Showing posts with label afya. Show all posts
Showing posts with label afya. Show all posts

Sunday, March 18, 2012

Kutoga Ulimi ama Mdomo

mouth piercing
tongue piercing
Katika zama hizi za utandawazi na muingiliano baina ya tamaduni zetu za asili na tamaduni za kimagharibi, imekuwa ni kawaida kwa vijana wa rika tofauti na jinsia zote kutoga ulimi, mdomo, kitovu ama kivimbe cha nyusi kwa sababu tofauti tofauti sana.

Hivyo basi, ni muhimu sana kufahama ukweli kuhusu faida ama hasara za kutoga ulimi ama mdomo kabla hujatekeleza azma yako ya kutoga viungo hivi vya mwili.

Kutoga Ulimi ama Mdomo kunaweza kukusababishia madhara yasiyotarajiwa

Matokeo mazuri zaidi ya kutoga ulimi ama mdomo ni kutokutokea kwa kidonda ama kivimbe, wakati matokeo mabaya kutokea kwa baadhi ya watu ni pamoja na kuvunjika kwa meno/jino, kuvuja kiasi kikubwa cha damu, ama maambukuzi ya bakteria kwenye kidonda. Kutoga ulimi hujumuisha kutumika kwa sindano inayopenyezwa katikati ulimi ili kupitisha na kuhifadhi kipini, ama ndoana ama hereni ya urembo. Kazi hii ya kutoga ulimi mara nyingi ganzi huwa haitumiki. Baada ya kutoga, kuvimba kwa ulimi na maumivu ya muda hutokea.

Madhara ya kutoga Ulimi

  • Kuvuja damu kiasi kidogo hutarajiwa, kuna hatari ya mishipa ya damu kuharibiwa wakati wa kutoga ulimi, hali inayoweza kusababisha kuvuja damu kwa kiasi kikubwa kuliko ilivyotarajiwa.
  • Ingawa kuvimba kwa ulimi kunatarajiwa baada ya kitendo cha kutoga ulimi, wakati mwingine ulimi huvimba kwa kiasi cha kuziba kwa njia ya hewa. Kuziba kwa njia ya hewa kunaweza kusababisha kifo.
  • Ikiwa fundi wako wa kutoga ulimi hana uzoefu wa kutosha kufanya kazi hiyo, anaweza kuharibu mishipa ya fahamu ya ulimi hivyo kuharibu uwezo wa ulimi kuhisi/kutambua hisia za joto,baridi ama ladha ya chakula na vinyaji, vile vile kuathiri mienendo ya viungo vya eneo la kinywa na uso. Kwani nyuma ya ulimi kuna mishipa ya fahamu,mishipa hii ikiharibiwa ulimi utapooza hivyo kusababisha ganzi la kudumu, kuathirika kwa uwezo kuongea na kushindwa kutambua ladha za chakula/vinywaji
  • Vilevile kutoga ulimi kunakuweka kwenye hatari ya kupata maambukizi kwenye ulimi hasa ikiwa hutaweza kutunza hali ya usafi wa kinywa na meno kila wakati, hivyo kusababisha wadudu jamii ya bakteria kupenya na kuingia ndani ya ulimi na kusababisha maambuzi kwenye ulimi.
  • Hali ya kutoga ulimi inapodumu kwa muda mrefu, inaweza kusababisha nyufa kwenye meno, ama kuvunjika kwa nyuso za jino/meno kwa sababu ya msuguano wa muda mrefu kati ya jino/meno na hereni/kipini ama ndoana ya chuma/plastiki iliyohifadhiwa kwenye ulimi kwa muda mrefu. Nyufa hizi kwenye meno, kwa kawaida husababisha maumivu makali ya jino/meno. Hivyo basi meno haya yenye nyufa yanaweza kutibiwa kwa kuvalishwa kofia “ dental crown”. Si kawaida kupata magonjwa ya fizi ama kuta za ndani za shavu ikiwa umetoga ulimi na unatunza afya ya kinywa na meno vizuri.

Kutoga Mdomo

Kutoga mdomo ni pale pete ya urembo inapovalishwa ama kuhifadhiwa ndani ya mdomo. Majeraha ya kutoga mdomo hupona haraka zaidi, hata hivyo unapaswa kutunza kidonda cha jeraha hili kwa umakini

mkubwa wakati wa kupona. Vyakula, vinywaji na moshi wa sigara vinapofikia kidonda hiki, vinaongeza hatari ya kupata maambukizi kwenye kidonda.

Kishikizo vishikizo vya pete hii ya urembo kinaweza kusababisha vidonda kwenye fizi ama kuharibu jino. Kwa baadhi ya watu, tiba ya kupandikiza fizi hutumika kurejesha fizi zilizoathirika. Kama ilivyo kwa kutoga ulimi, kutoga mdomo pia kunaweza kuathiri mshipa wa fahamu hivyo kuathiri mienendo ya misuli ya kwenye eneo la kinywa na mdomo.

Je, una mpango wa kutoga Ulimi ama Mdomo?

Ikiwa unapanga kutoga viungo hivi vya mwili, unashauriwa ufanye mambo yafuatayo yatakayo kuwezesha kupata huduma ambayo haita athiri afya yako:

  • Hakikisha ngariba mtoga ulimi ama mdomo sio tu ana uzoefu wa kutosha kwenye kazi anayofanya, bali pia anazingatia usafi kufanya kazi zake.
  • Nenda hospitali kupata ushauri tiba mara tu unapoona ama maumivu ni makali sana, kuvimba kwa ulimi ama damu zinavuja kwa muda mrefu (zaidi ya dakika 30) ama ikiwa jeraha linapata maambukizi ya bakteria.
  • Unapokuwa na hereni, pete ama ndoana ya urembo kwenye ulimi ama mdomoni, unashauriwa kumwona daktari wa kinywa na meno kila baada ya miezi sita (6). Daktari wa meno atafanya kazi ya kuhakiki ikiwa kidude kilichovalishwa kina madhara kwenye meno ama fizi, hivyo kudhibiti athari zinazoweza kutokea kwa kutoga ulimi ama mdomo.
  • Wana michezo wanashauriwa kutovaa hereni, pete ama ndoana ya urembo iliyopo kwenye ulimi ama mdomoni wanapokuwa mchezoni, kwani vyombo hivi vya urembo vinaweza kunasa kwenye ngozi bila kutarajia hivyo kusababisha madhara yasiyotarajiwa.

Dalili na Ishara za Ujauzito

Mstari wima mweusi hutokea tumboni kuanzia chini ya kitovu

Dalili za ujauzito hutofautiana kati ya mwanamke na mwanamke, ingawa kuchelewa au kukosa hedhi ni dalili moja muhimu sana

Ni muhimu kuzitambua na kuzifahamu dalili hizi kwa sababu zinaweza kusaidia kuelezea au kutofautisha matatizo mengine mbali ya ujauzito.

Hebu sasa tuangalie dalili na ishara za Ujauzito:

  • Kutokwa damu kidogo ukeni wakati kiumbe kikipandikizwa kwenye mfuko wa uzazi, ingawa siyo wanawake wote hupatwa na dalili hii
  • Kukosa hedhi, hii ni moja ya dalili kubwa za ujauzito
  • Maumivu ya matiti na kuvimba matiti (huweza kutokea kati ya wiki ya 1 hadi ya 2)
  • Uchovu, wanawake wengi hujihisi uchovu na hali ya kutopenda kufanya lolote.
  • Kupoteza ladha au kuhisi ladha ya chuma mdomoni
  • Kuongezeka kwa hisia ya harufu, kipindi cha ujauzito wanawake wengi huongezeka hisia ya harufu
  • Kichefuchefu na kutapika
  • Maumivu ya kichwa
  • Kizunguzungu
  • Kukojoa mara kwa mara (hasa kati ya wiki 6-8)
  • Kubadilika rangi kwa ngozi inayozunguka chuchu kuwa nyeusi
  • Kutamani baadhi ya vyakula na kuchukia vingine
  • Kupanuka kwa mfuko wa uzazi
  • Tumbo kujaa au kuvimbiwa
  • Kununa na kukasirika haraka
  • Kiungulila au kupata choo kigumu
  • Kolostramu kuanza kutoka kwenye matiti
  • Kuongezeka uzito
  • Kuweza kupapasa mtoto (palpation of the baby)
  • Kulainika na kuvimba kwa shingo ya uzazi (Hegars sign) - kuanzia wiki ya 6
  • Shingo ya uzazi kubadilika rangi kuwa ya samawati kutokana na msongamano wa damu katika mishipa ya vena. Ishara hii huitwa pia Chadwick's sign

Dalili nyingine ni pamoja na

  • Mstari wima mweusi hutokea tumboni kuanzia chini ya kitovu (linea nigra)
  • Mama kuhisi mtoto akicheza (kuanzia wiki ya 20)
  • Maumivu ya mgongo hasa mimba ikishakuwa kubwa.
  • Kipimo cha mimba kuwa chanya (positive).
  • Kusikia mapigo ya moyo ya mtoto
  • Mtoto kuonekana kwenye kipimo cha ultrasound

Korodani Bandia Kutengeneza Shahawa

shahawa
Wanasayansi nchini Marekani wako mbioni kutengeneza korodani bandia (artificial testicle) zitakazokuwa zikitengeneza shahawa ili kusaidia wanaume wenye matatizo ya uzazi.

Timu ya wanasayansi katika jimbo la San Fransisco nchini Marekani chini ya Dk Paul Turek wamepewa ruhusa ya kuendelea na utafiti huu baada ya kuahidiwa kupewa pesa za kutosha kutekeleza mradi huu.

Kwa muda mrefu, wanasayansi wamejaribu kutengeneza seli za shahawa (Sperm Cells) bila mafanikio kwa vile wamefanikiwa kutengeneza robo tatu tu ya mchakato wa kupata shahawa kamili. Hii inatokana na mazingira maalum yanayopatikana katika korodani kuhitajika kukamilisha utengenezaji wa shahawa hizo. Mazingira hayo ya uhalisia ni tofauti na mazingira yoyote yale ya nje katika utengenezaji shahawa.
Korodani hizo zitakuwa katika umbo la duara (cylindrical shape) na zitakuwa na urefu wa inchi kadhaa na hazitahitaji kupachikwa kwenye mwili wa binadamu. Aidha kifaa hiki kitakuwa tofauti na korodani nyingine bandia ambazo huwekewa wanaume waliokosa korodani moja kutokana na sababu mbalimbali.Kwa kawaida korodani za namna hii huwa hazitengenezi shahawa kwa vile hujazwa maji maalum ya saline solution ili kutumika kama mapambo.
Ili kufanikisha hili, wanasayansi hao itabidi kubuni utaalamu wa kutengeneza chembechembe za shahawa na wamepanga kutumia seli za asili (human embryonic stem cells) zilizoongezewa jena (genes) ili kuzifanya kuwa seli zinazoweza kuzaa chembechembe za shahawa na hivyo kutumika katika njia za kutungisha mimba kwenye maabara zinazojulikana kama In Vitro Fertilization (IVF)
Wakati tafiti zimeonesha ya kwamba inawezekana kutibu panya dume mwenye matatizo ya uzazi kutoka katika seli zao za asili yaani embryonic stem cells, kwa binadamu tafiti hizi zimeshindwa kuzaa matunda yoyote yale mpaka sasa.
Kyle Orwig, Profesa wa masuala ya uzazi na magonjwa ya wanawake (Obstetrics and Gynecology) na sayansi ya uzazi (Reproductive Sciences) anasema “Ni mradi wa matumaini sana lakini nina wasiwasi kama utafanikiwa, ukifanikiwa itakuwa ni mafanikio makubwa sana katika sayansi ya tiba ya uzazi.” Kwa kawaida, shahawa hutengenezwa na kuhifadhiwa katika korodani za mwanaume.
Matatizo ya kushindwa kutungisha mimba kwa wanaume hutokana na hitilafu katika mfumo wa uzalishaji shahawa kwenye korodani unaosababishwa na magonjwa ya cystic fibrosis, matatizo ya jena (genetic defects), korodani ambazo hazijashuka katika sehemu sahihi (undescended testis), madhara katika korodani kama ajali na saratani ya kwenye korodani.

Kukosa Usingizi Husababisha Upungufu wa Homoni ya Testosterone

Kukosa Usingizi
Mnamo mwaka 2007, watafiti nchini Marekani walifanikiwa kutoa ripoti inayojaribu kuhusisha ukosefu wa usingizi na upungufu wa homoni ya testosterone miongoni mwa wanaume watu wazima.

Kwa kawaida kiwango cha homoni ya testosterone hupungua kadiri mwanaume anavyozidi kuwa mtu mzima, na kwa baadhi ya wanaume, kupungua huku kwa testosterone huweza kusababisha ulegevu wa mwili, kukosa hamu ya ngono na hata kuvunjika mifupa ya mwili.

Watafiti wanasema kuwa, wapo baadhi ya wanaume walio kwenye miaka 80 bado huweza kuwa na kiwango cha juu cha testosterone sawa na kile kinachopatikana kwa wanaume vijana. Hata hivyo sababu kubwa inayofanya kuwepo na utofauti katika viwango vya testosterone miongoni mwa rika hizo mbili bado hazieleweki sawasawa, ingawa watafiti wanasema kuwa ukosefu wa usingizi miongoni mwa watu wazima na wazee unaweza kuwa chanzo kimojawapo cha kuwepo kwa hali hiyo.

"Matokeo ya utafiti wetu yanaongeza uwezekano kuwa wanaume watu wazima na wazee ambao hupata muda mfupi sana wa kulala nyakati za usiku huwa na kiwango kidogo sana cha homoni ya testosterone wakati wa asubuhi," anasema mtafiti Plamen Penev, wa kutoka Chuo Kikuu cha Chicago, nchini Marekani.

Wakati wa utafiti, wataalamu waliofanya uchunguzi huo walipima kiwango cha homoni ya testosterone katika damu kila asubuhi cha wanaume watu wazima wenye umri kati ya miaka 64 na 74 waliojitolea kushiriki kwenye utafiti huo. Aidha, mtindo wao wa kulala pamoja na kupata usingizi pia vilichunguzwa kila siku kwa muda wa wiki nzima.

Matokeo ya uchunguzi huo yalionesha kuwa kiasi cha usingizi walicholala kilikuwa na uhusiano wa karibu sana na kiwango cha testosterone katika damu wakati wa asubuhi. Wale waliopata usingizi mzuri na kwa muda mrefu (walau saa nane) walikuwa na kiwango kikubwa cha testosterone wakati wale waliopata usingizi wa kubabaisha (saa nne) walikutwa na kiwango cha chini cha homoni hiyo. Wastani wa muda wa kulala ulikuwa masaa sita.

"Pamoja na kwamba matokeo ya utafiti huu yanaonesha kuwa urefu wa muda wa kulala wa mtu waweza kuwa kiashiria cha mabadiliko ya homoni katika mwili yanayohusiana na umri, matokeo ya utafiti huu yanatoa tu picha ya nini kinachotokea mwilini kama mtu asipopata usingizi wa kutosha. Hata hivyo, tafiti zaidi zinahitajika ili kuthibitisha umuhimu wa uhusiano kati ya usingizi na mabadiliko ya homoni katika mwili," anasema Dr. Penev.

Wataalamu wa masuala ya afya ya usingizi wanashauri watu wazima kupata wastani wa angalau saa saba mpaka nane za kulala kila usiku ili kuwa na afya bora. Ripoti kamili ya matokeo ya utafiti huu inapatikana katika toleo la mwezi April, 2007 la jarida la afya la Sleep.

Msongo wa mawazo kipindi cha ujauzito husababisha ulemavu kwa mtoto

stress in pregnant women

Watafiti wa magonjwa wanadai kuwa msongo mkali wa mawazo wakati wa ujauzito unaweza kusababisha hitilafu katika uumbaji wa mtoto na hatimaye mtoto kuzaliwa akiwa mlemavu.

Ripoti ya watafiti hao inazidi kuthibitisha matokeo ya tafiti zilizopita kuwa mama mwenye msongo wa mawazo wakati wa ujauzito kutokana na mambo kama kufukuzwa au kuachishwa kazi, kutengana na mwenza wake au kufiwa ana hatari ya kuzaa mtoto mwenye ulemavu kama vile midomo sungura (cleft lip na cleft palate) au matatizo kwenye uti wa mgongo (spina bifida).

Jopo la watafiti wa kidenmark likiongozwa na Dr Dorthe Hansen walifanya uchunguzi ili kuthibiitisha ukweli na uhakika wa dhana hii.

Wakitumia rikodi za taarifa za kitabibu za kipindi cha miaka 12 kutoka 1980 mpaka 1992 kutoka masjala ya Taifa ya kitabibu, watafiti hao waliweza kuwatambua wajawazito wote waliokumbwa na matatizo makubwa ya kimaisha wakati wa ujauzito na hata miezi 16 kabla ya kupata ujauzito. Matatizo makubwa ya kimaisha yaliyochunguzwa yalikuwa kukumbwa na msiba wa ndugu au jamaa wa karibu, ndugu au jamaa wa karibu kulazwa hospitali kwa mara ya kwanza baada ya kugundulika kuwa na kansa ya aina yeyote au ndugu au jamaa wa karibu kupatwa na ugonjwa wa mshtuko wa moyo. Mambo haya yalichunguzwa kwa kigezo kuwa, mjamzito yeyote aliyewahi kukumbana nayo ana hatari kubwa ya kuwa katika msongo wa mawazo bila kujali tabia yake, kama ana watu wa kumfariji au uwezo wake wa kukabiliana nayo.

Jopo hilo lilichunguza maendeleo ya mimba kwa wajawazito 3,560 ambao walikumbana na matukio hayo kwa kulinganisha na wajawazito wengine 20,299 ambao hawakukumbana na hali yeyote ambayo ingewasababishia kupata msongo wa mawazo wakati waujauzito.

Matokeo ya uchunguzi wao yalionesha kuwa ulemavu na hitilafu za viungo kwa watoto waliozaliwa ulikuwa mara mbili miongoni mwa kundi la wajawazito waliokumbwa na msongo mkali wa mawazo ikilinganishwa na kundi la kinamama ambao hawakuwa na hali hiyo.

Kadhalika ilionekana kuwa wanawake waliowahi kukumbwa na hali kama hiyo katika ujauzito mbili mfululizo za nyuma walikuwa katika hatari kubwa zaidi ya kuzaa watoto wenye ulemavu wa viungo tofauti na wale waliowahi kupatwa na hali hiyo mara moja tu au wale ambao hawakupatwa kabisa.

Ilionekana pia kuwa tukio lililoongeza uwezekano wa mtoto kuzaliwa akiwa na ulemavu wa viungo ilikuwa ni iwapo mjamzito atafiwa na mtoto wake mwingine mkubwa wakati akiwa katika miezi mitatu ya mwanzo wa ujauzito wake huu wa sasa. Hatari ya kuzaa mtoto mlemavu iliongezeka iwapo kifo cha mtoto huyo mkubwa kingetokea bila kutarajiwa kwa mfano kwa ajali.

Watafiti wanasema kwamba, msongo mkali wa mawazo huchangia kuathiri uumbaji wa mtoto aliye tumboni kwa kusisimua uzalishaji wa homoni ya cortisone. Homoni hii husababisha ongezeko la kiwango cha sukari katika damu na upungufu wa usambazaji wa hewa safi ya oksijeni kwa mtoto, mambo ambayo husababisha kutokea kwa hitilafu katika uumbaji wa viungo vya mtoto hatimaye kusababisha ulemavu wa viungo vya mtoto.

Uwezekano mwingine ni kuwa msongo mkali wa mawazo humchochea mama mjamzito kutumia zaidi vileo vyenye alcohol na pia kula lishe duni hali ambayo huongeza madhara zaidi kwa kiumbe kilicho tumboni.

Hata hivyo Professor Peter Hepper wa Chuo Kikuu cha Queen's cha Belfast, anasema hakushangazwa na mtokeo ya utafiti huo.

Anasema kuwa, "tunafahamu msongo wa mawazo husababisha mabadiliko ya kifiziolojia katika mfumo wa mwili wa mjamzito, na hivyo hakuna sababu kwanini mabadiliko hayo yasimfikie pia mtoto aliye tumboni kupitia kondo la nyuma na kumuathiri. Matokeo haya yanazidi kuthibitisha kile tulichokuwa tukikifahamu tangu awali kuwa msongo wa mawazo wa muda mrefu kwa mwanamke una madhara makubwa kwa mendeleo ya uumbaji wa mtoto aliye tumboni na hivyo basi hakuna budi kufanyike kila njia kuwasaidia wajawazito walio katika hali hii ili waweze kujifungua watoto walio na afya njema na salama."

Unene Uliopitiliza (Obesity)

Unene Uliopitiliza (Obesity)
Tatizo la Unene Uliopitiliza (Obesity)

Tatizo hili la unene uliopitiliza kuliko inavyohitajika kiafya huwa linaletwa na kuongezeka kwa kiwango cha mafuta mwilini. Njia rahisi na inayokubalika ya kuweza kugundua kama mtu ni mnene kupita kiasi (obese) inafahamika kama kipimo cha Body Mass Index (BMI). Vipimo hivi vya BMI ndio vinaweza kukujulisha kama unene ulionao unastahili kulingana na umri, urefu na uzito wako. Vipimo hivi ni kama ifuatavyo:

Jinsi ya kupima BMI yako

Kanuni ya BMI hutumia uzito wa mtu pamoja na urefu wake. Uzito wa mtu hupimwa katika kilograms (kg) na urefu wake katika mita (m) au sentimita (cm). Ikumbukwe pia kuwa mita moja ni sawa na sentimita 100 na mita² = mita x mita.

Category BMI range – kg/m2
Emaciation less than 14.9
Underweight from 15 to 18.4
Normal from 18.5 to 22.9
Overweight from 23 to 27.5
Obese from 27.6 to 40
Morbidly Obese greater than 40

BMI (kg/m2) = Uzito katika kilograms/Urefu katika meters². Maana yake ni kwamba ili kuweza kupata BMI itakayokuwezesha kujifahamu kama u mnene ama la, chukua uzito wako gawa kwa kipeo cha pili cha urefu wako.

Tatizo la unene uliopitiliza husababishwa na nini ?

Kuna mambo kadhaa yanayoweza kusababisha unene uliopitiliza. Mambo hayo ni pamoja na

  • Vyakula vya mafuta - Ulaji wa vyakula venye mafuta mengi au calories nyingi.
  • Kutofanya mazoezi - Wale wasiofanya mazoezi mara kwa mara huwa wanene tofauti na wale wanaofanya mazoezi.
  • Kurithi viashiria vya asili (genes) - Viashiria hivi vinaweza kuwa moja ya vichocheo vya kuongeza uzito kwani ndivyo huamua wapi mafuta huhifadhiwa mwilini na kwa kiwango gani. Lakini haimanishi kuwa mtu akiwa navyo basi ndio atakumbwa na tatizo hili.
  • Umri - Watu wengi huongezeka uzito au hunenepa kadri umri unavyoongezeka kwa sababu wanakuwa hawajishughulishi sana (less active) na huwa wanapungua maumbile ya miili yao (muscles mass)
  • Matatizo ya kisaikolojia - Wakati mwengine watu wenye matatizo ya kisaikolojia au msongo wa mawazo (stress) huwa na tabia ya kula sana, matokeo yake ni kunenepa.
  • Dawa - Baadhi ya dawa zenye madhara ya kuongeza unene ni kama corticosteroids, blood pressure medications, tricyclic medications na kadhalika.
  • Matatizo ya afya - Baadhi ya magonjwa yanachangia kuongezeka kwa uzito au kenenepa kama cushings syndrome, hypothyroidism, osteoarthritis na kadhalika

Vihatarishi vya tatizo la unene wa kupitiliza

Aidha yapo mambo kadhaa ambayo yanaweza kumuhatarisha mtu kupata unene wa kupitiliza. Mambo haya ni pamoja na

  • Kukua kwa uchumi wa nchi - Wananchi wengi wanaoishi kwenye nchi zilizoendelea au wenye kipato kikubwa ndio wanaopata tatizo hili kutokana na kuishi mfumo wa maisha ya kivivu na hali ya kutokufanya mazoezi (sedentary lifestyle).
  • Historia ya kuongezeka uzito uliopitiliza kwenye familia nayo yaweza kuhatarisha mtu kupata tatizo hili. Aidha, si jambo la kushangaza kuona karibu familia nzima au wengi wa wanafamilia kuwa wanene kupitiliza.
  • Kutojishughulisha na chochote (inactive).
  • Kupenda kula sana kuliko kawaida (overeating).
  • Kula vyakula vya mafuta mengi
  • Kutumia dawa zenye madhara ya kuongeza uzito uliopitiliza.
  • Kuwa na ugonjwa wa vichocheo mwilini (hormonal disorders) kama cushing syndrome, hypothyroidism.
  • Kuwa na msongo wa mawazo au kuathirika kisaikolojia.

Magonjwa yanaoweza kuambatana na tatizo la unene uliopitiliza

  • Kisukari
  • Shinikizo la damu (hypertension)
  • Kiharusi (Stroke)
  • Magonjwa ya moyo
  • Tatizo la kutopumua vizuri wakati mtu yupo usingizini (Sleep apnea)
  • Vijiwe katika mfuko wa nyongo (Gallstones)
  • Kiwango cha juu cha lijamu kwenye damu (cholesterol ikiwemo triglycerides)
  • Ugonjwa wa mifupa kama yabisi (osteoarthritis).
  • Saratani ya matiti
  • Saratani ya tezi dume (prostate cancer)
  • Saratani ya utumbo mpana pamoja na maeneo ya haja kubwa (Colorectal cancer)
  • Matatizo ya mzunguko na mishipa ya damu kama vile kuvimba kwa vena za miguuni (varicose veins)

Tiba ya kuongezeka unene kupita kiasi

Tiba ya tatizo hili ni mhusika kujitambua ya kwamba ana tatizo na kuwa tayari kupunguza uzito. Mabadiliko ya tabia ya mhusika ni muhimu sana, mabidiliko haya yawe ndio mfumo wa maisha yake ya kila siku.

Kupungua uzito na kujilinda au kutunza uzito ulionao baada ya kupunguza uzito ni jambo la msingi sana na inahusisha mazoezi, chakula na madiliko ya tabia ya mtu.

  • Mabadiliko ya tabia - Hii inahusisha muhusika kupunguza kiwango cha chakula anachokula lakini kiwe chenye virutubisho vyote muhimu vya afya na kuongeza kiwango cha ufanyaji mazoezi.
  • Mazoezi - Mazoezi husaidia kupunguza uzito hasa kipindi cha miezi sita ya mwanzo na hutunza uzito uliokusudiwa kwa muda mrefu. Pia hupunguza mafuta ya mwilini, huongeza ufanisi wa moyo, hupunguza tatizo la shinikizo la damu (hypertension), na kuweka sukari katika kiwango kinachohitajika mwilini.

Kama hujazoea kufanya mazoezi ni vizuri uanze taratibu na ujiwekee lengo kwa kufanya mazoezi kwa muda wa nusu saa kila siku, siku tano kwa wiki,(dakika 30 kila siku kwa siku tano kwa wiki). Mazoezi mazuri ni kama kuogelea, kuendesha baiskeli, kutembea, kunyanyua vitu vizito (visiwe vyenye uzito mkubwa), mazoezi ya viungo na kadhalika. Kama mtu ni mnene sana basi ni bora kuzungumza na daktari wako kabla ya kuanza mazoezi mapya. Baada ya kuanza mazoezi kwa mara ya kwanza, mwili utakuwa na maumivu, hii ni kawaida lakini kama mtu atapata maumivu zaidi ya masaa 2 baada ya kufanya mazoezi ni vizuri kumuona daktari.

  • Dawa - Zipo dawa nyingi za kupunguza uzito lakini ikumbukwe ya kwamba hakuna tiba ya tatizo hili na dawa hizi zina madhara mengi kama kuongeza shinikizo la damu (hypertension), matatizo ya moyo, kuharisha,msongo wa mawazo (depression) na mengineyo.
  • Chakula - Msingi wa kupunguza uzito au unene ni kujua ni kiwango gani cha calories mwili wako unahitaji kwa siku ili uwe unakula chakula ambacho hakitazidisha au kupunguza kiwango cha calories unazohitaji kwa siku. Mlo mzuri ni ule ulio na matunda kwa wingi, mboga za majani, nafaka ambazo hazijakobolewa, mafuta kidogo (less saturated fat). Vyakula vengine ni kama mayai, nyama isiokuwa ya mafuta (lean meat), samaki, kuku na vingineyo.
  • Tiba ya upasuaji - Kuna aina nyingi za upasuaji ambao unasaidia kupunguza uzito aina hizi ni kama gastric banding, gastric bypass (Roux-en-Y-procedure), liposuction. Kabla ya kufanyiwa upasuaji, muhusika atahitaji kupimwa kisaikolojia (psychological testing) na kupewa ushauri nasaha kwani tiba hii pia ina madhara yake.

Wanawake ambao wana uzito wa kupitiliza (obese women) wakiwa wajawazito wako kwenye hatari ya kupata madhara yafuatayo;

  • Kisukari cha mimba (Gestatitional diabetes) - kisukari hiki kinatokea wakati wa ujauzito na hupotea baada ya kujifungua mtoto.
  • Shinikizo la damu (hypertension)
  • Shinikizo la damu wakati wa ujauzito pamoja na kifafa cha mimba (pre-eclampsia & eclampsia)
  • Kuzaa kwa njia ya upasuaji (caesarean section)
  • Tatizo la kiumbe kutopata hewa vizuri wakati wa ujauzito (fetal distress)

Jinsi ya Kuandaa Chakula cha Mtoto

 Chakula cha Mtoto

Mtoto ale chakula muda gani?

Chai ya asubuhi: Saa 12:00 mpaka 2:00 kutegemeana na ni muda gani mtoto anakwenda shule. Jambo la muhimu ni kuwa, mzazi/mlezi ahakikishe mtoto anakula asubuhi ili asiende shle akiwa na njaa, ikibidi mzazi/mlezi amfungie mtoto chakula abebe.

Chakula cha mchana: Muda wa kati ya saa 5:30 mpaka saa 7:00 mchana.

Chakula cha jioni: Saa 10:00

Chakula cha usiku: Saa 1:00 usiku

Jinsi ya kuandaa chakula cha siku ya Jumatatu

Asubuhi: Kifungua kinywa (Breakfast)

Mlo 1: Chapati Maji Na Juisi Ya Chungwa

Mahitaji: 250 gram Unga wa ngano, 1 yai, 100 gram maziwa ya maji, 20 gram mafuta ya mahindi, 10 gram baking powder

Jinsi ya kuandaa chapati maji: Changanya vitu vyote katika bakuli kisha piga na mchapo mpaka upate mchanganyiko safi na laini kabisa. Iwapo mchanganyiko bado mzito ongeza maji kiasi.

Jinsi ya kuandaa juisi ya chungwa: Menya chungwa safi kabisa ili kuondoa uchungu wa gesi iliyopo katika maganda. Kisha tumia chombo maalumu cha kukamulia juice, kamua kisha hifadhi katika friji bila kuweka sukari ili ikae kwa muda bila kuharibika. Kumbuka pia kuweka sukari wakati wa kunywa.

Mlo 2: Uji wa Ulezi na Mtindi

Mahitaji: 200 gram unga wa ulezi, 100 gram maziwa ya maji, 350 gram maji, 100 gram mtindi usio na ladha ya matunda

Jinsi ya kuandaa uji wa ulzei na mtindi: Changanya unga wa ulezi na maziwa katika bakuli kisha chukua sufuria weka maji kiasi cha gram 350. Chemsha maji yakishachemka weka mchanganyiko wa maziwa na unga wa ulezi koroga mpaka uchemke na kuchanganyika safi kabisa ili uji wako usishike chini na kuungua. Acha uchemke vizuri kisha onja ukipata ladha ya kuiva kwa nafaka utakua tayari.

Toa jikoni weka katika bakuli litakalotumiwa na mtoto kisha changanya mtindi usio na ladha ya matunda pamoja na sukari tayari kwa mtoto kunywa.

Mchana: Chakula cha mchana

Mlo: Glass ya maziwa na mkate wa nyama za kusindika

Jinsi ya kuandaa: Mpatie mtoto 200 gram za maziwa sawa na glasi moja ya uvuguvugu au ya baridi lakini kumbuka yawe yamechemshwa vizuri na yakapoa kwa ajili ya usalama.

Kisha chukua vipande viwili vya mkate paka siagi au mayonaisi. Kisha chukua beef salami na beef backon weka kati kati pamoja na slice ya nyanya na tango mbichi mpatie mtoto ale.

Jioni: Chakula cha jioni

Mlo: Sahani ya mchanganyiko wa mboga mbichi

Jinsi ya kuandaa: Chukua caroti, tango, pilipili hoho nyekundu na ya kijani zote mbichi na zuchini ichemshe kidogo kisha weka mtindi wenye ladha ya matunda kwa ajili ya kulia hizo mboga

Huu ndio muonekano wa sahani ya mchanganyiko wa mboga kama mtoto ni mdogo sana zisage kwenye mashine ya kusagia nyama kisha utapata mchanganyiko laini mpatie mtoto asiyeweza kutafuna hizo mboga mbichi.

Usiku: Chakula cha usiku

Mlo 1: Supu ya uyoga

Mahitaji: 300gram Uyoga fresh au wa kopo, 50 gram kitunguu maji, 10 gram kitunguu swaumu, 10 gram tangawizi, 50 gram leeks, 100 gram viazi mbatata, 100 gram maziwa fresh, 50 gram mafuta ya kupikia, 300 gram maji

Jinsi ya kuandaa supu ya uyoga: Kaanga katika mafuta ya kupikia vitunguu maji na vitunguu swaumu pamoja na tangawizi. Kisha weka viazi mbatata, leeks na uyoga kaanga tena kiasi kisha weka maziwa na maji acha ichemke mpaka viazi viive kisha toa na saga kwenye blenda. Rudisha jikoni kama itakuwa nzito sana ongeza maziwa au maji kiasi. Usisahau kuweka chumvi kulingana na ladha.

Mlo 2: Kuku maziwa, muhogo na njegere

Mahitaji: 200 gram nyama ya kuku isiyo na mifupa, 100 gram njegere, 200 gram maziwa, 150 mihogo iliyochemshwa kwanza, 300 gram maji

Kulia ni machine ya kusagia nyama utakayoitumia kwa ajili ya kusagia vyakula mbali mbali.

Jinsi ya kuandaa kuku maziwa, muhogo na njegere: Chemsha vyote kwa pamoja kuku na njegere mbichi pamoja na muhogo uliokwisha chemshwa kwanza mpaka ikaribie kukauka mchuzi kisha toa jikoni. Chuja kisha weka mchuzi pembeni.

Chukua mchanganyiko wa njegere, kuku na muhogo. Tumia machine ya kusagia nyama weka huo mchanganyiko kisha saga upate rojo zito kisha rudisha katika sufuri, changanya na ule mchuzi uliochuja ongeza chumvi kulingana na ladha mpe mtoto ale chakula kikiwa cha moto.

Kama huna mashine ya kusagia nyama tumia mwiko kuponda itakua safi kabisa kisha unachanganya na ule mchuzi uliochuja.

Kwa mtoto mkubwa usisage. Baada ya kuchemsha ikaiva ongeza chumvi kisha mpakulie ale chakula cha moto atafurahia sana mchanganyiko wa ladha ya chakula hiki.

Orodha kwa ajili ya manunuzi siku ya Jumatatu

Uyoga wa kopo au fresh, mihogo mibichi, pili pili hoho, tangawizi, unga wa ngano, mayai, maziwa, sukari, chumvi, njegere, nyama ya kuku, tango, zucchini, mtindi usio na ladha ya matunda, mtindi wa ladha ya matunda, baking powder, viazi mbatata, mafuta ya mahindi na leeks.

Vitu hivi vyote sio vingi na unaweza kuvitumia siku inayofuata maana menu yetu ina uwiano safi kabisa. Vitu vingi vinatumika karibu kila siku na manunuzi yake sio ghali kabisa. Mpe mwanao raha kwa kula chakula safi na salama.

Machungwa, Zabibu Hupunguza Uwezekano wa Kupata Kiharusi

zabibu
machungwa
Utafiti mpya uliofanyika nchini Marekani umesema ya kwamba kula machungwa na zabibu kunaweza kupunguza uwezekano wa kupata kiharusi (Stroke).
Utafiti huo uliangalia faida za matunda chachu (Citrus Fruit) pekee kwa mara ya kwanza tofauti na tafiti nyingi ambazo tumezizoea zinazoangalia umuhimu wa matunda na mboga za majani kwa afya kiujumla.
Utafiti huu umehusisha maelfu ya wanawake wanaoshiriki katika tafiti ya manesi Nurse’s Health Study lakini wataalamu wanaamini faida hizo za machungwa na zabibu pia zinapatikana kwa wanaume.
Timu ya watafiti katika chuo cha Norwich Medical School katika Chuo Kikuu cha East Anglia wamechunguza umuhimu wa kemikali aina ya flavonoids ambayo ni jamii ya antioxidant (kemikali zinauwa kemikali hatari za kwenye mwili) inayopatikana katika matunda, mboga za majani, chocolate nyeusi na wine nyekundu.
Utafiti huu ulifuatilia takwimu za miaka 14 za wanawake 69,222 ambao walikuwa wakishirki katika tafiti kwa kuandika kiwango chao cha kula matunda na mboga za majani kwa kila kipindi cha miaka 4. Timu hiyo ya utafiti iliangalia uhusiano wa aina sita ya flavonoids - flavanones, anthocyanins, flavan-3-ols, flavonoid polymers, flavonols na flavones na hatari ya aina mbalimbali za kiharusi kama Ischaemic, Hemorrhagic na Total Stroke. Ilionekna wanawake waliokula kiwango kikubwa cha flavanones kwenye matunda chachu walikuwa na asilimia 19 ya uwezekano wa kupunguza kiharusi kulinganisha na wanawake ambao walikula kiwango kidogo cha matunda hayo.
Kiwango kikubwa cha flavanones kilikuwa 45mg kwa siku kulinganisha na kiwango kidogo cha 25mg kwa siku. Utafiti huu ulichapishwa katika jarida la Medical Journal Stroke umesema flavanones hupatikana kwa asilimia 82 kwenye machungwa na juisi ya machungwa na hupatikana kwa asilimia 14 kwenye zabibu na juisi ya zabibu. Hata hivyo watafiti hao wamesema kwa wale wenye kusudio la kuongeza kiwango kikubwa cha flavanones itawalazimu kula tunda la chungwa kwa wingi na si juisi za machungwa zinazotengenezwa kiwandani kutokana na kiwango kikubwa cha sukari kinachopatikana katika juisi hizo za viwandani.
Professa Aedin Cassidy wa masuala ya lishe bora (nutrition) na ambaye alikuwa kiongozi wa utafiti huo amesema “kula kwa wingi kwa matunda, mboga za majani, na hasa Vitamin C uhusishwa na kupunguza uwezekano wa kupata kiharusi”. Flavanones hutoa kinga dhidhi ya kiharusi kutokana na kuongeza ufanisi wa mishipa ya damu kwenye ubongo na kutokana na kuwa na uwezo wa kuzuia maambukizi mwilini (Anti-inflammatory effect).
Utafiti uliofanyika hapo awali ulionyesha ya kwamba ulaji wa matunda chachu na juisi yake na si matunda ya aina nyingine yoyote hupunguza uwezekano wa kupata kiharusi aina ya Ischaemic Stroke na kuvuja damu kwenye ubongo (Intracerebral Haemorrhage).

Utafiti mwingine uliofanyika kipindi cha nyuma ulionyesha hakuna uhusiano wowote wa matunda ya njano na machungwa katika kupunguza uwezekano wa kupata kiharusi lakini ulionyesha ya kwamba kuna uhusiano wa zabibu na mapeasi wa kupunguza uwezekano wa kupata kiharusi.
Katika utafiti mwingine uliofanyika nchini Sweden umeonyesha ya kwamba wanawake ambao walikula kiwango kikubwa cha antioxidant karibia asilimia 50 kutoka kwenye matunda na mboga za majani, ni wachache tu kati yao waliopata kiharusi ikilinganishwa na wanawake ambao walikuwa na kiwango kidogo cha antioxidant.
Matokeo ya utafiti huu yasiwafanye watu kuacha kula matunda ya aina nyingine pamoja na mboga za majani kwani nayo yana faida kubwa katika mwili wa binadamu.
Kupunguza uwezekano wa kupata kiharusi inawezekana kama mtu atakula lishe bora iliyo na virutubisho vyote muhimu, kula matunda na mboga za majani kwa wingi, kufanya mazoezi mara kwa mara, kupunguza kiwango cha ulaji chumvi (kwani watu wenye asili ya Kiafrika wana kiashiria cha asili kinachojulikana kama salt retention gene ambacho hufanya kiwango kidogo cha matumizi ya chumvi mwilini kuonekana kama kiwango kikubwa na hivyo kuongeza hatari ya kupata kiharusi), kupunguza uzito (kuwa kwenye uzito unaotakikana kiafya kulingana na umri na urefu wako), kupunguza kiwango cha matumizi ya mafuta katika chakula, kulala masaa ya kutosha na kupunguza msongo wa mawazo.

Dawa za Usingizi Chanzo cha Saratani na Kifo

Dawa za Usingizi
Utafiti uliofanywa nchini Marekani hivi karibuni umetoa matokeo ya kushangaza kwa kusema ya kwamba matumizi ya dawa za usingizi huongeza hatari ya kupata saratani pamoja na mtu kufa mapema. Utafiti huo umesema wale wanaotumia dozi kubwa ya dawa ya usingizi wako kwenye hatari ya kupata magonjwa ya saratani.
Utafiti huo ambao ulifanywa na watafiti wa kitengo cha usingizi katika kituo cha Jackson Hole Centre for Preventive Medicine in Wyoming and the Scripps Clinic Viterbi Family Sleep Centre kilichopo jijini California nchini Marekani ili kuangalia hatima ya watu wanaotumia dawa za usingizi aina ya benzodiazepines kama temazepam, diazepam (valium), dawa mpya aina ya zolpidem, zopiclone, zaleplon, dawa za jamii ya barbiturates na zile zinazotumiwa kutibu mcharuko mwili (allergy) na ambazo huleta usingizi.
Matokeo ya utafiti huo yanasema wale wanaotumia dawa za usingizi (Hypnotics) walizoandikiwa na Daktari wako kwenye hatari ya 4.6 kufa ndani ya miaka 2 na nusu ukilinganisha na watu ambao hawatumii dawa za usingizi. Wale ambao wanatumia dozi ndogo ya dawa za usingizi yaani wanaotumia wastani wa vidonge 4-18 kwa mwaka wako kwenye hatari ya mara 3.6 zaidi kufa kulinganisha na wale ambao hawatumii dawa za usingizi.
Wale wanaotumia dozi kubwa yaani vidonge 18-132 kwa mwaka wako kwenye hatari kubwa ya mara 4.4 zaidi kufa, na wale wanaotumia zaidi ya vidonge 132 kwa mwaka wako kwenye hatari ya mara 5.3 zaidi kufa kulinganisha na wale ambao hawatumii dawa za usingizi. Asilimia 93 ya wale walioshiriki katika utafiti huu walikuwa ni wale wanaotumia dozi kubwa ya dawa za usingizi. Pia wale wanaotumia dozi kubwa ya dawa hizi wako kwenye hatari ya asilimia 35 kupata saratani kubwa. Kwa wale wanaotumia dawa aina ya zolpidem wako kwenye hatari ya mara 5.7 kufa huku wale wanaotumia dawa aina ya temazepam wako kwenye hatari ya mara 6.7 kufa kulinganisha na wale wasiotumia dawa za usingizi.
Utafiti huo umesema wale walio kwenye hatari ya madhara haya ya dawa za usingizi ni wale walio katika umri wa miaka 18-55 ingawa sababu halisi haikuelezwa katika matokeo ya utafiti huo. Wagonjwa 10,500 wanaotumia dawa za usingizi walishiriki katika utafiti huo wakilinganishwa na watu 23,500 ambao hawatumii dawa za usingizi walioshiriki katika utafiti huo.
Watafiti hao walisema tiba ya kutotumia dawa yaani ya tiba ya utambuzi wa tabia (cognitive behavior therapy) inaweza kuwa na manufaa zaidi kuliko matumizi ya dawa za usingizi na hata matumizi ya dawa za usingizi kwa muda mfupi yanapaswa kuangaliwa kwa makini. Watafiti hao wakiandika katika jarida la British Medical Journal walisema “Faida chache zinazopatikana kutokana na matumizi ya dawa za usingizi ambazo zilitafitiwa kwa kina na makundi ambayo hayana maslahi yoyote na dawa hizi haziwezi kuhalalisha madhara yatokanayo na matumizi ya dawa hizi za usingizi”.
Matokeo ya utafiti huu ni changamoto kubwa katika fani ya afya hasa ukizingatia ya kwamba watu wengi hutumia dawa za usingizi kutokana na kupatikana kiurahisi katika maduka mbalimbali ya dawa katika Afrika Mashariki. Pia ni changamoto kubwa sana kutokana na dawa hizi kutumika wakati wa upasuaji, kutibu magonjwa ya akili, kutibu mcharuko mwili, msongo wa mawazo na hata kwa wazee.
Kulingana na matokeo haya ni vizuri kuangalia upya matumizi ya dawa za usingizi na utafiti zaidi unahitajika kufanyika kabla ya kutoa msimamo kuhusu matumizi ya dawa za usingizi.

Upandikizaji wa seli za mfumo wa fahamu waweza kutibu kisukari

Watafiti nchini Japan wamegundua jinsi seli za mfumo wa fahamu zinavyoweza kutumika kama seli mbadala zinazofaa kupandikizwa kwenye seli kongosho ili kutibu kisukari. Ripoti ya utafiti huo ambayo imechapishwa kwenye jarida la kitafiti la EMBO Molecular Medicine, inaonesha kuwa seli zinazovunwa kutoka katika mfumo wa fahamu zinaweza kupandikizwa katika tezi kongosho na hivyo kumaliza tatizo la ukosefu wa seli za beta ambazo huitajika kwa ajili ya uzalishaji wa insulin.

Kisukari ni ugonjwa unaosababishwa na ukosefu wa kichocheo cha insulin kinachozalishwa na tezi kongosho, na ambao huathiri karibu watu milioni 200 duniani. Mpaka sasa hakuna tiba yeyote ya ugonjwa huu, hali inayowafanya wagonjwa wa kisukari kutegemea zaidi matumizi ya dawa au njia nyingine mbadala kuthibiti kiwango cha sukari mwilini.

Utafiti huo ulioongozwa na Dr Tomoko Kuwabara kutoka taasisi ya tafiti za Afya ya AIST ya Tsukuba nchini Japan, ulilenga katika kuchunguza jinsi seli za binadamu zinavyokua na kijiwagawa kulingana na kazi mbalimbali za mwili, na pia kuchunguza uwezekano wa kutumia seli mbalimbali kutekeleza kazi zilizo nje ya majukumu yake ya kawaida.

Katika kufafanua, Dr. Kubawara anasema kuwa kwa vile kisukari ni ugonjwa unaosababishwa na ukosefu wa aina moja ya seli, ugonjwa huu unaweza kutibika kwa kutumia njia ya upandikizaji wa seli mpya zitakazotumika kuzalisha kichocheo cha insulin. Anasema, hata hivyo kwa vile kupandikiza seli za beta kutoka tezi kongosho za watu wengine ni ngumu kwa sababu ya ukosefu wa watoaji, njia muafaka ni kutumia seli za mfumo wa fahamu wa mgonjwa mwenyewe katika kufanikisha upandikizaji huo.

Seli za mfumo wa fahamu zinazoweza kupandikizwa kwenye tezi kongosho kwa urahisi zaidi ni zile zilizopo katika maeneo ya ubongo wa mbele yajulikanayo kitaalamu kama hippocampus na olfactory bulb.

Kwa kawaida seli za mfumo wa fahamu huzalisha kiwango kidogo sana cha insulin tofauti na seli za tezi kongosho, hata hivyo, mara tu baada ya kupandikizwa kwenye tezi kongosho, seli hizo zilianza kutoa kiwango kikubwa cha kichocheo cha insulin na kiwango cha sukari katika damu kilionekana kupungua kwa kiwango kikubwa. Na hata seli zilizopandikizwa zilipoondolewa, kiwango cha insulin kilishuka na kusababisha kupanda tena kwa kiwango cha sukari katika damu.

Utafiti huo ulifanyika kwa kutumia panya waliokuwa na ugonjwa wa kisukari.

Upandikizaji uliofanywa katika majaribio haya wa seli za mfumo wa fahamu kwenda kwenye tezi kongosho, siyo tu umeonesha uwezo wa seli za mfumo wa fahamu kuthibiti uzalishaji wa kichocheo cha insulin, bali pia ukweli kuwa seli zinazotajika kwa ajili ya upandikizaji zinaweza kutoka kwa mgonjwa mwenyewe bila kuhitaji uwepo wa mtoaji (donor).

Akihitimisha, Dr. Kubawara alisema kuwa, matokeo ya utafiti wao yameonesha uwezo mkubwa wa seli za mfumo wa fahamu katika kutibu kisukari bila kuhitaji kufanya mabadiliko ya kinasaba au mtoaji (donor), hali ambayo inaleta matumaini ya kuondokana na tatizo la ukosefu wa watoaji wa seli za upandikizaji siku za mbele.

Kuoza kwa Kasi kwa Meno Mengi kwa Watoto Wadogo (Rampant Caries in Children)

Rampant Caries in Children-kuoza kwa meno watoto

Tafsiri za maneno “rampant caries” ni nyingi katika fani ya meno lakini la msingi ni kuoza kwa meno kunako enea kwa kasi na kuharibu vichwa (crowns) vya meno mengi au yote yaliyoota. Hii ni hali mbaya ya kuoza kwa meno ambayo hushambulia zaidi meno ya utotoni (milk teeth or primary dentition), japo wakati mwingine hata ukubwani.

Ugonjwa huu unajidhihirisha kwa kuanza na kuongezeka kwa kasi na kwa namna unavyo yashambulia meno na vyanzo vyake. Meno hushambuliwa kwa mpigo hasa kuanzia meno ya juu mbele, ingawa meno ya chini mbele ni mara chache kushambuliwa kwa vile yanakingwa na visababisha vya kuoza na ulimi.

Ugonjwa huu hushambulia hata maeneo ya meno ambayo kwa hali ya kawaida si rahisi kuoza, kama sehemu ya kukatia kwa meno ya mbele (incisal edges) na sehemu ya mbele kati na nyuma kati (facial and lingual surfaces).

Nini husababisha meno kuoza kwa kasi utotoni?

Nadharia nyingi zinaonesha kuna uhusiano mkubwa kati ya ugonjwa huu na tabia ya ulaji ya mtoto (feeding habits). Mfano kisababishi kikubwa ni watoto kunywa vinywaji vyenye sukari kwa muda mrefu na mara nyingi kwa kutumia chupa za kunyonyea (nursing bottles) ndiyo maana ugonjwa huu wakati mwingine huitwa nursing bottle caries. Hii hujitokeza hasa kwa watoto wanaochwa na yaya zao, ambao huwapa vinywaji hivyo kila wanapohitaji au wakilia.

Pamoja na kwamba ugonjwa huu hutokana zaidi na chupa za kunyonyea, japo mara chache, lakini pia yawezekana kutokana na mama kumnyonyesha mtoto mara kwa mara au tuseme kila anapo hitaji; vile vile wale akina mama ambao hawataki usumbufu usiku hivyo kutumbukiza nyonyo zao kwenye vinywa vya watoto na wao kujilalia, hapa mtoto hujinyonyea usiku kucha hali hii kitaalamu hujulikana kama at will breast feeding.

Vijino vilivyoathirika huonekana brauni au vyeusi kama mkaa

Watoto walio katika hatari ya kupata ugonjwa huu

  • Watoto wa masikini ambao hawapigi mswaki kwa kizingizio cha kwamba mtoto ni mdogo, kumbuka meno ya utotoni yana madini kidogo
  • Watoto wa wafanyakazi wanashinda maofisini wakati wa kunyonyesha na waacha watoto kutumia chupa za kufyonzea kwa muda mrefu ambao hawapo nao
  • Watoto wagonjwa sugu wanaotumia dawa zenye sukari (syrups) mara kwa mara.
  • Watoto wanaoachwa kunyonyeshwa mapema na hivyo kutumia chupa kama mbadala

Namna ya kumkinga mtoto wako

  • Punguza matumizi ya chupa za kufyonzea
  • Msipende kuwanyonyesha watoto kila wanapotaka hivyo, hasa kunyonyesha inapotumika kama njia ya kupoza mtoto anayelia
  • Jenga tabia ya kuwakagua watoto vinywani mara kwa mara na ukiona tatizo mpeleke hospitali mapema
  • Wasaidieni watoto kupiga mswaki mara baada ya meno kuanza kuota
  • Dhibiti matumizi ya vinywaji na na vitu vya sukari mara kwa mara
  • Msipende kuwapa watoto wadogo fedha kwani matumizi yake ni pipi na ice water au vinavyo fanana na hivyo

Matibabu

  • Kuziba meno yanayoweza kuzibika
  • N’goa yanayouma na hayawezi kuzibika na kutumia vitunza nafasi (space maintainers).
  • Acha yasiyoweza kuzibika lakini hayaumi yatatoka wakati wake ukifika
  • Pakaza madini ya fluorini kwa watoto walio katika hatari kubwa

Kuyafanya Meno Yenye Rangi kuwa Meupe (Teeth Whitening)

Kuyafanya Meno Yenye Rangi kuwa Meupe

Wakati wa muongo uliopita mahitaji ya kuboresha muonekano au kurembesha meno yameongezeka kwa kiwango kikubwa hasa katika nchi zilizoendelea. Hii imechochewa na kupatikana kemikali mpya za meno (dental meterials) na vifaa kwa kasi ikiendana na kuboresha vile vya zamani. Sehemu nyingine iliyosababisha madaktari na mainjinia wa meno kuyafanya meno kuwa meupe ni sehemu ya fani ya taaluma ya meno chini ya urembeshaji wa meno, fani hii uhusika na kuboresha muonekano wa meno hasa yale yanayoonekana wakati wa kutabasamu na kuongea. Inahusisha matibabu kama kuyafanya meno yenye rangi kuwa meupe, kunyoosha meno yaliyojipanga vibaya pamoja na kukarabati meno yaliyovunjika na yale yaliyoumbika visivyo (malformed teeth). Huko Uingereza na sehemu nyingine za magharibi wanawake walio wengi wanatumia maelfu ya paundi/euro kuboresha muonekano wa meno yao hali ambayo inaanza pia kuingia huku kwetu.

Nini husababisha meno kugeuka rangi?
Meno kugeuka rangi husababishwa na kimojwapo au muunganiko wa vitu vifutavyo: -

  1. Vyakula na vinywaji kama vile vinyaji vyenye kaboni, wine na sigara.
  2. Utumiaji wa maji yenye kiwango cha juu cha madini aina ya magadi (fluoride) na utumiaji wa magadi katika kulainisha vyakula wakati wa kuandaa vyakula vigumu kama maharage na makande. Utafiti uliofanywa na Prof. Mabelya na wenzake nchini Tanzania umeonesha kuwa kubadilika kwa rangi ya meno kutokana na magadi kwa kiwango kikubwa husababishwa na matumizi ya magadi katika mapishi ya vyakula hasa makande kule maeneo ya mkoa wa Kilimanjaro/Moshi kuliko inavosababishwa na matumizi ya maji.
  3. Maumbile yasiyo sahihi ya sehemu ngumu za jino (enamel and dentine defects). Iwapo sehemu ngumu ya meno imeumbwa ikiwa laini ni rahisi kufyonza rangi na jino kuota likiwa limegeuka rangi au kubadilika baada ya kuota.
  4. Matumizi ya madawa kwa mama mjamzito ambaye tayari meno ya mtoto aliye tumboni yameanza kuumbwa lakini hayajapata madini ya kutosha na hata watoto wachanga ambao meno yao hayajakomaa.
  5. Kufa kwa kiini cha jino hasa kutoka na kujigonga wakati wa ajali au kupigana ngumi usoni (pulp necrosis), jino likigongwa kwa nguvu damu huvuja ndani ya kiini cha jino na baadaye huchachuliwa na kutoa kemikali ambayo hupenya kwenye vitundu vidogo vidogo kwenye dentine na kujidhihirisha kama kijivu, zambarau au hata nyeusi. Hali hii yaweza tokea mapema baada ya kupata ajali lakini wakati mwingine inaweza kuchukua miaka kadhaa hata arobaini kipindi ambapo mtu hakumbuki kuwa aliwahi kutwangwa ngumi.

Kuyafanya meno yenye rangi yasimpendeza mwenye nayo kuwa meupe
(Bleaching or teeth whitening)

Huku ni kuyafanya meno yen
ye rangi kuwa meupe au kuongeza weupe wa yale yenye rangi ya kawaida kufikia kiwango cha weupe atakacho muhitaji kwa kutumia kemikali maalum. Rangi ya kawaida ya meno kwa walio wengi ni uweupe kama wa maziwa (milky white). Rangi yeyote nje ya hiyo si ya kawaida (abnormal color or discoloration).

Kuwa na rangi isiyo ya kwaida hasa kwa meno ya mbele linaweza kuwa tatizo kubwa la urembo na kumsumbua mhusika kisaikolojia. Kuyafanya meno kuwa meupe kumelenga kuwaondolea wahusika tatizo hili japo mafanikio yake yanategemea kiwango cha rangi isiyo ya kawaida.

Kufanya meno kuwa meupe kwa kutumia kemikali, kunaweza kubadili yaliyo na rangi isiyo ya kawaida kutoka yale yaliyoathirika kwa kiwango kidogo mpaka cha kati.

Kufanya meno yawe meupe kwa kutumia kemikali huunguza (oxidises) rangi ya jino na kuiondoa. Kemikali zinazotumika zina hydrogen peroxide 30%-35% na baadhi carbamide peroxide 10%. Kemikali hizi huweza kuondoa rangi zilizosababishwa na vyakula, vinywaji, dawa za tetracycline, rangi kidogo iliyotokana na utumiaji wa madini ya magadi kwenye vyakula au kwenye maji (mild fluorosis) na meno yenye rangi ya njano au kijivu itokanayo na umri kuwa mkubwa. Inaweza pia kuondoa rangi itokanayo na uvutaji wa sigara na matumizi ya ugoro. Kwa wavutaji wa sigara sharti waache pindi watumiapo kemikali hizi kwani muunganiko wa hydrogen peroxide na kemikali zilizopo kwenye moshi wa sigara unahisiwa kuongeza madhara zaidi ambayo tayari moshi wa sigara husababisha kwenye mwili wa binadamu. Haishauriwi kwa akina mama wanaonyonyesha kutumia dawa hizi pamoja na kwamba hakuna madhara yanayojulikana mpaka sasa


Kupiga meno viraka (Veneeri
ng)


Kupiga meno viraka



Hii hufanyika kwa kuondoa sehemu ndogo ya juu ya jino kwenye enamel kama 0.5-1mm na baadaye kupandika dawa yenye rangi nyeupe kulingana na mgonjwa anavyotaka mwenyewe. Picha inayonesha meno yaliyobadlika rangi kutokana na magadi kabla na baada ya kupigwa viraka


Kabla ya kiraka Baada ya kupigwa kiraka (veneer)

Kumbuka: kuna rangi zaidi ya 26 nyeupe ambazo miongoni mwake mgonjwa anaweza kuchagua anayoitaka

Unyongovu Waweza Kusababisha Magonjwa ya Moyo kwa Vijana

jaribio la kujiua

Katika tafiti mpya zilizofanywa hivi karibuni zinaonyesha kuwa unyongovu na jaribio la kujiua ni viashiria hatari ambavyo huleteleza vijana kufa kwa magonjwa ya moyo.

Katika utafiti mkubwa uliohusisha washiriki zaidi ya 7000 walio chini ya miaka 40 ulionyesha kuwa kwa wale waliokuwa na historia ya unyongovu au jaribio la kujiua walikuwa na hatari kubwa zaidi ya kufa kutokana na magonjwa ya moyo hasa yale ambayo moyo hukosa oksijeni ya kutosha (ischemic heart disease) ukilinganisha na wale ambao hawakuwa na historia hiyo.

Ingawa jinsia zote zilikuwa kwenye hatari zaidi ya kufa kutokana na magonjwa ya moyo, lakini wanawake wenye unyongovu au waliofanya jaribio la kujiua walikuwa na hatari mara 14 zaidi ya kufa kwa magonjwa ya moyo yatokanayo na kukosa oksijeni ya kutosha (ischemic heart disease) kulinganisha na wale ambao hawakuwa na unyongovu au jaribio la kujiua.

Katika utafiti huu uliofanywa na Profesa Viola Vaccarino kutoka chuo kikuu cha Emory, Atlanta, Georgia aligundua jinsi matatizo ya kisaikolojia yanavyopelekea kuongeza hatari ya kufa mapema na magonjwa ya moyo katika idadi ya vijana.

Taarifa nyingi zilizopo za magonjwa ya moyo ambazo zilizokwisha tolewa huwa za umri wa kati na wazee, maana imekuwa ikizoeleka magonjwa haya huathiri zaidi rika hiyo, ambayo ni kweli kabisa hasa katika magonjwa yanao athiri zaidi mishipa ya damu ya moyo (CHD).

Kutokana na watatifi mkazo humewekwa zaidi kwa wazee ingawa magonjwa mengi ya moyo huanza katika kipindi cha ujanani.

Katika utafiti huu taarifa zilichukuliwa kutoka kwa washiriki 7641, wenye umri kati ya 17 hadi 34, kutoka mwaka 1988 hadi 1994.

Katika ratiba ya uchunguzi, tathmini ilikuwa kuhusu unyongovu na jaribio la kujiua , na matokeo baada ya ufuatiliaji yalikuwa kama ifuatavyo: washiriki 51 walikufa kutokana na magonjwa ya moyo, na kati ya hao 28 walikufa kutokana na moyo hukosa oksijeni ya kutosha (ischemic heart disease).

Wagonjwa 538 walikutwa na historia ya unyongovu na 419 kuwa na jaribio la kujiua. Na 136 walikuwa na historia ya vyote viwili.

kubadilishwa athari ya uwiano (HR) kwa ajili ya hatari kwa CVD kifo 2.38 kwa ajili ya wagonjwa walio na unyogovu (95% ya muda kujiamini [CI], 0.93-6.08) na 3.21 kwa ajili ya wale walio na majaribio ya kujiua zamani (95% CI, 1.36-7.56)

Kuna mjadala mkubwa kuhusu madhara ya unyogovu na ugonjwa wa moyo na mishipa katika vifo vya wanawake kama ikilinganishwa na wanaume. Nadhani ushahidi kutoka kwa utafiti huu ni imara lakini masomo ya baadaye ni wazi kuwa ni muhimu.

Mmoja wa watafiti wengine Dr Scherrer alisema “kwa madaktari, anadhani matokeo ya jumla yanazidi kuongeza wasiwasi ni wakati gani hutambua unyongovu, ambapo ni kawaida kwa watu wenye umri mdogo, kuna uwezekano wa haja ya kuweka mkazo mkubwa katika kufuatilia afya yao ya moyo. Na kwamba sio kitu ambacho madaktari wengi hufanya mara kwa mara kwa wagonjwa wenye umri mdogo sana.

Na hii huacha swali kubwa la kujiuliza:

Je inawezekana kuzuia magonjwa ya moyo yahusishwayo na unyongovu, kwa kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa mambo ya hatari yanayoweza kupelekea magonjwa ya moyo kwa kundi la vijana?

Watu wengine wanaweza kuwa na wenza wenye ukimwi bila kuambikizwa kwa muda mrefu au hata wasiambukizwe kabisa

Neno ukimwi ni kifupisho cha maneno “Upungufu wa Kinga Mwilini”. Ugonjwa huu usabishwa na virusi ambavyo hushambulia chembe chembe za kinga na kuufanya mwili ushindwe kujilinda dhidi ya maradhi ipasavyo au hata kushindwa kupambana na maradhi yaliyoingia tayari.

Ukimwi huambukizwa kwa njia mbali mbali kama;

  1. kuingia damu ya mtu mwenye ukimwi kwa hasiye nao-hapo ndo kuna vitu kama kuchangia nyembe, sindano, kuwekewa damu isiyo salama n.k.
  2. Kujamiiana- wadudu wa ukimwi wameonekana kuwemo kwenye majimaji ya sehemu za sili, hivyo kama kuna michubuko mtu akafanya tendo hili na mhadhilika kuna nafasi ya kuambukizwa.
  3. Mama mjamzito kumuambukiza kiumbe kilichopo kwenye mfuko wakewa uzazi.

Japo si jukumu la makala hii lakini kinga ni pamoja na kuzuia kuchangia vifaa vyenye ncha kali, kutumia kinga unapofanya tendo la ndoa, kuacha kufanya tendo la ndoa kama unaweza na mengine.

Kwa vile kuna uwezekano wa kupata ukimwi kwa kutenda tendo la ndoa, wanandoa ambao kimsingi wengi wao kama si wote, hawatumii kinga wanapofanya tendo hili. Katika hali hii, kama kuna uwezekano mmoja ni muathirika, basi nafasi ya kumuambukiza mwenzake huongezeka.

Taarifa ya kwanza (case report 1)

Mwaka tisini na na sita, rafiki yangu mmoja, mtoto wake wa miezi mitatu alilazwa Muhimbili. Baada ya kuona maendeleo ya tiba si mazuri waliamua kumpima, majibu yakaonesha ana virusi vya ukimwi. Majibu haya yalimfanya daktari aliyekuwa anamtibu mtoto kuwashauri wazazi nao wapime na wakakubali. Walipopima mama alikuwa muathirika baba hapana, na watu hawa walikuwa kwenye ndoa kwa muda wa miaka miwili, wakila tunda lao bila kinga.

Baada ya taarifa kufika kwa ndugu wa mwanaume wakashauri waachane wagawane walichochuma pamoja. Wakati wamepelekana mahakamani, mwanamke akakana kwamba hawakuwahi kupima. Mahakama ikaamuru wapime, wakapima tena kwa hospitali chaguo la mwanamke. Majibu yakawa yale yale mama anao baba hana. Wakakubali kuachana na kugawana walivyochuma pamoja kama walivyoorodhesha mahakamani na baba kupangiwa kiwango cha kumlipa mama kwa malezi ya mtoto. Baada ya mwaka na nusu mtoto akapimwa tena na kugundulika hana ukimwi tofauti na alipokuwa amepimwa mwanzoni. Mpaka hapa ninapoandika wote wapo na afya njema, baba alioa mwanamke mwingine na wana watoto wawili na mama bado yupo anaendelea kutumia dawa za ARVs.

Uchunguzi usio rasmi ulionesha kuwa mama alikuwa na ugonjwa huo kabla hata ya ndoa hiyo.

Taarifa ya pili

Jamaa yangu mmoja naye alikuwa ameoa na kujaliwa kupata watoto wanne katika ndoa yake ya miaka 15. Baadaye mwaka 2008 mke wake akaanza kuugua magonjwa ya ajabu ajabu, yanapona yanarudi na mapya yanajitokeza. Analazwa hospitali anarudi tena baada ya muda, akaamua kwenda kwa mganga Mpemba ambaye alimwambia mumewe ana mke mwingine kamtupia jini la damu. Akampa dawa hazikusaidia. Kutokana na lawama za mahawara kuingia na bado hospitali na kwa waganga haponi, ikashauriwa wapime HIV. Wakakubali. Walipopimwa iligundulika kuwa mama anao na baba hana. Mama akazidi kuamini kuwa hata kama ameonekana ana Ukimwi basi atakuwa ametumiwa na huyo hawara wa mumewe. Ikawa kazi kumeza dawa, anameza na kuacha anakwenda kwa waganga wake, mara ya mwisho akaamua kuokoka sasa japo hapo kichwa nacho kilishaanza kuvurugika. Huko ndo kabisa akaambiwa aache dawa kabisa YESU atamponya. Mwanzoni mwa mwaka huu tumemzika.

Ninazo taarifa za namna hii nne lakini mbili zinatosha kutoa mjadala.

Mjadala

Katika taarifa zote mbili inaonyesha wahusika wote walishakaa pamoja wakila matunda yao bila kinga ndo maana wakapata watoto. Kwanini hawakuambukizana inawezekana walikuwa wanakula tunda lao bila michubuko yeyote katika kipindi chote walichokuwa pamoja. Sababu nyingine yawezekana wanaume hao wana kinga dhidi ya virusi vya ukimwi au chembe chembe zao za kinga hazina vipokezi (receptors) vya wadudu wa ukimwi. Tafiti zimeonyesha virusi wa ukimwi huweza kuingia kwenye chembe chembe za kinga kupitia vipokezi katika hali ya kama ufunguo na kitasa au au nati na boriti. Kama mtu hana vipokezi hivi hawezi kuambukizwa.

Dr Matthew Dolan, daktari bingwa katika jeshi la anga la marekani anasema, anasema "Genetic resistance to AIDS works in different ways and appears in different ethnic groups. The most powerful form of resistance, caused by a genetic defect, is limited to people with European or Central Asian heritage. An estimated 1 percent of people descended from Northern Europeans are virtually immune to AIDS infection, with Swedes the most likely to be protected. One theory suggests that the mutation developed in Scandinavia and moved southward with Viking raiders.

All those with the highest level of HIV immunity share a pair of mutated genes -- one in each chromosome -- that prevent their immune cells from developing a "receptor" that lets the AIDS virus break in. If the so-called CCR5 receptor -- which scientists say is akin to a lock -- isn't there, the virus can't break into the cell and take it over. (haya yamenizengua kuyatafsiri)

Mtoto kuonekana ana ukimwi akiwa na miezi miatu na baada ya mwaka mmoja na nusu hana hii ni kutokana na ukweli kwamba mtoto anayezaliwa na mama mwenye virusi vya ukimwi huwa na antibodies dhidi ya virusi vya ukimwi kutoka kwa mama yake. Unapopima ukimwi kutumia kipimo cha eliza ambacho uangalia antibodies hizi, basi mtoto huonekana hanao, lakini kama mtoto hakuambukizwa wadudu basi, antibodies hizi huondoka kwenye damu yake kadri muda unavyo kwenda.

Hitimisho

Kuna baadhi ya watu si rahisi kuwaambukiza ukimwi

Mapendekezo

Kutokupa ukimwi kwa muda mrefu huku ukila tunda na mwenye nao kwa muda mrefu haikuhakikishii kuwa huwezi kuupata kwa hakikisha unafuata masharti ya kinga

Mtoto anayezaliwa na mama au wazazi wenye ukimwi si lazima awe nao fuata ushauri wa daktari na hasa kupima wakati wa ujauzito

Tuangalie namna ya kuwadhibiti waganga wa jadi na watumishi wa mungu wanaoshauri watu wasitumie dawa za kuongeza maisha