Showing posts with label mjamzito. Show all posts
Showing posts with label mjamzito. Show all posts

Sunday, March 18, 2012

Upungufu wa Damu Kipindi cha Ujauzito


Upungufu wa damu (anaemia) hutafsiriwa kama kupungua kwa kiwango cha hemoglobin katika damu damu chini ya kiwango kinachokubalika kiafya. Kiwango cha kawaida cha haemoglobin (Hb) katika mwili wa binadamu ni kati ya gramu 12 mpaka 14 kwa kila mililita ya damu. Hata hivyo shirika la afya duniani (WHO) linatambua kiwango cha mpaka 11gm/mililita kuwa cha kawaida kwa mama mjamzito. Hivyo basi mjamzito mwenye kiwango chochote cha haemoglobin chini ya 11 gm/mililita hutafsiriwa kuwa na upungufu wa damu. Hata hivyo nchi nyingi hasa zinazoendelea hutambua kiwango cha mpaka gramu 10 kwa mililita kuwa ni upungufu wa damu kwa mjamzito.

Kwa mjamzito anayehudhuria kliniki kwa mara ya kwanza, upungufu wa damu kipindi cha ujauzito humaanisha kiwango cha hemoglobin chini ya <11.0 g/dL, na mimba inapofikisha wiki 28 upungufu wa damu hutambuliwa iwapo hemoglobin itashuka na kuwa chini ya 10.5 g/dL.
Kwa kuzingatia hilo, mama mjamzito hushauriwa kupima wingi wa damu siku anapohudhuria kliniki kwa mara ya kwanza na pindi mimba inapofikisha wiki 28.

Viwango vya Anaemia
Upungufu wa damu unaweza kugawanywa katika viwango vikuu vinne, yaani upungufu wa damu wa kawaida (mild anaemia) ambao ni kati ya 9-11 gm/ml, upungufu wa damu wa kati (moderate anaemia) ambao ni kati ya 7-9 gm/ml, upungufu wa damu mkali (severe anaemia) ambao ni kati ya 4-7 gm/ml na upungufu wa damu mkali zaidi (very severe anaemia) ambao ni chini ya 4gm/ml.

Mzunguko wa madini ya chuma mwilini
Kwa kawaida mwili wa mwanamke huifadhi gramu 3.5 mpaka 4.5 za madini ya chuma. Asilimia 75 huifadhiwa kama hemoglobin katika chembe damu nyekundu, asilimia 20 kama ferritin katika mifupa na asilimia 5 inayobaki huifadhiwa katika misuli na vimeng’enyo vingine vya mwili.
Wanawake wasio wajawazito hupoteza karibu gramu 1 za madini ya chuma kutoka katika seli za mwili zinazokufa kila siku na gramu 1 zaidi kila siku wanayokuwa kwenye hedhi.

Ukubwa wa tatizo
Upungufu wa damu kipindi cha ujauzito ni tatizo linalowakumba kina mama wajawazito wengi sana, siyo tu Tanzania bali nchi nyingi zinazoendelea. Inakisikiwa kuwa karibu theluthi moja ya wajawazito katika miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito hukumbwa na tatizo hili.
Kwa mujibu wa WHO, inakadiriwa kuwa karibu asilimia 56 ya wajawazito huko kusini mashariki ya Asia hukumbwa na tatizo hili. Kwa hapa Tanzania, hakuna takwimu sahihi kuhusu tatizo hili. Sehemu nyingine duniani, inakadiriwa kuwa karibu asilimia 4-16 ya vifo vinavyotokana na ujauzito husababishwa na upungufu wa damu. Aidha upungufu wa damu wakati wa ujauzito huongeza uwezekano wa madhara kwa mtoto ikiwemo kifo.

Chanzo cha upungufu wa damu wakati wa ujauzito
Kipindi cha ujauzito huambatana na mabadiliko mbalimbali ya mwili. Moja ya mabadiliko hayo ni ongezeko la maji (plasma volume) katika mzunguko wa damu. Katika hali hii, pamoja na kwamba kiasi cha damu huonekana kuongezeka, kiwango cha hemoglobini hupungua mpaka kufikia 11.5mg/dl.
Karibu asilimia 85 ya anaemia wakati wa ujauzito husababishwa na upungufu wa madini ya chuma mwilini. Upungufu wa madini ya chuma unaweza kusababishwa na kula chakula chenye kiasi kidogo cha madini haya au mwili wa mjamzito kushindwa kutunza madini ya chuma ya kutosha kutokana na ama mimba zilizopita au kupoteza kiasi kingi wakati wa hedhi kabla ya kushika mimba.

Vyanzo vingine ni pamoja na
  • Upungufu wa folic acid
  • Ugonjwa wa sickle cell
  • Lishe duni kabla na wakati wa ujauzito
  • Kupoteza damu kwa sababu ya kuumia au kuwa na minyoo (hookworms)
  • Ugonjwa wa malaria wakati wa ujauzito
  • Ugonjwa wa chembe damu nyekundu ujulikanao kama beta thalassaemia. Ugonjwa huu huwapata zaidi watu wanaoishi Asia ya kusini, Ulaya ya kusini na Afrika.
  • Upungufu wa vitamin B12
  • Ugonjwa sugu wa kuvunjika chembe damu nyekundu (chronic haemolysis) kama vile ugonjwa kurithi wa chembe damu nyekundu (hereditary spherocytosis)
  • Ugonjwa wa kupoteza hemoglobin kupitia mkojo (paroxysmal nocturnal hemoglobinuria)
  • Saratani ya damu (leukemia)
  • Matatizo ya kupoteza damu kwenye njia ya chakula (gastrointestinal bleeding)
  • Matatizo katika utumbo hasa wakati wa ujauzito.
Vihatarishi vya tatizo hili
  • Masuala ya kijamii kama vile umri wa mjamzito, kiwango chake cha elimu na uelewa kuhusu afya yake, kama ana mwenza wa kumsaidia kiuchumi, makazi anayoishi vinaweza kuchangia mjamzito kupata upungufu wa damu
  • Vihatarishi vingine ni vile vinavyohusu masuala ya uzazi kama vile idadi ya mimba zilizotanguli (waliowahi kuzaa wana hatari ya kupata anaemia kuliko wanaopata mimba kwa mara ya kwanza), kuwa na mimba ya mapacha na kuwa na historia ya kuzaa mtoto njiti
  • Vihatarishi vingine vinahusu tabia za mjamzito kama vile uvutaji sigara, unywaji wa pombe na kutohudhuria kliniki wakati wa ujauzito
  • Pia kuwa na magonjwa kama vile kisukari, magonjwa ya figo, pamoja na shinikizo sugu la damu
Madhara ya upungufu wa damu kwa mama na mtoto
Sehemu nyingine duniani, inakadiriwa kuwa karibu asilimia 4-16 ya vifo vinavyotokana na ujauzito husababishwa na upungufu wa damu. Aidha upungufu wa damu wakati wa ujauzito huongeza uwezekano wa madhara kwa mama na mtoto ikiwemo kifo. Madhara haya ni pamoja na
  • Madhara kwa mama kipindi cha ujauzito: kukonda au kuongezeka uzito kwa kiasi kidogo sana, kuhisi uchungu kabla ya muda, kondo la nyuma kutunga pasipostahili, shinikizo la damu wakati wa ujauzito, na chupa kupasuka kabla ya wakati.
  • Madhara kwa mama wakati wa kujifungua: kupatwa na uchungu usioeleweka na usio wa kawaida, mtoto kuvuja damu ndani kwa ndani, kupatwa na shock, hatari ya ganzi (anesthesia risk) kwa anayefanyiwa upasuaji, na moyo kushindwa kufanya kazi.
  • Madhara kwa mama baada ya kujifungua: maambukizi baada ya kujifungua, kizazi kushindwa kurudi katika hali ya kawaida au damu kuganda kwenye mishipa.
  • Madhara kwa mimba na mtoto atakayezaliwa: Madhara ni pamoja na mtoto kuzaliwa njiti, mtoto kuzaliwa na uzito mdogo, mtoto kuwa na score ndogo (poor Apgar score), mtoto kuzaliwa akiwa amechoka (fetal distress), na upungufu wa damu kwa mtoto
Watoto wanaozaliwa wakiwa na upungufu wa damu hukua kwa tabu, huwa na maendeleo duni ya kiakili na kimatendo (poorer intellectual developmental milestones), uwezekano mkubwa wa kuwa na kasoro mwilini na hata kifo. Kasoro hizo ni pamoja na matatizo ya magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo (congenital heart diseases

Dalili
Mjamzito mwenye upungufu wa damu wa kawaida mara nyingi anaweza asioneshe dalili zozote. Hata hivyo iwapo upungufu ni mkubwa, dalili za awali ni pamoja na uchovu wa mara kwa mara na kupumua kwa shida, kukosa hamu ya kula, mapigo ya moyo kwenda kasi, na kuchafuka kwa tumbo.
Wakati wa uchunguzi mjamzito anaweza kuonekana mweupe kuliko kawaida hasa sehemu za viganjani, kucha za vidoleni, ulimi, au macho. Anaweza pia kuwa na dalili za kuvimba miguu.

Vipimo na uchunguzi
Uchunguzi wa upungufu wa damu hufanywa kuwa kupima kiasi cha haemoglobin pamoja kufanya kipimo kingine cha damu kijulikanacho kama peripheral smear.
Vipimo vingine vya maabara ni pamoja na kipimo cha kufahamu uwezo wa kuhifadhi madini ya chuma yaani total iron binding capacity (TIBC), kiasi cha feritin katika damu, kiasi cha folic acid. Katika mazingira mengine kipimo cha kuchukua sehemu ya supu ya mifupa na kuichunguza maabara yaani bone marrow biopsy kinaweza kufanywa. Hata hivyo hivi si vipimo vinavyofanywa mara kwa mara.

Matibabu
Mama mjamzito huitaji miligramu 2 mpaka 4.8 za madini ya chuma kila siku. Ili aweze kupata kiasi hiki, inampasa kula kati ya miligramu 20 mpaka 48 za madini ya chuma. Kwa jamii ambayo upatikanaji wa vyakula vyenye madini hayo ni wa shida, suala hili linaweza kuwa gumu sana kutekelezeka, ndiyo maana Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeweka mpango maalum wa kuwapa wajawazito wanaohudhuria kliniki madini ya chuma na folic acid ili kufidia pengo hilo.
Vidonge vya madini ya chuma ni salama, nafuu na njia makini ya kuongeza na kurekebisha upungufu wa damu mwilini. Kwa wajawazito ambao hawawezi kunywa, kwa sababu yeyote ile, njia ya sindano inaweza pia kutumika.
Wajawazito wanashauriwa kutumia miligramu 60 za madini ya chuma (ferrous sulphate) na 500mg za folic acid kila siku, ambapo utaratibu huu huendelea kwa miezi mitatu mpaka sita ili kuongeza hifadhi ya madini ya chuma mwilini, hata kama kiwango kinachotakiwa kitakuwa kimefikiwa.

Utumiaji wa vidonge vya madini ya chuma na baadhi ya vyakula: Kuna baadhi ya vyakula kama vile chai ya rangi ambavyo vikiliwa wakati mjamzito amekunywa vidonge vya madini ya chuma vinaweza kupunguza unyonyaji wake katika utumbo. Kwa upande mwingine baadhi ya vyakula vyenye vitamini C kama vile matunda ya jamii ya machungwa huongeza uwezo wa utumbo kunyonya madini ya chuma mwilini.

Vyakula vya kuongeza damu: Pamoja na mkakati huo, wajawazito hushauriwa pia kula vyakula vyenye madini ya chuma kwa wingi kama vile nyama, maini, mayai, samaki, mimea jamii ya kunde, maharage makavu, mboga za majani, matembele, na mikate iliyoongezwa madini ya chuma.

Matibabu ya upungufu wa damu mkali kwa wajawazito walio katika wiki za mwisho (baada ya wiki ya 32): Wagonjwa wa kundi hili hutibiwa hospitali. Wengi wanaweza pia kuwa na dalili za matatizo ya moyo, hivyo wanapaswa kulazwa na kupumzika kitandani, na wakati fulani kuongezewa hewa ya oksijeni. Pamoja na kutibiwa matatizo ya moyo, huongezewa pia damu (packed red cells) kwa vile vidonge vya madini ya chuma havitafaa kurekebisha tatizo hili kwa haraka kabla ya muda wa kujifungua kufika.

Matibabu ya maradhi mengine: kwa mazingira yetu, magonjwa kama malaria na minyoo huchangia kwa kiasi kikubwa kutokea kwa upungufu wa damu kwa wajawazito, hivyo basi magonjwa haya hayana budi kutibiwa kikamilifu ili yasilete madhara kwa mjamzito. Wajawazito wanaoishi maeneo yenye malaria kwa wingi hupewa dawa za SP kwa ajili ya kuwalinda wasipatwe na ugonjwa huu. Pia dawa za minyoo za Albendazole au mebendazole hutolewa kwa wajawazito baada ya miezi mitatu ya mwanzo ili kuua minyoo. Ili kuzuia kujiridia kwa minyoo, wajawazito pia hushauriwa kuvaa viatu/kandambili kila wakati, na kuhakikisha miili na mazingira yao yapo safi.

Dalili na Ishara za Ujauzito

Mstari wima mweusi hutokea tumboni kuanzia chini ya kitovu

Dalili za ujauzito hutofautiana kati ya mwanamke na mwanamke, ingawa kuchelewa au kukosa hedhi ni dalili moja muhimu sana

Ni muhimu kuzitambua na kuzifahamu dalili hizi kwa sababu zinaweza kusaidia kuelezea au kutofautisha matatizo mengine mbali ya ujauzito.

Hebu sasa tuangalie dalili na ishara za Ujauzito:

  • Kutokwa damu kidogo ukeni wakati kiumbe kikipandikizwa kwenye mfuko wa uzazi, ingawa siyo wanawake wote hupatwa na dalili hii
  • Kukosa hedhi, hii ni moja ya dalili kubwa za ujauzito
  • Maumivu ya matiti na kuvimba matiti (huweza kutokea kati ya wiki ya 1 hadi ya 2)
  • Uchovu, wanawake wengi hujihisi uchovu na hali ya kutopenda kufanya lolote.
  • Kupoteza ladha au kuhisi ladha ya chuma mdomoni
  • Kuongezeka kwa hisia ya harufu, kipindi cha ujauzito wanawake wengi huongezeka hisia ya harufu
  • Kichefuchefu na kutapika
  • Maumivu ya kichwa
  • Kizunguzungu
  • Kukojoa mara kwa mara (hasa kati ya wiki 6-8)
  • Kubadilika rangi kwa ngozi inayozunguka chuchu kuwa nyeusi
  • Kutamani baadhi ya vyakula na kuchukia vingine
  • Kupanuka kwa mfuko wa uzazi
  • Tumbo kujaa au kuvimbiwa
  • Kununa na kukasirika haraka
  • Kiungulila au kupata choo kigumu
  • Kolostramu kuanza kutoka kwenye matiti
  • Kuongezeka uzito
  • Kuweza kupapasa mtoto (palpation of the baby)
  • Kulainika na kuvimba kwa shingo ya uzazi (Hegars sign) - kuanzia wiki ya 6
  • Shingo ya uzazi kubadilika rangi kuwa ya samawati kutokana na msongamano wa damu katika mishipa ya vena. Ishara hii huitwa pia Chadwick's sign

Dalili nyingine ni pamoja na

  • Mstari wima mweusi hutokea tumboni kuanzia chini ya kitovu (linea nigra)
  • Mama kuhisi mtoto akicheza (kuanzia wiki ya 20)
  • Maumivu ya mgongo hasa mimba ikishakuwa kubwa.
  • Kipimo cha mimba kuwa chanya (positive).
  • Kusikia mapigo ya moyo ya mtoto
  • Mtoto kuonekana kwenye kipimo cha ultrasound

Msongo wa mawazo kipindi cha ujauzito husababisha ulemavu kwa mtoto

stress in pregnant women

Watafiti wa magonjwa wanadai kuwa msongo mkali wa mawazo wakati wa ujauzito unaweza kusababisha hitilafu katika uumbaji wa mtoto na hatimaye mtoto kuzaliwa akiwa mlemavu.

Ripoti ya watafiti hao inazidi kuthibitisha matokeo ya tafiti zilizopita kuwa mama mwenye msongo wa mawazo wakati wa ujauzito kutokana na mambo kama kufukuzwa au kuachishwa kazi, kutengana na mwenza wake au kufiwa ana hatari ya kuzaa mtoto mwenye ulemavu kama vile midomo sungura (cleft lip na cleft palate) au matatizo kwenye uti wa mgongo (spina bifida).

Jopo la watafiti wa kidenmark likiongozwa na Dr Dorthe Hansen walifanya uchunguzi ili kuthibiitisha ukweli na uhakika wa dhana hii.

Wakitumia rikodi za taarifa za kitabibu za kipindi cha miaka 12 kutoka 1980 mpaka 1992 kutoka masjala ya Taifa ya kitabibu, watafiti hao waliweza kuwatambua wajawazito wote waliokumbwa na matatizo makubwa ya kimaisha wakati wa ujauzito na hata miezi 16 kabla ya kupata ujauzito. Matatizo makubwa ya kimaisha yaliyochunguzwa yalikuwa kukumbwa na msiba wa ndugu au jamaa wa karibu, ndugu au jamaa wa karibu kulazwa hospitali kwa mara ya kwanza baada ya kugundulika kuwa na kansa ya aina yeyote au ndugu au jamaa wa karibu kupatwa na ugonjwa wa mshtuko wa moyo. Mambo haya yalichunguzwa kwa kigezo kuwa, mjamzito yeyote aliyewahi kukumbana nayo ana hatari kubwa ya kuwa katika msongo wa mawazo bila kujali tabia yake, kama ana watu wa kumfariji au uwezo wake wa kukabiliana nayo.

Jopo hilo lilichunguza maendeleo ya mimba kwa wajawazito 3,560 ambao walikumbana na matukio hayo kwa kulinganisha na wajawazito wengine 20,299 ambao hawakukumbana na hali yeyote ambayo ingewasababishia kupata msongo wa mawazo wakati waujauzito.

Matokeo ya uchunguzi wao yalionesha kuwa ulemavu na hitilafu za viungo kwa watoto waliozaliwa ulikuwa mara mbili miongoni mwa kundi la wajawazito waliokumbwa na msongo mkali wa mawazo ikilinganishwa na kundi la kinamama ambao hawakuwa na hali hiyo.

Kadhalika ilionekana kuwa wanawake waliowahi kukumbwa na hali kama hiyo katika ujauzito mbili mfululizo za nyuma walikuwa katika hatari kubwa zaidi ya kuzaa watoto wenye ulemavu wa viungo tofauti na wale waliowahi kupatwa na hali hiyo mara moja tu au wale ambao hawakupatwa kabisa.

Ilionekana pia kuwa tukio lililoongeza uwezekano wa mtoto kuzaliwa akiwa na ulemavu wa viungo ilikuwa ni iwapo mjamzito atafiwa na mtoto wake mwingine mkubwa wakati akiwa katika miezi mitatu ya mwanzo wa ujauzito wake huu wa sasa. Hatari ya kuzaa mtoto mlemavu iliongezeka iwapo kifo cha mtoto huyo mkubwa kingetokea bila kutarajiwa kwa mfano kwa ajali.

Watafiti wanasema kwamba, msongo mkali wa mawazo huchangia kuathiri uumbaji wa mtoto aliye tumboni kwa kusisimua uzalishaji wa homoni ya cortisone. Homoni hii husababisha ongezeko la kiwango cha sukari katika damu na upungufu wa usambazaji wa hewa safi ya oksijeni kwa mtoto, mambo ambayo husababisha kutokea kwa hitilafu katika uumbaji wa viungo vya mtoto hatimaye kusababisha ulemavu wa viungo vya mtoto.

Uwezekano mwingine ni kuwa msongo mkali wa mawazo humchochea mama mjamzito kutumia zaidi vileo vyenye alcohol na pia kula lishe duni hali ambayo huongeza madhara zaidi kwa kiumbe kilicho tumboni.

Hata hivyo Professor Peter Hepper wa Chuo Kikuu cha Queen's cha Belfast, anasema hakushangazwa na mtokeo ya utafiti huo.

Anasema kuwa, "tunafahamu msongo wa mawazo husababisha mabadiliko ya kifiziolojia katika mfumo wa mwili wa mjamzito, na hivyo hakuna sababu kwanini mabadiliko hayo yasimfikie pia mtoto aliye tumboni kupitia kondo la nyuma na kumuathiri. Matokeo haya yanazidi kuthibitisha kile tulichokuwa tukikifahamu tangu awali kuwa msongo wa mawazo wa muda mrefu kwa mwanamke una madhara makubwa kwa mendeleo ya uumbaji wa mtoto aliye tumboni na hivyo basi hakuna budi kufanyike kila njia kuwasaidia wajawazito walio katika hali hii ili waweze kujifungua watoto walio na afya njema na salama."