Kuna mtu aliulizia juu ya tabia ya mpenzi wake kuonyesha hamuamini kwa kila analofanya, akichelewa kupokea simu, akirudi asimkute, akienda dukani akachelewa kidogo, vyote kwake huonekana ni matatizo.
Tabia hizi ni kero pale mpenzi wako anapoonyesha hakuamini kwa kila unalolifanya. Unajiuliza ni kwa nini akuone si muaminifu na bado yupo na wewe?
Hapa kuna kitu cha kuangalia. Pengine huyo mpenzi wako ana wivu wa kupindukia na kuona kila ukiwa peke yako basi akili yako inawaza kusaliti.
Si kweli, si kila mwanamke akiwa peke yake anawaza ngono, kufikiri hivyo ni kosa kubwa na inaonyesha jinsi wanaume wa mfumo huo walivyo na ufinyu wa kufikiria.
Mwanamke anatakiwa kupewa uhuru wa kufanya mambo ya kimaendeleo ambayo wewe mwenyewe unatakiwa kuwa msimamizi.
Wapo wanaokaa nyumbani kwa vile hawana shughuli lakini hawawazi kufanya ngono tu, tabia ya umalaya ni ya mtu wala si kwa sababu ya kubaki peke yake.
Lakini kuna kitu ambacho napenda kukizungumza kwa wapendanao wote hasa wewe mwenye mpenzi mwenye wivu sana. Unapoona huaminiwi basi jenga mazingira ya kuaminiwa ili uwe huru.
Nina maana gani?
Kuna baadhi wa wanawake huwa hawajui wakiwa peke yao waishi vipi na wakiwa ndani ya uhusiano iweje pia. Wengi hujiwekea mazingira hatarishi ambayo kwa mwanaume yeyote rijali, hawezi kuyakalia kimya.
Mfano: Simu unazopigiwa hazieleweki na wakati mwingine ukakwenda kuzungumzia pembeni, kwa nini mwenzako asihoji? Unatoka nyumbani bila ruhusa hata ukiulizwa huna majibu ya kujitosheleza, kwa nini asihoji?
Unakwenda dukani kwa muda mrefu au unasimama na mwanaume na kuzungumza naye vichochoroni, hata kama hamzungumzii mapenzi lakini mpenzio lazima ahoji.
Mazingira ya kuaminiwa
Kwanza, jiheshimu mwenyewe kwa mavazi na muonekano wako, jiepushe na mazoea na wanaume yaliyopitiliza, jiepushe kugeuza simu kama kichaka cha kuficha maovu yako. Mlindie heshima mwenzio hata akiwa mbali nawe.
Punguza vikao na mashoga wasiokuwa wa lazima. Fanya kile anachokitaka mwenzio na kukiacha asichokitaka, kuwa sehemu ya maendeleo yake, onyesha umeolewa kwa kulisema wazi na siyo kuwa msiri ili kujiweka mbali na wanaume wakware.
Ukivifanya vyote hivi vitamfanya mumeo au mpenzio, akuamini hata akiwa mbali na nyumbani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment