Sunday, March 18, 2012

Kushindwa Kujizuia Kujikojolea /Kupitisha Haja Kubwa kwa Wanawake. (VVF)

Kwa kitaalamu fistula hujulikana kama njia isiyo ya kawaida inayounganisha mfuko wa mkojo na uke, ambayo huruhusu mkojo na/au haja kubwa kutoka bila kujizuia kwenye kuta za uke.

Nini hutokea?

Tatizo la kushindwa kujizuia kujikojolea na/au kupitisha haja kubwa kwenye tupu ya mwanamke linalojulikana kama fistula hutokea baada ya mwanamke kupata madhara kipindi cha kujifungua kutokana na kuwa kwenye uchungu wa kujifungua kwa muda mrefu (Prolonged and obstructed labor), kutokana na kichwa cha mtoto kushindwa kupita kwa urahisi kwenye tupu ya mwanamke.

Hali hii husababisha tishu za kwenye tupu ya mwanamke, kibofu cha mkojo na puru (rectum), kugandamizwa kati ya kichwa cha mtoto na nyonga za mwanamke. Hii husababisha mfumo wa damu kwenye tishu hizi kuharibika na tishu kukosa damu na kuwa katika hali inayojulikana kitaalamu kama ischemic necrosis. Baadaye tundu hutokea kati ya tupu ya mwanamke na kibofu cha mkojo au kati ya tupu ya mwanamke na puru.

Matokeo yake ni mwanamke kutoa mkojo na/au haja kubwa bila kujizuia kupitia tupu yake

Ukubwa wa tatizo

Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) linakadiria kuwa wasichana na wanawake wapatao millioni 4 duniani wanaishi na tatizo hili wakati kila mwaka wasichana na wanawake wengine 50,000 - 100,000 hupatwa na tatizo hili.

Fistula huonekana sana kwenye bara la Afrika na Asia ya kusini. Kwa Tanzania, wanawake na wasichana 1,200 kila mwaka hupatwa na tatizo hili. Katika tafiti mbili zilizofanyika Tanzania, iliripotiwa kuwa wanawake walio katika umri kati ya miaka 22-24 ndiyo hupatwa na tatizo hili zaidi.

VVF husababishwa na nini?

  • Uchungu wa muda mrefu (Prolonged labour) ambao husababishwa na
    • Kutokuwa na usawa wa uwiano wa nyonga ya mama na ukubwa wa mtoto (CPD)
    • Mtoto kulala vibaya (malpresentation)
  • Upasuaji wa kuondoa kizazi (hysterectomy)
  • Upasuaji wa njia ya mkojo (repair of urethral diverticulum, electrocautery of bladder papilloma)
  • Upasuaji wa kansa za nyonga (pelvic carcinomas).

Dalili

  • Mkojo kutoka bila kujizuia kwenye kuba ya uke ndio dalili muhimu
  • Kuna uwezekano wa kupata maambukizi hivyo dalili zifuatazo huweza kuambatana na dalili ya mwanzo homa na maumivu ya tumbo hasa ubavu na chini ya kitovu.

Vipimo

  • Majimaji yanatoka kwenye kuta za uke huchunguzwa vitu vifuatavyo:
    • Urea, creatinine, na potassium ili kuwa na uhakika kuwa ni VVF na sio Vaginitis (maambukizi ya uke)
    • Mkojo huoteshwa kuangalia kama kuna vimelea na kujua dawa gani yaweza kuvimaliza vimelea hivyo
  • Rangi ya indigo carmine hutolewa kwa njia ya mshipa na pindi inapoonekana ukeni huthibitisha VVF
  • Cystourethroscopy
  • Intravenous urogram

Matibabu

Kama tatizo limegundulika siku chache baada ya upasuaji mpira wa kukojolea (urinary catheter either transurethral or suprapubic) huwekwa kwa siku 30. Fistula ndogo (chini ya sentimita 1) huweza kupona yenyewe au kupungua.

Upasuaji ili kurekebisha VVF, aina za upasuaji:

  • V@#ginal approach
  • Abdominal approach
  • Electrocautery
  • Fibrin glue
  • Endoscopic closure using fibrin glue with or without adding bovine collagen
  • Laparascopic approach
  • Using interposition flaps or grafts

Baada ya upasuaji

  • Mgonjwa huwekewa Suprapubic catheter (mpira wa mkojo) kwa siku 6 hadi 60 ili kupunguza mvutano wa nyuzi
  • Vitamin C 500mg mara tatu kwa siku ili mkojo uwe wa asidi ili kuzuia maambukizi na kutengenezwa kwa mawe.
  • Tiba ya kichochezi cha ostrogeni kwa wakina mama walikwisha acha kupata siku zao (postmenopausal)
  • Dawa za kuzuia mshtuko wa mfuko wa mkojo-methylene blue na Atropine sulfate
  • Antibaotiki
  • Pumzisha nyonga kwa kuzuia tendo la ndoa kwa kipindi cha wiki 4 hadi 6. Ingawa wengine hushauri hadi miezi mitatu.

Hiatus Hernia (Ngiri ya Kwenye Kifua)

Hiatus Hernia (Ngiri ya Kwenye Kifua)
Hiatus Hernia ni tundu linalotokea baada ya sehemu ya juu ya mfuko wa kuhifadhia chakula (tumbo) kuingia kwenye sehemu ya kifua kupitia uwazi unaojulikana kama esophageal hiatus. Kwa kawaida uwazi huu (esophageal hiatus) hupitisha mrija wa chakula kwenda kwenye tumbo yaani esophagus na si utumbo.
Mara nyingi, tatizo hili huonekana kwa takribani ya 60% ya watu wenye umri wa miaka 50 na kuendelea, ingawa pia linaweza kuwapata wale walio na umri wa chini ya huo.
Kuna aina mbili kuu za hiatus hernia
  • Sliding type : Kama jina lake linavyomaanisha, aina hii hutokea iwapo sehemu ya juu ya utumbo inaposukumwa juu na kuingia kwenye upenyo wa esophagus hiatus baada ya kutokea kwa ongezeko la presha katika maeneo ya tumbo (increased pressure in the abdominal cavity) na kurudi kama kawaida wakati presha inapopungua.
  • Fixing type: Aina hii hutokea iwapo sehemu ya juu ya utumbo inapokuwa kwenye maeneo ya kifua na haishuki chini.
Vihatarishi vya Ugonjwa huu
1. Ongezeko la presha tumboni kutokana na;
  • Kunyanyua vitu vizito au kuinama sana
  • Kukohoa sana au kukohoa mara kwa mara kutokana na sababu mbalimbali
  • Kutapika sana (violent vomiting)
  • Kupiga chafya sana (Hard sneezing)
  • Ujauzito -Kutokana na mfuko wa uzazi (uterus) kusukuma viungo kwenda juu kutokana na kuongezeka ukubwa wake.
  • Wakati wa kujifungua- Kutokana na kuongezeka kwa presha ndani ya tumbo wakati mama anajitahidi kusukuma mtoto. Si wanawake wote wanaopata tatizo hili.
  • Kujikamua wakati wa kwenda haja kubwa (straining during constipation)
  • Uzito uliopitiliza -Kutokana na kuongezeka uzito ambao unasukuma viungo kwenye maeneo ya kifua kwenda chini na hivyo kuongeza presha tumboni.
  • Kujisaidia haja kubwa wakati mtu amekaa - Kutokana na maendeleo ya binadamu, watu wengi sasa hivi wameanza utamaduni wa kutumia vyoo vya kukaa wakati wa kujisaidia haja kubwa, katika tafiti iliyofanywa na Dr Denis Burkitt (1), imeonekana ya kwamba kujisaidia wakati mtu amekaa hufanya mtu kujikamua zaidi na hivyo kuongeza presha ndani ya utumbo (Increased intraabdominal pressure) na hivyo kusukuma mfuko wa kuhifadhia chakula (utumbo) kupitia kwenye upenyo wa esophagus hiatus na hivyo kusababisha hiatus hernia.
2. Tatizo la kurithi (Heredity)
3. Uvutaji sigara
4. Matumizi ya madawa ya kulevya kama cocaine
5. Kuwa na kiwambo hewa (diaghram) dhaifu
6. Msongo wa mawazo (depression)
7. Matatizo ya kuzaliwa (congenital defects).
Dalili na Viashiria
  • Maumivu ya kifua
  • Kichomi (pleurisy) ambacho kinakuwa kikali sana wakati wa kuinama au mtu anapolala chini
  • Matatizo katika kumeza chakula
  • Kupumua kwa shida Kutokana na hiatus hernia kupunguza uwezo wa ufanyaji kazi wa kiwambo hewa (diaphragm).
  • Mapigo ya moyo kwenda kasi Kutokana na mkwaruzo wa neva inayojulikana kama vagus nerve.

Mara nyingi sana hiatus hernia haioneshi dalili zozote zile isipokuwa inapokuwa kubwa sana. Maumivu na kichomi hutokana na kurudishwa kwa tindikali ya kwenye tumbo (gastric acid) kwenye kifua. Pia tindikali aina ya bile acid na hewa huwa inasukumwa juu kwenye kifua.

Vipimo vya Uchunguzi
1. Barium Swallow X-ray – X-ray ya kuangalia viungo vya ndani, mgonjwa hupewa au huchomwa sindano yenye dawa maalum ambayo huonekana vizuri kwenye X-ray, na baada ya hapo hupigwa picha za X-ray akiwa amekaa au amesimama. Kawaida kipimo hiki huchukua masaa 3-6.
2. Esophagogastroduodenoscopy (OGD) - Mpira maalum wenye taa na camera kwa mbele unaoingizwa mdomoni kwenye mpira wa kupitisha chakula (esophagus) na hutazama kama kuna magonjwa yoyote kwenye esophagus hadi kwenye sehemu inayojulikana kama duodenum.
3. Electrocardiography (ECG)- Kipimo cha kuangalia kama kuna matatizo katika jinsi moyo unavyopiga
4. Chest X-ray- Kuangalia kama kuna magonjwa kama homa ya mapafu (Pneumonia), kama kuna pafu lolote ambalo halifanyi kazi, madhara kwenye moyo (injury to the heart) na pia kuangalia matatizo yoyote yale.
5. Complete Blood Count- Kipimo cha kuangalia wingi wa damu, kuangalia aina mbalimbali za chembechembe za damu kama zipo katika maumbo yao ya kawaida, wingi wao kama ni wa kawaida.
Tiba ya Hiatus Hernia
Kama ilivyoelezwa hapo awali, hiatus hernia mara nyingi haioneshi dalili zozote na hivyo mtu anaweza kuendelea na shughuli zake za kila siku bila madhara yoyote. Tiba ya hiatus hernia inahusisha dawa na upasuaji.
Tiba ya Dawa
  • Dawa za kuyeyusha tindikali mwilini (antacids) hutumika kama Gelusil, Maalox nk.
  • H2 receptor antagonist –Dawa zinazopunguza kiwango cha utolewaji wa tindikali kama cimetidine, ranitidine nk.
  • Dawa ambazo huzuia utolewaji wa tindikali na kuponya tishu za esophagus (Proton Pump Inhibitors) dawa hizi ni omeprazole, lansoprazole nk.
Tiba ya Upasuaji
Upasuaji hufanyika kwa wagonjwa wa dharura au pale ambapo mgonjwa hajapata nafuu hata baada ya kutumia dawa na hali yake inazidi kuwa mbaya. Upasuaji huu hufanywa na daktari wa upasuaji kwa kuchana (incision) kwenye kifua (thoracotomy) au tumbo (laparatomy) na kuvuta sehemu ya utumbo iliyopanda juu kwenye kifua ili kuirudisha katika sehemu yake ya kawaida na kupunguza ule uwazi uliopo kwenye diaphgram, kurekebisha sphincters (nyama zinazosaidia katika kufunga na kufungua uwazi kwenye diaphragm) za esophagus ambazo zimekuwa dhaifu. Pia daktari anaweza kufanya upasuaji huu kwa kuchana sehemu ndogo sana kwenye tumbo na kwa kutumia kifaa maalum chenye kumsaidia kurekebisha henia hii. Aina hii ya upasuaji hujulikana kama endoscopic surgery.
Madhara ya Hiatus Hernia
Madhara ya hiatus hernia hutokana na kurudishwa juu kwa tindikali aina ya gastric acid na hivyo kusababisha ugonjwa unaojulikana kama Gastroesophageal Reflux Disease (GERD).
Madhara haya ni;
  • Kichomi
  • Ugonjwa wa esophagitis
  • Barretts esophagus
  • Saratani ya kwenye mpira wa kupitisha chakula (esophageal cancer)
  • Kuoza kwa meno (dental erosion)
  • Strangulation of the stomach (kunyongwa kwa sehemu ya juu ya tumbo na hivyo kusababisha sehemu hii kukosa damu ya kutosha na hivyo tishu zake kufa na kuoza (ischemic and necrosis)
  • Kuzuia pafu kujaa hewa na hivyo kushindwa kutanuka na kusababisha mtu kupumua kwa shida sana.
Jinsi ya kujikinga
1. Kuacha kunywa pombe
2. Kuacha matumizi ya madawa ya kulevya kama cocaine
3. Kupunguza uzito uliopitiliza
4. Kula milo midogo mara nyingi kwa siku
5. Epuka vyakula vinavyoongeza kichomi kama chocolate, vitunguu, vyakula vikali, vinywaji venye limau, ndimu nk.
6. Kula chakula cha usiku masaa matatu kabla ya kwenda kulala
7. Pumzika kwa kukaa baada ya kula usilale chini.
8. Nyanyua sehemu unayoweka kichwa chako wakati wa kulala kwa angalau 15cm (6 inches)
9. Punguza msongo wa mawazo
10. Acha kuvuta sigara.
Marejeo
1. Burkitt DP (1981). "Hiatus hernia: is it preventable?". Am. J. Clin. Nutr. 34 (3): 428–31. PMID 6259926
2. Sontag S (1999). "Defining GERD". Yale J Biol Med 72 (2-3): 69–80. PMC 2579007. PMID 10780568

Faida za Kiafya za Kitunguu Swaumu (Garlic)

garlic
Kitunguu swaumu ni jamii ya vitunguu ambayo kwa kitaalamu huitwa Allium sativum. Jamii hii ilianza kutumika katika mabara mbalimbali duniani hususani Asia, Afrika na Ulaya takribani miaka 6000 iliyopita. Matumizi makuu nyakati hizo yakiwa viungo katika mboga na tiba.

Kitunguu swaumu kimetajwa kwenye vitabu mbalimbali vya dini vikielezea faida zake katika kutibu maradhi mbalimbali yasababishwayo na bakteria, matatizo katika mapafu, matatizo katika mfumo wa umen'genyaji chakula, na matatizo ya kuishiwa nguvu.

Historia inaonesha kuwa, vitunguu swaumu vilianza kutumika China mwaka 510 K.K na pia vilitumiwa na wanajeshi wa Ugiriki na Roma. Aidha wasafiri wa vyombo vya baharini na vijijini pamoja na wakulima barani Afrika walivitumia sana.

Mwaka 1858, mtafiti na mwanasayansi wa nyakati hizo, Louis Pasteur aligundua uwezo wa kitunguu swaumu katika kuua vimelea mbalimbali vinavyosababisha magonjwa, na hivyo vikaanza kutumika kama dawa ya kusafishia vidonda na kuzuia kidonda ndugu hasa zama za vita ya kwanza na pili ya dunia. Isitoshe, mpaka sasa zipo dawa kadhaa zilizotengenewa kwa kutumia jamii hii ya vitunguu swaumu ikiwemo dawa ya kusafisha mdomo (mouth wash) ingawa watumaiji wake wengi huilalamikia dawa hiyo kwa sababu ya harufu mbaya ya dawa hiyo inayowasababishia kunuka kwa mdomo.

Faida za vitunguu swaumu

Katika tafiti mbalimbali vitunguu swaumu vimeonekana kuwa na uwezo wa kutibu maambukizi ya bakteria, fangasi na virusi vya aina mbalimbali. Aidha husaidia kuzuia magonjwa ya moyo ikiwemo kuondoa lijamu katika mishipa ya damu na hivyo kusaidia katika kurekebisha shinikizo la damu. Faida nyingine za vitunguu swaumu ni pamoja na
  • Kutibu saratani ikiwemo saratani ya tumbo na utumbo mkubwa. Tafiti zinaonesha idadi ndogo ya wagonjwa wa saratani katika nchi ambazo wakazi wake wana utamaduni wa kutumia vitunguu swaumu kwa wingi.
  • Vitunguu swaumu husaidia kudhibiti kiwango cha sukari katika damu. Hata hivyo inashauriwa kwamba wagonjwa wa kisukari wanaotumia sindano za insulin wasitumie kitunguu swaumu kwa wingi mpaka watakaposhauriwa na daktari.
  • Huzuia kusanyiko la chembe sahani zinazosaidia kuganda kwa damu (platelet aggregation)
  • Husaidia ufyozwaji wa thiamin, hivyo kusaidia kuepusha mwili na ugonjwa wa beriberi
  • Ina kiasi kikubwa cha vitamini C ambayo husaidia kuzuia ugonjwa wa kiseyeye
  • Hutumika kutibu magonjwa nyemelezi kama toxoplasmosis, hasa kwa watu wenye upungufu wa kinga mwilini.
Ushahidi wa Kitafiti

Katika utafiti uliofanyika nchini Czech ilionekana kuwa matumizi ya vitunguu swaumu yalisaidia sana katika kupunguza kusanyiko la lijamu (cholesterol) pamoja na mafuta yasiyofaa mwilini (low density lipoproteins) katika mishipa ya damu. Aidha, mwaka 2007 BBC iliripoti matumizi ya vitunguu swaumu katika kusaidia kumkinga mtumiaji dhidi ya aina fulani ya mafua iliyosababishwa na virusi. Mwaka 2010, ulifanyika utafiti mwingine ambao ulijumuisha wagonjwa 50 wenye shinikizo la damu sugu ambalo lilikuwa ni vigumu kudhibitiwa hata kwa matibabu yaliyozoeleka ya dawa na njia nyingine. Kama njia ya kuchunguza ufanisi wa vitunguu swaumu katika kutibu shinikizo la damu, baadhi ya wagonjwa hao walipewa vitunguu swaumu wakati wengine walipewa dawa isiyohusika na matibabu ya shinikizo la damu (au placebo). Ilionekana kuwa wale waliopewa vitunguu swaumu kama dawa ya shinikizo la damu walionesha maendeleo mazuri kwa vitunguu swaumu kuweza kushusha vizuri kiwango cha shinikizo la damu, hususani systolic pressure, tofauti na wale waliopewa placebo.

Nini siri ya kitunguu swaumu?

Sifa kuu zinazokifanya kitunguu swaumu kuwa na uwezo na faida zilizoainishwa hapo juu ni kule kuwa kwake na viasili kadhaa (ingredients) ambavyo vinafanya kazi tofauti tofauti. Uwezo wake wa kiutendaji unatokana na mambo yafuatayo;
  • Vina uwezo wa kusababisha kutanuka kwa mishipa ya damu (vasodilation) kwa kubadilisha polysulfides zilizopo ndani yake kuwa hydrogen sulfides kwenye seli nyekundu za damu.
  • Husaidia uthibiti wa kiwango cha sukari mwilini kwa kushusha kiwango cha kemikali ya homocystine na kupunguza madhara ya kisukari.
  • Iwapo vitapondwa pondwa vizuri, vitunguu swaumu hutoa kemikali iitwayo Allicin ambayo ni dawa dhidi ya bateria, na phytoncide ambayo huua fangasi wa aina mbalimbali.
  • Harufu mbaya ya kitunguuu swaumu hutokana na gesi aina ya hydrogen sulfide ambayo inayotolewa baada ya kuvila.
Nini Madhara ya vitunguu swaumu?

Ukiacha faida zake, vitunguu swaumu pia vina hasara na madhara mbalimbali kwa mtumiaji. Madhara hayo ni pamoja na;
  • Harufu mbaya mdomoni ambayo hutokana na kemikali ya AMS (allyl methyl sulfide). Harufu mbaya hii, hata hivyo, yaweza kupunguzwa kwa kunywa maziwa au kunywa maji mengi.
  • Kwa baadhi ya watumiaji, vinaweza kuwaletea mzio au mcharuko mwili (allergies au inflammatory reactions)
  • Kichefuchefu, Kutapika na kuharisha.
  • Huweza kusababisha hatari ya kuvuja damu, kwa sababu huzuia kazi ya seli sahani (platelets) zenye kusaidia kuganda kwa damu kushindwa kufanya kazi yake vizuri, na hususani kwa mama wajawazito, baada ya upasuaji au mara baada ya kujifungua.
  • Huingiliana katika utendaji kazi wake na dawa kadhaa kama vile warfarin, antiplatelets, saquinavir, dawa za shinikizo la damu kwa ujumla hasa calcium channel blockers, na antibiotiki za jamii ya quinolone kama vile ciproflaxacillin.
  • Aidha, vinaelezwa pia kuwa na madhara kwa wanyama jamii ya paka na mbwa.

Kupungua au Kukosa Hamu ya Kufanya Mapenzi

kukosa hamu ya kufanya mapenzi
Matatizo ya kufanya mapenzi au kujamiana kwa wanawake yanatambulika kama tatizo linalojirudia kwa muda mrefu ambapo huathiri mzunguko wa tendo la kujamiana (kusisimka, kufikia kilele, kurudia) na hivyo kusababisha msongo wa mawazo au kuharibu uhusiano wa mwanamke na mpendwa wake. Tatizo hili huathiri asilimia 43 ya wanawake wa rika zote duniani na huonekana sana kwa wanawake wenye umri kati ya 45-64.
Visababishi vya tatizo hili kwa wanawake ni;
  • Msongo wa mawazo – Asilimia kubwa ya tatizo hili linaweza kutokea kutokana na msongo wa mawazo ambapo huchangiwa na ugumu wa maisha (uchumi), matatizo katika uhusiano (ugomvi, kutoelewana, kutoaminiana au kukosa uaminifu katika uhusiano {infedility} nk) na magonjwa mbalimbali.
  • Kupungua au kukosekana upendo/mapenzi katika uhusiano au ndoa
  • Kujifungua mtoto – Hii ni kutokana na homoni aina ya prolactin kuwa katika kiwango cha juu wakati mama ananyonyesha, homoni hii pia hufanya kazi ya kumfanya mtu kuridhika baada ya tendo la ndoa/kujamiana kwa kuingiliana na ufanyaji kazi wa homoni/kichocheo chengine kinachojulikana kama dopamine (ambayo ndio humfanya mtu kufikia kilele wakati wa kujamiana). Mbali na kunyonyesha, homoni ya prolactin pia huongezeka wakati mtu amelala (usingizi mzito au REM sleep), wakati wa alfajiri, baada ya kufanya mazoezi, kula,baada ya tendo la kujamiana, baada ya upasuaji mdogo na hata baada ya kupata degedege. Sababu nyengine ya kuongezeka kiwango cha kichocheo hiki cha prolactin ni kuwa na saratani katika ubongo (anterior pitituary tumors). Dalili za saratani hii ni pamoja na kutonyonyesha vizuri kwa mama, kukosa hedhi, ugumba kwa wanawake na uhanithi kwa wanaume (impotence).
  • Kupungua mzunguko wa damu katika tupu ya mwanamke na hivyo kusababisha maumivu wakati wa kujamiana.
  • Hypothyroidism – Matatizo ya homoni ya tezi la koo, huonekana sana kwa wanawake kuliko wanaume.
  • Utumiaji wa vidonge vya kupanga uzazi au vya majira kwa muda mrefu
  • Unywaji pombe kupindukia – Kinyume na fikira potofu za watu wengi ambao huamini kwamba unywaji pombe kali huongeza hamu ya kujamiana au kupunguza uzito lakini ukweli ni kwamba pombe kali au kilevi cha aina yoyote hupunguza hamu ya kujamiana na pombe huongeza uzito na kusababisha utapia mlo.
  • Ugonjwa wa kisukari
  • Uvutaji sigara
  • Ujauzito – Kutokana na mabadiliko katika mfumo wa homoni au vichocheo wakati wa ujauzito, na pia kutokana na mabadiliko ya maumbile ya wanawake wakati huu na hivyo kuchangia kutojiamini kwa mwanamke.
  • Uzito uliopitiliza (obesity)
  • Ugonjwa wa mifupa (arthritis)
  • Utumiaji madawa ya kulevya
  • Madhara katika neva inayohusika na kuongeza msisimko wakati wa kujamiana (pudendal nerve damage) wakati wa upasuaji wa kuondoa mfuko wa uzazi kwa mwanamke mwenye matatizo ya uzazi au katika mfuko wa kizazi.
  • Madhara ya dawa – Kama dawa za kutibu shinikizo la damu, antidepressant medication, dawa za saratani nk.
  • Uchovu – Kuzidiwa kwa mwanamke na majukumu ya kulea mtoto/watoto, kazi na kumhudumia mume wake hivyo kusababisha uchovu.
  • Ugonjwa wa moyo
  • Saratani ya aina yoyote ile
  • Kuwa na wasiwasi (anxiety), depression nk.
  • Historia ya kubakwa, au kupata maumivu wakati wa kujamiana hapo awali kutokana na mwanamke kutokuwa tayari kujamiana au kutotayarishwa vyema kabla ya kujamiana au magonjwa ya zinaa.
  • Tatizo la vaginismus – Hii ni tatizo ambalo husababisha tupu ya mwanamke kuwa ndogo wakati wa kujamiana na hivyo husababisha mwanamke kupata maumivu wakati wa kujamiana.
  • Kupenda inataneti kupita kiasi (addiction) – Katika tafiti mpya iliyofanyika mwaka huu nchini marekani, imeonyesha ya kwamba kati ya ndoa 6,000 zilizovunjika asilimia 57 zimesababishwa na mwenza mmoja au wote kupenda kuchat au kutumia intaneti kupita kiasi na hivyo kusababishwa msisimko kupotea kati ya wenza wawili na hatimaye mwisho ni kupungua uwezo au hamu ya kujamiana.
Ni kundi gani la wanawake lililo katika hatari ya kukumbwa na tatizo hili?

  • Wanawake ambao wana historia ya kupungua hamu ya kujamiana
  • Wale ambao wamefanyiwa upasuaji wa kuondoa mayai yao ya uzazi kutokana na sababu mbalimbali
  • Wanawake ambao waliofika umri wa kuacha kupata hedhi (menopause- miaka 42-58)) na kupata dalili mbalimbali kama kutokwa na jasho usiku, kukosa usingizi mzuri na depression.
Kwa wanaume, visababishi vya tatizo la kupungua hamu au uwezo wa kujamiana ni kama ifuatavyo;
  • Msongo wa mawazo kama nilivyoeleza hapo juu
  • Kupungua au kukosekana upendo/mapenzi katika uhusiano/ndoa
  • Unywaji pombe kupindukia kama nilivyoeleza awali
  • Utumiaji wa dawa za kulevya
  • Uvutaji sigara – Hupunguza kiwango na uzito wa shahawa kwa wanaume. Uzito wa shahawa (concentration of spermatozoa in semen) hupungua kwa asilimia 22-57 kwa wale wanaovuta sigara. Uwezo wa shahawa kuogelea kwenye mirija ya uzazi ya mwanamke pia nao hupungua kwa asilimia 20 kwa wale wanaovuta sigara ikilinganishwa na wale wanaume wasiovuta sigara.
Tafiti nyengine zimethibitisha kuwa wanaume wanaovuta sigara wana asilimia kubwa ya kutoa shahawa ambazo hazina maumbile mazuri au ya kawaida na hivyo kuongeza uwezekano wa mimba kutoka (spontaneous abortion) au kuzaa mtoto mwenye maumbile ambayo sio ya kawaida (birth defects). Tafiti mbalimbali pia zimethibitisha kuwa uvutaji sigara huharibu mirija ya seminiferous tubules ambayo hupatikana kwenye korodani na ni sehemu ambapo shahawa hutengenezwa, hivyo uharibifu wake hupunguza wingi na uzito wa shahawa.
Pia uvutaji sigara hupunguza vichocheo aina ya testerone, growth hormone, na nk.Wanaume wenye kiwango kidogo cha testerone huwa na tatizo la kupungukiwa uwezo wa kujamiana na kiwango kidogo cha shahawa.Uvutaji sigara hupunguza mzunguko wa damu unaopita/kwenda kwenye moyo na kwenye uume na hivyo basi kumfanya mwanamume kushindwa kusimika na kupata tatizo la kupungua uwezo wa kujamiana (vascular impotence).
Katika tafiti zilizofanyika, asilimia 97 ya wale waliogunduliwa na tatizo la vascular impotence walikuwa wavutaji sigara na katika tafiti nyengine asilimia 87 ya wale wenye tatizo hili la vascular impotence walikuwa pia wavutaji sigara. Katika tafiti iliyohusisha wapenzi 290 hapo mwaka 1999, ilionyesha ya kwamba wanaume ambao walikuwa wavutaji sigara walifanya tendo la ndoa na wake zao mara 6 tu kwa mwezi mzima na wale ambao hawakuwa wavutaji sigara walifanya tendo la ndoa mara mbili zaidi ya wale wavutaji sigara.
Uvutaji sigara, huusishwa pia na kuongezeka kwa chembechembe nyeupe za damu kwenye shahawa ambazo kwa kawaida hutolewa kukiwa na ugonjwa ndani ya mwili, chembechembe hizi ambazo zinakuwepo kwa wingi kwenye shahawa pasi na kuwepo kwa ugonjwa, hupunguza uwezo wa shahawa kuingia na kuungana na yai (ovum) kutoka kwa mwanamke na hivyo kusababisha kutotunga kwa mimba.
  • Ugonjwa wa kisukari
  • Uzito uliopitiliza (obesity) – Kutokana na kuongezeka kwa mafuta ambayo husababisha mishipa ya damu inayopeleka damu kwenye moyo na uume kuwa midogo na kupungua uwezo wa kujamiana. Kupungua uwezo wa kujamiana au kufanya mapenzi kwa wanaume ni ishara mojawapo ya ugonjwa wa moyo na kiharusi.
  • Hypothyroidism – Matatizo ya vichocheo katika tezi la koo
  • Kuwa na wasiwasi (anxiety), depression
  • Kupenda mambo ya intaneti kupita kiasi (addiction to internet) kama nilivyoeleza awali.
  • Umri – Kuanzia miaka ya 40,kiwango cha kichocheo aina ya prolactin huongezeka na kusababisha kuongezeka kwa kichocheo chengine aina ya dihydro-testerone ambacho husababisha tezi dume kuongezeka na hatimaye kupunguza uwezo wa kusimika kwa mwanamume (rudia makala ya kuvimba tezi dume – Benign Prostate Hyperplasia, BPH)
  • Madhara katika neva inayohusika na kusimika kwa uume (pudendal nerve damage)
  • Kuendesha baiskeli muda mrefu (kwa kipindi kimoja) – Hii hugandamiza neva na mishipa ya damu inayopeleka damu kwenye uume na kusababisha tatizo la kupungua kwa uwezo wa kusimika kwa mwanamume kwa muda tu (temporary).
Vipimo vya uchunguzi
Kabla ya kufanya vipimo vya uchunguzi, Daktari atachukua historia ya mgonjwa inayohusisha matumizi ya dawa aina mbalimbali, historia ya magonjwa, pamoja na kuangalia dalili za magonjwa mbalimbali. Vipimo vya uchunguzi vitatokana na historia ya mgonjwa ambayo Daktari ameweza kuipata kutoka kwake. Vipimo hivyo vinaweza kuwa
  • Kuangalia magonjwa kwenye tupu ya mwanamke au kama kuna bakteria aina yoyote.
  • – Kuangalia magonjwa ya zinaa
  • Vipimo vya mkojo (urinalysis)
  • Kipimo cha kuangalia mabadiliko yoyote kwenye tupu ya mwanamke (physical changes, thinning of genital tissues, decreased skin elasticity and scarring)
  • Kumpima mgonjwa akili ili kuweza kutambua kiini cha tatizo
  • Vipimo vya vichocheo kama T3, T4, testerone level, growth hormone, prolactin hormone nk.
  • Semen analysis – Kipimo cha kuangalia shahawa, wingi wake (volume), kiwango chake, mvutano wake (liquefaction time), sperm count, maumbile yake (sperm morphology), PH yake, uwezo wake wa kuogelea (sperm motility), kiwango cha sukari na chembechembe nyeupe za damu.
  • BMI – Kipimo cha kuangalia kama mtu anauzito unaolingana na urefu wake pamoja na umri wake au ana uzito uliopitiliza
  • Vipimo vya ugonjwa wa shinikizo la damu – Kwa wale wenye shinikizo la damu au dalili zake au wanaotumia dawa za shinikizo la damu
  • Vipimo vya ugonjwa wa kisukari – Fasting Blood Glucose test, Oral Glucose Tolerance Test (OGTT), glycosylated hemoglobin (Hb A1C) rudia makala ya Kisukari kwenye tovuti ya Tanzmed.
Tiba ya tatizo hili
Tiba ya tatizo hili inahusisha
1.Kubadilisha mfumo wa maisha
  • Kufanya mazoezi mara kwa mara – Mazoezi huongeza stamina, hupunguza uzito,humfanya mtu kuwa na umbile zuri, furaha na kuongeza ufanisi wakati wa kujamiana
  • Kupunguza msongo wa mawazo kwa kukubali kwamba tatizo lipo baina ya wanandoa na hivyo kutafuta suluhu pamoja na kuacha ugomvi. Matatizo ya kimaisha (fedha, nk) lazima yatafutiwe ufumbuzi.Kufanya mazoezi ya pelvic muscles kwa kufanya kama unazuia mkojo wakati unahisi haja ndogo na kuhesabu kutoka moja hadi tano, baada ya tano pumzika na halafu rudia. Haya mazoezi (kegel exercise) huongeza uwezo wa kujamiana kwa wanawake
2. Kubadilisha mfumo wa maisha kwa wapenzi
  • Zungumza na mwenza wako – Malumbano na matatizo ni vitu vya kawaida katika uhusiano wowote, ni vizuri kwa wenza kukaa pamoja na kuzungumza matatizo yao, kuwa wakweli, waaminifu, kuaminiana, kujaliana na kuzungumza juu ya tendo la ndoa kwa pamoja. Ni vizuri kila mmoja kuainisha vitu anavyopenda na asivyopenda kufanyiwa wakati wa kujamiana. Pale inapotokea mmoja hajapendezwa au kufurahishiwa na uwajibikaji au ufanisi wa mwenzie basi hana budi kutumia lugha nzuri kutafuta kiini cha tatizo na kulitafutia ufumbuzi.
  • Weka mazingira mazuri na muda wa kufanya tendo la ndoa na mwenza wako ili mupate kudumisha uhusiano wenu
  • Ongeza msisimko katika uhusiano wenu kwa kujaribu aina au staili mbalimbali wakati wa kujamiana, kubadilisha muda wa kufanya mapenzi (sio usiku tu hata asubuhi, mchana) au sehemu tofauti na ile muliyoizoea wakati wa kufanya mapenzi (sio kila siku kitandani)
  • Kupata ushauri nasaha kutoka kwa wataalamu wa mambo ya uhusiano, marriage counsellors na hata madaktari wa magonjwa ya akili kwani hawa ni weledi zaidi katika kazi yao.
3.Tiba ya dawa
  • Kutibu ugonjwa ambao ni kiini cha tatizo hili – Kisukari, magonjwa ya moyo, magonjwa ya zinaa nk.
  • Daktari kumbadilishia mgonjwa dawa zinazoleta madhara kama ya msongo wa mawazo, depression nk.
  • Kutibu tatizo la depression na anxiety
  • Kutumia dawa au jelly zinazolainisha tupu ya mwanamke wakati wa tendo la ndoa kwa wale wanaopata maumivu au kupunguza tupu kuwa kavu au kuwasha (irritation).
  • Tiba ya homoni au vichocheo – Estrogen Replacement Therapy (ERT) and androgen therapy.
  • Dawa aina ya Yohimbine Hydrochloride
4.Vyakula vinavyosaidia kupunguza tatizo hili
Ikumbukwe ya kwamba vyakula hivi sio tiba mbadala bali husaidia tu kupunguza ukubwa wa tatizo hili la kupungua au kukosa hamu ya kufanya mapenzi na kuboresha kwa wale ambao hawana tatizo hili na hivyo kudumisha uhusiano.
  • Kitunguu swaumu – Kitunguu swaumu kina kemikali aina ya allicin ambayo huongeza mzunguko wa damu kwenda kwenye uume, huongeza hamu ya kufanya mapenzi na utolewaji wa shahawa.
  • Habat al soda (black caraway seeds) – Mafuta,mbegu,au unga wa habat soda kama wengi wanavyoita na ambazo zimetumika kwa miaka mingi sana kupunguza tatizo hili na waandishi wengi wameeleza umuhimu wake. Tumia kidogo kwenye chai au maji ya uvuguvugu mara mbili kila siku. Mbegu hizi hupatikana kwa wingi katika nchi za asia kama Saudi Arabia, Syria, Iran, Dubai (UAE), na hata Misri, Tanzania (Dar-es-salaam katika maduka ya dawa za asili ya kariakoo, mbagala, na Zanzibar)
  • Celery au giligilani – Hii huchochea hamu ya tendo la ndoa kutokana na uwepo kwa wingi wa kichocheo aina ya androsterone.
  • Ndizi – kuwepo kwa wingi kwa enzyme aina ya bromelain na madini ya potassium huongezeka msisimko wa kufanya mapenzi kwa wanaume.Potassium pia hupatikana kwenye tikiti maji ambalo pia lina kemikali aina ya arginine ambayo huongeza wingi wa damu katika mishipa ya damu na hivyo kusaidia katika kusimika kwa uume.
  • Parachichi – Huwa na kiwango kikubwa cha folic acid ambayo huvunjavunja protini. Vitamini B6 kwenye parachichi huchochea kutengeza kichocheo aina ya testerone kwa wingi.
  • Mayai – Mayai yana kiwango kikubwa sana cha vitamini aina ya B5 na B6, ambazo husaidia kuleta usawa wa viwango vya vichocheo mwilini na kupunguza msongo wa mawazo.
  • Nyanya/Tungule (tomatoes) – Zina kiwango kikubwa cha virutubisho aina ya bio-active phyto-nutrients, lycopene, na beta carotene ambazo husaidia kuleta damu kwa wingi kwenye uume na hivyo kusaidia kusimika kwa uume
  • Chocolate – Ina kiwango kikubwa cha kemikali aina ya theobromine na phenylethylamine ambazo huongezeka hamu ya kufanya mapenzi.
  • Vitamin A – Husaidia katika kuweka usawa wa vichocheo vya mapenzi (sexual hormones). Vyakula venye wingi wa vitamin hii ni pamoja na karoti, maini,tikiti maji, spinach, maziwa nk.
  • Vitamin B complex – Huongeza kiwango cha kichocheo cha testerone ambacho husaidia katika kuongeza ufanisi wa tendo la ndoa kwa wanaume na wanawake. Vitamini B complex hupatikana kwa wingi kwenye ndizi, viazi tamu, lentils, mboga za majani, parachichi (avocado), mayai, nyama aina ya tuna, bata mzinga, maini nk.
  • Vitamin C – Tafiti zilizofanywa karibuni zimeonyesha ya kwamba vitamini C inapotumiwa pamoja na vitamini nyengine, husaidia L-enantiomer ya ascorbic acid kudhibiti msongo wa mawazo, wasiwasi (anxiety), utolewaji wa homoni ya prolactin na huongeza mzunguko wa damu pamoja na kutolewa kwa kichocheo cha aina ya oxytocin na hivyo kuongeza ufanisi wa tendo la ndoa. Vyakula venye vitamin C ni ndimu, chungwa, limao, brussels sprouts, mapera, tikiti maji, nyanya, broccoli, kiwi, papai, strawberries, pilipili hoho na pilipili mbuzi nk.
  • Vitamin E – Husaidia kudhibiti matamanio ya mwanamume pamoja na kusimika kwa uume kutokana na uwepo wa vichocheo aina androgens na estrogen ambavyo huchanganyikana na homoni za mayai (ovarian hormones) na testerone. Vyakula venye vitamin E ni pilipili hoho, nyanya, olives, tunda aina ya kiwi, papai, mafuta ya alizeti, karanga nk.
  • Madini ya Zinc – Muhimu katika utengenezaji wa testerone
  • Madini ya selenium – Huongeza uwezo na nguvu ya kufanya mapenzi kwa wanaume.
  • Madini ya magnesium na calciumCalcium ni muhimu katika kusaidia ufanisi wa kufanya mapenzi. Huweka mawasiliano ya karibu kati ya ubongo na tezi zinazotoa vichocheo vya mapenzi pamoja na kusaidia katika ufanyaji kazi wao. Madini ya magnesium husaidia kuondoa madhara ya madini ya calcium katika kusaidia kuhimili kusimika kwa uume. Vyakula venye madini ya calcium ni maziwa, mtindi, cheese, siagi, chungwa, almonds, walnuts, maharage meupe, ice cream, chocolate nk.
  • Cinnamon stick (mdalasini) na Asali (Honey) – Mchanganyiko wa vitu hivi viwili husaidia sana katika kuongeza ufanisi kwa wale wenye tatizo hili. Jinsi ya kuandaa, chukua mdalasini robo na changanya na asali nusu lita kisha weka kwa siku tatu, baada ya siku tatu anza kunywa kwa kutumia kikombe cha kahawa mara tatu kwa siku kwa muda wa wiki mbili (kama utatumia mdalasini nusu basi changanya na asali lita moja).

Sababu za Watoto Wachanga Kulia Mara kwa Mara na Namna ya Kuwabembeleza

kulia mtoto
Ni kawaida kwa watoto kulia. Hata watoto wanaozaliwa na afya njema kabisa wanaweza kulia kwa jumla ya wastani wa kati ya saa moja mpaka matatu kwa siku. Kwa vile watoto hawawezi kujifanyia chochote wao wenyewe zaidi ya kutegemea wazazi, walezi ama watu wengine wanaowazunguka katika kuwapatia chakula, joto, na faraja, kilio ni njia ya mtoto ya kuwasilisha moja ya mahitaji hayo.

Kama mzazi mpya, wakati mwingine inakuwa vigumu kutambua mtoto wako anahitaji nini anapolia. Mzazi anaweza kuwa na maswali kadhaa kichwani mwake, je, mtoto ana njaa, anasikia baridi, ana kiu, anaumwa ama amechoka? Katika siku za mwanzo, hali ya namna hii inawawia vigumu wazazi wengi, wasijue nini la kufanya. Hata hivyo, kwa kadiri siku zinavyopita mzazi mpya ataweza kutambua kuwa kilio cha mtoto wake kinamaanisha anahitaji nini kutokana na mfumo wake wa kulia.

Kadiri watoto wanavyokua ndivyo ambavyo hujifunza hatua mbalimbali za kuwasiliana na wazazi ama walezi wao. Wanakuwa na namna nzuri ya kuwasiliana kwa mfano kwa macho, na kutoa sauti, na hata kutabasamu ambavyo vyote kwa pamoja hupunguza haja ya kulia.

Sababu zinazofanya watoto kulia

Tuangalie sababu kadhaa zinazosababisha mtoto kulia na nini anachotakiwa mzazi ama mlezi kufanya pindi mtoto anapolia.

1. Hitaji la chakula

Njaa ni mmoja ya sababu kubwa inayowafanya watoto wengi kulia. Uwezekano wa mtoto kulia unaendana sana na umri wa mtoto. Kadiri jinsi mtoto alivyo mdogo zaidi ndivyo uwezekano wa kulia sana pindi anapohisi njaa unavyokuwa mkubwa, isipokuwa katika siku mbili za mwanzo baada ya kuzaliwa ambapo watoto hula kwa kiasi kidogo sana. Kwa kawaida katika siku mbili za mwanzo tangu mtoto kuzaliwa, maziwa ya kujilimbikizia mapema sana yaani ‘colostrum’ huwa ni kidogo sana kwa mama walio wengi na huanza kuongezeka kuanzia siku ya tatu baada ya kujifungua. Pia tumbo la mtoto katika kipindi hiki huwa bado dogo sana na hivyo uwezo wake wa kuhifadhi maziwa anayonyonya huwa bado mdogo hali ambayo humfanya mtoto kujisikia njaa. Hivyo kama mtoto wako analia, uwezekano mkubwa ni kuwa ana njaa na hivyo mzazi unashauriwa kumnyonyesha. Inawezekana mtoto asiache kulia mara moja, lakini mama unashauriwa kuendelea kumnyonyesha taratibu na mtoto anaweza kuacha kulia kwa kadiri anavyoburudika na chakula na kuanza kushiba. Iwapo mama unadhani mtoto wako ameshiba lakini bado anaendelea kulia, inawezekana kuna sababu nyingine zaidi.

2. Hitaji la starehe

Baadhi ya watoto wanakuwa na hisia kali pindi vitu kama nguo inapoelekea kumbana sana au iwapo anahisi kuna kitu chochote ndani ya nguo yake kinachomsababishia maumivu. Wapo baadhi ya watoto ambao hawaoneshi kuhangaika pale nepi zinapokuwa zimelowa sababu ya mkojo au kinyesi, kwa vile baadhi yao huihisi joto na hivyo kupendezewa na hali hiyo, wakati watoto wengine hulia na kuhitaji kubadilishwa nguo walizovaa mara moja, hasa kama ngozi zao laini zinasumbuliwa. Ni vyema kwa mzazi ama mlezi kumchunguza mtoto wako kama amechafua nepi na kumbadilisha. Vilevile ni vyema kuangalia kama nguo alizovikwa hazibani na hakuna chochote ndani ya nguo kinachomletea maumivu.

3. Hitaji la kuwa na joto la wastani

Baadhi ya watoto hawapendi kubadilishwa nepi au kuogeshwa. Hawajazoea kuhisi hewa yenye joto tofauti juu ya ngozi zao. Wengi wao hupendelea sana kuwa na hali ya jotojoto lililohifadhiwa. Kwa hiyo ni vyema kumbadilisha mtoto nepi haraka ili kuweza hifadhi joto lake. Inashauriwa pia kutokumvalisha nguo nyingi zaidi ya mahitaji ili mtoto asije akahisi joto zaidi ya analolihitaji mwilini na hivyo kupelekea kuanza kulia.

Inashauriwa pia kutomfunika mtoto kwa mashuka au mablanketi mengi hasa wakati wa kumlaza. Kabla ya kuamua ni kiasi gani cha nguo unachohitaji kumfunika mtoto wakati wa kulala, ni vyema kuangalia kama mwili wa mtoto ni wa moto au baridi isivyo kawaida. Unaweza kufanya hivi kwa kuhisi joto la tumbo lake kwa kutumia kiganja chako. Iwapo mtoto ana joto sana, unashauriwa kupunguza idadi ya nguo za kumfunika vivyo hivyo iwapo unahisi mtoto ana baridi isivyo kawaida inashauriwa kuongeza idadi ya nguo za kumfunikia. Usipime joto la mwili wa mtoto kwa kutumia joto la mikono au miguu yake kwani si kitu cha uhakika na mara nyingi huleta matokeo yasiyo sahihi kwa vile ni kawaida ya mikono au miguu ya watoto kuwa ya baridi.

4. Hitaji la kushikwa ama kubebwa

Baadhi ya watoto wanahitaji kuwa karibu na wazazi wao kwa kubebwa na kubembelezwa. Watoto wakubwa wanapata faraja kwa kuwaona wazazi wao wakiwa karibu na kusikia sauti zao, lakini mara nyingi watoto wachanga wanahitaji kushikiliwa na kubembelezwa kwa faraja. Kama umemlisha mtoto wako na kumbadilisha nepi wakati mwingine mtoto anahitaji kubebwa pia.

Baadhi ya wazazi uhofia kuwa wanaweza kuwaharibu watoto wao kimakuzi pindi wanapowabeba sana. Hiyo si kweli hususani kwa miezi michache ya mwanzo tangu kuzaliwa kwa mtoto. Wakati baadhi ya watoto hawapendi kubebwa, wapo wengine ambao hutaka kubebwa karibu muda mwingi. Iwapo mtoto wako ni wa namna hiyo, unaweza kumbeba mgongoni au kwa jinsi yeyote ile ambayo itakuruhusu kuendelea na shughuli zako nyingine.

5. Hitaji la mapumziko

Ni rahisi kudhani kuwa mtoto atapata usingizi wakati wowote popote pale alipo. Hata hivyo, kwa baadhi ya watoto, hali kama za ujio wa wageni, kelele au hali ya fujo zinaweza kumfanya mtoto kusisimka na hivyo kuwa vigumu kwake kutulia. Watoto wachanga wanaweza kupata ugumu wa kukabiliana na mambo ya kusisimua sana kwa mfano vitu kama taa, kelele, au kubebwa kwa kupokezana kutoka kwa ndugu au mgeni mmoja mpaka mwingine hasa wanapokuja kumtembelea mama. Hali hii humfanya mtoto kushindwa kustahamili na hivyo kuzidiwa na hayo yote. Wazazi wengi wamegundua kwamba watoto wao hulia zaidi kuliko kawaida wakati ndugu au jamaa wakiwatembelea hususani nyakati za jioni. Kama hakuna sababu nyingine maalum inayopelekea mtoto wako kulia, yawezekana basi kilio chake kinasababishwa na uchovu. Mzazi ama mlezi anashauriwa kumpeleka mtoto sehemu tulivu iwe chumbani au sehemu nyingine ambapo patamwondolea hali ya kusisimuliwa na hivyo kumfanya aweze kuacha kulia na kupata usingizi.

6. Hitaji la kitu cha kumfanya mtoto ajisikie vizuri

Iwapo umemlisha mtoto wako na kuhakikisha kuwa yupo vizuri lakini akawa bado anaendelea kulia, mzazi ama mlezi unaweza kuwa na hofu kuwa mtoto ni mgonjwa au ana maumivu. Ni vigumu sana nyakati za mwanzo kwa mzazi kutambua kuwa mtoto wake analia kwa sababu ya kutokuwa na furaha au kuna kitu kinachomuumiza. Mtoto ambaye ni mgonjwa mara nyingi hutoa sauti ya kilio kilicho tofauti na sauti yake ya kawaida. Sauti hii inaweza kuwa ya haraka zaidi au kali sana. Vile vile kwa mtoto ambaye amezoea kulia mara kwa mara, pindi anapoonesha hali ya utulivu isiyo ya kawaida inaweza kuwa dalili ya kwamba ni mgonjwa. Jambo muhimu la kukumbuka ni kwamba hakuna mtu anayemjua mtoto wako vizuri zaidi kuliko wewe. Kwa hiyo basi kama mzazi ama mlezi unahisi kwamba kuna kitu tofauti kwa mtoto wako ni vyema ukaonana na wataalimu wa afya. Wataalamu wa afya daima watayachunguza matatizo ya mtoto wako kwa umakini mkubwa na hivyo kujua sababu ya mtoto kulia. Mzazi ama mlezi unashauriwa kuonana na daktari iwapo mtoto wako ana shida ya kupumua pindi anapolia, au kama kulia kwa mtoto kunaambatana na kutapika, kuharisha ama kutopata choo.

7. Mtoto anahitaji kitu, lakini hujui ni nini

Wakati mwingine unaweza kushindwa kufahamu ni nini kinachomsababishia mtoto wako kulia. Wakati mwingine watoto wanakosa furaha. Hali hii ya kukosa furaha bila sababu inaweza kudumu dakika chache au saa kadhaa ambapo mtoto huendelea tu kulia mara kwa mara. Wakati mwingine baadhi ya watoto hulia kwa muda mrefu huku wakirusha rusha miguu. Hii hali yaweza kusababishwa na maumivu ayapatayo mtoto kwenye tumbo. Kwa kitaalamu hali hii hujulikana kama colic. Huwawia vigumu sana wazazi wengi kukabiliana na mtoto ambaye ana colic. Hakuna tiba ya uchawi kwa colic, aidha ni mara chache sana hali hii inadumu kwa zaidi ya miezi mitatu. Hata hivyo ni vyema kupata ushauri wa daktari pindi unapohisi mtoto wako ana colic.

Je, nini cha kufanya mtoto anapolia?

Kuna vitu ambavyo mzazi unaweza kufanya ili kumpa faraja mtoto wako pindi anapolia. Yawezekana baadhi ya mambo yatakayoshauriwa hapa yasiwasaidie watoto wote, hivyo basi mzazi ama mlezi ni vizuri ukamjua mtoto wako na kufahamu kwa undani ni kitu gani hasa kinachoweza kusaidia kumtuliza.

1. Kumbeba mtoto

Watoto wachanga huonyesha upendeleo fulani wa hisia, kama vile walivyokuwa ndani ya tumbo, hivyo basi unaweza kujaribu kumvingirisha mtoto wako katika blanketi au nguo zozote za kumbebea kama khanga au vitenge ili kuona kama atapenda hali hiyo. Watoto wengine hawapendi kuvingirishwa kwenye blanketi na hupenda aina nyingine ya kupata faraja kama vile kubebwa. Wapo wazazi wanaopenda kumbeba mtoto kiasi cha kumfanya mtoto asikie mapigo ya moyo, kitendo ambacho humpa faraja sana mtoto.

2. Kumwimbia nyimbo au sauti za kumbembeleza

Akiwa tumboni mwa mama, mara kwa mara mtoto alikuwa akisikia mapigo ya moyo ya mama. Hali hii ndiyo sababu kubwa ya watoto wengi kupendelea kubebwa na mama zao. Hata hivyo kuna aina nyingine za sauti zinazoweza pia kusaidia kumtuliza mtoto. Mzazi ama mlezi unaweza kujaribu kuweka muziki wa taratibu au kumuimbia mtoto nyimbo za kubembeleza kwa sauti ya chini sana. Unashauriwa kutokuweka miziki ya haraka au yenye sauti kubwa kwa sababu inaweza kumwondolea hali yake ya utulivu na hivyo kumfanya ashindwe kuacha kulia.

3. Jaribu kumkanda au kumsugua taratibu (masaji)

Kumkanda kanda au kumsugua mtoto taratibu mgongoni au tumboni kunaweza kumsaidia sana kumfariji mtoto. Iwapo inaonekana mtoto anapata tabu wakati wa kubeua au kucheua, jaribu kumlisha akiwa wima zaidi na kila baada ya kumlisha mweke juu ya bega lako na kumsugua taratibu mgongoni ili kumsaidia atoe gesi kwa kubeua. Baadhi ya watoto ambao wana “colic” wakati mwingine hutulia hasa wanaposuguliwa taratibu tumboni na hii huweza kuwafanya wajisikie vizuri kwa vile huihisi kwamba angalau mzazi ama mlezi unajitahidi kufanya kitu fulani kusaidia kumwondolea shida yake.

4. Mpatie kitu cha kunyonya

Kwa baadhi ya watoto waliozaliwa, haja ya kunyonya ni kubwa sana na hivyo kumpatia chuchu safi iliyotengenezwa kwa ajili hiyo au kidole kisafi cha mama inaweza kuleta faraja kubwa kwao. Kunyonya kutamsababishia mapigo ya moyo wake kuwa katika kiwango chake cha kawaida, kupumzisha tumbo lake, na kutulia.

Ulezi wa watoto wachanga ni kitu kigumu lakini ulezi wa mtoto ambaye hulia mara kwa mara ni ngumu zaidi. Kupata msaada na kuungwa mkono wakati unapohitaji msaada ni muhimu zaidi. Mzazi hana budi kufahamu kuwa kwa jinsi siku zinavyopita, na kwa kadri mtoto anavyokua, mtoto anajifunza njia mpya ya kuwa na uwezo wa kuwasilisha mahitaji yake na hivyo ni muhimu mzazi naye kujifunza njia hizo ili kumuwezesha kumpatia mtoto mahitaji yake anayohitaji kwa haraka na wakati unaostahili.

Magonjwa ya Moyo ya Kuzaliwa (Congenital Heart Diseases)

Magonjwa ya Moyo ya Kuzaliwa
Muundo ya moyo na mishipa ya damu ni mojawapo ya vinavyooathirika katika magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo. Vijusi(fetuses) kati ya 8 hadi 10 huathirika kwa kila 1000.

Magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo huweza kutoa dalili mara tu baada ya kuzaliwa, utotoni na wakati mwingine husubiri mpaka ukubwani.

Magonjwa ya Moyo ya Kuzaliwa husababishwa na nini?

Kwa wengi sababu huwa haijulikani. Ila huwa kuna vitu hatarishi ambavyo hupelekea kuongezeka kwa uwezekano wa kupata magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo, vitu hivyo hatarishi ni:

  • Matatizo ya kijenetekia utotoni kama Downs syndrome, Turner’s syndrome, Marfan syndrome,
  • Matumizi ya dawa ya kutibu chunusi (acne) aina ya retinoic acid, madawa ya kulevya na unywaji wa pombe wakati wa ujauzito
  • Maambukizi ya virusi vya Rubella (German measles) kipindi cha kwanza cha ujauzito (1st trimester)

Kuna aina mbili za magonjwa ya moyo ya kuzaliwa:

  1. Cyanotic
  2. Non-cyanotic

Cyanosis ni hali ya kuwa na rangi ya samawati (katika midomo,ulimi, ganja za mikono na miguuni) kutokana na kukosa oksijeni ya kutosha mwilini.

1. Cyanotic

Magonjwa ya moyo ya asili ambayo yanaangukia katika kundi hili ni pamoja na

  • Tetralogy of fallots
  • Transposition of great vessels
  • Tricuspid atresia
  • Total anomalous pulmonary venous return
  • Truncus arteriousus
  • Hypoplastic left heart
  • Pulmonary atresia
  • Ebstein anomaly

2. Non-cyanotic

Magonjwa ya moyo ya asili yaliyo kwenye kundi hili hujumuisha

  • Ventricular septal defect (tundu katika kuta za ventrikali)
  • Atrial septal defect (tundu katika kuta za atria)
  • Patents ductus arteriousus
  • Aortic stenosis
  • Pulmonic stenosis
  • Coarctation of the aorta
  • Atrioventricular canal (endocardial cushion defect)

Dalili za Magonjwa ya Moyo ya Kuzaliwa

Kwa ujumla, wagonjwa wa moyo wa asili huwa na dalili zifuatazo;

  • Kupumua kwa shida
  • Kushindwa kula vizuri
  • Matatizo ya ukuaji
  • Matatizo ya ukuaji wa misuli ya mikono na miguu
  • Maambukizi ya mfumo wa hewa
  • Cyanosis kwa aina ya kwanza(rangi ya samawati katika midomo,ulimi, viganja vya mikono na miguuni)
  • Ongezeko la sauti ya ziada katika sauti za moyo kutokana na tatizo (heart murmur)
  • Mabadiliko kwenye kucha hasa za vidole vya mikononi (digital clubbing)

Vipimo na Uchunguzi

Baadhi ya vipimo vinavyotumika kwa ajili ya uchunguzi wa magonjwa haya ni

  • Echocardiogram/transesophageal echocardiogram
  • Cardiac catheterization
  • Magnetic Resonance Imaging
  • Electrocardiogram
  • Chest x-ray

Matibabu

Matibabu hutegemea aina ya ugonjwa wa moyo wa kuzaliwa nao, hivyo hapa nitaelezea kwa kifupi ila, maelezo zaidi nitatoa katika makala zinazokuja za ugonjwa mmoja mmoja.

Aina nyingi za magonjwa haya huwa na madhara makubwa hivyo huhitaji upasuaji kurekebisha kasoro hizo, pamoja na matibabu ya dawa (diuretics ambazo husaidia kupunguza maji na chumvi mwilini, digoxin ambayo husaidia kuongeza nguvu katika mapigo ya moyo).

Vilevile kuna tiba nyengine ambayo badala ya upasuaji kitaalamu Transcatheter ambapo kifaa cha kufunga au kupachika huwekwa kwenye catheter maalumu ambayo hupita kwenye mishipa ya damu mpaka kwenye kasoro na kurekebisha kwa kuziba tundu nakadhalika.