Hiatus Hernia ni tundu linalotokea baada ya sehemu ya juu ya mfuko wa kuhifadhia chakula (tumbo) kuingia kwenye sehemu ya kifua kupitia uwazi unaojulikana kama esophageal hiatus. Kwa kawaida uwazi huu (esophageal hiatus) hupitisha mrija wa chakula kwenda kwenye tumbo yaani esophagus na si utumbo.
Mara nyingi, tatizo hili huonekana kwa takribani ya 60% ya watu wenye umri wa miaka 50 na kuendelea, ingawa pia linaweza kuwapata wale walio na umri wa chini ya huo.
Kuna aina mbili kuu za hiatus hernia
- Sliding type : Kama jina lake linavyomaanisha, aina hii hutokea iwapo sehemu ya juu ya utumbo inaposukumwa juu na kuingia kwenye upenyo wa esophagus hiatus baada ya kutokea kwa ongezeko la presha katika maeneo ya tumbo (increased pressure in the abdominal cavity) na kurudi kama kawaida wakati presha inapopungua.
- Fixing type: Aina hii hutokea iwapo sehemu ya juu ya utumbo inapokuwa kwenye maeneo ya kifua na haishuki chini.
Vihatarishi vya Ugonjwa huu
1. Ongezeko la presha tumboni kutokana na;
- Kunyanyua vitu vizito au kuinama sana
- Kukohoa sana au kukohoa mara kwa mara kutokana na sababu mbalimbali
- Kutapika sana (violent vomiting)
- Kupiga chafya sana (Hard sneezing)
- Ujauzito -Kutokana na mfuko wa uzazi (uterus) kusukuma viungo kwenda juu kutokana na kuongezeka ukubwa wake.
- Wakati wa kujifungua- Kutokana na kuongezeka kwa presha ndani ya tumbo wakati mama anajitahidi kusukuma mtoto. Si wanawake wote wanaopata tatizo hili.
- Kujikamua wakati wa kwenda haja kubwa (straining during constipation)
- Uzito uliopitiliza -Kutokana na kuongezeka uzito ambao unasukuma viungo kwenye maeneo ya kifua kwenda chini na hivyo kuongeza presha tumboni.
- Kujisaidia haja kubwa wakati mtu amekaa - Kutokana na maendeleo ya binadamu, watu wengi sasa hivi wameanza utamaduni wa kutumia vyoo vya kukaa wakati wa kujisaidia haja kubwa, katika tafiti iliyofanywa na Dr Denis Burkitt (1), imeonekana ya kwamba kujisaidia wakati mtu amekaa hufanya mtu kujikamua zaidi na hivyo kuongeza presha ndani ya utumbo (Increased intraabdominal pressure) na hivyo kusukuma mfuko wa kuhifadhia chakula (utumbo) kupitia kwenye upenyo wa esophagus hiatus na hivyo kusababisha hiatus hernia.
2. Tatizo la kurithi (Heredity)
3. Uvutaji sigara
4. Matumizi ya madawa ya kulevya kama cocaine
5. Kuwa na kiwambo hewa (diaghram) dhaifu
6. Msongo wa mawazo (depression)
7. Matatizo ya kuzaliwa (congenital defects).
Dalili na Viashiria
- Maumivu ya kifua
- Kichomi (pleurisy) ambacho kinakuwa kikali sana wakati wa kuinama au mtu anapolala chini
- Matatizo katika kumeza chakula
- Kupumua kwa shida Kutokana na hiatus hernia kupunguza uwezo wa ufanyaji kazi wa kiwambo hewa (diaphragm).
- Mapigo ya moyo kwenda kasi Kutokana na mkwaruzo wa neva inayojulikana kama vagus nerve.
Mara nyingi sana hiatus hernia haioneshi dalili zozote zile isipokuwa inapokuwa kubwa sana. Maumivu na kichomi hutokana na kurudishwa kwa tindikali ya kwenye tumbo (gastric acid) kwenye kifua. Pia tindikali aina ya bile acid na hewa huwa inasukumwa juu kwenye kifua.
Vipimo vya Uchunguzi
1. Barium Swallow X-ray – X-ray ya kuangalia viungo vya ndani, mgonjwa hupewa au huchomwa sindano yenye dawa maalum ambayo huonekana vizuri kwenye X-ray, na baada ya hapo hupigwa picha za X-ray akiwa amekaa au amesimama. Kawaida kipimo hiki huchukua masaa 3-6.
2. Esophagogastroduodenoscopy (OGD) - Mpira maalum wenye taa na camera kwa mbele unaoingizwa mdomoni kwenye mpira wa kupitisha chakula (esophagus) na hutazama kama kuna magonjwa yoyote kwenye esophagus hadi kwenye sehemu inayojulikana kama duodenum.
3. Electrocardiography (ECG)- Kipimo cha kuangalia kama kuna matatizo katika jinsi moyo unavyopiga
4. Chest X-ray- Kuangalia kama kuna magonjwa kama homa ya mapafu (Pneumonia), kama kuna pafu lolote ambalo halifanyi kazi, madhara kwenye moyo (injury to the heart) na pia kuangalia matatizo yoyote yale.
5. Complete Blood Count- Kipimo cha kuangalia wingi wa damu, kuangalia aina mbalimbali za chembechembe za damu kama zipo katika maumbo yao ya kawaida, wingi wao kama ni wa kawaida.
Tiba ya Hiatus Hernia
Kama ilivyoelezwa hapo awali, hiatus hernia mara nyingi haioneshi dalili zozote na hivyo mtu anaweza kuendelea na shughuli zake za kila siku bila madhara yoyote. Tiba ya hiatus hernia inahusisha dawa na upasuaji.
Tiba ya Dawa
- Dawa za kuyeyusha tindikali mwilini (antacids) hutumika kama Gelusil, Maalox nk.
- H2 receptor antagonist –Dawa zinazopunguza kiwango cha utolewaji wa tindikali kama cimetidine, ranitidine nk.
- Dawa ambazo huzuia utolewaji wa tindikali na kuponya tishu za esophagus (Proton Pump Inhibitors) dawa hizi ni omeprazole, lansoprazole nk.
Tiba ya Upasuaji
Upasuaji hufanyika kwa wagonjwa wa dharura au pale ambapo mgonjwa hajapata nafuu hata baada ya kutumia dawa na hali yake inazidi kuwa mbaya. Upasuaji huu hufanywa na daktari wa upasuaji kwa kuchana (incision) kwenye kifua (thoracotomy) au tumbo (laparatomy) na kuvuta sehemu ya utumbo iliyopanda juu kwenye kifua ili kuirudisha katika sehemu yake ya kawaida na kupunguza ule uwazi uliopo kwenye diaphgram, kurekebisha sphincters (nyama zinazosaidia katika kufunga na kufungua uwazi kwenye diaphragm) za esophagus ambazo zimekuwa dhaifu. Pia daktari anaweza kufanya upasuaji huu kwa kuchana sehemu ndogo sana kwenye tumbo na kwa kutumia kifaa maalum chenye kumsaidia kurekebisha henia hii. Aina hii ya upasuaji hujulikana kama endoscopic surgery.
Madhara ya Hiatus Hernia
Madhara ya hiatus hernia hutokana na kurudishwa juu kwa tindikali aina ya gastric acid na hivyo kusababisha ugonjwa unaojulikana kama Gastroesophageal Reflux Disease (GERD).
Madhara haya ni;
- Kichomi
- Ugonjwa wa esophagitis
- Barretts esophagus
- Saratani ya kwenye mpira wa kupitisha chakula (esophageal cancer)
- Kuoza kwa meno (dental erosion)
- Strangulation of the stomach (kunyongwa kwa sehemu ya juu ya tumbo na hivyo kusababisha sehemu hii kukosa damu ya kutosha na hivyo tishu zake kufa na kuoza (ischemic and necrosis)
- Kuzuia pafu kujaa hewa na hivyo kushindwa kutanuka na kusababisha mtu kupumua kwa shida sana.
Jinsi ya kujikinga
1. Kuacha kunywa pombe
2. Kuacha matumizi ya madawa ya kulevya kama cocaine
4. Kula milo midogo mara nyingi kwa siku
5. Epuka vyakula vinavyoongeza kichomi kama chocolate, vitunguu, vyakula vikali, vinywaji venye limau, ndimu nk.
6. Kula chakula cha usiku masaa matatu kabla ya kwenda kulala
7. Pumzika kwa kukaa baada ya kula usilale chini.
8. Nyanyua sehemu unayoweka kichwa chako wakati wa kulala kwa angalau 15cm (6 inches)
9. Punguza msongo wa mawazo
10. Acha kuvuta sigara.
Marejeo
1. Burkitt DP (1981). "Hiatus hernia: is it preventable?". Am. J. Clin. Nutr. 34 (3): 428–31. PMID 6259926
2. Sontag S (1999). "Defining GERD". Yale J Biol Med 72 (2-3): 69–80. PMC 2579007. PMID 10780568
No comments:
Post a Comment