Wanasayansi wamegundua seli asilia (Stem Cells) kwenye mayai ya mwanamke (Ovaries) ambazo baadae zinaweza kutengeneza kiwango kikubwa kisicho na ukomo cha mayai ya uzazi ya awali (Oocytes).
Kwa kawaida mwanamke huwa na mayai mengi ya uzazi ya awali (Oocytes) wakati akiwa kwenye tumbo la mamake yaani bado akiwa kijusi (Fetus) ambapo anakadiriwa kuwa na mayai milioni 7, na mayai hayo kupungua hadi kuwa milioni 1 wakati anazaliwa na kufikia mayai 300,000 wakati wa kuvunja ungo au kubaleghe. Mayai haya huisha kabisa akifika umri wa miaka 40 hadi miaka ya mwanzoni ya 50 (yaani kipindi cha ukomo wa kupata hedhi), na hii ndio huchangia mwanamke kutokuwa na uwezo tena wa kushika mimba ambao ni tofauti na wanaume ambao bado wanakuwa na uwezo wa kutoa shahawa hata wakiwa wazee.
Utafiti huo uliofanywa na wanasayansi katika hospitali ya Massacheutts nchini Marekani ambapo wanasayansi hao waliweza kuzitenganisha seli hizo kwenye maabara na kutengeneza mayai ambayo wamesema yanauwezo wa kurutubishwa (fertilized) na kuwa mimba.
Kutokana na utafiti huu, wataalamu wengi wa afya wamesema matokeo ya utafiti huu yatabadilisha kabisa tiba ya ugumba kwa wale wanawake wasioweza kushika mimba na pia yanaweza kusaidia wanawake kuwa na uwezo wa kushika mimba kwa muda mrefu zaidi kuliko ilivyo hivi sasa.
Ugunduzi huu ni changamoto kubwa wa dhana ya kwamba wanawake wana kiwango maalum cha mayai ambacho kikishaisha hawawezi tena kutoa mengine na hivyo kukosa uwezo wa kushika mimba tena.
Mayai hayo yaliyozalishwa maabara yalikuwa ya kawaida na hata yalipopandikizwa kwenye tishu ya mayai ya uzazi ya kawaida ya binadamu (Living human ovarian tissue) ambapo hapa walitumia panya, yalikuwa kama kawaida kwa muda wa wiki mbili. Ikumbukwe ya kwamba tafiti nyingi za mambo ya uzazi hufanywa kwenye panya kutokana na kuwa na maumbile ya uzazi yanayoshahabiana na ya binadamu.
Dk Jonathan Tilly ambaye aliongoza utafiti huu amesema ‘’Matokeo ya utafiti huu yamefungua milango mipya katika tekinolojia ya tiba ya ugumba kwa wanawake na pengine pia yanaweza kutumika kuchelewesha kushindwa kufanya kazi kwa mayai ya mwanamke (Delay timing of ovarian failure)’’.
“Hizi seli za asilia, zikiwekwa nje ya mwili wa binadamu zinafurahia kuzalisha mayai mapya zenyewe na kama tutaweza kuongoza hatua hii basi kuna uwezekano hapo baadae tukawa na uwezo wa kuzalisha mayai mengi ya uzazi ya binadamu bila ukomo wowote ule” Mwisho wa nukuu.
Timu yake iliweza kugundua seli hizi za asilia wakati wakitafuta protini maalum ya aina ya DDX4, inayopatika mahsusi katika seli za mayai ya mwanamke.
Kutokana na sababu za kisheria, wanasayansi hao hawawezi kutumia seli hizi kutengeneza kiinitete cha mwanadamu (Embryo). Lakini seli aina hizo hizo zilichukuliwa kutoka kwenye panya zimeweza kutumiwa kutengeneza kiinitete cha panya katika utafiti ulichapishwa katika jarida la Nature Medicine Journal.
Vitengo vingi vya kusaidia kutungisha mimba nje ya kizazi (In Vitro Fertilisation) vinakuwa na mayai ya uzazi machache sana yaliochangiwa na wanawake au vina uwezo mdogo sana wa kuchuma mayai kutoka kwa wanawake.
Wengi wa wanawake katika nchi zilizoendelea wamekuwa wakitoa mayai yao na kuhifadhiwa katika barafu (Frozen eggs) ili waweze kuendelea na mipango yao ya masomo na kazi mpaka hapo baadae watakapo kuwa tayari basi waweze kutimiza ndoto yao ya kuweza kushika mimba na hivyo kupata mtoto.
No comments:
Post a Comment