Ni kawaida kwa watoto kulia. Hata watoto wanaozaliwa na afya njema kabisa wanaweza kulia kwa jumla ya wastani wa kati ya saa moja mpaka matatu kwa siku. Kwa vile watoto hawawezi kujifanyia chochote wao wenyewe zaidi ya kutegemea wazazi, walezi ama watu wengine wanaowazunguka katika kuwapatia chakula, joto, na faraja, kilio ni njia ya mtoto ya kuwasilisha moja ya mahitaji hayo.
Kama mzazi mpya, wakati mwingine inakuwa vigumu kutambua mtoto wako anahitaji nini anapolia. Mzazi anaweza kuwa na maswali kadhaa kichwani mwake, je, mtoto ana njaa, anasikia baridi, ana kiu, anaumwa ama amechoka? Katika siku za mwanzo, hali ya namna hii inawawia vigumu wazazi wengi, wasijue nini la kufanya. Hata hivyo, kwa kadiri siku zinavyopita mzazi mpya ataweza kutambua kuwa kilio cha mtoto wake kinamaanisha anahitaji nini kutokana na mfumo wake wa kulia.
Kadiri watoto wanavyokua ndivyo ambavyo hujifunza hatua mbalimbali za kuwasiliana na wazazi ama walezi wao. Wanakuwa na namna nzuri ya kuwasiliana kwa mfano kwa macho, na kutoa sauti, na hata kutabasamu ambavyo vyote kwa pamoja hupunguza haja ya kulia.
Sababu zinazofanya watoto kulia
Tuangalie sababu kadhaa zinazosababisha mtoto kulia na nini anachotakiwa mzazi ama mlezi kufanya pindi mtoto anapolia.
1. Hitaji la chakula
Njaa ni mmoja ya sababu kubwa inayowafanya watoto wengi kulia. Uwezekano wa mtoto kulia unaendana sana na umri wa mtoto. Kadiri jinsi mtoto alivyo mdogo zaidi ndivyo uwezekano wa kulia sana pindi anapohisi njaa unavyokuwa mkubwa, isipokuwa katika siku mbili za mwanzo baada ya kuzaliwa ambapo watoto hula kwa kiasi kidogo sana. Kwa kawaida katika siku mbili za mwanzo tangu mtoto kuzaliwa, maziwa ya kujilimbikizia mapema sana yaani ‘colostrum’ huwa ni kidogo sana kwa mama walio wengi na huanza kuongezeka kuanzia siku ya tatu baada ya kujifungua. Pia tumbo la mtoto katika kipindi hiki huwa bado dogo sana na hivyo uwezo wake wa kuhifadhi maziwa anayonyonya huwa bado mdogo hali ambayo humfanya mtoto kujisikia njaa. Hivyo kama mtoto wako analia, uwezekano mkubwa ni kuwa ana njaa na hivyo mzazi unashauriwa kumnyonyesha. Inawezekana mtoto asiache kulia mara moja, lakini mama unashauriwa kuendelea kumnyonyesha taratibu na mtoto anaweza kuacha kulia kwa kadiri anavyoburudika na chakula na kuanza kushiba. Iwapo mama unadhani mtoto wako ameshiba lakini bado anaendelea kulia, inawezekana kuna sababu nyingine zaidi.
2. Hitaji la starehe
Baadhi ya watoto wanakuwa na hisia kali pindi vitu kama nguo inapoelekea kumbana sana au iwapo anahisi kuna kitu chochote ndani ya nguo yake kinachomsababishia maumivu. Wapo baadhi ya watoto ambao hawaoneshi kuhangaika pale nepi zinapokuwa zimelowa sababu ya mkojo au kinyesi, kwa vile baadhi yao huihisi joto na hivyo kupendezewa na hali hiyo, wakati watoto wengine hulia na kuhitaji kubadilishwa nguo walizovaa mara moja, hasa kama ngozi zao laini zinasumbuliwa. Ni vyema kwa mzazi ama mlezi kumchunguza mtoto wako kama amechafua nepi na kumbadilisha. Vilevile ni vyema kuangalia kama nguo alizovikwa hazibani na hakuna chochote ndani ya nguo kinachomletea maumivu.
3. Hitaji la kuwa na joto la wastani
Baadhi ya watoto hawapendi kubadilishwa nepi au kuogeshwa. Hawajazoea kuhisi hewa yenye joto tofauti juu ya ngozi zao. Wengi wao hupendelea sana kuwa na hali ya jotojoto lililohifadhiwa. Kwa hiyo ni vyema kumbadilisha mtoto nepi haraka ili kuweza hifadhi joto lake. Inashauriwa pia kutokumvalisha nguo nyingi zaidi ya mahitaji ili mtoto asije akahisi joto zaidi ya analolihitaji mwilini na hivyo kupelekea kuanza kulia.
Inashauriwa pia kutomfunika mtoto kwa mashuka au mablanketi mengi hasa wakati wa kumlaza. Kabla ya kuamua ni kiasi gani cha nguo unachohitaji kumfunika mtoto wakati wa kulala, ni vyema kuangalia kama mwili wa mtoto ni wa moto au baridi isivyo kawaida. Unaweza kufanya hivi kwa kuhisi joto la tumbo lake kwa kutumia kiganja chako. Iwapo mtoto ana joto sana, unashauriwa kupunguza idadi ya nguo za kumfunika vivyo hivyo iwapo unahisi mtoto ana baridi isivyo kawaida inashauriwa kuongeza idadi ya nguo za kumfunikia. Usipime joto la mwili wa mtoto kwa kutumia joto la mikono au miguu yake kwani si kitu cha uhakika na mara nyingi huleta matokeo yasiyo sahihi kwa vile ni kawaida ya mikono au miguu ya watoto kuwa ya baridi.
4. Hitaji la kushikwa ama kubebwa
Baadhi ya watoto wanahitaji kuwa karibu na wazazi wao kwa kubebwa na kubembelezwa. Watoto wakubwa wanapata faraja kwa kuwaona wazazi wao wakiwa karibu na kusikia sauti zao, lakini mara nyingi watoto wachanga wanahitaji kushikiliwa na kubembelezwa kwa faraja. Kama umemlisha mtoto wako na kumbadilisha nepi wakati mwingine mtoto anahitaji kubebwa pia.
Baadhi ya wazazi uhofia kuwa wanaweza kuwaharibu watoto wao kimakuzi pindi wanapowabeba sana. Hiyo si kweli hususani kwa miezi michache ya mwanzo tangu kuzaliwa kwa mtoto. Wakati baadhi ya watoto hawapendi kubebwa, wapo wengine ambao hutaka kubebwa karibu muda mwingi. Iwapo mtoto wako ni wa namna hiyo, unaweza kumbeba mgongoni au kwa jinsi yeyote ile ambayo itakuruhusu kuendelea na shughuli zako nyingine.
5. Hitaji la mapumziko
Ni rahisi kudhani kuwa mtoto atapata usingizi wakati wowote popote pale alipo. Hata hivyo, kwa baadhi ya watoto, hali kama za ujio wa wageni, kelele au hali ya fujo zinaweza kumfanya mtoto kusisimka na hivyo kuwa vigumu kwake kutulia. Watoto wachanga wanaweza kupata ugumu wa kukabiliana na mambo ya kusisimua sana kwa mfano vitu kama taa, kelele, au kubebwa kwa kupokezana kutoka kwa ndugu au mgeni mmoja mpaka mwingine hasa wanapokuja kumtembelea mama. Hali hii humfanya mtoto kushindwa kustahamili na hivyo kuzidiwa na hayo yote. Wazazi wengi wamegundua kwamba watoto wao hulia zaidi kuliko kawaida wakati ndugu au jamaa wakiwatembelea hususani nyakati za jioni. Kama hakuna sababu nyingine maalum inayopelekea mtoto wako kulia, yawezekana basi kilio chake kinasababishwa na uchovu. Mzazi ama mlezi anashauriwa kumpeleka mtoto sehemu tulivu iwe chumbani au sehemu nyingine ambapo patamwondolea hali ya kusisimuliwa na hivyo kumfanya aweze kuacha kulia na kupata usingizi.
6. Hitaji la kitu cha kumfanya mtoto ajisikie vizuri
Iwapo umemlisha mtoto wako na kuhakikisha kuwa yupo vizuri lakini akawa bado anaendelea kulia, mzazi ama mlezi unaweza kuwa na hofu kuwa mtoto ni mgonjwa au ana maumivu. Ni vigumu sana nyakati za mwanzo kwa mzazi kutambua kuwa mtoto wake analia kwa sababu ya kutokuwa na furaha au kuna kitu kinachomuumiza. Mtoto ambaye ni mgonjwa mara nyingi hutoa sauti ya kilio kilicho tofauti na sauti yake ya kawaida. Sauti hii inaweza kuwa ya haraka zaidi au kali sana. Vile vile kwa mtoto ambaye amezoea kulia mara kwa mara, pindi anapoonesha hali ya utulivu isiyo ya kawaida inaweza kuwa dalili ya kwamba ni mgonjwa. Jambo muhimu la kukumbuka ni kwamba hakuna mtu anayemjua mtoto wako vizuri zaidi kuliko wewe. Kwa hiyo basi kama mzazi ama mlezi unahisi kwamba kuna kitu tofauti kwa mtoto wako ni vyema ukaonana na wataalimu wa afya. Wataalamu wa afya daima watayachunguza matatizo ya mtoto wako kwa umakini mkubwa na hivyo kujua sababu ya mtoto kulia. Mzazi ama mlezi unashauriwa kuonana na daktari iwapo mtoto wako ana shida ya kupumua pindi anapolia, au kama kulia kwa mtoto kunaambatana na kutapika, kuharisha ama kutopata choo.
7. Mtoto anahitaji kitu, lakini hujui ni nini
Wakati mwingine unaweza kushindwa kufahamu ni nini kinachomsababishia mtoto wako kulia. Wakati mwingine watoto wanakosa furaha. Hali hii ya kukosa furaha bila sababu inaweza kudumu dakika chache au saa kadhaa ambapo mtoto huendelea tu kulia mara kwa mara. Wakati mwingine baadhi ya watoto hulia kwa muda mrefu huku wakirusha rusha miguu. Hii hali yaweza kusababishwa na maumivu ayapatayo mtoto kwenye tumbo. Kwa kitaalamu hali hii hujulikana kama colic. Huwawia vigumu sana wazazi wengi kukabiliana na mtoto ambaye ana colic. Hakuna tiba ya uchawi kwa colic, aidha ni mara chache sana hali hii inadumu kwa zaidi ya miezi mitatu. Hata hivyo ni vyema kupata ushauri wa daktari pindi unapohisi mtoto wako ana colic.
Je, nini cha kufanya mtoto anapolia?
Kuna vitu ambavyo mzazi unaweza kufanya ili kumpa faraja mtoto wako pindi anapolia. Yawezekana baadhi ya mambo yatakayoshauriwa hapa yasiwasaidie watoto wote, hivyo basi mzazi ama mlezi ni vizuri ukamjua mtoto wako na kufahamu kwa undani ni kitu gani hasa kinachoweza kusaidia kumtuliza.
1. Kumbeba mtoto
Watoto wachanga huonyesha upendeleo fulani wa hisia, kama vile walivyokuwa ndani ya tumbo, hivyo basi unaweza kujaribu kumvingirisha mtoto wako katika blanketi au nguo zozote za kumbebea kama khanga au vitenge ili kuona kama atapenda hali hiyo. Watoto wengine hawapendi kuvingirishwa kwenye blanketi na hupenda aina nyingine ya kupata faraja kama vile kubebwa. Wapo wazazi wanaopenda kumbeba mtoto kiasi cha kumfanya mtoto asikie mapigo ya moyo, kitendo ambacho humpa faraja sana mtoto.
2. Kumwimbia nyimbo au sauti za kumbembeleza
Akiwa tumboni mwa mama, mara kwa mara mtoto alikuwa akisikia mapigo ya moyo ya mama. Hali hii ndiyo sababu kubwa ya watoto wengi kupendelea kubebwa na mama zao. Hata hivyo kuna aina nyingine za sauti zinazoweza pia kusaidia kumtuliza mtoto. Mzazi ama mlezi unaweza kujaribu kuweka muziki wa taratibu au kumuimbia mtoto nyimbo za kubembeleza kwa sauti ya chini sana. Unashauriwa kutokuweka miziki ya haraka au yenye sauti kubwa kwa sababu inaweza kumwondolea hali yake ya utulivu na hivyo kumfanya ashindwe kuacha kulia.
3. Jaribu kumkanda au kumsugua taratibu (masaji)
Kumkanda kanda au kumsugua mtoto taratibu mgongoni au tumboni kunaweza kumsaidia sana kumfariji mtoto. Iwapo inaonekana mtoto anapata tabu wakati wa kubeua au kucheua, jaribu kumlisha akiwa wima zaidi na kila baada ya kumlisha mweke juu ya bega lako na kumsugua taratibu mgongoni ili kumsaidia atoe gesi kwa kubeua. Baadhi ya watoto ambao wana “colic” wakati mwingine hutulia hasa wanaposuguliwa taratibu tumboni na hii huweza kuwafanya wajisikie vizuri kwa vile huihisi kwamba angalau mzazi ama mlezi unajitahidi kufanya kitu fulani kusaidia kumwondolea shida yake.
4. Mpatie kitu cha kunyonya
Kwa baadhi ya watoto waliozaliwa, haja ya kunyonya ni kubwa sana na hivyo kumpatia chuchu safi iliyotengenezwa kwa ajili hiyo au kidole kisafi cha mama inaweza kuleta faraja kubwa kwao. Kunyonya kutamsababishia mapigo ya moyo wake kuwa katika kiwango chake cha kawaida, kupumzisha tumbo lake, na kutulia.
Ulezi wa watoto wachanga ni kitu kigumu lakini ulezi wa mtoto ambaye hulia mara kwa mara ni ngumu zaidi. Kupata msaada na kuungwa mkono wakati unapohitaji msaada ni muhimu zaidi. Mzazi hana budi kufahamu kuwa kwa jinsi siku zinavyopita, na kwa kadri mtoto anavyokua, mtoto anajifunza njia mpya ya kuwa na uwezo wa kuwasilisha mahitaji yake na hivyo ni muhimu mzazi naye kujifunza njia hizo ili kumuwezesha kumpatia mtoto mahitaji yake anayohitaji kwa haraka na wakati unaostahili.
No comments:
Post a Comment