Showing posts with label tiba. Show all posts
Showing posts with label tiba. Show all posts

Sunday, March 18, 2012

Kuharibika kwa Chujio za Figo

Kuharibika kwa Chujio za Figo
Kuharibika kwa chujio ama Glomerulonephritis ni aina ya ugonjwa wa figo unaoathiri sehemu maalum ya figo (chujio) inayohusika na uchujaji wa maji pamoja na uchafu kutoka katika damu. Sehemu hii huitwa glomelurus au chujio kama tutakavyokuwa tukitumia katika mada hii.

Visababishi

Mara nyingi chanzo halisi cha kuharibika kwa chujio za figo (glomerulonephritis) huwa hakijulikani. Hata hivyo wakati mwingine uharibifu huu unaweza kusababishwa na kushambuliwa na mfumo wa kinga ya mwili. Uharibifu katika chujio husababisha damu pamoja na protini kuingia katika mkojo.
Tatizo hili hukua kwa haraka na figo linaweza kupoteza uwezo wake wa kuchuja maji na uchafu kwa kasi ndani ya muda mfupi wa kati wiki chache mpaka miezi kadhaa. Aina hii ya kuharibika kwa chujio za figo kwa haraka hujulikana kitalaamu kama rapidly progressive glomerulonephritis.

Ukubwa wa tatizo na vihatarishi vyake

Takribani robo ya watu wanaopatwa na tatizo sugu la glomerulonephritis huwa hawana historia ya kuwa na ugonjwa wowote wa figo hapo kabla.
Kuna mambo kadhaa yanayoweza kumfanya mtu awe katika hatari ya kupata glomerulonephritis. Mambo hayo ni pamoja na:
  • Matatizo katika mfumo wake wa damu au lymph
  • Kuwahi kutumia vimiminika vilivyotengenezwa kwa kemikali za hydrocarbon
  • Wenye historia ya saratani
  • Maambukizi ya bakteria aina ya streptococcus, virusi, majipu au maambukizi katika moyo
  • Mambo mengine yanayoweza kuongeza hatari ya kupatwa na glomerulonephritis ni pamoja na:
  • Magonjwa ya mishipa ya damu kama vile vasculitis au polyarteritis
  • Matumizi yaliyopitiliza ya dawa za kutuliza maumivu za jamii ya Non steroidal anti-inflammatory drugs kama vile aspirin
  • Magonjwa ya mfumo wa kinga ya mwili kama vile Anti-glomerular basement membrane antibody disease na IgA nephropathy
  • Makovu katika chujio (Focal segmental glomerulosclerosis) au hali ya chujio kuwa na kuta nene kuliko kawaida (Membranoproliferative GN)
  • Magonjwa yanayoathiri viungo mbalimbali vya mwili kama vile Henoch-Schonlein purpura, Goodpasture’s syndrome au Lupus nephritis
  • Ugonjwa wa kimetaboliki wa Amyloidosis
Dalili

Dalili kuu za glomerulonephritis ni kuwa na damu katika mkojo (hali inayoufanya mkojo kuwa na rangi kama nyeusi, kutu au samawati; mkojo kuwa kama wenye povu jingi (kwa sababu ya kuwa na protini nyingi kuliko kawaida) na kuvimba uso, macho, miguu au tumbo (hali inayojulikana kama edema)
Dalili nyingine ni pamoja na
  • Maumivu ya tumbo
  • Kutapika damu
  • Kuharisha au kupata choo kikubwa chenye kuchanganyika na damu
  • Kukohoa pamoja na kupumua kwa shida
  • Kukojoa kupita kiasi
  • Homa
  • Maumivu ya misuli na viungo, uchovu, maumivu ya mwili mzima pamoja na kukosa hamu ya kula
  • Kutokwa na damu puani
Baada ya muda, figo hushindwa kufanya kazi na mgonjwa huanza kuwa na dalili za mtu mwenye ugonjwa sugu wa figo.

Uchunguzi na vipimo

Kwa kawaida tatizo la uharibifu wa chujio za figo hutokea tatratibu sana hali inayoweza kufanya ugunduzi wake kuchelewa pia. Wengi wa wagonjwa wenye tatizo hili hugunduliwa pale wanapokwenda hospitali kwa ajili ya uchunguzi wa matatizo mengine. Mara nyingi hali hii hujidhihirisha kwa kuwepo na hitilafu katika kipimo cha urinalysis.
Mambo makuu matatu yanaweza kuonesha kuwepo kwa uharibifu katika chujio za figo. Mambo hayo ni upungufu wa damu (anemia), shinikizo la damu kuwa juu na ishara za kupungua kwa utendaji kazi wa figo.
Vipimo vinavyoweza kufanywa hujumuisha vipimo vya mkojo, damu pamoja na picha kama vile Ultrasound, CT au SPECT/CT.
Vipimo vya mkojo kama vile urinalysis husaidia kuonesha:
  • Utendaji kazi wa figo yaani Creatinine clearance pamoja na Urine creatinine
  • Uchunguzi wa mkojo kwa kutumia hadubini
  • Kiasi cha protini katika mkojo
  • Kiasi cha tindikali ya urea katika mkojo
  • Chembe nyekundu za damu (RBC) katika mkojo
  • Specific gravity ya mkojo na kiasi cha chumvi kwenye mkojo (yaani urine osmolality)
Vipimo vingine ni pamoja na CT scan, ultrasound ya figo, X-ray ya kifua au Intravenous pyelogram (IVP)
Vipimo vya damu husaidia kuonesha:
  • Kiasi cha protini ya albumin katika damu
  • Utendaji kazi figo kuchunguza kiasi cha BUN na creatinine katika damu
  • Viasili vinavyohusika katika mfumo wa kinga ya mwili kama vile Anti-glomerular basement membrane antibody, Anti-neutrophil cytoplasmic antibodies (ANCAs), Anti-nuclear antibodies au Complement levels.
Ili kuthibitisha uwepo wa tatizo hili na aina yake, kipimo cha biopsy (renal biopsy) hutumika.

Matibabu

Matibabu ya glomerulonephritis hutegemea sana na kisababishi cha tatizo hili, aina yake pamoja na ukubwa wa tatizo lenyewe yaani wingi wa dalili pamoja na uzito wake. Dalili ya muhimu sana kuithibiti ni ongezeko la shinikizo la damu ingawa kwa kawaida huwa ni ngumu sana kuthibiti shinikizo la damu kuwa katika kiwango cha kawaida.
Mgonjwa anashauriwa pia kupunguza kiasi cha chumvi katika chakula chake na pia kiasi cha protini na maji anayokunywa ili kusaidia utendaji kazi wa figo.
Dawa zinazoweza kutumika kwa mgonjwa mwenye tatizo hili ni pamoja na:
  • Zile za kushusha na kuthibiti shinikizo la damu hususani za jamii ya Angiotensin-converting enzyme (ACE) inhibitors kama vile captopril, Lisinopril au Enalapril; na zile za jamii ya Angiotensin receptor blockers kama vile losartan, Valsartan na Irbesartan.
  • Zile za jamii ya Corticosteroids kwa ajili ya kupunguza na kuondoa mcharuko mwili
  • Zile za kupunguza nguvu ya mfumo wa kinga ya mwili
Iwapo dawa za kupunguza nguvu ya kinga ya mwili zimeshindwa kufanya kazi na kuna uthibitisho kuwa glomerulonephritis imesababishwa na mashambulizi ya seli za kinga ya mwili katika figo, mgonjwa anaweza kufanyiwa tiba inayoitwa plasmapheresis. Katika tiba hii, sehemu ya damu yenye seli za kinga ya mwili zijulikanazo kama antibodies huondolewa kwa kubadilishwa na maji maji (plasma) yasiyo na antibodies zozote zile. Kuondoa antibodies husaidia kupunguza mcharuko mwili na uharibifu zaidi katika chujio za figo.
Iwapo figo zitashindwa kufanya kazi kabisa, mgonjwa anaweza kuhitaji kufanyiwa dialysis au kupandikizwa figo mpya.

Matarajio

Kuharibika kwa chujio za figo kunaweza kuwa ni tatizo la muda na lenye kurekebishika au linaweza kudorora na kuwa la kudumu. Kudorora kwa chujio za figo kunaweza kusababisha kupungua kwa utendaji kazi wa figo au ugonjwa sugu wa figo kushindwa kufanya kazi (chronic renal failure), au kufa kabisa kwa figo zote (end-stage renal disease).

Madhara

Pamoja na kusababisha shinikizo la damu kuwa juu, uharibifu katika chujio za figo unaweza pia kusababisha mlinganyo usio sawa wa madini katika damu (electrolytes imbalance) kama vile ongezeko la madini ya potassium (hyperkalemia); maambukizi yanayojirudia katika njia ya mkojo, uwezekano wa kupata maambukizi ya mwili, mrundikano wa maji mwilini hali inayoweza kusababisha moyo kushindwa kufanya kazi (congestive heart failure) au maji kujaa katika mapafu (pulmonary edema); au ugonjwa wa figo ujulikanao kama Nephrotic syndrome (utaelezwa katika makala zijazo).

Kinga

Inawezekana kuzuia uharibifu wa chujio za figo kwa baadhi ya watu ingawa, kwa ujumla ni ngumu kufanya hivyo. Baadhi ya mambo ya kufanya ili kuepuka kupatwa na tatizo hili ni pamoja na kuepuka matumizi ya vimiminika vyenye kemikali za hydrocarbons, matumizi ya madini ya zebaki pamoja na matumizi ya muda mrefu ya dawa za jamii ya nonsteroidal anti-inflammatory drugs (NSAIDs) kama vile Aspirin.

Mtu Mwenye Mioyo Miwili apata Mishtuko ya Mioyo na Kupona

Mtu Mwenye Mioyo Miwili
Raia mmoja nchini Italia mwenye umri wa miaka 71 alipata mishtuko ya mioyo yake yote miwili na kupoteza fahamu kwa sekunde kadhaa lakini hatimaye aliweza kuokolewa maisha yake. Mtu huyo alikimbizwa katika hospitali ya Verona nchini Italia baada ya kupata maumivu ya kifua na mapigo ya mioyo yake kuwa si ya kawaida.

Taarifa kutoka jarida la American Emergency Medical Journal inaeleza kuwa mtu huyo aliwahi kufanyiwa upasuaji wa moyo na kupandikizwa moyo mwingine miaka kadhaa iliyopita katika upasuaji unaojulikana kama double heart transplant (heterotopic heart transplantation). Hii ni aina ya upasuaji ambapo moyo hupandikizwa na kufanya kazi sambamba na moyo wa awali (wa mgonjwa mwenyewe) ambao huwa umeadhirika kutokana na maradhi. Chemba za damu za kwenye mioyo hiyo huunganishwa ili moyo uliopandikizwa uweze kusaidia moyo wa mgonjwa.
Ripoti zinasema kuwa moyo mmoja ulianza kuwa na nguvu zaidi kuliko mwingine na hivyo kusababisha mapigo yake kutofautiana na mwingine. Madaktari walijaribu kurekebisha mapigo ya mioyo hiyo ili yaendane sawa kwa kutumia dawa lakini mioyo hiyo iliacha kupiga kabisa na mtu huyo kuacha kupumua. Hata hivyo, waliweza kumrejesha katika hali ya kupumua kwa kutumia kifaa maalum cha Defibrillator kabla ya kumfanyia upasuaji na kubadilisha kifaa kinachosaidia kuweka sawa mapigo ya moyo kinachojulikana kama pacemaker.
Mtu huyo ambaye bado ana mioyo hiyo miwili, yupo hai na afya yake ni nzuri tangu alipofanyiwa upasuaji huo mwaka 2010.
Dk Giacomo Mugnai ambaye alihusika katika kumtibu mtu huyo anakiri kupitia barua pepe aliyotuma kwenda kwa mtandao wa msnbc.com kuwa hawajawahi kuona mgonjwa kama huyo hapo awali.
Dk Rade Vukmir, Profesa wa kitengo cha tiba ya dharura (Emergency Medicine) wa Chuo Kikuu cha America’s Temple University na msemaji wa American College of Royal Physicians anasema amewahi kushuhudia namna hiyo ya upasuaji ikifanywa katika moyo na figo huko nyuma.
Madaktari wa upasuaji kawaida huacha figo au moyo katika sehemu yake ya kawaida na kupandikiza mwingine ikiwa figo/moyo huo utakuwa kazi kubwa sana kutoa, au kama kuna matarajio ya figo/moyo huo kupona hapo siku za usoni ikiwa utasaidiwa na figo/moyo wa kupandikizwa.
Aina hii ya upasuaji (double heart transplant) ni nadra sana siku hizi kutokana na vifaa maalum ambavyo vingesaidia moyo huu wa pili wa kupandikizwa vinavyojulikana kama Ventricular Assist Devices ambavyo vilikuwa vikubwa sana na ghali miaka 20 iliyopita kuwa ni vidogo na rahisi kuvibeba katika miaka ya hivi karibuni.
Watu wanaofanyiwa upasuaji huu huishi kwa wastani wa miaka 15 baada ya kuwekea moyo wa pili lakini mtu atahitaji kufundishwa jinsi ya kuishi na moyo mwingine wa ziada, kuhudhuria hospitali mara kwa mara kuangaliwa maendeleo yake pamoja na kutumia dawa kwa muda mrefu.

Ugonjwa wa Nephrotic syndrome

Ugonjwa wa Nephrotic syndrome

Ugonjwa wa Nephrotic syndrome ni hali ya maradhi inayokumba figo na kusababisha kupoteza kiasi kingi cha protini kutoka kwenye damu kuingia kwenye mkojo. Kiasi cha protini kinachopotea ni wastani wa gram 3.5 kwa siku kwa kila mita za mraba 1.73 za mwili.

Chujio za figo (glomeruli) huwa na vitundu vidogo vidogo viitwavyo podocytes ambavyo hufanya kazi ya kuchuja uchafu na sumu nyingine kutoka mwilini na kuzitoa nje. Vitundu hivi vina uwezo wa kuzuia protini isichujwe kuingia kwenye mkojo. Hata hivyo, figo zenye Nephrotic syndrome huwa na podocytes kubwa kiasi cha kuweza kupitisha protini za ukubwa mbalimbali (zikiwepo albumin ambazo ni protini zenye kipenyo kikubwa zaidi). Pamoja na kuharibika huku kwa chujio, podocytes bado hazina ukubwa wa kuweza kupitisha seli nyekundu za damu ndiyo maana mkojo wa mgonjwa wa Nephrotic syndrome hauna damu ndani yake.

Ukubwa wa tatizo
Nephrotic syndrome huathiri karibu watu wa rika zote. Hata hivyo watoto walio katika umri wa miaka 2 mpaka sita ndiyo waathirika wakuu wa ugonjwa huu. Ugonjwa huu umeonekana kuwapata zaidi watoto wa kiume kuliko wa kike.

Visababishi vya Nephrotic syndrome
Visababishi vya Nephrotic syndrome vimegawanyika katika makundi mawili; yale yanayosababishwa na magonjwa yaliyo ndani ya figo zenyewe (primary nephrotic syndrome), au yale yanayosababishwa na magonjwa yaliyo nje ya figo (secondary nephotic syndrome).

Visababishi vilivyo ndani ya figo (primary nephrotic syndrome)
Kipimo cha biopsy husaidia kutambua magonjwa yanayosababisha Nephrotic syndrome ndani ya figo lenyewe. Kwa watoto wadogo, chanzo kikuu cha Nephrotic syndrome ndani ya figo zenyewe ni ugonjwa unaoitwa Minimal change disease (MCD) wakati kwa watu wazima ni Focal segmental glomerulosclerosis (FSGS) pamoja na Membraneous nephropathy (MN). Magonjwa haya yote husababisha uharibifu katika chujio na hivyo kuruhusu upotevu wa protini katika mkojo.

Visababishi vilivyo nje ya figo (secondary nephrotic syndrome)
Kama ilivyo kwa magonjwa yanayosababisha nephrotic syndrome ndani ya figo, magonjwa yanayosababisha nephrotic syndrome nje ya figo (secondary causes) nayo pia husababisha uharibifu katika chujio za figo. Magonjwa haya ni pamoja na

  • Maambukizi katika ini (hepatitis B na C)
  • Ugonjwa wa kisukari
  • Matumizi ya baadhi ya dawa kama vile dawa za kupunguza mcharuko mwili (corticosteroids) pamoja na NSAIDS kama vile Aspirin.
  • Matumizi ya madawa ya kulevya kama vile heroin
  • Baadhi ya kemikali kama madini ya dhahabu
  • Maambukizi ya bacteria kama kaswende na bacteria wanaosababisha ukoma
  • Ugonjwa wa malaria
  • Saratani za aina mbalimbali kama vile saratani ya damu (leukemia)
  • Kung’atwa na nyuki
  • Ukimwi
  • Shinikizo la damu
  • Magonjwa yanayoathiri mwili mzima kama vile Sarcoidosis, systemic lupus erythematosus au Sjogren’s syndrome

Viashiria pamoja na dalili
Ugonjwa huu ni mkusanyiko wa mambo/dalili kuu nne (ingawa mgonjwa anaweza kuwa na dalili nyingine kadhaa).

Mambo hayo ni

  • Kupoteza kiasi kikubwa cha protini katika mkojo (protenuria) zaidi ya gram 3.5 kwa siku
  • Kuwa na upungufu wa protini aina ya albumin katika damu (hypoalbuminemia)
  • Kuwa na ongezeko la mafuta (lipids) katika damu (hyperlipidemia), na
  • Kuvimba (edema) mwili mzima (generalized edema au anasarca)

Ongezeko la mafuta katika damu yaani hyperlipidemia husababishwa na mambo mawili; kwanza upotevu wa protini katika mkojo husababisha upungufu mkubwa wa protini kwenye damu.

Ili kufidia upungufu huo, ini hulazimika kutengeneza protini nyingi kuliko kawaida hali ambayo husababisha ongezeko siyo tu la protini bali viasili vyenye mchanganyiko wa protini na mafuta yaani lipoproteins. Pili, upungufu wa protini husababisha pia upungufu wa baadhi ya vimeng’enyo muhimu mwilini, kimojawapo kikiwa lipoprotein lipase ambacho huchochea kuvunjika kwa mafuta mwilini. Kukosekana kwa kimeng’enyo hiki hufanya mafuta yasiweze kuvunjwa na hatimaye kusababisha mrundikano wa mafuta katika damu.

Kupungua kwa protini hususani protini aina ya albumin katika damu (hypoalbuminemia) husababisha kupungua kwa shinikizo linalosaidia kutunza maji katika mzunguko wa damu (oncotic pressure). Madhara ya kupungua kwa shinikizo hilo husababisha maji kutoka katika mzunguko wa damu na kurundikana katika sehemu mbalimbali za mwili. Madhara yake ni kufanya kiasi cha maji katika mzunguko wa damu kuwa chini (hypovolemia) kwa sababu maji mengi huingia kwenye nafasi zilizo katika ya seli na seli. Mrundikano wa maji mwilini husababisha

  • kuvimba uso hasa sehemu za macho, hususani nyakati za asubuhi (morning facial puffiness)
  • Kuvimba kwa miguu (hubonyea kama ikiminywa kwa vidole) (pitting edema)
  • Maji katika kifua na mapafu (pleural effusion)
  • Maji kujaa tumboni (ascites), na
  • Kuvimba mwili mzima (anasarca)

Dalili nyingine ni pamoja

  • upungufu wa damu (anaemia)
  • Kupumua kwa shida
  • Kukojoa mkojo mzito kama povu kwa sababu ya protini nyingi kwenye mkojo
  • Dalili zinazoambatana na kisababishi cha nephrotic syndrome kama vile dalili za kisukari, malaria na magonjwa mengine
  • Kiwango cha kawaida cha shinikizo la damu. Wagonjwa wa nephrotic syndrome huwa na BP za kawaida isipokuwa kwa nadra sana BP inaweza kuwa juu.

Vipimo na uchunguzi
Baada ya kusikiliza historia ya mgonjwa na kufahamu mambo yanayomsumbua (dalili), daktari humfanyia mgonjwa uchunguzi wa mwili (physical examination) ili kutambua vishiria zaidi vya tatizo hili.

Vipimo vya maabara hufanyika ili kuchunguza utendaji kazi wa figo, ni kwa kiasi gani yameathirika na pia kufahamu visababishi vya tatizo hili ikiwa ni pamoja na kuchunguza magonjwa mengine ambayo yanaweza kufanana na nephrotic syndrome kidalili.

Vipimo ni pamoja na:

  • kuchunguza kiasi cha albumin katika damu
  • Kuchunguza kiasi cha madini katika damu (comprehensive metabolic panel)
  • Vipimo vya utendaji kazi figo kama vile Blood Urea Nitrogen (BUN), Serum creatinine pamoja na creatinine clearance
  • Kipimo cha mkojo cha urinalysis
  • Kuchunguza kiasi cha mafuta katika damu (blood cholesteroal na triglycerides levels), pamoja na
  • Biopsy ya figo (renal biopsy)

Vipimo vya kutambua visababishi vya nephrotic syndrome ni pamoja;

  • kipimo cha VVU
  • Kipimo cha kaswende
  • Kipimo cha maambukizi katika ini (Hepatitis B na C antibodies/Hepatitis panel)
  • Vipimo vya mfumo wa kinga ya mwili (antinuclear antibody tests, complement levels na cryoglobulins levels) na mcharuko mwili (Rheumatoid factor)
  • Vipimo vya kisukari
  • Kiasi na aina za protini katika damu na mkojo (serum protein elecrophoresis na urine protein elecrophoresis)

Kadhalika, vipimo vya kutambua madhara yaliyosababishwa na nephrotic syndrome ni pamoja na;

  • Kiwango cha vitamin D katika damu
  • Kiasi cha madini chuma kwenye damu
  • Na uwepo wa casts katika mkojo

Matibabu
Malengo ya tiba ya nephrotic syndrome ni kupunguza dalili za ugonjwa, kupunguza madhara ya ugonjwa na pia kupunguza kasi ya uharibifu katika figo. Ili kuthibiti vizuri nephrotic syndrome ni vema sana kutibu chanzo cha tatizo lenyewe. Wakati mwingine mgonjwa anaweza kuhitaji matibabu kwa maisha yake yote.

Matibabu yamegawanyika katika; yale ya kusaidia kupunguza dalili na kumpatia nafuu mgonjwa, yale ya kutibu chanzo cha ugonjwa, na ya kutumia lishe maalum ili kupunguza ongezeko la vitu visivyohitajika mwilini au kurejesha baadhi ya vitu vilivyopungua.

Matibabu kwa ajili ya kupunguza dalili ni pamoja na

  • kuthibiti na kuhakikisha kiasi cha maji katika mwili kipo katika viwango sahihi. Hili hufanyika kwa kupima mara kwa mara kiasi cha mkojo kinachotolewa pamoja na shinikizo, kupunguza unywaji maji kufikia angalau lita moja kwa siku na kutumia dawa za kupunguza maji mwilini kama vile frusemide.
  • Njia nyingine ni kupima utendaji kazi wa figo mara kwa mara
  • Kushusha kiasi cha mafuta mwilini kwa kutumia dawa ili kuzuia madhara zaidi katika mishipa ya damu
  • Dawa za kuzuia damu kuganda pia zaweza kutumika

Matibabu ya chanzo cha nephrotic syndrome ni pamoja na

  • ili kupunguza mcharuko mwili na pengine kumaliza kabisa tatizo hilo, dawa za jamii ya cosrticosteroids kama vile prednisolone hutumika ili kuthibiti na kushusha kwa muda kinga ya mwili
  • Kushusha na kuthibiti shinikizo la damu kuhakikisha lipo 130/80mmHg au chini yake. Lengo kuu ni kuzuia uharibifu zaidi katika figo. Kufanikisha hili, dawa za jamii ya Angiotensin-converting enzyme (ACE) inhibitors kwa mfano captopril au angiotensio receptor blockers (ARBs) hutumika. Dawa za jamii ya ACE inhibitors pia husaidia kupunguza upotevu zaidi wa protini katika mkojo.
  • Kutibu na kuthibiti kisukari iwapo mgonjwa ana kisukari

Matibabu kwa njia ya lishe hujumuisha

  • kupunguza matumizi ya chumvi katika chakula kufikia angalau gramu 1000 mpaka 2000 kwa siku. Epuka matumizi ya vyakula vya makopo, nyama za kuoka, na vyakula vya magengeni au madukani (fast foods). chumvi kidogo husaidia kupunguza mrundikano wa maji mwilini na uvimbe
  • Kula lishe yenye kiasi cha wastani cha protini inayotokana na wanyama kama vile nyama ya ng’ombe isiyo na mafuta, samaki au ndege (kuku, bata). Kiasi kinachoshauriwa ni walau gramu moja ya protini kwa kila kilo moja ya mlo unaokula.
  • Ingawa baadhi ya tafiti zinaonesha hakuna faida ya kula chakula chenye mafuta na lehemu kidogo kwa mgonjwa wa nephrotic syndrome, lakini kiujumla wataalamu wengi wanashauri kuepuka kula vyakula vyenye mafuta kwa wingi, hasa yale yenye lehemu (cholesterol). Ni vema kuepuka vyakula vyenye mafuta yasiyofaa (saturated fats) kama vile jibini, siagi, vyakula vya kuokwa, nyama yenye mafuta, kiini cha yai, na ngozi ya ndege kama kuku. Inashauriwa kula zaidi vyakula vyenye mafuta yanayofaa (unsaturated fats) kwa mfano mafuta ya mizeituni (olive oil), mafuta ya karanga, maparachichi, samaki pamoja na vyakula vya jamii ya njugu. Aidha dawa za kupunguza kiasi cha mafuta (statins) nazo husaidia sana. Lengo kuu la matibabu haya ni kupunguza uwezekano wa kupata maradhi ya moyo na mishipa ya damu kwa ujumla.
  • Inashauriwa pia kuongeza ulaji wa matunda na mboga za majani.
  • Na pia matumizi ya vidonge vya kuongeza vitamini D

Madhara ya nephrotic syndrome
Ugonjwa wa nephrotic syndrome huathiri karibu kila sehemu ya mwili. Baadhi ya madhara ya ugonjwa huu ni;

  • Upungufu wa damu mwilini
  • Kuziba kwa vena (mishipa ya damu inayorudisha damu kwenye moyo) (venous thrombosis) hususani vena za figo (renal veins).
  • Maambukizi ya bacteria mbalimbali (kwa mfano Haemophilus influenzae na Streptococcus pneumoniae) kwa sababu ya upungufu wa protini zinazosaidia kutengeneza seli za mfumo wa kinga ya mwili (immunoglobulins).
  • Kujaa maji katika mapafu (pulmonary edema)
  • Figo kushindwa kufanya kazi kwa ghafla (ARF) kwa sababu ya upungufu wa maji katika mzunguko wa damu.
  • Matatizo ya mifupa kwa sababu ya upungufu wa vitamini D
  • Ukuaji wa kusuasua ambao husababishwa na upotevu wa protini nyingi katika mkojo, matumizi ya dawa za kupunguza mcharuko mwili na hata ulaji wa shida kwa sababu ya mgonjwa kujihisi kichefuchefu cha mara kwa mara.
  • Upungufu wa homoni ya thyroid (hypothyroidism) kwa sababu ya upotevu wa protini (thyroid binding globulin) inayosaidia utengenezaji wa homoni hiyo.
  • Upungufu wa madini ya calcium, na hata
  • Ugonjwa wa homoni wa Cushing’s syndrome.
  • Moyo kushindwa kufanya kazi (congestive cardic failure)
  • Utapiamlo
Matarajio
Matokeo ya ugonjwa huu hutofautiana kati ya mgonjwa na mgonjwa kulingana na chanzo chake. Kwa wengine ugonjwa unaweza kuja kwa ghafla na kupona baada ya muda mfupi wakati kwa wengine huwa sugu na kuchukua muda mrefu kupona au pengine kuhitaji mgonjwa kubadilishwa figo. Kwa ujumla, watoto wenye nephrotic syndrome iliyosababishwa na ugonjwa wa minimal change disease wana matokeo mazuri baada ya kutibiwa na dawa za kupunguza mcharuko mwili (steroids) wakati watu wazima wenye nephrotic syndrome iliyosababishwa na ugonjwa wa focal segmental glomerulosclerosis mara nyingi huishia kupata uharibifu mkubwa katika figo hatimaye figo hufa kabisa (End stage renal disease, ESRD).

Kinga
Ni muhimu kufahamu vyanzo vinavyosababisha nephrotic syndrome. Kuweza kuthibiti vyanzo hivyo, kwa mfano maambukizi kama ya Ukimwi, malaria, kaswende, ukoma, na mengineyo, husaidia kupunguza uwezekano na kujikinga dhidi ugonjwa wa nephrotic syndrome.

Saratani ya tezi ya thyroid (Thyroid cancer)


Hii ni aina ya saratani inayokumba tezi ya thyroid. Ikumbukwe kuwa tezi ya thyroid ipo sehemu ya mbele ya shingo ya mwanadamu ikiwa na sehemu mbili (lobes) moja kila upande wa shingo.

Visababishi na ukubwa tatizo
Saratani ya thyroid huwapata watu wa umri mbalimbali, kuanzia watoto mpaka watu wazima. Watu waliowahi kupigwa mionzi sehemu ya mbele ya shingo wapo katika hatari kubwa ya kupata aina hii ya saratani. Kadhalika watu wazima ambao waliwahi kupigwa mionzi kipindi cha utotoni nao pia wana hatari kubwa zaidi ya kupata saratani ya thyroid hata kama hawakuwahi kupata tatizo hilo wakati wanakua.

Tiba ya mionzi maeneo ya shingoni ilikuwa ikitumika sana zamani kwenye miaka ya 50 mpaka 60 kwa ajili ya matibabu ya uvimbe wa tezi ya thymus, mafindofindo (tonsils), au baadhi ya magonjwa ya ngozi. Hata hivyo ni nadra sana kwa tiba hii kutumika katika zama hizi.

Vihatarishi vingine vya saratani ya tezi ya thyroid ni pamoja na kuwepo kwa historia ya tatizo hili miongoni mwa wanafamilia na kuwa na goita iliyodumu muda mrefu bila kutibiwa.

Aina za saratani ya tezi ya thyroid
Kulingana na aina ya seli zinazounda tezi ya thyroid zinazoshambuliwa, saratani ya thyroid inaweza kugawanywa katika aina zifuatazo:
• Aina inayojulikana kitaalamu kama papillary carcinoma. Hii ni aina maarufu zaidi miongoni mwa watu wenye saratani ya tezi ya thyroid. Kwa kawaida, aina hii huwapata zaidi wanawake walio katika umri wa kuzaa. Aina hii husambaa taratibu sana na haina madhara sana kwa mgonjwa ikilinganishwa na aina nyingine za saratani ya tezi ya thyroid.
• Aina nyingine ni ile inayofahamika kwa jina la follicular carcinoma. Aina hii hutokea katika asilimia karibu 10 ya watu wanaopata saratani ya thyroid. Follicular carncinoma huwa na tabia ya kupotea lakini pia huwa na uwezo wa kumrudia mgonjwa na kisha kusambaa kwa kasi.
• Aina ya tatu ni ile inayojulikana kama anaplastic carcinoma. Aina hii, japokuwa ni nadra sana kuonekana miongoni mwa wagonjwa wenye saratani ya thyroid, ndiyo aina ya hatari zaidi miongoni mwa aina zote za saratani ya thyroid. Anaplastic carcinoma husambaa kwa kasi kubwa na haiwezi kutibika kwa kutumia tiba ya madini ya nuklia ya Iodine.
• Aina nyingine huitwa medullary carcinoma. Hii ni aina ya saratani ya thyroid ambayo hutokea katika seli ambazo si za tezi ya thyroid lakini zipo ndani ya tezi hiyo (kuna baadhi ya seli ambazo si za tezi ya thyroid lakini zinapatikana na kuishi ndani ya tezi ya thyroid, mfano wa mgeni anayeishi katika nyumba isiyo yake). Aina hii huwapata zaidi wanafamilia na watafiti wameihusisha na mabadiliko ya kinasaba (genetic mutations), na kwa ujumla matibabu yake hutofautiana sana na yale ya aina nyingine za saratani ya thyroid.

Dalili
Dalili hutofautiana kulingana na aina ya saratani, ingawa kiujumla zaweza kujumuisha:
• kikohozi
• Shida wakati wa kumeza chakula, vinywaji hata mate
• Kuvimba kwa tezi ya thyroid
• Mabadiliko katika sauti, sauti kufifia au kuwa ya mikwaruzo
• Uvimbe kwenye shingo
• Tezi ya thyroid kuwa na nundu au vinundu

Vipimo na uchunguzi
Mgonjwa anayehisiwa kuwa na saratani ya thyroid hufanyiwa uchunguzi wa mwili kabla ya kufanyiwa vipimo kadhaa ili kujiridhisha kuwa ni kweli ana tatizo la saratani ya thyroid. Uchunguzi wa mwili unaweza kuonesha uwepo wa nundu au uvimbe katika thyroid na/ kuvimba kwa tezi za mitoki katika shingo.

Vipimo ni pamoja na:
• Ultrasound ya tezi ya thyroid
• Kukata sehemu ya thyroid na kukichunguza kimaabara (thyroid biopsy)
• Picha ya utendaji kazi wa tezi ya thyroid (thyroid scan)
• Uchunguzi wa sehemu ya ndani ya koo (laryngoscopy)
• Kupima damu ili kuchunguza kiwango cha homoni ya calcitonin. Iwapo kiwango kitakuwa juu kuliko kawaida, hii yaweza kuashiria uwepo wa medullary carcinoma.
• Kupima damu ili kuchunguza kiwango cha viasili vya thyroglobulin ambavyo vywaweza kuashiria uwepo wa saratani aina ya papillary carcinoma au follicular carcinoma.
• Kupima damu ili kuchunguza kiwango cha homoni za thyroid za T3, T4 na TSH.

Matibabu
Matibabu hutegemea sana aina ya saratani, ingawa upasuaji wa tezi ya thyroid ndiyo aina ya tiba inayoongoza. Wakati wa upasuji, kwa kawaida tezi yote huondolewa, na iwapo daktari atahisi kuwa hata tezi za mitoki zilizo karibu na thyroid nazo pia zimeathirika pia huondolewa.

Aidha mgonjwa anaweza pia kupatiwa tiba ya mionzi ambayo hutolewa kwa njia ya kupigwa mionzi ya moja kwa moja (external beam radiation) au kwa kutumia (kunywa) vidonge vya madini ya Iodine vyenye nguvu ya nyuklia yaani radioactive iodine. Njia hii inaweza kufanyika ikiambatana pia na upasuaji au bila upasuaji.

Baada ya matibabu, mgonjwa anapaswa kuendelea kutumia dawa maalum za kumrejeshea homoni za thyroid ili kurudisha kile alichopoteza baada ya kuondolewa kwa tezi. Kwa kawaida dozi inayotolewa huwa kubwa kuliko ile inayohitajika mwilini ili kusaidia saratani isijirudie tena.

Iwapo upasuaji au mionzi haujasaidia kuondoa kansa, na kwamba saratani inaendelea kusamabaa sehemu nyingine za mwili, mgonjwa anaweza kuanishiwa dawa za kutibu saratani (chemotherapy) ingawa nayo inaweza ikawa na manufaa kwa baadhi ya wagonjwa tu na si wagonjwa wote.

Nini cha kutarajia
Saratani aina ya Anaplastic carcinoma ina matokeo mabaya zaidi kuliko aina zote zilizobaki, na mara nyingi mgonjwa hufariki hata baada ya matibabu ya uhakika ya muda mrefu. Follicular carcinomas pamoja na kuwa na tabia ya kusambaa kwa kasi kwenye maeneo mengine ya mwili huwa na matokeo mazuri ikitibiwa. Matokeo ya wagonjwa wenye aina ya medullary carcinoma yanatofautiana kati ya mgonjwa na mgonjwa, ambapo wanawake wenye umri chini ya miaka 40 wameonekana kuwa na matokeo mazuri zaidi baada ya tiba kuliko walio na zaidi ya umri huo. Aidha wagonjwa wengi wenye Papillary carcinomas hupona kabisa na kuendelea na maisha yao ya kawaida.

Jambo la kukumbuka ni kuwa, mara baada ya tiba, mgonjwa anapaswa kuendelea kutumia vidonge vya kurejesha homoni za thyroid kila siku za maisha yake.

Madhara ya saratani ya thyroid
Madhara ya saratani ya thyroid ni pamoja na madhara katika sanduku la sauti kabla ya upasuaji, na sauti ya mikwaruzo baada ya upasuaji, kupungua kwa kiwango cha madini ya calcium mwilini iwapo tezi ya parathyroid ambayo ipo juu kidogo ya thyroid itaodolewa kwa bahati mbaya wakati wa upasuaji, na kusambaa kwa kansa katika sehemu nyingine za mwili kama vile mifupa, au mapafu.

Kinga
Mpaka sasa hakuna kinga rasmi ya ugonjwa huu. Hata hivyo, ni vizuri jamii ikawa makini na mionzi isiyohitajika sehemu za mbele ya shingo. Aidha wale wenye historia ya tatizo hili katika familia zao ni vema wakamuona daktari kwa ajili ya uchunguzi kabla tatizo halijajitokeza, au kuwa kubwa.

Matibabu ya Mzizi wa Jino (Root Canal Treatment)

matibabu ya mzizi wa jino
Haya ni matibabu ambayo hutolewa kwa jino ambalo sehemu ya uhai wake imeharibika kiasi kwamba haliwezi kutibika kwa kuziba tu, kwa maneno mengine hii ndiyo njia mbadala ya kutibu jino bila kung’oa.

Matibabu uhusisha kutoboa jino hadi sehemu ya uhai wa jino yenye mishipa ya damu na ile ya fahamu na chembechembe za meno na kuviondoa nikimaanisha kuondoa mishipa ya fahamu, ya damu na chembe pamoja na ugonjwa na baadae kuijaza sehemu hii na vitu maalumu vinavyokubaliana na mwili (biocompatible).

Aina za matibabu ya mzizi wa jino
Kuna aina kuu mbili za matibabu ya mzizi wa jino

1. Njia ya kawaida (conventional root canal treatment)
Njia hii ni kama nilivyoeleza hapo juu, kuingia kwenye kiini cha jino na kuondoa kila kitu kilichomo na kisha kujaza uwazi uliobaki na vitu maalumu vinavyokubaliana na mwili

2. Matibabu ya mzizi wa jino yanayohusisha upasuaji
kwa njia hii mbali na kutumia njia ya kwanza, upasuaji hufanyika pia ili kondoa mfupa uliofunika ncha ya mzizi wa jino kusafisha eneo lililozunguka ncha ya mzizi na baadaye kukata ncha husika kisha kuziba kutokea kwa nyuma (retro grade filling). Njia hii hutumika pale njia ya kawaida inaposhindwa kuondoa tatizo au inapoonekana kabisa kuwa haitaweza kuondoa tatizo. Huu ni upasuaji mdogo, unaofanyika kwa ganzi ndogo ya eneo husika (local anaesthesia).
Mafanikio ya matibabu haya ni makubwa sana.

Ni meno yapi yanahitaji matibabu hayo?
• Meno yaliyooza hadi uoza kufikia kiini cha jino (dental pulp) - sehemu ya uhai wa jino.
• Meno yaliyopata ajali na kupasuka na kuacha kiini cha jino kikiwa wazi (traumatic pulp exposure)
• Meno yaliyopata ajali na kusababisha mishipa ya damu kukatika au kupasuka na kuvunjika ndani ya jino, kitu ambacho hupelekea jino kufa (pulp necrosis) na baadaye kusabisha jipu au kubadilika rangi
• Wakati mwingine japo ni mara chache, ni pale tunapokuwa tunataka kuliweka sawa jino/meno ambalo/ambayo hayapo kwenye mstari sawa ili yaendane na meno mengine.
• Pia wakati mwingine, tunapo lisaga jino ili liweze kubeba meno bandia ya daraja (bridge) huku tukiwa na mashaka na uhai wake.

Nini dalili zinazoashiria jino kuhitaji matibabu haya?
• Jino linalouma - kuuma kwa jino kunashiria ugonjwa kuwa umeingia ndani ya kiini cha jino na au hata kupitiliza na kuingia kwenye mfupa ulioshikilia jino
• Jino lililooza na kusababisha uvimbe, liwe linauma au haliumi
• Jino lililokatika na kupoteza zaidi ya nusu ya kichwa cha jino (crown) kukatika kuwe kwa ajali au kuoza au vyote kwa pamoja
• Jino linalobadilika rangi huku kukiwa na historia ya kuligonga mahali au kuchapwa ngumi usoni, hapa jino linaweza kuanza kubadilika rangi miezi sita tangu siku ya ajali mpaka wakati mwingine hadi miaka ishirini wakati mgonjwa alishasahau hata ajali yenyewe.

Meno yasiyofaa kwa matibabu haya
• Meno yaliyoharibika vibaya kiasi kwamba hayatibiki tena japo ni machache, kwani hata kama jino limebaki mzizi tu, ukiwa bado imara twaweza fanya matibabu haya na baadae kujenga kichwa (crown)
• Meno yaliyolegea sana kutokana na magonjwa ya fizi ambayo hayawezi kuimarishwa tena.
• Magego ya mwisho (wisdom teeth) kwa kawaida meno haya huwa yana maumbile yasiyotabirika kiasi kwamba hata mafanikio ya matibabu huwa hayatabiriki, hii ikiambatana na kuwa yako nyuma sana kiasi cha kuwa vigumu kuyafikia kwa ufasaha na vifaa vyetu na pia yana mchango kidogo kwa usagaji chakula (2%)
• Meno ambayo mifereji ya mizizi ambayo hupitisha mishipa ya fahamu na damu imeziba (calcified root canals)

Mafanikio ya matibabu haya
Kiwango cha mafanikio ya matibabu haya ni kati ya asilimia sabini na saba hadi tisini na nane (77-98%). Haya ni mafanikio ya hali ya juu kwa matibabu ya aina yeyote ile, mafanikio huongezeka zaidi pale tabibu anapotumia vifaa vya kumuongezea uwezo wa kuona kama dental loops na operating microscope.

Kutokufanikiwa kwa matibabu haya
Ziko sababu mbali mbali zinazoweza kusababisha matibabu haya yasifanikiwe, baadhi zikitokana na udhaifu wa tabibu na zingine kutokana na jino lenyewe lilivyo (internal tooth morphology)
.

Tabibu: Iwapo tabibu hakusafisha jino vizuri na kuliziba sawasawa upo uwezekano mkubwa wa matibabu haya kutokufanikiwa. Pia ikiwa tabibu hafahamu vizuri maumbile ya ndani ya jino, kuna uwezekano sehemu zingine kuachwa bila kusafishwa.

Meno: Meno mengine yana maumbile yasiyo ya kawaida, mfano katika hali ya kawaida meno ya mbele yana mfereji mmoja wa kupitisha mishipa ya fahamu na damu, lakini kuna jino lingine linakuwa na mifereji miwili au mitatu, hapa kwa mazoea na kwa kukosa vifaa vya kisasa ni rahisi kusafisha mfereji mmoja na kuacha mingine, vivyo hivyo kwa magego ambayo kwa kawaida yana mifereji mitatu hadi mine, lakini mengine mitano, sita, saba hata utafiti fulani huko China umegundua baadhi ya magego kuwa na matundu nane. Meno ya namna hii ni vigumu kufanikiwa.

Nini kifanyike ili kupunguza uwezekano wa matibabu kutofanikiwa?
Tabibu lazima ajikumbushe maumbile ya ndani ya jino analotaka kulitibu kabla ya kuanza matibabu na pia ajue kwamba jino laweza kuwa na mifereji ya ziada hivyo ajitahidi kuitafuta. Matumizi ya vifaa vya kusaidia kuona ni muhimu na hata matumizi ya x-ray za kisasa kama 3-dimensional digital x-ray ili kuweza kuona pande tatu za jino
.

Kwanini meno yanaendelea kutolewa wakati matibabu haya yapo?
• Matibabu haya ni gharama ukilinganisha na kung’oa jino hii ikiendana pamoja na umaskini wa wananchi walio wengi ambao hushindwa kugharamia na hivyo kuchagua kung’oa.
• Baadhi ya hospitali hazina wataalamu au vifaa vya matibabu haya au vyote kwa pamoja
• Mwamko mdogo wa wananchi kuhusu matibabu ya meno, hii inachangiwa pia na tabibu wa meno kutokuelezea matibabu mbadala zaidi ya kung’oa. Tafiti zimeonesha baadhi ya tabibu wa meno hutoa maelezo kwa yale matibabu wanayoyaweza tu, badala ya kuwaeleza pia upatikanaji wa matibabu mbadala katika sehemu zingine.
• Watu kuchelewa kufika hospitalini, wakija baadhi yao matibabu pekee yanayokuwa yamebaki ni kung’oa tu, hapa napo kuna mchango wa umaskini na uelewa mdogo
• Imani potofu kuwa tiba ya kudumu ya jino ni kuling’oa
• Uzoefu wa zamani, kwa mtu ambaye aliwahi kuziba jino na likauma tena, ukimwambia matibabu haya ni vigumu kuyakubali

Hitimisho
• Jali meno yako kama unavyojali viungo vingine vya mwili wako
• Kungoa jino kama tiba ya ugonjwa wa jino, ni pale tu ambapo jino hilo haliwezi tibika kwa njia mbadala kama hii ya mzizi wa jino au pale inapobainika kuwa jino husika kuendelea kubaki pale hata likiwa limetibika linaweza kuwa chanzo cha kuleta madhara makubwa mwilini kama uoto mpya n.k.

Mafua ya Ndege

Huu ni ugonjwa unaoathiri zaidi ndege wa jamii mbalimbali. Hata hivyo virusi wanaosababisha ugonjwa huu, wana uwezo wa kujibadilisha umbo na tabia zake (mutation) na kisha kumuathiri mwanadamu. Mabadiliko haya ya kimaumbile na kitabia husababisha kutokea kwa milipuko (epidemic) ya mafua ya ndege sehemu mbalimbali duniani hali ambayo isipothibitiwa inaweza kusambaa na kuathiri sehemu kubwa ya dunia kwa wakati mmoja (pandemic).

Visababishi vya mafua ya ndege
Mafua ya ndege husababishwa na jamii ya virus wajulikanao kama Avian Influenza virus. Virusi vya kwanza kabisa kumuathiri binadamu na kumsababishia mafua ya ndege vilihusishwa na kuku na viligunduliwa mwaka 1997 huko nchini Hong Kong na kupewa jina la avian influenza A (H5N1). Huu ulikuwa ni mlipuko wa kwanza wa ugonjwa huu kuwahi kuripotiwa. Kuna matukio machache sana ya maambukizi kutoka kwa binadamu kwenda binadamu yaliyowahi kuripotiwa mpaka sasa.

Influenza virus ni nini?
Kuna aina kuu tatu za virusi wa influenza, A, B na C. Mafua ya ndege husababishwa na jamii ya influenza A ambao wana uwezo wa kuingia na kuishi katika seli za ndege. Umbo la kinasaba la virusi hawa wa influenza A limeundwa na kamba nane za protein aina ya RNA. Aidha virus wa Influenza wanaweza pia kuainishwa kulingana na aina ya protein inayounda maumbo yao. Protini hizo zipo katika aina mbili nazo ni hemagglutinin (H) pamoja na neuraminidase (N). Protini hizi zina kazi mbalimbali katika umbo la virusi. Kadhalika protini hizi nao pia zimeganyika katika aina mbali, ambapo virusi hatari wa mafua ya ndege wanaundwa na aina ya 5 ya protin ya hemagglutinin na aina ya 1 ya protini ya neuraminidase na hivyo ndiyo maana hujulikana kama H5N1 influenza A virus.

Wapo virusi wa influenza ambao huishi katika mwili wa binadamu tu, hawa hujulikana kama human influenza; na wapo wengine ambao huishi katika miili ya wanyama kama vile nguruwe, chui, na hata paka. Hata hivyo wakati fulani, muingiliano kati ya virusi hawa na wenyeji wao yaani waathirika hutokea.

Ukubwa wa tatizo
Tangu hapo, matukio kadhaa ya milipuko ya ugonjwa wa mafua ya ndege kwa binadamu inayohusishwa na virusi wa avian influenza A (H5N1) yamepata kuripotiwa katika sehemu kadhaa za mabara ya Asia, Afrika, Ulaya na pia nchi za Vietnam, Indonesia, na maeneo kadhaa ya Mashariki ya mbali. Mamia ya watu wameripotiwa kufa kutokana na milipuko hiyo ambapo inakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 60 ya watu wote waliopatwa na ugonjwa huu walifariki dunia.

Vihatarishi vya ugonjwa wa mafua ya ndege
Kadiri jinsi virusi wa mafua ya ndege wanavyosambaa ndivyo uwezekano wa kutokea kwa milipuko ya ugonjwa huu inayoathiri binadamu sehemu mbalimbali duniani unavyokuwa mkubwa. Watafiti wameonesha kuwepo kwa hatari ya kutokea kwa mlipuko mkubwa (pandemic) unaoweza kusababishwa na kusambaa kwa virusi hawa duniani.

Watu walio katika hatari ya kukumbwa na ugonjwa wa mafua ya ndege ni pamoja na:
• Wakulima na wale wanaojishughulisha na ufugaji wa jamii mbalimbali za ndege
• Wasafiri wanaotembelea maeneo yaliyokumbwa na mlipuko
• Yeyote anayegusa ndege aliyeathirika na mafua ya ndege
• Mtu anayekula nyama
ya ndege aliyeambukizwa virusi wa avian influenza ikiwa mbichi au isiyoiva vizuri au kula mayai au damu za ndege wenye virusi hao
• Aidha, watoa huduma za afya pamoja na ndugu za wagonjwa wenye ugonjwa huu nao pia wapo katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya mafua ya ndege.

Imeonekana kuwa virusi wa avian flu virus (H5N1) wana uwezo mkubwa wa kuishi katika mazingira kwa muda mrefu bila kuathirika. Katika hali hii, maambukizi yanaweza pia kusababishwa na mtu kugusa maeneo walipo virusi hawa.

Ndege walioambukizwa ugonjwa huu huendelea kutoa virusi kupitia katika vinyesi vyao au mate yao kwa muda wa mpaka siku kumi tangu waambukizwe.

Dalili za mafua ya ndege
Dalili za mafua ya ndege kwa binadamu hutegemeana na aina ya virusi waliomshambulia muhusika. Dalili pia zinaweza kuanza kujitokeza siku saba mpaka kumi tangu mtu anapopatwa na maambukizi ya virusi wa H5N1.
Maambukizi yanayosababishwa na virusi vya jamii ya H5N1 kwa binadamu husababisha mgonjwa kuwa na dalili zote za mafua makali kama vile
• kukohoa (kikohozi kikavu au wakati mwingine kinachotoa makohozi),
• kuharisha sana,
• kutapika
• kichefuchefu
• kupumua kwa shida, (Acute Respiratory Distress Syndrome)
• homa zaidi ya nyuzijoto 38 centigrade,
• kuumwa na kichwa,
• kujihisi uchovu wa mwili,
• maumivu ya misuli ya mwili mzima,
• kutokwa na makamasi mepesi yanayotiririka bila ukomo na
• kuwashwa na koo.

Vipimo na uchunguzi
Kabla daktari hajaagiza kufanyika kwa vipimo, anaweza kwanza kutaka kujua historia ya mgonjwa ili kufahamu dalili zinazomsumbua. Kisha atamchunguza mgonjwa kwa kumpima kifua (kusikiliza sauti za hewa zinazoingia na kutoka katika mfumo wa njia ya hewa), kumpima joto la mwili, na pia kuchunguza pua na koo.

Baada ya uchunguzi wa mwili, daktari anaweza kuagiza vipimo vifuatavyo kufanyika.

  • X-ray ya kifua ili kuchunguza iwapo kuna athari zozote katika mapafu,
  • kuchukua sehemu ya makamasi na makohozi kutoka kwenye koo na pua yaani nasopharyngeal culture na kuotesha maabara ili kufahamu aina ya virusi na bakteria wanaomsumbua mgonjwa
  • kipimo cha damu yaani Full Blood Picture mkazo ukiwekwa kwenye kuangalia chmbe nyeupe za damu kama zipo sawa au zimeongezeka,
  • vipimo vya utendaji kazi wa mafigo, ini pamoja na moyo pia ni muhimu kufanyika.

Ingawa vipimo vya kutambua virusi wa mafua ya ndege kama vile PCR vipo, lakini havijasambaa sehemu nyingi duniani. Hata hivyo, vipimo hivi hutumia muda mfupi sana (chini ya saa tano) kutoa majibu ya kutambua jamii ya virusi inayomuathiri mgonjwa na hivyo kumuwia urahisi tabibu kushughulika navyo.

Matibabu
Kama tulivyoona hapo juu kuwa, jamii mbalimbali za virusi wa avian flu huweza kusababisha dalili tofauti tofauti. Hivyo basi hata matibabu pia yaweza kutofautiana kati ya mgonjwa na mgonjwa.

Kwa ujumla, iwapo ndani ya saa 48 tangu kujitokeza kwa dalili, mgonjwa atapatiwa dawa za kuua virusi za aina ya zanamir au oseltamivir kuna uwezekano mkubwa wa kupunguza makali ya ugonjwa na hivyo kuongeza uwezekano wa mgonjwa kupona.

Pia ndugu na jamaa wanaoishi nyumba moja na mgonjwa wanaweza kupewa dawa ya Oseltamivir ili kuwakinga wasipatwe na maambukizi ya virusi hawa, na iwapo watakuwa wameambukizwa, kuwaua kabla hawajasambaa zaidi mwilini.

Dawa za amantadine na rimantadine ambazo hutumiwa mara kwa mara kwa ajili ya kutibu maambukizi ya aina mbalimbali za virusi imeonekana kuwa hayana uwezo wa kuua virusi wanaosababisha mafua ya ndege na hivyo inshauriwa kutoyatumia pindi mlipuko wa mafua ya ndege unapotokea.

Baadhi ya wagonjwa wanaweza kuwa na hali mbaya sana kuliko wengine. Wapo ambao hufikia hatua ya kushindwa kupumua wenyewe. Wagonjwa wa namna hii hawana budi kulazwa katika vyumba vya uangalizi maalum na kusaidiwa kupumua kwa kutumia mashine. Aidha inashauriwa sana na wataalamu wa magonjwa ya mlipuko kuwatenga wagonjwa wote wa mafua ya ndege katika sehemu maalum ili kuzuia kusambaa zaidi kwa ugonjwa huu.

Chanjo dhidi ya mafua ya ndege
Watafiti wamefanikiwa kutengeneza chanjo dhidi ya virusi wanaosambaza ugonjwa wa mafua ya ndege. Chanjo hiyo ambayo imethibitishwa na mamlaka mbalimbali za madawa duniani imetengenezwa kwa lengo la kumkinga binadamu dhidi ya maambukizi ya mafua ya ndege na inaweza kutumika iwapo virusi wa H5N1 atabdilika tabia na kuanza kusambaa kutoka kwa binadamu kwenda kwa binadamu mwingine.

Kadhalika, wataalamu wanashauri sana watu kupata chanjo dhidi ya virusi wa influenza (wale wanaosababisha mafua ya kawaida kwa binadamu) ili kupunguza uwezekano wa virusi wa mafua ya ndege kujichanganya na virusi wa mafua ya kawaida (yaani human influenza) na kuzaa virusi wapya ambao wanaweza kuwa na uwezo wa kusambaa kwa urahisi zaidi na kuwa hatari zaidi kuliko hawa waliopo sasa.

Matarajio
Matokeo ya ugonjwa hutegemea sana ukali wa maambukizi pamoja na aina ya virusi waliomshambulia mgonjwa. Ikumbukwe kuwa karibu nusu ya wagonjwa wanaopatwa na mafua ya ndege hufariki.

Madhara
Madhara ya ugonjwa wa mafua ya ndege ni pamoja na
• Kupata shida wakati wa kupumua (Acute Respiratory Distress)
• Kushindwa kufanya kazi kwa viungo mbalimbali vya mwili (multi-organs failure)
• Homa ya mapafu
• Maambukizi katika damu (septicemia)

Kinga
Inashauriwa sana kuepuka njia zote ambazo zinaweza kukufanya upate maambukizi ya ugonjwa huu. Njia hizo ni pamoja na
• Kwa wasafiri, ni muhimu kuepuka kutembelea maeneo wanapouzwa au kufungwa ndege hususani sehemu zilizoripotiwa au kuhisiwa kuwa na milipuko ya ugonjwa huu
• Wafugaji wa ndege wanaohisiwa kuwa na virusi vya mafua ya ndege wanapaswa kuvaa vifaa maalum vya kujikinga ili wasipatwe na maambukizi
• Nawa mikono kwa sabuni mara baada ya kushika ndege au mazao ya ndege wenye maambukizi
• Inashauriwa kuepuka kula nyama mbichi au isiyoiva vizuri ya ndege (kuku, bata, njiwa) ili kupunguza uwezekano wa maambukizi
• Iwapo utaamua kupika nyama ya ndege, hakikisha unaipika katika nyuzijoto si chini ya 165 Farenheit
• Epuka kugusa ndege au mazao ya ndege (vinyesi, damu, mayai) wanaohisiwa kuwa na virusi vya H5N1
• Nenda hospitali haraka iwapo utajihisi kuwa na dalili za mafua ya ndege (kama zilivyotajwa hapo juu) ndani ya siku kumi baada ya kushika ndege au mazao ya ndege wanaohisiwa kuwa na virusi vya H5N1 au iwapo ulisafiri kwenda eneo lenye mlipuko wa mafua ya ndege.
• Epuka kunywa dawa za kuua virusi wa mafua ya ndege bila kupata ushauri wa daktari.