Saturday, March 17, 2012

WANAUME TUSIWALAZIMISHE WAKE ZETU KUWA NA ‘VIDUMU’

KATIKA mapenzi ya sasa, mahaba ‘chakula cha usiku’ yanapewa nafasi kubwa sana katika kuleta furaha kwa wawili waliotokea kupendana kwa dhati.
Asikuambie mtu, kumnyima mpenzi wako penzi wakati anapolihitaji unamuumiza kuliko maelezo na anaweza kufikia hatua ya kuhisi humpendi. Atafikiria hivyo kwa kuwa umemnyima raha aliyotarajia kuipata kutoka kwako.
Hapa tunatakiwa kufahamu tu kwamba, furaha ya maisha ya binadamu yeyote inakamilika kwa kuwa na mtu mwenye mapenzi ya dhati kwake na akapatiwa kila alichotarajia yakiwemo ‘mahabati’.
Katika siku za hivi karibuni kumeibuka tatizo la baadhi ya wanawake kulia kunyimwa ‘mambo’ na waume zao. Mfano wa wanawake hao ni Jastina wa Morogoro ambaye anaeleza kuwa, amefikia hatua ya kutaka kumsaliti mumewe kutokana na kutotimiziwa haki yake hiyo ya ndoa.
“Mimi ni mwanamke bwana, nina hisia na kuna wakati najisikia kabisa hamu ya kukutana na mume wangu faragha lakini sasa mume wangu akirejea nyumbani na nikamwambia kuhusu hilo, anakuwa mkali, eti kachoka!
“Ingekuwa ni siku moja moja sawa lakini yeye kila siku akirudi anakula, analala tena anageukia huko… inakuja kweli? Hivi na mimi nikisema nitafute kidumu changu cha kuniliwaza pale ninapojisikia nitakuwa nakosea?” alilalamika mama huyo.
Malalamiko haya yanaingia akilini licha ya kwamba mawazo aliyonayo Jastina ambayo naamini wapo wengine walio katika mazingira kama hayo siyo sahihi. Mke ana haki ya kupewa ‘chakula cha usiku’ na kama kuna sababu za msingi ni suala la wawili kuzungumza na kuafikiana.
Kitendo cha mume kumbania penzi mkewe kwa maelezo kwamba amechoka kutokana na kazi za kutwa nzima kinaweza kuchangia usaliti katika ndoa.
Najua katika maisha ya sasa watu hasa wanaume wanatumia muda mwingi sana kusaka fedha kwa kufanya kazi na mwisho wake wakirudi nyumbani wanakuwa wamechoka kiasi cha kutokuwa na hamu ya kufanya mapenzi. Lakini sasa ni sahihi kwa wanandoa kukaa muda mrefu bila kupeana mambo? Jibu ni hapana!
Kama ni hivyo, nawashauri wanaume wanapofanya kazi wakumbuke kuna wake zao wapendwa wanawasubiri nyumbani. Wakumbuke hawajaoa kazi bali wameoa wake licha ya kwamba kazi nayo ina umuhimu wake.
Pia kuna jambo ambalo wanaume na hata wanawake hawalijui vizuri, hili ni lile linalohusu mazoezi. Unapofanya mazoezi unawezesha damu kuzunguka na kufika sehemu zote za mwili kwa kiwango kinachotakiwa.
Kukaa ofisini kutwa nzima na kurudi nyumbani na kukaa kwenye kochi kisha kuangalia TV siyo aina ya maisha inayoshauriwa tuishi. Mwili unapochangamka kwa damu kufika kila mahali kwa kiwango kinachotakiwa hamu ya kutoa ‘chakula cha usiku’ na kukipokea huwa kubwa.
Lakini wanawake nao kuna wanaoishi kizamani sana. Hawa ni wale wanaosubiri waume zao wawachokoze, wasipofanya hivyo, basi hata mwaka watakaa wakilalamika kwamba hawapati ‘chakula cha usiku’.

No comments:

Post a Comment