Sunday, March 18, 2012

Heri upweke kuliko mpenzi asiyejua maana I

MAPENZI yana siri kubwa. Kila mmoja ana ugonjwa wake wa kupenda. Wengine wanawapenda wapenzi warefu, lakini kuna kundi ambalo huchanganyikiwa zaidi kwa wafupi. Pamoja na mchanganuo huo, kuachwa inauma hata kama anayekutosa hukuwa na mapenzi naye.

Ile dhana tu ya kuachwa ndiyo hutesa watu. Kuna dhana kwamba anayeacha mara nyingi hujiona mshindi dhidi ya aliyemuacha. Na hiyo ndiyo sababu ya wengi kuumia wanapofungiwa milango ya kukatisha uhusiano ambao pengine hata hawakuwa na masilahi nao.

Mathalan, mwanamke anaweza kuwa havutiwi na mtu aliyenaye kwa maana moja au nyingine. Ilitokea kuwa naye kama ajali tu! Kutokana na kutokuwa na hisia naye, hakuona tatizo kumsaliti kwa mwanaume mwingine, lakini huwezi kuamini siku akiambiwa basi, atalia machozi na kuomba msamaha.

Si kwamba atalia kwa sababu ya mapenzi ya dhati aliyonayo kwa mwenzi wake, kwamba inamuuma kuachana naye, ila kinachomtesa ni zile hisia za kuachwa. Na ingetokea kuwa yeye ndiye anayeamua kuacha, tafsiri ingekuwa kinyume chake.

Macho yangekuwa makavu na ikiwezekana angekwenda kusimulia kwa marafiki: “Aah, James nimempiga chini kanililia huyo!” Anafurahi dada yetu na wenzake watampongeza kwa kugongesheana viganja!

Tatizo kubwa ambalo linawagharimu wengi ni kuwa mapenzi yanabebwa kama aina ya mchezo wa kuigiza. Watu wanaingia kwenye uhusiano kwa kujaribu. Kuna waliofunga ndoa si kwa kuchaguana, isipokuwa walidanganyana kwa hisia za “mapozeo” mwisho wa siku wakazoeana, ikawa ngumu kuachana.

Wapo wanaoingia kwenye ndoa si kwa kuvutwa na nyoyo zao, ila wanakabiliwa na fikra za “waoaji wenyewe hawapo, acha nimkubali huyu huyu!” Mapenzi ni nguzo maalum mno kwa maisha ya binadamu, kwa hiyo ni vema yabebe heshima inayostahili.

Ogopa sana mtu anayekuwa na wewe kwa sababu haoni chaguo lake. Adhabu yako ni kubwa mbele ya safari ingawa unaweza kujiona upo kwenye bwawa la asali mwanzoni. Kiama chako ni pale atakapomuona anayedhani ndiye sahihi kwake. Utasilitiwa upende usipende!

Nimekuwa nikisisitiza hili kuwa ni bora kuacha kumsogelea kabisa kuliko kumdanganya unampenda wakati unamcheza shere. Ukatili wako ni mkubwa kwa maana yeye anaweza kudhani amefika na akatuliza ‘mizuka’ yote, hivyo akapandikiza matarajio juu yako.

Siku atakapojua haupo naye atajisikiaje? Unaweza kuua bila kukusudia kwa sababu binadamu tumeumbwa na roho tofauti. Utamuona aliyekunywa sumu kwa mapenzi ni mjinga kwa sababu hayajakufika. Kuna waliosema wao ni ngangari lakini ukurasa ulipofunguka kwao, waliona dunia chungu.

USIJARIBU MAPENZI

Dhana ya mapenzi duniani kote inaelekeza kwamba asili yake ni moyoni. Hii ina mantiki kuwa ndani ya kila mtu kuna vitu ambavyo anahisi kuhitaji mwenzi wake awe navyo. Sura, umbo na tabia.

Hata hivyo, kuna nakshi nyingi ambazo si za lazima lakini hutokea kuwavutia watu na kufunika hata yale ya msingi.

USHAURI: Zingatia sifa muhimu na kuachana na vionjo vya ziada (accessories).
Kuna mwanamke yeye huvutiwa na mwanaume mwenye kucha ndefu.

Ukimuuliza, anakwamba basi tu napenda. Mwingine anaweza kusema: “Nikiwa naye napenda kuichezea, naskia raha!” Yupo atakayekueleza: “Ile kucha yake akinipitishia mgoni au shingoni kwangu taabani!”

Ni vionjo tu vya ziada! Kuna wasiotaka mambo mengi ila wakikutana na watu ambao wananukia ni balaa! Wapo watakaosema wanataka wachangamfu, ingawa mapepe yakizidi nayo ni tatizo kubwa, ila mwingine atadai anahitaji mpenzi anayejua Kiingereza.

Ipo sifa nyeti kwenye dimbwi la mahaba. Kama karata zako unazicheza vizuri kwa mwandani wako na kuhakikisha kila mnapoachiana anakuwa ameridhika kwa 100% ni turufu ya kulinda penzi lako.

JAMBO MUHIMU KWAKO

Penda kujiona mtu nambari moja kwa ubora kwa sababu Mungu aliona una umuhimu ndiyo maana akakuumba. Linda thamani na heshima yako, usikubali mapenzi yakuondolee nguvu ambayo Mfalme wa Mbingu na Ardhi amekupa.

Ni rahisi kudharauliwa ikiwa utakuwa na mtu ambaye hana mapenzi ya dhati na wewe. Atakusaliti, watu watazungumza pembeni. Atakusema vibaya, ukipita mitaani utaonekana kituko. Mpenzi mwenye uelewa na anayekupenda kwa dhati, atakulinda mahali popote.

Hatakusaliti, ataishi ndani yako. Linalokuuma, litamtesa. Wasiokupenda atawachukia. Marafiki zako atawageuza ndugu. Kinyume chake ni kwamba mwenzi asiyekupenda kwa dhati, si ajabu akashiriki kukumaliza.

Kuna watu hawaoni hili umuhimu, mpenzi maana yake ni msiri wa maisha yako. Unapokuwa umelala fofofo hujitambui, ubavuni kwako yupo yeye. Anaweza kukufanya lolote wakati wewe unaogelea ndotoni. Mpende akupendaye, vinginevyo utakumbana na maumivu yafuatayo;

HATOKUSIKILIZA IPASAVYO

Mapenzi ni hisia. Ni rahisi kwako kujua kwamba uliyenaye anakupenda kwa dhati mnapokuwa mnazungumza. Je, anakusikiliza kiasi gani?

Mtu ambaye hana mapenzi na wewe, hata umwambie kwa lugha gani hawezi kukuelewa. Tena inawezekana ulizungumza naye jana kwa herufi kubwa, lakini leo jua limechomoza anarudia yale yale.

Inawezekana ulimuonya kuhusu tabia ambazo zinakufanya heshima yake ipotee. Hakatazwi kuwa na marafiki wa jinsia nyingine, lakini mazoea yake siyo mazuri kiasi kwamba wanaweza kutembea barabarani wameshikana viuno. Ikiwa unamueleza habadiliki, huyo hakupendi.

Hakusikilizi kwa sababu hana hisia na wewe.

No comments:

Post a Comment