Hivi karibuni mama mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Sarafina aliniambia jambo la kusikitisha sana na kama wewe ni mmoja wa watu walio kwenye ndoa au unayetarajia kuingia kwenye maisha hayo, naamini utajifunza kitu.
Mama huyo mkazi wa Kimara jijini Dar anasema: “Mume wangu hivi karibuni alichukua simu yangu na alipoipekua alikuta sms ya mwanaume ambaye kusema ukweli simjui.
“Inavyoonekana huyo jamaa alikosea namba na alikuwa akimtumia mtu wake akimwambia kuwa amefurahishwa na mapenzi aliyompatia jana yake. Nilijitahidi kumwambia mume wangu kuwa huyo mwanaume simjui lakini aling’ang’ania kuwa namjua.
“Nilimsihi asinihukumu kwa kwa kosa ambalo sijalitenda lakini hakunielewa na hapa ninapoongea nina wiki sijakutana naye faragha. Anachelewa kurudi nyumbani na akija nikimwambia ‘nimemmisi’ anakuwa mkali.”
Maneno ya Sarafina yaliniumiza sana na nikaona sehemu ya kuweza kulizungumzia hili ni hapa kwenye mashamsham. Kwa kweli kukoseana tunakoseana lakini ifike mahali linapotokea tatizo kwa wawili waliopendana, ufumbuzi upatikane haraka na isifike hatua ya kununiana na hata kunyima ‘chakula cha usiku’ bila sababu za msingi.
Wapo wanandoa ambao wakikoseana kidogo tu adhabu ni kunyimana penzi, jamani hivi hamjui unapomnyima mpenzi wako haki yake hiyo unamsukuma kukusaliti? Wangapi leo hii wamesababisha waume zao kutafuta nyumba ndogo baada ya kunyimwa vile walivyostahili kupewa na wake zao?
Jamani ifike wakati tuwe makini na maamuzi tunayoyachukua, tusichukue yale ambayo yatatufanya tujute. Hebu jiulize leo unambania mumeo chakula cha usiku eti kwa sababu tu hali ni ngumu, hakuacha fedha za kutosha kwa matumizi, hivi ukimkuta katulizwa na mwanamke mwingine utajisikiaje?
Makala haya yawe fundisho kwako, kosa dogo lisiwe sababu ya kunyimana penzi, ombaneni msamaha yaishe na muendelee kupeana raha. Tabia ya kunyimana inaweza kuleta madhara makubwa kwenye uhusiano wako na ukajuta.
No comments:
Post a Comment