Saturday, March 17, 2012

Njia sahihi za kutatua migogoro ya kimapenzi

Siku hazisimami, daima zinasonga mbele kwa mbele. Mungu ambaye ndiye mfalme wa kila kilichomo mbinguni na ardhini, anawezesha mabadiliko ya kutisha ndani ya sayari ya dunia. Hakukosea Judith Wambura ‘Lady Jaydee’ alipoimba Siku Hazigandi.

Kwa kila nukta tunayoivuka, mabadiliko yanayotokea, neema zinazotufikia, mitihani inayotukabili, hatuna budi kumshukuru yeye muweza wa yote. Hakika, mimi na wewe binadamu ni viumbe dhaifu, kwa hiyo hatuna ujanja wa kufanya jambo lolote, isipokuwa kwa matakwa yake.

Tunayatazama mapenzi. Tunatoa mada nzuri ambazo lengo lake ni kukuzindua wewe msomaji wangu ili ufanye tafakuri ya kina kuhusu uhusiano wako. Uziangalie hatua zote ulizopita wewe na mpenzi wako kila siku. Naamini kuwa unajifunza na unafanikiwa.

Aidha, shabaha ya kila mada ni kutengeneza mwanzo wa kikomo cha mateso kwenye mapenzi. Hii ni kukuweka sawa, kuangalia machungu ambayo kwa maana moja au nyingine yanakukabili, hivyo ujipange upya, kurekebisha pale ulipojikwaa kisha unafungua ukurasa mpya ambao hautakuumiza tena.


MIGOGORO, neno hili linamaanisha nini?

Tafsiri: Migogoro ni neno linalomaanisha wingi wa mgogoro ambalo linatafsiriwa kama hali ya kutoafikiana baina ya pande mbili au zaidi. Pia inawezekana ikawa ni sura ya fujo.

Tunapoizungumzia migogoro, kwa hali yoyote ile haiepukiki. Na unapoitaja katika uhusiano ni tatizo lisilo na mwenyewe. Maana ya kusema hivyo ni kuwa kila mtu aliye ndani ya ndoa, uchumba au vinginevyo analia kwa staili yake.

Sababu ya kusema hivyo ni kwamba migogoro ni sehemu ya maisha ya kila mtu ambaye yupo katika uhusiano. Kuna usemi wa Kiswahili kuwa vikombe ndani ya kabati vinagongana, itakuwa watu wawili waliopitia makuzi tofauti?

Hivyo basi, usemi huo ndiyo unaothibitisha uwepo wa migogoro katika uhusiano wa kila mtu, ingawa inatofautiana ukubwa kati ya mtu na mtu, kulingana na staili ya maisha ya wahusika.

Sambamba na hilo, jinsi ya kutatua migogoro ni kipimo kingine kinachochangia utofauti kati ya uhusiano wa mtu mmoja hadi mwingine. Inawezekana pia, hasira, busara na ustahimilivu ulionao ukawa chachu ya wewe kutofautiana na jirani yako.

Sababu hiyo, pia inayo matawi mengi, mojawapo ikiwa kuvunjika kwa uhusiano wa kimapenzi, au kufikia kipindi ambacho makosa yanakuwa hayagawanyiki huku kila mmoja anakuwa hataki kukubali kosa.

Kimsingi, silaha ya kwanza inayoweza kuuokoa uhusiano wowote ule, ni kwa wapenzi wawili kukubali kuwa na wajibu sawa katika kutafuta suluhu ya migogoro yao. Nafikiri hapo tuko pamoja!

Kikubwa ni kuelewa kuwa ni watu wawili ambao hufanya uhusiano wao uwe wenye afya, pia ni katika idadi hiyo hiyo ambayo husababisha penzi lao lisifike popote. Sababu ni ipi na utofauti huu unasababishwa na nini?

Penzi ni fumbo zito, ndiyo maana huwaunganisha hata wale watu wenye njozi zinazosigana. Inawezekana kicheche akadumu kwenye penzi lake mpaka watu wakashangaa, wakati mtu anayesadikiwa ni mtulivu akawa anahama uhusiano mmoja kwenda mwingine kila siku.

Hata hivyo, muhimu ni kujua mbinu ‘tekniki’ za kutatua migogoro.

No comments:

Post a Comment