la ukosefu wa watoaji wa seli za upandikizaji siku za mbele.

Kuoza kwa Kasi kwa Meno Mengi kwa Watoto Wadogo (Rampant Caries in Children)

Rampant Caries in Children-kuoza kwa meno watoto

Tafsiri za maneno “rampant caries” ni nyingi katika fani ya meno lakini la msingi ni kuoza kwa meno kunako enea kwa kasi na kuharibu vichwa (crowns) vya meno mengi au yote yaliyoota. Hii ni hali mbaya ya kuoza kwa meno ambayo hushambulia zaidi meno ya utotoni (milk teeth or primary dentition), japo wakati mwingine hata ukubwani.

Ugonjwa huu unajidhihirisha kwa kuanza na kuongezeka kwa kasi na kwa namna unavyo yashambulia meno na vyanzo vyake. Meno hushambuliwa kwa mpigo hasa kuanzia meno ya juu mbele, ingawa meno ya chini mbele ni mara chache kushambuliwa kwa vile yanakingwa na visababisha vya kuoza na ulimi.

Ugonjwa huu hushambulia hata maeneo ya meno ambayo kwa hali ya kawaida si rahisi kuoza, kama sehemu ya kukatia kwa meno ya mbele (incisal edges) na sehemu ya mbele kati na nyuma kati (facial and lingual surfaces).

Nini husababisha meno kuoza kwa kasi utotoni?

Nadharia nyingi zinaonesha kuna uhusiano mkubwa kati ya ugonjwa huu na tabia ya ulaji ya mtoto (feeding habits). Mfano kisababishi kikubwa ni watoto kunywa vinywaji vyenye sukari kwa muda mrefu na mara nyingi kwa kutumia chupa za kunyonyea (nursing bottles) ndiyo maana ugonjwa huu wakati mwingine huitwa nursing bottle caries. Hii hujitokeza hasa kwa watoto wanaochwa na yaya zao, ambao huwapa vinywaji hivyo kila wanapohitaji au wakilia.

Pamoja na kwamba ugonjwa huu hutokana zaidi na chupa za kunyonyea, japo mara chache, lakini pia yawezekana kutokana na mama kumnyonyesha mtoto mara kwa mara au tuseme kila anapo hitaji; vile vile wale akina mama ambao hawataki usumbufu usiku hivyo kutumbukiza nyonyo zao kwenye vinywa vya watoto na wao kujilalia, hapa mtoto hujinyonyea usiku kucha hali hii kitaalamu hujulikana kama at will breast feeding.

Vijino vilivyoathirika huonekana brauni au vyeusi kama mkaa

Watoto walio katika hatari ya kupata ugonjwa huu

  • Watoto wa masikini ambao hawapigi mswaki kwa kizingizio cha kwamba mtoto ni mdogo, kumbuka meno ya utotoni yana madini kidogo
  • Watoto wa wafanyakazi wanashinda maofisini wakati wa kunyonyesha na waacha watoto kutumia chupa za kufyonzea kwa muda mrefu ambao hawapo nao
  • Watoto wagonjwa sugu wanaotumia dawa zenye sukari (syrups) mara kwa mara.
  • Watoto wanaoachwa kunyonyeshwa mapema na hivyo kutumia chupa kama mbadala

Namna ya kumkinga mtoto wako

  • Punguza matumizi ya chupa za kufyonzea
  • Msipende kuwanyonyesha watoto kila wanapotaka hivyo, hasa kunyonyesha inapotumika kama njia ya kupoza mtoto anayelia
  • Jenga tabia ya kuwakagua watoto vinywani mara kwa mara na ukiona tatizo mpeleke hospitali mapema
  • Wasaidieni watoto kupiga mswaki mara baada ya meno kuanza kuota
  • Dhibiti matumizi ya vinywaji na na vitu vya sukari mara kwa mara
  • Msipende kuwapa watoto wadogo fedha kwani matumizi yake ni pipi na ice water au vinavyo fanana na hivyo

Matibabu

  • Kuziba meno yanayoweza kuzibika
  • N’goa yanayouma na hayawezi kuzibika na kutumia vitunza nafasi (space maintainers).
  • Acha yasiyoweza kuzibika lakini hayaumi yatatoka wakati wake ukifika
  • Pakaza madini ya fluorini kwa watoto walio katika hatari kubwa

Kuyafanya Meno Yenye Rangi kuwa Meupe (Teeth Whitening)

Kuyafanya Meno Yenye Rangi kuwa Meupe

Wakati wa muongo uliopita mahitaji ya kuboresha muonekano au kurembesha meno yameongezeka kwa kiwango kikubwa hasa katika nchi zilizoendelea. Hii imechochewa na kupatikana kemikali mpya za meno (dental meterials) na vifaa kwa kasi ikiendana na kuboresha vile vya zamani. Sehemu nyingine iliyosababisha madaktari na mainjinia wa meno kuyafanya meno kuwa meupe ni sehemu ya fani ya taaluma ya meno chini ya urembeshaji wa meno, fani hii uhusika na kuboresha muonekano wa meno hasa yale yanayoonekana wakati wa kutabasamu na kuongea. Inahusisha matibabu kama kuyafanya meno yenye rangi kuwa meupe, kunyoosha meno yaliyojipanga vibaya pamoja na kukarabati meno yaliyovunjika na yale yaliyoumbika visivyo (malformed teeth). Huko Uingereza na sehemu nyingine za magharibi wanawake walio wengi wanatumia maelfu ya paundi/euro kuboresha muonekano wa meno yao hali ambayo inaanza pia kuingia huku kwetu.

Nini husababisha meno kugeuka rangi?
Meno kugeuka rangi husababishwa na kimojwapo au muunganiko wa vitu vifutavyo: -

  1. Vyakula na vinywaji kama vile vinyaji vyenye kaboni, wine na sigara.
  2. Utumiaji wa maji yenye kiwango cha juu cha madini aina ya magadi (fluoride) na utumiaji wa magadi katika kulainisha vyakula wakati wa kuandaa vyakula vigumu kama maharage na makande. Utafiti uliofanywa na Prof. Mabelya na wenzake nchini Tanzania umeonesha kuwa kubadilika kwa rangi ya meno kutokana na magadi kwa kiwango kikubwa husababishwa na matumizi ya magadi katika mapishi ya vyakula hasa makande kule maeneo ya mkoa wa Kilimanjaro/Moshi kuliko inavosababishwa na matumizi ya maji.
  3. Maumbile yasiyo sahihi ya sehemu ngumu za jino (enamel and dentine defects). Iwapo sehemu ngumu ya meno imeumbwa ikiwa laini ni rahisi kufyonza rangi na jino kuota likiwa limegeuka rangi au kubadilika baada ya kuota.
  4. Matumizi ya madawa kwa mama mjamzito ambaye tayari meno ya mtoto aliye tumboni yameanza kuumbwa lakini hayajapata madini ya kutosha na hata watoto wachanga ambao meno yao hayajakomaa.
  5. Kufa kwa kiini cha jino hasa kutoka na kujigonga wakati wa ajali au kupigana ngumi usoni (pulp necrosis), jino likigongwa kwa nguvu damu huvuja ndani ya kiini cha jino na baadaye huchachuliwa na kutoa kemikali ambayo hupenya kwenye vitundu vidogo vidogo kwenye dentine na kujidhihirisha kama kijivu, zambarau au hata nyeusi. Hali hii yaweza tokea mapema baada ya kupata ajali lakini wakati mwingine inaweza kuchukua miaka kadhaa hata arobaini kipindi ambapo mtu hakumbuki kuwa aliwahi kutwangwa ngumi.

Kuyafanya meno yenye rangi yasimpendeza mwenye nayo kuwa meupe
(Bleaching or teeth whitening)

Huku ni kuyafanya meno yen
ye rangi kuwa meupe au kuongeza weupe wa yale yenye rangi ya kawaida kufikia kiwango cha weupe atakacho muhitaji kwa kutumia kemikali maalum. Rangi ya kawaida ya meno kwa walio wengi ni uweupe kama wa maziwa (milky white). Rangi yeyote nje ya hiyo si ya kawaida (abnormal color or discoloration).

Kuwa na rangi isiyo ya kwaida hasa kwa meno ya mbele linaweza kuwa tatizo kubwa la urembo na kumsumbua mhusika kisaikolojia. Kuyafanya meno kuwa meupe kumelenga kuwaondolea wahusika tatizo hili japo mafanikio yake yanategemea kiwango cha rangi isiyo ya kawaida.

Kufanya meno kuwa meupe kwa kutumia kemikali, kunaweza kubadili yaliyo na rangi isiyo ya kawaida kutoka yale yaliyoathirika kwa kiwango kidogo mpaka cha kati.

Kufanya meno yawe meupe kwa kutumia kemikali huunguza (oxidises) rangi ya jino na kuiondoa. Kemikali zinazotumika zina hydrogen peroxide 30%-35% na baadhi carbamide peroxide 10%. Kemikali hizi huweza kuondoa rangi zilizosababishwa na vyakula, vinywaji, dawa za tetracycline, rangi kidogo iliyotokana na utumiaji wa madini ya magadi kwenye vyakula au kwenye maji (mild fluorosis) na meno yenye rangi ya njano au kijivu itokanayo na umri kuwa mkubwa. Inaweza pia kuondoa rangi itokanayo na uvutaji wa sigara na matumizi ya ugoro. Kwa wavutaji wa sigara sharti waache pindi watumiapo kemikali hizi kwani muunganiko wa hydrogen peroxide na kemikali zilizopo kwenye moshi wa sigara unahisiwa kuongeza madhara zaidi ambayo tayari moshi wa sigara husababisha kwenye mwili wa binadamu. Haishauriwi kwa akina mama wanaonyonyesha kutumia dawa hizi pamoja na kwamba hakuna madhara yanayojulikana mpaka sasa


Kupiga meno viraka (Veneeri
ng)


Kupiga meno viraka



Hii hufanyika kwa kuondoa sehemu ndogo ya juu ya jino kwenye enamel kama 0.5-1mm na baadaye kupandika dawa yenye rangi nyeupe kulingana na mgonjwa anavyotaka mwenyewe. Picha inayonesha meno yaliyobadlika rangi kutokana na magadi kabla na baada ya kupigwa viraka


Kabla ya kiraka Baada ya kupigwa kiraka (veneer)

Kumbuka: kuna rangi zaidi ya 26 nyeupe ambazo miongoni mwake mgonjwa anaweza kuchagua anayoitaka

Unyongovu Waweza Kusababisha Magonjwa ya Moyo kwa Vijana

jaribio la kujiua

Katika tafiti mpya zilizofanywa hivi karibuni zinaonyesha kuwa unyongovu na jaribio la kujiua ni viashiria hatari ambavyo huleteleza vijana kufa kwa magonjwa ya moyo.

Katika utafiti mkubwa uliohusisha washiriki zaidi ya 7000 walio chini ya miaka 40 ulionyesha kuwa kwa wale waliokuwa na historia ya unyongovu au jaribio la kujiua walikuwa na hatari kubwa zaidi ya kufa kutokana na magonjwa ya moyo hasa yale ambayo moyo hukosa oksijeni ya kutosha (ischemic heart disease) ukilinganisha na wale ambao hawakuwa na historia hiyo.

Ingawa jinsia zote zilikuwa kwenye hatari zaidi ya kufa kutokana na magonjwa ya moyo, lakini wanawake wenye unyongovu au waliofanya jaribio la kujiua walikuwa na hatari mara 14 zaidi ya kufa kwa magonjwa ya moyo yatokanayo na kukosa oksijeni ya kutosha (ischemic heart disease) kulinganisha na wale ambao hawakuwa na unyongovu au jaribio la kujiua.

Katika utafiti huu uliofanywa na Profesa Viola Vaccarino kutoka chuo kikuu cha Emory, Atlanta, Georgia aligundua jinsi matatizo ya kisaikolojia yanavyopelekea kuongeza hatari ya kufa mapema na magonjwa ya moyo katika idadi ya vijana.

Taarifa nyingi zilizopo za magonjwa ya moyo ambazo zilizokwisha tolewa huwa za umri wa kati na wazee, maana imekuwa ikizoeleka magonjwa haya huathiri zaidi rika hiyo, ambayo ni kweli kabisa hasa katika magonjwa yanao athiri zaidi mishipa ya damu ya moyo (CHD).

Kutokana na watatifi mkazo humewekwa zaidi kwa wazee ingawa magonjwa mengi ya moyo huanza katika kipindi cha ujanani.

Katika utafiti huu taarifa zilichukuliwa kutoka kwa washiriki 7641, wenye umri kati ya 17 hadi 34, kutoka mwaka 1988 hadi 1994.

Katika ratiba ya uchunguzi, tathmini ilikuwa kuhusu unyongovu na jaribio la kujiua , na matokeo baada ya ufuatiliaji yalikuwa kama ifuatavyo: washiriki 51 walikufa kutokana na magonjwa ya moyo, na kati ya hao 28 walikufa kutokana na moyo hukosa oksijeni ya kutosha (ischemic heart disease).

Wagonjwa 538 walikutwa na historia ya unyongovu na 419 kuwa na jaribio la kujiua. Na 136 walikuwa na historia ya vyote viwili.

kubadilishwa athari ya uwiano (HR) kwa ajili ya hatari kwa CVD kifo 2.38 kwa ajili ya wagonjwa walio na unyogovu (95% ya muda kujiamini [CI], 0.93-6.08) na 3.21 kwa ajili ya wale walio na majaribio ya kujiua zamani (95% CI, 1.36-7.56)

Kuna mjadala mkubwa kuhusu madhara ya unyogovu na ugonjwa wa moyo na mishipa katika vifo vya wanawake kama ikilinganishwa na wanaume. Nadhani ushahidi kutoka kwa utafiti huu ni imara lakini masomo ya baadaye ni wazi kuwa ni muhimu.

Mmoja wa watafiti wengine Dr Scherrer alisema “kwa madaktari, anadhani matokeo ya jumla yanazidi kuongeza wasiwasi ni wakati gani hutambua unyongovu, ambapo ni kawaida kwa watu wenye umri mdogo, kuna uwezekano wa haja ya kuweka mkazo mkubwa katika kufuatilia afya yao ya moyo. Na kwamba sio kitu ambacho madaktari wengi hufanya mara kwa mara kwa wagonjwa wenye umri mdogo sana.

Na hii huacha swali kubwa la kujiuliza:

Je inawezekana kuzuia magonjwa ya moyo yahusishwayo na unyongovu, kwa kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa mambo ya hatari yanayoweza kupelekea magonjwa ya moyo kwa kundi la vijana?

Watu wengine wanaweza kuwa na wenza wenye ukimwi bila kuambikizwa kwa muda mrefu au hata wasiambukizwe kabisa

Neno ukimwi ni kifupisho cha maneno “Upungufu wa Kinga Mwilini”. Ugonjwa huu usabishwa na virusi ambavyo hushambulia chembe chembe za kinga na kuufanya mwili ushindwe kujilinda dhidi ya maradhi ipasavyo au hata kushindwa kupambana na maradhi yaliyoingia tayari.

Ukimwi huambukizwa kwa njia mbali mbali kama;

  1. kuingia damu ya mtu mwenye ukimwi kwa hasiye nao-hapo ndo kuna vitu kama kuchangia nyembe, sindano, kuwekewa damu isiyo salama n.k.
  2. Kujamiiana- wadudu wa ukimwi wameonekana kuwemo kwenye majimaji ya sehemu za sili, hivyo kama kuna michubuko mtu akafanya tendo hili na mhadhilika kuna nafasi ya kuambukizwa.
  3. Mama mjamzito kumuambukiza kiumbe kilichopo kwenye mfuko wakewa uzazi.

Japo si jukumu la makala hii lakini kinga ni pamoja na kuzuia kuchangia vifaa vyenye ncha kali, kutumia kinga unapofanya tendo la ndoa, kuacha kufanya tendo la ndoa kama unaweza na mengine.

Kwa vile kuna uwezekano wa kupata ukimwi kwa kutenda tendo la ndoa, wanandoa ambao kimsingi wengi wao kama si wote, hawatumii kinga wanapofanya tendo hili. Katika hali hii, kama kuna uwezekano mmoja ni muathirika, basi nafasi ya kumuambukiza mwenzake huongezeka.

Taarifa ya kwanza (case report 1)

Mwaka tisini na na sita, rafiki yangu mmoja, mtoto wake wa miezi mitatu alilazwa Muhimbili. Baada ya kuona maendeleo ya tiba si mazuri waliamua kumpima, majibu yakaonesha ana virusi vya ukimwi. Majibu haya yalimfanya daktari aliyekuwa anamtibu mtoto kuwashauri wazazi nao wapime na wakakubali. Walipopima mama alikuwa muathirika baba hapana, na watu hawa walikuwa kwenye ndoa kwa muda wa miaka miwili, wakila tunda lao bila kinga.

Baada ya taarifa kufika kwa ndugu wa mwanaume wakashauri waachane wagawane walichochuma pamoja. Wakati wamepelekana mahakamani, mwanamke akakana kwamba hawakuwahi kupima. Mahakama ikaamuru wapime, wakapima tena kwa hospitali chaguo la mwanamke. Majibu yakawa yale yale mama anao baba hana. Wakakubali kuachana na kugawana walivyochuma pamoja kama walivyoorodhesha mahakamani na baba kupangiwa kiwango cha kumlipa mama kwa malezi ya mtoto. Baada ya mwaka na nusu mtoto akapimwa tena na kugundulika hana ukimwi tofauti na alipokuwa amepimwa mwanzoni. Mpaka hapa ninapoandika wote wapo na afya njema, baba alioa mwanamke mwingine na wana watoto wawili na mama bado yupo anaendelea kutumia dawa za ARVs.

Uchunguzi usio rasmi ulionesha kuwa mama alikuwa na ugonjwa huo kabla hata ya ndoa hiyo.

Taarifa ya pili

Jamaa yangu mmoja naye alikuwa ameoa na kujaliwa kupata watoto wanne katika ndoa yake ya miaka 15. Baadaye mwaka 2008 mke wake akaanza kuugua magonjwa ya ajabu ajabu, yanapona yanarudi na mapya yanajitokeza. Analazwa hospitali anarudi tena baada ya muda, akaamua kwenda kwa mganga Mpemba ambaye alimwambia mumewe ana mke mwingine kamtupia jini la damu. Akampa dawa hazikusaidia. Kutokana na lawama za mahawara kuingia na bado hospitali na kwa waganga haponi, ikashauriwa wapime HIV. Wakakubali. Walipopimwa iligundulika kuwa mama anao na baba hana. Mama akazidi kuamini kuwa hata kama ameonekana ana Ukimwi basi atakuwa ametumiwa na huyo hawara wa mumewe. Ikawa kazi kumeza dawa, anameza na kuacha anakwenda kwa waganga wake, mara ya mwisho akaamua kuokoka sasa japo hapo kichwa nacho kilishaanza kuvurugika. Huko ndo kabisa akaambiwa aache dawa kabisa YESU atamponya. Mwanzoni mwa mwaka huu tumemzika.

Ninazo taarifa za namna hii nne lakini mbili zinatosha kutoa mjadala.

Mjadala

Katika taarifa zote mbili inaonyesha wahusika wote walishakaa pamoja wakila matunda yao bila kinga ndo maana wakapata watoto. Kwanini hawakuambukizana inawezekana walikuwa wanakula tunda lao bila michubuko yeyote katika kipindi chote walichokuwa pamoja. Sababu nyingine yawezekana wanaume hao wana kinga dhidi ya virusi vya ukimwi au chembe chembe zao za kinga hazina vipokezi (receptors) vya wadudu wa ukimwi. Tafiti zimeonyesha virusi wa ukimwi huweza kuingia kwenye chembe chembe za kinga kupitia vipokezi katika hali ya kama ufunguo na kitasa au au nati na boriti. Kama mtu hana vipokezi hivi hawezi kuambukizwa.

Dr Matthew Dolan, daktari bingwa katika jeshi la anga la marekani anasema, anasema "Genetic resistance to AIDS works in different ways and appears in different ethnic groups. The most powerful form of resistance, caused by a genetic defect, is limited to people with European or Central Asian heritage. An estimated 1 percent of people descended from Northern Europeans are virtually immune to AIDS infection, with Swedes the most likely to be protected. One theory suggests that the mutation developed in Scandinavia and moved southward with Viking raiders.

All those with the highest level of HIV immunity share a pair of mutated genes -- one in each chromosome -- that prevent their immune cells from developing a "receptor" that lets the AIDS virus break in. If the so-called CCR5 receptor -- which scientists say is akin to a lock -- isn't there, the virus can't break into the cell and take it over. (haya yamenizengua kuyatafsiri)

Mtoto kuonekana ana ukimwi akiwa na miezi miatu na baada ya mwaka mmoja na nusu hana hii ni kutokana na ukweli kwamba mtoto anayezaliwa na mama mwenye virusi vya ukimwi huwa na antibodies dhidi ya virusi vya ukimwi kutoka kwa mama yake. Unapopima ukimwi kutumia kipimo cha eliza ambacho uangalia antibodies hizi, basi mtoto huonekana hanao, lakini kama mtoto hakuambukizwa wadudu basi, antibodies hizi huondoka kwenye damu yake kadri muda unavyo kwenda.

Hitimisho

Kuna baadhi ya watu si rahisi kuwaambukiza ukimwi

Mapendekezo

Kutokupa ukimwi kwa muda mrefu huku ukila tunda na mwenye nao kwa muda mrefu haikuhakikishii kuwa huwezi kuupata kwa hakikisha unafuata masharti ya kinga

Mtoto anayezaliwa na mama au wazazi wenye ukimwi si lazima awe nao fuata ushauri wa daktari na hasa kupima wakati wa ujauzito

Tuangalie namna ya kuwadhibiti waganga wa jadi na watumishi wa mungu wanaoshauri watu wasitumie dawa za kuongeza maisha

Hofu iliyopitiliza (Generalized Anxiety Disorder, GAD)

Hofu iliyopitiliza

Utangulizi
Mada hii ina lengo la kuzungumzia tatizo la kuwa na hofu au wasiwasi uliopita kiasi au kwa kitaalamu Generalized anxiety disorder (GAD).
Kwa ajili ya kutofautisha kati ya hofu iliyopitiliza na hofu ya kawaida ambayo yaweza kumkumba mwanadamu yeyote, wakati fulani fulani mwandishi atatumia maneno anxiety au GAD katika kuwasilisha ujumbe wake.

Hofu iliyopitiliza au au anxiety au GAD huambatana na hali ya kuwa na wasiwasi kupita kiasi juu ya maisha ya kila siku pamoja na matukio yake bila hata muhusika kuwa na sababu maalum ya kuwa na hofu hiyo. Kwa maneno mengine ni kuwa, watu wenye anxiety hujihisi hofu kubwa bila ya kuwa na sababu yeyote ya msingi ya kuwafanya wawe hivyo. Mara nyingi watu wenye tatizo hili huwa na tabia ya kuhisi kwamba janga kubwa litawatokea karibuni au maafa yatamkumba katika maisha yake na daima hawaachi kuwa na hofu isiyo na sababu juu ya familia zao, pesa, afya, ajira, masomo au hata biashara zao.

Maisha yao ya kila siku huwa na mchanganyiko wa hofu, wasiwasi na huzuni, kiasi kwamba hatimaye hofu hutawala mawazo ya muhusika kiasi cha kuingilia utendaji wake wa kila siku ikiwemo kazi, masomo, shughuli zake za kijamii, na hata mahusiano na mwenza wake wa ndoa.

Dalili za hofu iliyopitiliza (anxiety) ni nini?
Kama tulivyoona hapo juu kwenye utangulizi, hofu isiyo na kikomo huathiri zaidi uwezo wa mtu katika kufikiri, ingawa baadaye humletea matatizo ya kiafya katika mwili. Hali hii inaweza kuambatana na dalili mbalimbali, siyo tu zile zinazohusu uwezo wa kufikiri na akili bali hata zinazohusiana na utendaji kazi wa mwili.

Baadhi ya dalili hizo ni:
• Kuwa na hisia ya kuwepo kwa janga, kwamba kitu kibaya kitatokea muda wowote, na kwamba hatari kubwa inamnyemelea
• Hali ya hofu kuu
• Hali ya kujihisi kutaka kukimbia, kuondoka mbali na hatari hiyo
• Rangi ya ngozi kuwa ‘nyeupe’ kama mtu aliyeishiwa damu
• Kujihisi ngozi kuwaka moto
• Hali ya koo kubana, kujihisi kama koo limefunga, au umekabwa na kitu kooni
• Hali ya kuchanganyikiwa
• Kujihisi kutengwa na ulimwengu, kupoteza hisia, kupoteza kujitambua nafsi yako mwenyewe
• Kujihisi kama mtu anayeota
• Kizunguzungu, kuhisi kichwa kuwa chepesi, kupepesuka unapotembea
• Kuwa na mvurugano wa hisia
• Hofu ya kurukwa akili
• Hofu ya kupoteza uwezo wa kujithibiti mwenyewe
• Kujihisi kama vile kuna kitu kinachobana kichwani (kama uliyezungushiwa kamba au rubber-band)
• Kujihisi baridi sana au joto sana (ingawa hali ya hewa yaweza kuwa kinyume)
• Kushindwa kujituliza
• Kujihisi kitu kinabana tumboni
• kichefuchefu
• kujihisi ganzi au hali ya kuchomachoma sehemu fulani fulani za mwili
• kuwa na hisia za kupanic
• kuhisi kuziba masikio
• moyo kudunda sana
• Moyo kwenda kasi isivyo kawaida
• Maumivu makali kifuani, shingoni, kwenye bega, kichwani au usoni
• Hali ya kuhisi kukosa hewa au kupumua kwa shida
• Kutokwa na jasho
• Kubanwa na kifua
• Kutetemeka (kunaweza kuonekana waziwazi au kutetemeka kwa ndani bila mtu mwingine kutambua)
• Kuchafuka kwa tumbo
• Kujihisi haja ndogo au kubwa mara kwa mara
• Kutapika
• Uchovu wa mara kwa mara
• Shida ya kupata usingizi au kulala usingizi wa mang’amung’amu

Hofu iliyopitiliza (GAD) husababishwa na nini?
Chanzo halisi cha matatizo ya kuwa na hofu kupita kiasi hakifahamiki. Hata hivyo kuna baadhi ya vitu ambavyo vimegundulika kuwa vinachangia sana kuwepo kwa tatizo hili miongoni mwa watu.

Vitu/mambo hayo ni pamoja na:
• Nasaba (genetics): baadhi ya tafiti zimeonesha kuwa nasaba ina nafasi kubwa ya kumfanya mtu wa familia yenye matatizo ya hofu iliyopitiliza naye kuwa na uwezekano mkubwa wa kupata haya. Hii inaamnisha kwamba, hofu iliyopitiliza inaweza kurithiwa miongoni mwa wanafamilia.
• Mfumo wa kemikali za ubongo: Kuwepo kwa hofu iliyopitiliza kumehusishwa na kuwepo kwa kiwango kisicho sahihi cha baadhi ya kemikali zinazosaidia kusafirisha taarifa katika ubongo yaani neurotransmitters. Kazi ya kemikali hizi ni kupitisha taarifa na ujumbe mbalimbali kutoka seli moja ya neva mpaka seli nyingine. Iwapo kemikali hizi zitakuwa katika kiwango kisicho sahihi (ama kupungua au kuongezeka) taarifa hazitaweza kusafirishwa kati ya seli za neva na hatimaye hazitaweza kuufikia ubongo inavyotakiwa. Hali hii inaweza kusababisha mabadiliko katika utendaji kazi wa ubongo na hatimaye kusababisha mtu kupatwa na hofu iliyopitiliza.
• Sababu za kimazingira: matukio kama vile ajali, kuumia au matukio yenye msongo mkubwa kama vile kunyanyaswa kwa namna yeyote ile, kufiwa na mtu unayempenda, talaka, kubadilisha kazi au kuachishwa/kufukuzwa kazi, kubadilisha shule au kufukuzwa/kuacha shule nayo pia yanaweza kusababisha kuwa na hali ya hofu iliyopitiliza. Hofu (GAD) pia huwa mbaya zaidi kipindi ambapo muhusika huwa katika hali ya msongo mkubwa wa kimaisha (stress). Aidha matumizi ya vitu vyenye kulevya kama pombe (alcohol), sigara (nicotine) au hata kahawa nayo pia yanaweza kuongeza ukubwa wa tatizo hili. Kadhalika, watu waliokuwa watumiaji wakubwa wa vitu hivyo kisha wakaacha ghafla, nao wapo katika hatari kubwa ya kukumbwa na tatizo hili.

Ukubwa wa tatizo
Bahati mbaya, takwimu za ukubwa wa tatizo nchini Tanzania hazikuweza kupatikana. Hata hivyo, inakadiriwa kuwa takribani watu wazima milioni 4 mpaka 5 huko nchini Marekani hukumbwa na tatizo hili kila mwaka.

Kwa kawaida, wanawake huathiriwa zaidi kuliko wanaume. Aidha hofu iliyopitiliza mara nyingi huanza kipindi cha utoto au utoto kabla ya ujana ingawa pia inaweza kutokea wakati wa utu uzima.

Vipimo na uchunguzi
Iwapo mgonjwa ana dalili za hofu iliyopitiliza, kwanza daktari atataka kufahamu historia yake kwa kumuuliza maswali juu ya maisha yake na dalili zinazomsumbua kabla ya kumfanyia uchunguzi wa mwili mzima ili kufahamu kama hana tatizo jingine la mwili linaweza kumletea dalili kama hizo.

Kuweza kutambua kama mgonjwa ana tatizo hili, daktari atatilia mkazo kwenye ukubwa wa tatizo lenyewe, muda tangu dalili zilipoanza kujitokeza, na iwapo tatizo hili linamfanya mgonjwa kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kila siku.

Iwapo daktari ataweza kubainisha katika historia ya mgonjwa kuwa mgonjwa amekuwa akisumbuliwa na dalili hizi karibu kila siku (au muda mwingi) katika kipindi cha miezi sita, hapo tunaweza kusema kwa hakika kuwa ni kweli mgonjwa ana tatizo la hofu iliyopitiliza (GAD). Dalili hizi pia ni lazima ziingilie na kuathiri mfumo wake wa maisha ya kila siku.

Pamoja na kuwa hakuna kipimo cha kuweza kugundua ugonjwa huu, daktari pia anaweza kuagiza kufanyika kwa vipimo vingine ili kuchunguza iwapo mgonjwa ana tatizo jingine lolote la kiafya.

Matibabu
Iwapo uchunguzi utaonesha mgonjwa hana tatizo lolote la kiafya katika mwili, daktari atampeleka kwa wataalamu wa masuala ya afya ya akili kwa ajili ya matibabu zaidi. Matibabu ya tatizo hili kwa kawaida hujumuisha matumizi ya dawa pamoja na tiba isiyohitaji dawa (au tiba ya kujitambua yaani cognitive-behavioral therapy).
• Matumizi ya dawa: kwa watu ambao tatizo hili linaingiliana na maisha yao ya kila siku, matumizi ya dawa yameonekana kusaidia sana kuwafanya warejee katika hali yao ya kawaida. Dawa hizo ambazo pia huitwa tranquilizers husaidia kumtuliza mgonjwa na kumfanya ajihisi kupumzika. Dawa zinazotumika zipo katika jamii ya benzodiazepines nazo hufanya kazi ya kupunguza dalili za GAD kama vile kukaza misuli ya mwili au hali ya mgonjwa kutotulia. Baadhi ya dawa zilizo kwenye jamii hii ni kama vile diazepam (valium) na Ativan. Jamii nyingine ya dawa ni zile za kuondoa msongo wa mawazo (depression) yaani Antidepressants, kama vile Prozac, na Zoloft. Hizi nazo hutumika katika matibabu ya muda mrefu ya watu wenye hofu iliyopitiliza.
• Tiba ya kujitambua (cognitive-behavioral therapy): watu wenye matatizo ya hofu iliyopitiliza wanaweza pia kupatiwa tiba hii ambapo mgonjwa hufundishwa jinsi ya kutambua na kubadili namna anavyofikiri na tabia zinazomfanya awe na hisia za hofu. Aina hii ya tiba husaidia kuzuia kuibuka kwa mawazo ya hofu kwa vile humfanya mgonjwa kuyachunguza na kuziangalia hofu zake katika hali ya uhalisia.

Aidha mbinu mbalimbali za kuutuliza mwili (relaxation) kama vile kuvuta pumzi nyingi ndani kisha kuiachia taratibu nazo pia husaidia kuondoa kukaza kwa misuli kunakoambatana na kuwepo kwa hofu iliyopitiliza.

Pamoja na kwamba baadhi ya watu wenye tatizo hili hawawezi kutibiwa na kupona moja kwa moja kwa kuwa bado huendelea kupatwa na dalili hizi kwa kitambo fulani fulani, wengi wao hupata nafuu ya uhakika iwapo watapata tiba sahihi na wakatilia mkazo unaotakiwa kwenye tiba hiyo.

Kinga
Je kuna kinga dhidi ya tatizo hili?

Hofu iliyopitiliza haina kinga. Hata hivyo kuna baadhi ya mambo ambayo husaidia sana kupunguza makali ya dalili za tatizo hili. Mambo hiyo ni pamoja na:
• Kuacha au kupunguza matumizi ya vyakula au vinywaji kama vile kahawa, chai, cola au chokoleti.
• Kuepuka kutumia dawa zozote zenye vitu vinavyoweza kuchochea kutokea kwa hali bila kupata ushauri wa kitaalamu.
• Kujitahidi kufanya mazoezi ya mwili kila siku
• Kutafuta msaada wa ushauri nasaha pindi unapopatwa na matatizo yenye kuumiza moyo/nafsi, na
• Kujifunza kuthibiti msongo wa mawazo kwa kufanya mazoezi mbalimbali kama vile yoga