Saturday, March 17, 2012

Mambo ya kufanya unapopata msongo II

10. MAZOEZI YA MWILI
Pendelea kufanya mazoezi ya mwili na viungo kila siku au angalau mara tatu kwa wiki. Hii itasaidia kurekebisha mzunguko wa damu, hewa na maji mwilini na kukupa hisia tulivu. Tumia muda wa angalau nusu saa kila unapofanya mazoezi.

11. TENDO LA NDOA
Wataalamu mbalimbali wa saikolojia wanaeleza kuwa, tendo la ndoa lililofanywa kwa hisia na maandalizi ya kutosha kwa watu wanaopendana kwa dhati, husaidia sana kuondoa msongo (stress). Upo ushahidi wa watu waliopata nafuu kubwa baada ya ‘kubembelezwa’ kwa hisia na watu wanaowapenda.

NB: Tendo la ndoa lisipofanywa kwa ufanisi au likifanywa kwa watu wasio na mapenzi ya dhati kati yao, huzidisha msongo wa mawazo.

12. MATEMBEZI YA JIONI
Inaelezwa kuwa, matembezi ya jioni, hasa wakati jua likikaribia kuzama husaidia sana kutuliza mawazo na hisia za mwili hivyo kupunguza msongo. Jenga mazoea ya kutembelea sehemu tulivu kama bustani za maua au vivutio vingine.

13. KUJENGA PICHA YA UTOTONI
Zungumza na mtoto aliye ndani yako kwa kujenga taswira ya mambo uliyokuwa unayafanya na kuyafurahia ukiwa mtoto. Jitazame ukiwa na sura na akili ya kitoto, jaribu kufanya mambo mawili au matatu kama mtoto, hakika utafurahi na kiwango cha msongo kitashuka.

14. USIPANGE MALENGO YASIYOTEKELEZEKA
Imebainika kuwa, wengi hupatwa na msongo wa mawazo kwa kiwango kikubwa baada ya kuona malengo waliyojipangia hayatimii kama walivyotarajia. Wataalamu wa saikolojia ya mafanikio wanaelekeza umuhimu wa kutofautisha Matarajio (expectation) na uhalisia (reality). Ukiweza kupanga malengo yako na kuyagawanya katika vipande vidogovidgogo ambavyo ni rahisi kutekelezeka utakuwa katika nafasi nzuri ya kuushinda msongo.

15. JIFUNZE KUSEMA HAPANA
Jifunze kusema hapana kwa mambo ambayo hauko tayari kuyafanya au ambayo yako nje ya uwezo wako. Wengi wanajikuta katika mkumbo wa kuwa na msongo kwa sababu ya kukubali kila kitu na kuwa wagumu wa kusema hapana. Watu wa namna hii wako tayari hata kwenda kukopa kwa ajili ya kuwafurahisha wengine.

Kwa mfano: Ndugu yako anakuja akiwa na shida na anataka umsaidie. Kama huna uwezo kwa muda huo, mweleze kwa uwazi kuwa hutaweza kumsaidia kwa sababu huna badala ya kuanza kuumia na kuingia kwenye madeni ambayo hukurundikia mzigo wa msongo. Mweleze mtu ukweli hata kama hautamfurahisha. Jifunze kujitazama wewe kwanza ndiyo utakapoweza kuwatazama na wengine.

No comments:

Post a Comment