Sunday, March 18, 2012

Unavyopaswa Kufanya unapoachana na mwenzi wako

Kamwe usithubutu kumshusha thamani mwenzi wako wa zamani. Maneno kama ‘alikuwa hanitoshelezi’ na mengine yenye sura ya kumponda hayana nafasi. Maisha yanaendelea, usipoteze muda wako.

Una mengi yanayohitaji utekelezaji wako. Muda wa kumchukia mwenzi wako wa zamani na ule wa kufanya shughuli kwa ajili ya maendeleo yako, utaupanga vipi?
Watu wengi wamekuwa kama mandondocha kwenye mapenzi yao kutokana na tabia ya kushindwa kuchanganua busara za kuachana. Wanakimbilia kuchukia, matokeo yake wanateseka.

Mantiki ya kumchukia mwenzi wako mliyeachana ni matokeo ya kushindwa kuchukulia hali ya kutengana kwenu kama ya kawaida. Unadhani ni tukio kubwa, hivyo unaupa mzigo mzito moyo wako.

CHUKUA MFANO HUU:
Amos anampenda sana Catherine lakini anajua fika kwamba mwenzi wake hajatulia. Hata hivyo anashindwa kujipanga kuchukua hatua muafaka.

Amos anakuwa mtu wa kulipuka, akiudhiwa na mwenzi wake anatangaza kuachana naye bila kutafakari mara mbili. Haishii hapo, anaamka na chuki mtindo mmoja, hata akimkuta barabarani hamsalimii.

Je, hiyo ni dawa? La hasha, kwa kawaida chuki yako itakupeleka katika mawazo mengi. Utamkumbuka kwa mabaya yake lakini hutaishia hapo, utaanza kuyaona mazuri aliyokufanyia.
Ni kipindi hicho ambacho utaanza kuumia zaidi. Utatamani yale mazuri yake. Inawezekana ukakosa aibu na kujikuta wewe mwenyewe ndiyo unaomba msamaha mrudiane.

Ukiwa na chuki na mwenzi wako, maana yake hisia zako bado zipo kwake. Akija kuzungumza na wewe ni rahisi kumsamehe bila kuzingatia uzito wa kitu alichokufanyia.
Nakusisitiza kujua kwamba kinyume cha mapenzi siyo chuki. Ni kutojali (kupotezea). Yaani unapokosana na mwenzi wako, usianze bifu, badala yake anza kumpotezea na usimjali kwa chochote.

Unahitaji kuwa huru na hisia zako. Unapoamua kuacha basi simamia uamuzi wako. Ukizingatia mambo yafuatayo, yatakupa msaada mkubwa wa kuvuka kipindi kigumu cha kuachana na mwenzako.

1. Mara unapoachana na mwenzi wako, jitahidi kadiri uwezavyo kuhakikisha unasitisha mawasiliano naye. Iwe kwa simu, ana kwa ana na mengineyo.

2. Acha kukaribisha hisia kwamba ipo siku wewe na yeye mtarudiana. Amini kuwa hiyo imetoka jumla, kwa hiyo fanya mambo yako, huku ukiamini kwamba mwenzi wa maisha yako anakuja.

3. Fanya mambo chanya kama vile kujifunza vitu vipya, kuongeza ujuzi, kufanya kazi kwa bidii, kujitolea kwa ajili ya watu wengine, kutoa misaada na kufanya mazoezi ya viungo.

Ukiyafanya haya yatakuwezesha kuondoa mawazo hasi kwa mwenzi wako mliyeachana na kuzingatia vitu vya msingi ambavyo vinahusu ujenzi wa maisha yako ya sasa na ya baadaye.

MUHIMU:
Achana na hulka za chuki kwa mwenzi wako wa zamani. Tangu ulipokuwa mdogo mpaka sasa umekutana na marafiki wangapi ambao wengine leo hawamo kwenye kumbukumbu zako?

No comments:

Post a Comment