Saturday, March 17, 2012

Mjibu mpenzi wako maswali haya kwa vitendo

Nina imani uliyemchagua kuwa mpenzi wako ni chaguo la moyo wako, hasa nikizingatia kuna wanawake wengi au wanaume wengi lakini upo na huyo uliyenaye.
Inawezekana uliyenaye si wewe wa kwanza kumpenda, huenda yeye alikupenda kabla yako, ila akashindwa kukuanza kutokana na uzito wa mdomo wake au desturi ya mila zetu kuwa mmoja ndiye mwenye uwezo wa kuongea lile linalomsibu juu ya matamanio ya moyo na mwili.
Kwanza lazima tujue kukaa pamoja au kuchagua mpenzi ni bahati nasibu, unaweza ukapenda kiasi cha kufa na kuoza lakini mwenzako yupoyupo hajali mateso ya moyo wako, anachojali ni kuufurahisha mwili wake na siyo kufurahisha nafsi ya mpenziwe ambayo ndiyo inayotaabika.
Nina imani kila atafutaye mpenzi, hutafuta wa kufa na kuzikana, wapo wanaoanza uchumba mpaka ndoa kamili, pia wapo wanaowataka watu kwa ajili ya kuangalia mwanamke ana nini kutokana na sura yake, umbile lake au sauti ambayo hujiuliza akiwa hivi sauti yake ipo hivyo, je, kwenye shughuli inakuwaje?
Mwingine anavutiwa na utanashati wako au pengine ‘u-handsome’ au hata umbile lako la kimazoezi ndivyo vinavyomfanya ajisikie kufanya mapenzi na wewe lakini siyo kwamba anakupenda.
Wapo wanaofuata fedha zako na pale zinapoisha na mapenzi pia huisha. Wapo wanawake duniani wasiojua dunia inakwenda wapi na nini hatima ya maisha yao, hawa wanakutana na wanaume baa na kulala nyumba ya wageni na baada ya hapo hamjuani.
Lakini wapo ambao wana mapenzi ya dhati waliojitoa kimwili na kiakili, siku zote huwa na maswali magumu mioyoni mwao na kuwafanya waishi kwa mashaka kwa kuhofia kukupoteza.
Kama nilivyosema kuchagua mpenzi ni bahati nasibu, hakuna aliye mjuzi wa kuchagua mpenzi aliye safi, inategemea karata uliyofunua. Kama utapata karata nzuri hapo mshukuru Mungu kwa kukupatia mpenzi mzuri mwenye haruma na mapenzi ya kweli.
Nina imani ndani ya mapenzi umpendaye siku zote huumia moyoni na kujiuliza maswali haya ambayo ni wewe wa kuyajibu.
Kwa kupitia kona hii, unatakiwa kuyajibu kwa vitendo kwa kuwa wengi wamekuwa na mapenzi ya mdomoni.

Unajua wapenzi wametoka wapi? Tabu ngapi wamevumilia mpaka kupata mafanikio halafu wewe utokee kama kunguru wa Zanzibar unapitia vilivyo anikwa!
Haah! Wananiudhi sana, siyo siri siwapendi wanaodhurumu haki ya mtu, kwani wanaume wamekwisha au wanawake wamekwisha mpaka umchukue wa mwenzio? Haipendezi.
Wacha tuendelee najua wamesikia, siku zote dawa chungu ndiyo inayotibu.
Eeh! Nilishia wapi wiki iliyopita? Ooh nimekumbuka, niliishia kwa kujiuliza ni maswali gani mpenzio hujiuliza ndani ya mapenzi ambayo unatakiwa kuyajibu kwa vitendo hasa akiwa ana mapenzi ya dhati kutoka chini ya uvungu wa moyo wake?
Akupendaye kwa dhati hujiuliza maswali haya:
Mosi: Je, unaujua upendo wake wa dhati kwako?
Pili: Je, unampenda kama yeye anavyokupenda?
Tatu: Je, mapenzi anayokupa unaridhika nayo?
Nne: Ni kweli yupo peke yake?
Tano: Ni kweli penzi lenu litadumu?
Sita: Je, unampenda kwa sababu gani?
Haya maswali huwa moyoni mwa mtu, mara nyingi mtu hawezi kuzungumza mapema na hubaki kuwa siri yake. siku zote vitendo unavyomfanyia kwa bahati mbaya, humpa maswali mengi juu ya yale anayoyawaza.
Kwa mfano ukichelewa kurudi nyumbani, lazima atakuwa na wasiwasi kwamba una mwanamke au mwanamume mwingine. Mawazo hayo yataleta maumivu moyoni mwake, japo hawezi kuzunguza.
Pia ukimkaripia mwenzi wako, atazidi kujiuliza sana kwani ataona kama humpendi na pengine upo naye kwa shinikizo fulani na si mapenzi ya dhati. Lakini pia suala la kutompa nafasi ya kumsikiliza anachokisema au kushauri, humuumiza sana mpenzio na kuona kwamba karata aliyofunua si dume la mchezo kama alivyofikiria, bali ni galasha.
Kitu kingine ni kutoambatana naye katika safari zako zisizo za kikazi au kwenye sherehe. Katika hilo lazima atajua una mtu mwingine aliye muhimu kwako kuliko yeye.
Kingine ni kutomsifia kwa lolote alilolifanya ambalo alitegemea umsifie lakini wewe ukaona ni jambo la kawaida. Hili nalo humuumiza mpenzi wako na kumfanya ajiulize maswali mengi.
Kwa wanaume, ikiwa mwanamke haonyeshi furaha yoyote akimuona mwenzake amerudi kutoka kazini, yaani haonyeshi kama amemmisi, basi ni lazima aanze kujiuliza kulikoni.
Kutokufurahia zawadi yake anayokuletea na kuonyesha mbele yake kuwa hukuipenda na kuonyesha haupo makini naye hata anapokuaga wakati akielekea kazini, pia humfanya abaki na maswali.
Huna tabia ya kushukuru kwa chochote hata ukipewa busu, kwako sawa. Inawezekana ulikuwa hujui maswali ajiulizayo mpenzio kwa tabia zako. Sasa kama ulikuwa hujui, unatakiwa kufanya yafuatayo bila kuulizwa ili kuifanya nyumba yako ijae furaha siku zote.

Maswali gani ambayo unatakiwa kumjibu mwenzako ambayo huwa vigumu kuyasema kwa mdomo.
Baada ya kutambua maswali, nini cha kufanya?
Unapoanzisha uhusiano unatakiwa kumsoma mwenzako anapenda nini na kipi ambacho hakipendi. Vichukue vyote kisha kaeni chini na kuchambua kimoja baada ya kingine. Angalia mifano ifuatayo:
Mosi
Mpenzi wako anapenda baada ya kazi muwe pamoja, je, kwa upande wako nini kinakufanya usiwe pamoja na mwenzako? Kama kina sababu ya msingi basi kaeni chini na kujadiliana bila kutumia mabavu.

Pili
Mpenzi wako huenda anapenda muoge na kula chakula cha usiku pamoja, kuna sababu ya kukuchelewesha? Kama hakuna ni nafasi nyingine ya kuongeza upendo ndani ya nyumba.
Mara nyingi wafanyakazi huwa mbali na wapenzi wao kwa muda mwingi, lakini inapotokea unaoga na kula pamoja na wenzako, hali hiyo usababisha kuondoa upweke na kumfanya mwenzio ajione upendo wako kwake bado upo juu.
Kumekuwa na matatizo mengi katika uhusiano kwa wanaume wengi kuamini fedha ni kila kitu. Unaweza kumpa kila kitu mkeo kwa kumnunulia nguo, vyakula na kuhakikisha hana shida, lakini huna muda wa kukaa naye badala yake mawazo na akili vyote vipo kwenye kutafuta fedha na kusahau mwenzako naye anakuhitaji.
Hivyo basi pamoja na ugumu wa kazi unatakiwa kutenga muda angalau saa mbili ili kuzungumza na kubadilishana mawazo ikiwemo kula na kuoga pamoja. Siyo kumkuta kitandani na kumuacha kitandani.

Tatu
Mpenzi wako anahitaji umuonyeshe unakijali chochote anachokupatia, kumekuwa na tabia za baadhi ya wanawake kutoshukuru zawadi zisizowafurahisha. Hii inapunguza upendo na kumfanya mwenza wako asiwe na hamu ya kukuletea kitu kwa kuhofia hutakipenda.
Siku zote onyesha kujali kile unachopewa hata kikiwa kidogo, kufanya hivyo ni kuonyesha unajali na kumfanya mwenzako akuletee kikubwa zaidi.

Mwisho
Jiepushe kuwa chanzo cha maumivu ya wenzetu, jaribu kuyafanya yote ambayo hayahitaji nguvu wala fedha kumfurahisha wenzako. Mpende mwenzako kwa vitendo kwa kuyafanya zaidi anayoyapenda na kuyaacha asiyoyapenda.
Muonyeshe unamjali kwa kuwa naye karibu hata kumshirikisha katika mambo yanayowahusu, kwani mwenzako ni sehemu yako, hivyo, ushauri wake ni muhimu. Kama utakuwa umefuatilia tangu mwanzo wa mada hii, nina imani nimeeleweka, kilichobakia ni utekelezaji.

No comments:

Post a Comment