Sunday, March 18, 2012

MAMBO 5 YA KUEPUKA MARA TU UNAPOCHUMBIWA

Kuna mambo kadhaa ambayo msichana anatakiwa kuwa makini nayo katika kuhakikisha uchumba wake unadumu na kufikia hatua ya kuolewa na kwenda kuanza maisha mapya.
Yapo mengi lakini nitagusia matano ambayo kwa utafiti wangu ndiyo
yamekuwa yakiwafanya wengi wakimbiwe na wachumba wao na kuachwa wakilia.

Mazoea na wanaume

Wapo ambao wamejikuta wakiachwa solemba kufuatia tabia zao za kuwa na mazoea ya kijinga na wanaume.
Yawezekana kabla ya kuchumbiwa marafiki zako wakubwa walikuwa wanaume (Wapo wanawake wa aina hiyo). Unachotakiwa kufahamu ni kwamba hakuna mwanaume anayefurahia ukaribu wa mchumba wake kwa wanaume wengine.
Hata kama hakuna uhusiano wa kimapenzi lakini epuka sana kujichekelesha kwao, kuongozana nao, kukaa nao au hata kuwasiliana nao. Ukifanya hivyo utakuwa unamkwaza mchumba wako na inaweza kuwa moja ya sababu za kukuchenga.

Marafiki micharuko

Ukishachumbiwa, kuna marafiki zako ambao ‘automatikale’ unatakiwa kuachana nao. Nazungumzia wale micharuko ambao hawawezi kukushauri vizuri juu ya maisha yako.
Hata wale ambao wamekuwa wakikushawishi kila wikiendi muende mkajirushe, baada ya kuchumbiwa unatakiwa kujiweka mbali nao ili kumpa amani mchumba wako.

Tabia za kisichana

Ukishachumbiwa wewe si msichana tena, utakuwa ni mama mtarajiwa wa familia yako. Tabia za kisichana kama vile kuvaa mavazi yasiyo ya heshima, kukaa vijiweni kuongea mambo ya umbeya na nyinginezo kama hizo hutakiwi kuendelea kuwa nazo.

Kujifanyisha

Alichokupendea huyo mchumba wako anakijua mwenyewe, kwa maana hiyo unatakiwa kuendelea kubaki wewe kama wewe. Usijifanyishe kwa namna yoyote kama ambavyo baadhi ya wasichana wamekuwa wakifanya.

Eti umeshaolewa

Kuolewa ni mpaka pale mtakapoingia kanisani, msikitini nk na kufungishwa ndoa. Kama bado hamjafika huko, wewe bado ni mchumba tu na hata kwenye ndoa unaweza usifike.
Kwa maana hiyo hutakiwi kuhamia kwa mwanaume kama ambavyo baadhi wamekuwa wakifanya. Unachotakiwa kufahamu ni kwamba kitendo cha wewe kuchumbiwa kisha kuamua kubeba virago vyako na kwenda kuishi na mwanaume ni kuwakosea wazazi.


Msomaji wangu, yapo mengi ya kuepuka mara tu unapochumbiwa lakini haya machache yanatosha kwa leo. Jiangalie tabia zako, zile ambazo unajua wanaume wengi haziwafurahishi, jiepushe nazo ili kumjengea mchumba wako mazingira ya kukamilisha taratibu za ndoa yenu.

No comments:

Post a Comment