Showing posts with label meno. Show all posts
Showing posts with label meno. Show all posts

Sunday, March 18, 2012

Kuoza kwa meno (Dental Caries) ni ugonjwa wa kuambukiza

kuoza meno
Miaka ya nyuma iliaminika kuwa ugonjwa wa kuoza kwa meno si wa kuambukiza; lakini tafiti nyingi zilizofanyika zimedhihirisha ni ugonjwa wa kuambukiza. Jino lililooza linaweza kuambukiza meno yaliyogusana nalo na pia mgonjwa aliyeoza meno au mwenye wadudu wanaosababisha kuoza kwa meno anaweza kuambukiza mwenzake/wenzake.

Wadudu wanaosababisha kuoza kwa meno ni sehemu ya wadudu wakazi kinywani (oral flora). Wadudu hawa hujishikiza kwenye meno na kufanya utando, wana uwezo wa kuchachua vyakula hasa vyenye asili ya sukari na kutoa tindikali. Ni tindikali hii ambayo huvuta madini kwenye meno na kuweka matobo. Utando huu wa wadudu kwenye jino moja unaweza kuwa na wadudu nusu bilioni, miongoni mwao wakiwemo jamii ya mutans streptococci ambao kimsingi ndiyo wasababishaji wakuu wa kuoza kwa meno. Wadudu wengine ni kama Lactobacillus na Actinomyces.

Jinsi wanavyoambukiza

Ndani ya jamii ya wadudu hawa ziko jamii zingine ndogondogo ambazo zinatofautiana kwa uwezo wa kuchachua vyakula na kutoa tindikali na hata uwezo wa kujishikiza kwenye meno. Kwa mtu mwenye wadudu wasio wakali anaweza kuambukizwa na mwenzake mwenye wadudu wakali na hivyo kuingia kwenye hatari zaidi ya kuoza meno. Tafiti zimeonesha wapenzi/wanandoa wanaweza kuambukizana kwa njia ya kubusiana. Watoto wanaochangia ice cream/ice water mashuleni pia wanaambukizana kwa njia hii. Tafiti pia zimeonesha wazazi wanaotafunia vyakula watoto wao kama sehemu ya kuvilainisha wanaweza kuwambukiza pia watoto wao.

Njia nyingine ni jino lililooza kuambukiza mengine yanayogusana nayo, tindikali inayozalishwa na wadudu katika jino lililooza inaweza kuathiri jino lililo jirani. Ndiyo maana inashauriwa ukiona jino limeanza kuoza muone mtaalamu akalitibu au akaling’oe kama halitibiki ili lisiambukize mengine.

Namna ya kujikinga

  • Njia muhimu ni kutembelea cliniki za meno angalau kila baada ya miezi sita
  • Kuzuia watoto kuchangia vyakula mudomoni
  • Kupima kuangalia kiwango na aina za bakiteria zilizi kwenye mate yake na kupata dawa ikibidi.
  • Kuhusu kubusiana sina la kusema

Kuoza kwa Kasi kwa Meno Mengi kwa Watoto Wadogo (Rampant Caries in Children)

Rampant Caries in Children-kuoza kwa meno watoto

Tafsiri za maneno “rampant caries” ni nyingi katika fani ya meno lakini la msingi ni kuoza kwa meno kunako enea kwa kasi na kuharibu vichwa (crowns) vya meno mengi au yote yaliyoota. Hii ni hali mbaya ya kuoza kwa meno ambayo hushambulia zaidi meno ya utotoni (milk teeth or primary dentition), japo wakati mwingine hata ukubwani.

Ugonjwa huu unajidhihirisha kwa kuanza na kuongezeka kwa kasi na kwa namna unavyo yashambulia meno na vyanzo vyake. Meno hushambuliwa kwa mpigo hasa kuanzia meno ya juu mbele, ingawa meno ya chini mbele ni mara chache kushambuliwa kwa vile yanakingwa na visababisha vya kuoza na ulimi.

Ugonjwa huu hushambulia hata maeneo ya meno ambayo kwa hali ya kawaida si rahisi kuoza, kama sehemu ya kukatia kwa meno ya mbele (incisal edges) na sehemu ya mbele kati na nyuma kati (facial and lingual surfaces).

Nini husababisha meno kuoza kwa kasi utotoni?

Nadharia nyingi zinaonesha kuna uhusiano mkubwa kati ya ugonjwa huu na tabia ya ulaji ya mtoto (feeding habits). Mfano kisababishi kikubwa ni watoto kunywa vinywaji vyenye sukari kwa muda mrefu na mara nyingi kwa kutumia chupa za kunyonyea (nursing bottles) ndiyo maana ugonjwa huu wakati mwingine huitwa nursing bottle caries. Hii hujitokeza hasa kwa watoto wanaochwa na yaya zao, ambao huwapa vinywaji hivyo kila wanapohitaji au wakilia.

Pamoja na kwamba ugonjwa huu hutokana zaidi na chupa za kunyonyea, japo mara chache, lakini pia yawezekana kutokana na mama kumnyonyesha mtoto mara kwa mara au tuseme kila anapo hitaji; vile vile wale akina mama ambao hawataki usumbufu usiku hivyo kutumbukiza nyonyo zao kwenye vinywa vya watoto na wao kujilalia, hapa mtoto hujinyonyea usiku kucha hali hii kitaalamu hujulikana kama at will breast feeding.

Vijino vilivyoathirika huonekana brauni au vyeusi kama mkaa

Watoto walio katika hatari ya kupata ugonjwa huu

  • Watoto wa masikini ambao hawapigi mswaki kwa kizingizio cha kwamba mtoto ni mdogo, kumbuka meno ya utotoni yana madini kidogo
  • Watoto wa wafanyakazi wanashinda maofisini wakati wa kunyonyesha na waacha watoto kutumia chupa za kufyonzea kwa muda mrefu ambao hawapo nao
  • Watoto wagonjwa sugu wanaotumia dawa zenye sukari (syrups) mara kwa mara.
  • Watoto wanaoachwa kunyonyeshwa mapema na hivyo kutumia chupa kama mbadala

Namna ya kumkinga mtoto wako

  • Punguza matumizi ya chupa za kufyonzea
  • Msipende kuwanyonyesha watoto kila wanapotaka hivyo, hasa kunyonyesha inapotumika kama njia ya kupoza mtoto anayelia
  • Jenga tabia ya kuwakagua watoto vinywani mara kwa mara na ukiona tatizo mpeleke hospitali mapema
  • Wasaidieni watoto kupiga mswaki mara baada ya meno kuanza kuota
  • Dhibiti matumizi ya vinywaji na na vitu vya sukari mara kwa mara
  • Msipende kuwapa watoto wadogo fedha kwani matumizi yake ni pipi na ice water au vinavyo fanana na hivyo

Matibabu

  • Kuziba meno yanayoweza kuzibika
  • N’goa yanayouma na hayawezi kuzibika na kutumia vitunza nafasi (space maintainers).
  • Acha yasiyoweza kuzibika lakini hayaumi yatatoka wakati wake ukifika
  • Pakaza madini ya fluorini kwa watoto walio katika hatari kubwa

Kuyafanya Meno Yenye Rangi kuwa Meupe (Teeth Whitening)

Kuyafanya Meno Yenye Rangi kuwa Meupe

Wakati wa muongo uliopita mahitaji ya kuboresha muonekano au kurembesha meno yameongezeka kwa kiwango kikubwa hasa katika nchi zilizoendelea. Hii imechochewa na kupatikana kemikali mpya za meno (dental meterials) na vifaa kwa kasi ikiendana na kuboresha vile vya zamani. Sehemu nyingine iliyosababisha madaktari na mainjinia wa meno kuyafanya meno kuwa meupe ni sehemu ya fani ya taaluma ya meno chini ya urembeshaji wa meno, fani hii uhusika na kuboresha muonekano wa meno hasa yale yanayoonekana wakati wa kutabasamu na kuongea. Inahusisha matibabu kama kuyafanya meno yenye rangi kuwa meupe, kunyoosha meno yaliyojipanga vibaya pamoja na kukarabati meno yaliyovunjika na yale yaliyoumbika visivyo (malformed teeth). Huko Uingereza na sehemu nyingine za magharibi wanawake walio wengi wanatumia maelfu ya paundi/euro kuboresha muonekano wa meno yao hali ambayo inaanza pia kuingia huku kwetu.

Nini husababisha meno kugeuka rangi?
Meno kugeuka rangi husababishwa na kimojwapo au muunganiko wa vitu vifutavyo: -

  1. Vyakula na vinywaji kama vile vinyaji vyenye kaboni, wine na sigara.
  2. Utumiaji wa maji yenye kiwango cha juu cha madini aina ya magadi (fluoride) na utumiaji wa magadi katika kulainisha vyakula wakati wa kuandaa vyakula vigumu kama maharage na makande. Utafiti uliofanywa na Prof. Mabelya na wenzake nchini Tanzania umeonesha kuwa kubadilika kwa rangi ya meno kutokana na magadi kwa kiwango kikubwa husababishwa na matumizi ya magadi katika mapishi ya vyakula hasa makande kule maeneo ya mkoa wa Kilimanjaro/Moshi kuliko inavosababishwa na matumizi ya maji.
  3. Maumbile yasiyo sahihi ya sehemu ngumu za jino (enamel and dentine defects). Iwapo sehemu ngumu ya meno imeumbwa ikiwa laini ni rahisi kufyonza rangi na jino kuota likiwa limegeuka rangi au kubadilika baada ya kuota.
  4. Matumizi ya madawa kwa mama mjamzito ambaye tayari meno ya mtoto aliye tumboni yameanza kuumbwa lakini hayajapata madini ya kutosha na hata watoto wachanga ambao meno yao hayajakomaa.
  5. Kufa kwa kiini cha jino hasa kutoka na kujigonga wakati wa ajali au kupigana ngumi usoni (pulp necrosis), jino likigongwa kwa nguvu damu huvuja ndani ya kiini cha jino na baadaye huchachuliwa na kutoa kemikali ambayo hupenya kwenye vitundu vidogo vidogo kwenye dentine na kujidhihirisha kama kijivu, zambarau au hata nyeusi. Hali hii yaweza tokea mapema baada ya kupata ajali lakini wakati mwingine inaweza kuchukua miaka kadhaa hata arobaini kipindi ambapo mtu hakumbuki kuwa aliwahi kutwangwa ngumi.

Kuyafanya meno yenye rangi yasimpendeza mwenye nayo kuwa meupe
(Bleaching or teeth whitening)

Huku ni kuyafanya meno yen
ye rangi kuwa meupe au kuongeza weupe wa yale yenye rangi ya kawaida kufikia kiwango cha weupe atakacho muhitaji kwa kutumia kemikali maalum. Rangi ya kawaida ya meno kwa walio wengi ni uweupe kama wa maziwa (milky white). Rangi yeyote nje ya hiyo si ya kawaida (abnormal color or discoloration).

Kuwa na rangi isiyo ya kwaida hasa kwa meno ya mbele linaweza kuwa tatizo kubwa la urembo na kumsumbua mhusika kisaikolojia. Kuyafanya meno kuwa meupe kumelenga kuwaondolea wahusika tatizo hili japo mafanikio yake yanategemea kiwango cha rangi isiyo ya kawaida.

Kufanya meno kuwa meupe kwa kutumia kemikali, kunaweza kubadili yaliyo na rangi isiyo ya kawaida kutoka yale yaliyoathirika kwa kiwango kidogo mpaka cha kati.

Kufanya meno yawe meupe kwa kutumia kemikali huunguza (oxidises) rangi ya jino na kuiondoa. Kemikali zinazotumika zina hydrogen peroxide 30%-35% na baadhi carbamide peroxide 10%. Kemikali hizi huweza kuondoa rangi zilizosababishwa na vyakula, vinywaji, dawa za tetracycline, rangi kidogo iliyotokana na utumiaji wa madini ya magadi kwenye vyakula au kwenye maji (mild fluorosis) na meno yenye rangi ya njano au kijivu itokanayo na umri kuwa mkubwa. Inaweza pia kuondoa rangi itokanayo na uvutaji wa sigara na matumizi ya ugoro. Kwa wavutaji wa sigara sharti waache pindi watumiapo kemikali hizi kwani muunganiko wa hydrogen peroxide na kemikali zilizopo kwenye moshi wa sigara unahisiwa kuongeza madhara zaidi ambayo tayari moshi wa sigara husababisha kwenye mwili wa binadamu. Haishauriwi kwa akina mama wanaonyonyesha kutumia dawa hizi pamoja na kwamba hakuna madhara yanayojulikana mpaka sasa


Kupiga meno viraka (Veneeri
ng)


Kupiga meno viraka



Hii hufanyika kwa kuondoa sehemu ndogo ya juu ya jino kwenye enamel kama 0.5-1mm na baadaye kupandika dawa yenye rangi nyeupe kulingana na mgonjwa anavyotaka mwenyewe. Picha inayonesha meno yaliyobadlika rangi kutokana na magadi kabla na baada ya kupigwa viraka


Kabla ya kiraka Baada ya kupigwa kiraka (veneer)

Kumbuka: kuna rangi zaidi ya 26 nyeupe ambazo miongoni mwake mgonjwa anaweza kuchagua anayoitaka

Matibabu ya Mzizi wa Jino (Root Canal Treatment)

matibabu ya mzizi wa jino
Haya ni matibabu ambayo hutolewa kwa jino ambalo sehemu ya uhai wake imeharibika kiasi kwamba haliwezi kutibika kwa kuziba tu, kwa maneno mengine hii ndiyo njia mbadala ya kutibu jino bila kung’oa.

Matibabu uhusisha kutoboa jino hadi sehemu ya uhai wa jino yenye mishipa ya damu na ile ya fahamu na chembechembe za meno na kuviondoa nikimaanisha kuondoa mishipa ya fahamu, ya damu na chembe pamoja na ugonjwa na baadae kuijaza sehemu hii na vitu maalumu vinavyokubaliana na mwili (biocompatible).

Aina za matibabu ya mzizi wa jino
Kuna aina kuu mbili za matibabu ya mzizi wa jino

1. Njia ya kawaida (conventional root canal treatment)
Njia hii ni kama nilivyoeleza hapo juu, kuingia kwenye kiini cha jino na kuondoa kila kitu kilichomo na kisha kujaza uwazi uliobaki na vitu maalumu vinavyokubaliana na mwili

2. Matibabu ya mzizi wa jino yanayohusisha upasuaji
kwa njia hii mbali na kutumia njia ya kwanza, upasuaji hufanyika pia ili kondoa mfupa uliofunika ncha ya mzizi wa jino kusafisha eneo lililozunguka ncha ya mzizi na baadaye kukata ncha husika kisha kuziba kutokea kwa nyuma (retro grade filling). Njia hii hutumika pale njia ya kawaida inaposhindwa kuondoa tatizo au inapoonekana kabisa kuwa haitaweza kuondoa tatizo. Huu ni upasuaji mdogo, unaofanyika kwa ganzi ndogo ya eneo husika (local anaesthesia).
Mafanikio ya matibabu haya ni makubwa sana.

Ni meno yapi yanahitaji matibabu hayo?
• Meno yaliyooza hadi uoza kufikia kiini cha jino (dental pulp) - sehemu ya uhai wa jino.
• Meno yaliyopata ajali na kupasuka na kuacha kiini cha jino kikiwa wazi (traumatic pulp exposure)
• Meno yaliyopata ajali na kusababisha mishipa ya damu kukatika au kupasuka na kuvunjika ndani ya jino, kitu ambacho hupelekea jino kufa (pulp necrosis) na baadaye kusabisha jipu au kubadilika rangi
• Wakati mwingine japo ni mara chache, ni pale tunapokuwa tunataka kuliweka sawa jino/meno ambalo/ambayo hayapo kwenye mstari sawa ili yaendane na meno mengine.
• Pia wakati mwingine, tunapo lisaga jino ili liweze kubeba meno bandia ya daraja (bridge) huku tukiwa na mashaka na uhai wake.

Nini dalili zinazoashiria jino kuhitaji matibabu haya?
• Jino linalouma - kuuma kwa jino kunashiria ugonjwa kuwa umeingia ndani ya kiini cha jino na au hata kupitiliza na kuingia kwenye mfupa ulioshikilia jino
• Jino lililooza na kusababisha uvimbe, liwe linauma au haliumi
• Jino lililokatika na kupoteza zaidi ya nusu ya kichwa cha jino (crown) kukatika kuwe kwa ajali au kuoza au vyote kwa pamoja
• Jino linalobadilika rangi huku kukiwa na historia ya kuligonga mahali au kuchapwa ngumi usoni, hapa jino linaweza kuanza kubadilika rangi miezi sita tangu siku ya ajali mpaka wakati mwingine hadi miaka ishirini wakati mgonjwa alishasahau hata ajali yenyewe.

Meno yasiyofaa kwa matibabu haya
• Meno yaliyoharibika vibaya kiasi kwamba hayatibiki tena japo ni machache, kwani hata kama jino limebaki mzizi tu, ukiwa bado imara twaweza fanya matibabu haya na baadae kujenga kichwa (crown)
• Meno yaliyolegea sana kutokana na magonjwa ya fizi ambayo hayawezi kuimarishwa tena.
• Magego ya mwisho (wisdom teeth) kwa kawaida meno haya huwa yana maumbile yasiyotabirika kiasi kwamba hata mafanikio ya matibabu huwa hayatabiriki, hii ikiambatana na kuwa yako nyuma sana kiasi cha kuwa vigumu kuyafikia kwa ufasaha na vifaa vyetu na pia yana mchango kidogo kwa usagaji chakula (2%)
• Meno ambayo mifereji ya mizizi ambayo hupitisha mishipa ya fahamu na damu imeziba (calcified root canals)

Mafanikio ya matibabu haya
Kiwango cha mafanikio ya matibabu haya ni kati ya asilimia sabini na saba hadi tisini na nane (77-98%). Haya ni mafanikio ya hali ya juu kwa matibabu ya aina yeyote ile, mafanikio huongezeka zaidi pale tabibu anapotumia vifaa vya kumuongezea uwezo wa kuona kama dental loops na operating microscope.

Kutokufanikiwa kwa matibabu haya
Ziko sababu mbali mbali zinazoweza kusababisha matibabu haya yasifanikiwe, baadhi zikitokana na udhaifu wa tabibu na zingine kutokana na jino lenyewe lilivyo (internal tooth morphology)
.

Tabibu: Iwapo tabibu hakusafisha jino vizuri na kuliziba sawasawa upo uwezekano mkubwa wa matibabu haya kutokufanikiwa. Pia ikiwa tabibu hafahamu vizuri maumbile ya ndani ya jino, kuna uwezekano sehemu zingine kuachwa bila kusafishwa.

Meno: Meno mengine yana maumbile yasiyo ya kawaida, mfano katika hali ya kawaida meno ya mbele yana mfereji mmoja wa kupitisha mishipa ya fahamu na damu, lakini kuna jino lingine linakuwa na mifereji miwili au mitatu, hapa kwa mazoea na kwa kukosa vifaa vya kisasa ni rahisi kusafisha mfereji mmoja na kuacha mingine, vivyo hivyo kwa magego ambayo kwa kawaida yana mifereji mitatu hadi mine, lakini mengine mitano, sita, saba hata utafiti fulani huko China umegundua baadhi ya magego kuwa na matundu nane. Meno ya namna hii ni vigumu kufanikiwa.

Nini kifanyike ili kupunguza uwezekano wa matibabu kutofanikiwa?
Tabibu lazima ajikumbushe maumbile ya ndani ya jino analotaka kulitibu kabla ya kuanza matibabu na pia ajue kwamba jino laweza kuwa na mifereji ya ziada hivyo ajitahidi kuitafuta. Matumizi ya vifaa vya kusaidia kuona ni muhimu na hata matumizi ya x-ray za kisasa kama 3-dimensional digital x-ray ili kuweza kuona pande tatu za jino
.

Kwanini meno yanaendelea kutolewa wakati matibabu haya yapo?
• Matibabu haya ni gharama ukilinganisha na kung’oa jino hii ikiendana pamoja na umaskini wa wananchi walio wengi ambao hushindwa kugharamia na hivyo kuchagua kung’oa.
• Baadhi ya hospitali hazina wataalamu au vifaa vya matibabu haya au vyote kwa pamoja
• Mwamko mdogo wa wananchi kuhusu matibabu ya meno, hii inachangiwa pia na tabibu wa meno kutokuelezea matibabu mbadala zaidi ya kung’oa. Tafiti zimeonesha baadhi ya tabibu wa meno hutoa maelezo kwa yale matibabu wanayoyaweza tu, badala ya kuwaeleza pia upatikanaji wa matibabu mbadala katika sehemu zingine.
• Watu kuchelewa kufika hospitalini, wakija baadhi yao matibabu pekee yanayokuwa yamebaki ni kung’oa tu, hapa napo kuna mchango wa umaskini na uelewa mdogo
• Imani potofu kuwa tiba ya kudumu ya jino ni kuling’oa
• Uzoefu wa zamani, kwa mtu ambaye aliwahi kuziba jino na likauma tena, ukimwambia matibabu haya ni vigumu kuyakubali

Hitimisho
• Jali meno yako kama unavyojali viungo vingine vya mwili wako
• Kungoa jino kama tiba ya ugonjwa wa jino, ni pale tu ambapo jino hilo haliwezi tibika kwa njia mbadala kama hii ya mzizi wa jino au pale inapobainika kuwa jino husika kuendelea kubaki pale hata likiwa limetibika linaweza kuwa chanzo cha kuleta madhara makubwa mwilini kama uoto mpya n.k.

IMANI POTOFU KUHUSU AFYA YA KINYWA NA MENO

afya ya meno

1. POTOFU: Kupiga mswaki mara nyingi na kwa nguvu huzuia kuoza kwa meno

UKWELI: Si mara ngapi unapiga mswaki na nguvu gani inatumika, suala ni unapigaje mswaki. Kupiga mswaki mara nyingi na kwa maguvu kunaweza kupelekea kukwangua sehemu ngumu ya nje ya jino, kulifanya laini na hatimaye kuuma au hata kuvunjika. Kupiga mswaki mara mbili, taratibu na kwa njia sahihi ndicho kinachosaidia meno kuwa na afya

2. POTOFU: Huna haja ya kumuona tabibu wa meno kama hujaona au kuhisi una tatizo la meno.

UKWELI: Kila mtu anatakiwa kumuona tabibu wa meno angalau mara mbili kwa mwaka bila kujali meno yake yanaonekana vizuri au imara kiasi gani. Si meno yote yanayoonekana mazuri na imara ni mazima, mengine yanaweza kuwa yameoza katika maeneo usiyoweza ona kama chini ya fizi na kwenye mizizi, si hivyo tu hata uoto mpya (neoplasm) uweza kugundulika mapema kabla ya kufanya uaribifu mkubwa kama utachunguzwa na wataalamu. Kumbuka pia mangonjwa ya mifumo mingine kama ukimwi, kisukari na mengine mengi hujidhihirisha mapema kinywani kabla mgonjwa hajapata dalili zingine.

3. POTIFU: Usile kitu chochote unapokwenda kung’oa jino

UKWELI: Njaa inaweza kukufanya uzirahi katika zoezi la kungoa jino, hofu ikichanganyika na sukari kidogo mwilini husababisha ubongo kushindwa kufanya kazi sawa sawa. Imani hii potofu inahusishwa na sindano ya ganzi, watu wengi wanafikiri kila ganzi inatakiwa mtu awe hakula kwa muda fulani. Hii kwa matibabu ya meno sio kweli kwani ganzi hutolewa kwenye eneo husika tu (local anaesthesia) hivyo haiathili mwili mzima.

4. POTOFU: Usitoe jino au kufanya matibabu ya mzizi wa jino kama una uvimbe hasa usaha

UKWELI: Kung’oa jino au matibabu ya mzizi wa jino yanasaidia kutoa nafasi/njia kwa usaha kutoka na hivyo kupona haraka pengine bila hata kuhitaji dawa (antibiotics). Yaweza kuwa kweli pale tu kama mgonjwa atukuwa na homa au hawezi fungua kinywa ambapo itabidi udhibiti homa kwanza, na kama ni kushindwa kufungua kinywa yabidi kuacha na kutibu kinacho mfanya ashindwe kufungua kinywa kwanza.

5. POTOFU: Mama mjamzito hastahili kutoa jino mpaka atakapo jifungua

UKWELI: Kumuacha mama mjamzito na maumivu pamoja na ugonjwa kwaweza kufanya ugonjwa kusambaa na kuingia kwenye ubongo hata kupelekea kifo cha mama na kiumbe chake. Pia maumivu makali yaweza kusababisha mimba kutoka.

6. POTOFU: Njia ya uhakika ya kutibu jino ni kuling’oa

UKWELI: Ziko njia nyingi na za uhakika za kutibu jino bila kungoa. Kung’oa jino kama tiba ni pale tu ambapo jino hilo haliwezi tibika kwa njia yeyote na kukaa kwake kwaweza kuleta madhara zaidi. Kutoa jino huleta madhara mengine na meno bandia pamoja na kwamba hayawezi kurejesha kazi za meno yaliyotoka kwa kiwango halisi, lakini pia utunzaji wake ni mgumu na gharama pia. Hata hivyo kama umelazimika kupoteza meno basi meno bandia ndilo chaguo pekee.

7. POTOFU: Kuweka dawa ya kutuliza maumivu kama aspirini kwenye tobo kunasaidia kutoa maumivu.

UKWELI: Kama ilivyo kwa magonjwa mengine, kutuliza maumivu wakati kisababishi cha maumivu hakijashugulikiwa ni kulikuza tatizo kwa gharama. Mbali na hivyo dawa kama aspirini uunguza fizi zilizozunguka jino ulimoiweka, pia ulilainisha (weaken) na kufanya uotaji wake uwe mgumu kwani uvunjika vunjika hovyo hovyo

8. POTOFU: Kutoa jino husababisha kifo

UKWELI: Kuendelea kukaa na jino lililooza na halifai kuzibwa hufanya ugonjwa kusambaa na kusababisha kifo. Unaonekana kama ukweli pale tu mgonjwa anakuja hospitalini kutoa jino

9. POTOFU: Meno mazuri urithishwa (inherited)

UKWELI: Eti kwa vile tu mama au baba ana meno mazuri na mazima na wewe utakuwa hivyo au kinyume chake. Urithi unachangia kiasi kidogo sana, utunzaji wa meno vizuri na kukutana na tabibu wa meno mara kwara ndio njia muhimu ya kuweka meno na kinywa chako sawa.

10. POTOFU: Hakuna haja ya kuhangaika na meno ya utotoni kwani yatatoka baada ya muda wake kufika

UKWELI: Meno ya utotoni yasipotunzwa vizuri yanaweza kusababisha kutoka/ kutolewa kabla ya muda wake na kupelekea meno ya ukubwani kuota kwa mpangilio usiopendeza, lakini pia katika kipindi cha mchanganyiko wa meno ya ukubwani na utotoni, meno ya utotoni yaliyooza yaweza ambukiza ya ukubwani.

11. POTOFU: Maumivu ya meno yatajiishia yenyewe baada ya muda.

UKWELI: Kama jino limeoza haliwezi pona kwa namna yoyote mpaka lipate tiba hata kama haliumi. Ukiendelea kulidharau ugonjwa unaweza kusambaa mpaka maeneo mengine kama ubongo, kifuani na hatimaye kusababisha kifo.

Angalizo: Ni asilimia tano tu kati ya wagonjwa ambao tatizo la jino limesambaa hadi kwenye ubongo ndio huweza kupona