Siku zote hatutaacha kuzungumza juu ya mapenzi kwani ni ukweli usiopingika kwamba mapenzi yanachukua nafasi kubwa sana katika maisha yetu.
Tunafanya kazi usiku na mchana, tunahangaika huku na huko, lakini mwisho tunafikiria jinsi gani tutaboresha na kufurahia maisha na wapenzi wetu.
Mpenzi msomaji wangu, katika maisha ya kimapenzi uaminifu ni kitu cha msingi. Bila uaminifu baina ya wawili waliotokea kupendana, hakuna mapenzi na hata safari yao inaweza isifike mbali.
Kwa sababu hiyo ndiyo maana wataalam wa mapenzi mara kwa mara wamekuwa wakizungumzia suala hili kwa nguvu zote wakiamini ni mhimili muhimu sana katika mapenzi.
Ifahamike kwamba uaminifu unaweza kujengwa. Kwa mfano unaweza kuingia kwenye uhusiano na mtu kisha ukapata malalamiko kutoka kwake kuwa, wewe si muaminifu. Katika mazingira haya ni suala la kujiangalia tu na ili kuepusha mgogoro, tengeneza mazingira ya kumfanya huyo mpenzi wako akuamini.
Unafanyaje? Zifuatazo ni baadhi ya mbinu zinazoweza kukusaidia katika kujenga uaminifu katika ndoa yako:
1. Kuwa mkweli
Hakuna kitu kibaya kama kuwa muongo kwa mwenzi wako. Unamfanya aamini kwamba wewe si muaminifu kwake na ndiyo maana unadanganya bila sababu za msingi. Kwa maana hiyo unachotakiwa kufanya ni kuwa mkweli kwake katika kila jambo.
2. Timiza kwa wakati
Uaminifu pia unajengwa kwa kutimiza mambo kadha wa kadha kwa mwenza wako hasa pale unapotoa ahadi. Kwa mfano mmekubaliana mkutane maeneo flani saa 2:00 asubuhi, hakikisha unakuwa pale kwa wakati. Huo ni mfano tu lakini kuna mambo mengi ambayo unatakiwa kumtimiza mtu wako kwa wakati ili kujenga mazingira ya wewe kuaminika.
3. Weka mipaka
Kama wewe ni mwanaume hakikisha unajiwekea mipaka ya mazoea na wasichana wengine. Punguza mazoea yasiyo ya lazima nao kwani hiyo inaweza kumjengea mpenzi wako hisia kwamba unamsaliti.
Epuka kuwapa namba za simu watu ambao wanaweza kukuletea usumbufu kwa mkeo. Epuka utani wa kijinga na watu wa jinsia nyingine. Hii ni kwa mwanaume na mwanamke.
Ukijiwekea mipaka madhubuti utakuwa unamuweka mwenza wako katika mazingira ya kukuamini kwamba huwezi kushawishika kumsaliti.
4. Jiamini mwenyewe
Hili ni la msingi sana. Kama unataka kujenga mazingira ya kuaminiwa anza kujiamini mwenyewe. Kama utashindwa kujiamini hata mpenzi wako hawezi kukuamini na matokeo uaminifu kati yenu hauwezi kuchukua nafasi.
5. Weka mambo sawa
Kwa mfano mkeo anakutuhumu kuwa na uhusiano na mwanamke mwingine. Kumbuka hisia hizo hata kama hazina ukweli usipojitahidi kuziondoa kwake, atajua ni kweli unamsaliti na ataamini hivyo katika kila siku ya maisha yake.
Kwa mazingira hayo elewa uaminifu hauwezi kuwepo kati yenu hivyo unachotakiwa kufanya ni kuhakikisha unamuweka sawa mpenzi wako na kumfanya aondoe hisia hizo. Kwa kufanya hivyo utakuwa umejenga mazingira ya uaminifu kati yenu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment