Saturday, March 17, 2012

Namna ya kuishughulikia na kuishinda hofu

Hofu na mashaka ndiyo adui namba moja anayefilisi nguvu au nishati ya mwili wa mwanadamu kwa haraka kuliko kitu kingine chochote. Wengi wameathiriwa katika maisha yao ya kielimu, kiafya, kijamii, kikazi na hata kiuchumi kwa sababu ya hofu au mashaka.

Wengi wameshindwa kufikia malengo na ndoto zao katika maisha kwa sababu ya hofu na mashaka.

Mara tu hofu na mashaka vinapoingia ndani ya mtu hudumu kwa muda mrefu huku vikileta uharibifu mkubwa katika nafasi, akili, na maendeleo ya mtu huyo kwa ujumla. Makala au mada hii itakuwezesha kufahamu kwa kiasi kikubwa mambo unayoweza kufanya ili kuondokana au kupunguza athari za hofu na mashaka na pia kuweza kutoa msaada kwa yeyote anayepitia tatizo hili kwa wakati fulani.

Hofu ni mjumuiko wa kujali kusiko na sababu yoyote (unnecessary concern) au kusiko na maana yoyote juu ya nafsi au utu wa mtu. Tunasema hakuna sababu wala umuhimu wowote kwa sababu kujali huku kumejengwa katika misingi ifuatayo;

Mtu kujali sana au kuweka mawazo sana katika vitu ambavyo viko nje ya uwezo wake.
Mtu kuanza kusikitikia mambo yajayo badala ya kujipanga na kujiandaa kuyakabili pale yatakapowadia.
Kuweka msisitizo zaidi katika jambo moja na kuyasahau mengine. Anayehofu hudhani kwamba ikiwa kile anachokiwekea msisitizo kitashindikana, basi kila kitu kitakuwa kimeharibika.

Mtu kushindwa kutumainia imani aliyonayo juu ya ufanisi wa jambo fulani. Hofu yake katika jambo fulani huizidi imani aliyonayo na kwahivyo hali ya kushindwa kuonekana dhahiri zaidi kuliko hali ya kushinda.

Kwa sababu hofu hujengwa katika fikra zisizo na maana wala uhalisi wowote, basi njia ya kuiweza hofu hiyo ni lazima iwe kwa kutumia fikra zenye maana na uhalisi ili kuushinda uwezo wako wa kufikiri kushindwa.
Yafuatayo yatakusaidia kukuwezesha kupunguza kiwango cha hofu katika maisha.

Jiulize swali “Je, nini kinachoniangamiza?”
Hofu ni kitu kinacho angamiza, tena huangamiza kwa viwango na hatua tofauti. Ngoja nijaribu kukupa mfano wa maelezo.

Hofu kwa lugha ya Kingereza ni “worry” neno “worry” limetokana na lugha ya Kidachi lenye maana ya “Worgen”. Maana ya neno “worgen” ukiipeleka moja kwa moja katika lugha ya Kiingereza humaanisha “strangle”. Maana ya neno “strangle” kwa lugha ya Kiswahili ni “Kunyonga kwa kamba”. Sasa yamkini hapa unanielewa kwanini ninasema hofu huua au kuangamiza.

Uzuri ni kwamba, hofu haiangamizi pasipo kutoa tahadhari kabla, baadhi ya tahadhari zinazotolewa katika mchakato wa kuangamizwa na hofu ni pamoja na hamaki za mara kwa mara, mvi za mapema, baadhi au upele fulani wa ngozi, vidonda vya tumbo (ulcers), matatizo ya kukosa usingizi, kuhitaji kwenda haja ndogo mara kwa mara n.k.

Swali hili la “ni nini kinachoniangamiza?” litakuwezesha kujitathmini wewe mwenyewe.

No comments:

Post a Comment