Kwa sababu wanawake nao wanaogopa kuachwa au wanatamani ndoa, kwa kuamini kwamba tendo hilo ni kila kitu wanajikuta wakikubali; sasa hapo inategemea, mwisho unaweza kuwa mzuri au mbaya!
MAPENZI NI NINI HASA?
Kila mmoja anaweza kuwa na maana yake, lakini kimsingi mapenzi hayana maana ya moja kwa moja! Kwa ujumla mapenzi ni hisia zenye msisimko wa pendo la dhati zinazotoka moyoni mwa mmoja kwenda kwa mwingine.
Pendo hukamilika ikiwa wawili hao kwa wakati mmoja watahisi hisia hizo, ingawa wakati mwingine mmoja ndiyo huwa wa kwanza kuanza kuhisi hisia hizo.
Tafsiri hii nimewahi kuitaja mara kadhaa katika makala zangu, kama wewe ni mdau wa kona hii utakuwa unakumbuka, kama ndiyo kwanza unasoma hapa, basi si vibaya maana utakuwa umeingiza kitu kichwani mwako.
Wakati mwingine inawezekana mkajikuta mmependana tangu siku ya kwanza tu mlipokutana, lakini wengine huchukua muda mrefu kidogo kabla hisia hizo hazijachukua nafasi sawasawa. Wapo wanaofikiria mapenzi ni ngono au ngono ni sehemu ya mapenzi. Hawa nitapingana napo kwa nguvu zangu zote.
HAKUNA ugonjwa mbaya kama utumwa wa fikra. Yaani uwezo wako wa kufikiria kuwa mikononi mwa mtu. Kwa maneno mengine naweza kusema kwamba, kukubaliana na jambo ambalo huna uhakika nalo, lakini kwa sababu wengi wanaamini na wewe unafuata mkumbo bila kuangalia athari zake.
Eti wakifanya mapenzi na wapenzi wao, ndiyo wataonesha kuwa wanawapenda! Ni sahihi kweli? Si sawa...
Msichana ambaye ameutunza usichana wake kwa miaka 22, auharibu kwa mtu mwenye tamaa zake halafu amuache? Nasema hapana...ni afadhali uendelee kuvumilia mpaka kwenye ndoa. Kwanza hakuna uvumilivu hapo; uvumilie nini wakati hujawahi kujaribu?
Heshima ya usichana wako ni zawadi nzuri sana kwa mwanaume ambaye ameitambua thamani yako na kuamua kufunga na wewe ndoa. Huyo ndiye anayestahili. Ikiwa utaamua kwa hiyari yako kutoa penzi, ni wewe tu, lakini isiwe kwa sababu ya kuonesha mapenzi.
LAZIMA NGONO?
Hakuna ulazima, wala faragha si kiashirio cha mapenzi ya dhati. Ngono ni kitu kingine na mapenzi ni kitu kingine. Hivi ni vitu viwili ambavyo havina uhusiano wowote. Asitokee mtu akakudanganya kwamba kwa kutoa penzi ndipo utaonesha unavyompenda. Si kweli. Kimsingi ngono huja baada ya tamaa kuingia kati ya wawili wanaopendana.
Hata hivyo, kuna uwezekano mkubwa, ukawa na tamaa ya kufanya ngono na mtu hata kama huna mapenzi katika moyo wako. Kimsingi suala la kufanya ngono siyo kithibitisho cha kuonesha mapenzi ya dhati.
Baadhi ya walio katika uhusiano, hudanyanywa na kipengele hiki. Utakuta msichana anaambiwa na ‘boyfriend’ wake kwamba ili aoneshe kuwa anampenda basi lazima akubali kufanya naye ngono.
Hata hivyo, baada ya kumaliza kufanya hivyo, kuna uwezekano mkubwa wa penzi hilo kuyeyuka! Ni kweli ni rahisi kuachwa kwenye mataa hasa kama mhusika alikuwa ameshikwa na tamaa badala ya mapenzi ya dhati.
MUDA GANI NI SAHIHI?
Kimsingi suala la kufanya mapenzi halina kanuni, hakuna muda maalum wa kuanza kufanya mapenzi na mpenzi wako mpya. Ngono ni hisia tu, tena basi huwa bora zaidi kama hisia hizo zikaja kwa wakati mmoja kati yako na huyo unayempenda.
Wataalam wa saikolojia ya mapenzi, wanashauri wapenzi wasishiriki tendo hilo mpaka pale watapokuwa wamefahamiana kiasi cha kutosha juu ya tabia zao na historia waliizopitia. Pamoja na hayo, suala la ngono halikwepeki ikiwa mtaruhusu kukutana sehemu tulivu mkiwa wawili.
Jambo la msingi ni kutulia na kujipanga, msifanye ngono kama sehemu ya mapenzi. Tambua kuwa ngono ni kitu kingine na mapenzi ni kitu kingine. Hata kama mtakuwa mmeamua kushiriki kitendo hicho, mfahamu kuwa mnastarehesha nafsi zenu tu na siyo kuoneshana mapenzi ya dhati.
TATIZO LIKO WAPI?
Tafiti mbalimbali za wataalam wa mambo ya uhusiano, zinaonesha kuwa wengi walio katika uhusiano huwa hawawezi kuvumilia kuendelea kuwepo katika uhusiano bila ya kufanya mapenzi. Hata hivyo, tafiti hizo za uhakika zinaeleza kuwa baada ya wapenzi kufanya ngono, ile hamu ya kuendelea kuwa pamoja hupungua!
Hiyo husababishwa na dharau za kimaumbile na kujihakikishia kuwa hakuna kitu asichokijua kwa patna wake. Wengi hulia baada ya kujikuta wakiingia katika mkumbo huu. Hebu jiulize, kama anakupenda, kwa nini ang’ang’anie kufanya mapenzi haraka?
Wewe ni wake na huenda mna ndoto za kuishi pamoja siku moja, kwa nini asivumilie mpaka wakati huo? Akitaka anaweza kuvumilia na kufaidi mambo hayo mkiwa katika ndoa.
NINI BADALA YA NGONO?
Yapo mambo mengi sana ya kufanya badala ya ngono, huna sababu ya kutoa kipaumbele kwenye ngono wakati kuna vitu vingine vingi unavyoweza kuvifanya na kuyafanya mapenzi yenu yakaendelea kudumu kila siku.
Mnaweza kukaa sehemu nzuri yenye utulivu kwa ajili kupanga maisha yenu ya baadaye. Epukeni sehemu zenye vificho, ambazo zinaweza kuwapa vishawishi vya kufanya mapenzi. Lakini pia, kutoka pamoja mitoko maalum hususan wikiendi hunogesha zaidi mapenzi.
Hata hivyo, kutumiana zawadi ni njia nyingine ambayo inaweza kunogesha penzi lenu na kuweka mambo ya ngono pembeni. Amini usiamini rafiki yangu, suala la faragha si muhimu sana katika uhusiano hasa unapokuwa mchanga. Mkifikia uamuzi huu ni lazima wote wawili mjadiliane na kufikia muafaka kabla ya kukimbilia, mwishowe ukaingia kwenye majuto.
No comments:
Post a Comment