KUMEKUWA na tabia za watu kuingilia matatizo ya wengine wakionyesha kutaka kutoa msaada ambao baada ya muda huwa kinyume cha matarajio. Badala ya kutengeneza wanaharibu kabisa.
Inakuwaje umekosana na mwenzako pengine kosa lenyewe lipo katika maisha yetu ya kila siku, kwa vile si wote tuliokamilika, lakini watu walishikie kidedea?
Kwa hali hiyo, tatizo lolote la ndani ya nyumba ukilitoa nje laweza kuwaangamiza ninyi wote. Unatakiwa kujua kuwa si wote wanaofurahia utulivu wa uhusiano wenu.
Kwa nini?
Kumekuwa na matukio mengi ambayo kwa hali ya kawaida huonekana si makubwa sana, lakini cha kushangaza yakifika kwa baadhi ya watu hutengenezewa mazingira ili wapendanao watengane.
Mara nyingi kunapotokea tatizo ndani ya uhusiano, unatakiwa kujua kuwa si wote huwa washauri wazuri, ndiyo maana kuna siku nilielezea sababu za mtu kutousemea moyo wa mwingine.
Uvumilivu
Huu ndiyo uliobeba mambo mengi katika uhusiano na ndiyo ambao umechangia wengi kuishi pamoja kwa muda mrefu katika ndoa zao. Si kwamba katika maisha yao waliishi kama malaika, bali walivumiliana.
Kuna kipindi mazungumzo yao ya ndani yalishindikana lakini wazazi au watu wenye busara walipowakalisha chini, waliwasikiliza na kumaliza tofauti zao.
Naamini wapo ambao kutengana kwao kulitokana na kukosa uvumilivu, hata huyo anayekutengenezea mazingira ya kukupatanisha na umpendaye, yawezekana ana matatizo makubwa lakini imekuwa ni siri yake.
Inashauriwa kuwa tutenganishe ndoa za watu zilizokosa mapatano ya wahusika moja kwa moja, lakini kwa yale matatizo ya kawaida, ni vema kupatanisha na si kuvunja.
Kuna baadhi ya ndoa za watu zimevunjika kwa vile aliyepelekewa hajui thamani yake, akatoa uamuzi kutokana na akili yake na si kuangalia faida na hasara kwa yale anayoyasema.
Hii imekuwa ikitokea mara kwa mara katika jamii yetu, mtu akikueleza tatizo lake badala ya kumpa ushauri wa kujenga wewe unabomoa kabisa.
Nitoe neno
katika ulimwengu wetu, kukosana ni sehemu ya maisha ya mwanadamu, mnapokosana kitu cha kwanza itafute suluhu ya ndani kwa kuzungumza na mwenzako, pengine alifanya kwa hasira lakini akitulia anaweza kugundua kosa lake.
Pili, kama ndani itashindikana basi tumieni wazazi wa pande mbili au watu wazima wenye busara, ikishindikana na hapo mnaweza kwenda mbele zaidi hata katika mabaraza ya usuluhishi, lakini kwa waliokubali moyoni mwao kuwa kitu kimoja, huwa ni wepesi kujirudi na kumaliza tatizo lao.
Namalizia kwa kusema, linapotokea kosa lolote usikurupuke kwanza kulipeleka mbele za watu, lipime kama ni bahati mbaya au makusudi, je, wewe upo sahihi kila siku? Ukipata jibu ni rahisi kumsamehe mwenzako.
Jiepushe kila tatizo lako la ndani kulitoa mbele za watu pia usikubali kila ushauri, upime kwanza kabla ya kuupokea na kuufanyia kazi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment