Saturday, March 17, 2012

Unajua Kwamba unaweza kuwa chanzo cha maumivu yako

Kama bado hujaingia kwenye ndoa, huu ni wakati wako sahihi wa kufanya uchaguzi bora ambao hautakuwa na majuto hapo baadaye. Hapa nazungumzia juu ya kutizama maisha yako yajayo.
Acha kuangalia leo, wakati kesho yako inaonekana wazi kuwa mbaya yenye majuto ya kila aina. Hapa nitachambua kwa mapana mambo mawili makubwa; Hisia na maisha!
Wapo rafiki zangu ambao wanakubali kuongozwa zaidi na hisia huku wakiacha maisha yao ya baadaye yawe mabaya. Ieleweke kwamba, maisha utakayoishi kesho ni matokeo ya jinsi unavyoishi leo.
Wakati mwingine mtu anakuwa na mpenzi wake, ana kasoro kibao, kila siku ugomvi, hakuna maelewano, lakini kila anapotaka kuachana naye, hisia kali za mapenzi dhidi yake zinamzidi na kujikuta akiendelea kuwepo kwenye penzi la mateso.
Huu si wakati wa kunyanyasika katika mapenzi, ni muda ambao unatakiwa kuangalia vyema tabia na mienendo ya mpenzi wako. Kama hairidhishi, usijiumize; Chukua hatua ya moja kwa moja huku ukizingatia kwamba, maisha yako yanayofuata yatakuwa bora ukijivunia ujana wako.

Hata kama unampenda sana, anajua mapenzi sana, ana faida gani kama kila siku ameendelea kukuumiza? Kukunyanyasa? Kukusimanga? Haoni faida yako, anakudharau waziwazi! Kwa nini uendelee kukaa kifungoni wakati kuna njia?
Mwamuzi wa maisha yako ni wewe, hatatokea mtu wa kukupangia maisha bora hapo baadaye, yote hayo unapaswa kufanya mwenyewe. Chagua maisha unayoyapenda.

Nina maana gani ninaposema maisha? Rafiki zangu, huu ni mustakabali wa maisha yanayofuata. Kwamba maisha yako baada ya leo ni yapi? Unahitaji kuishi maisha gani?

Maana kama ukiwa hujui unataka kuishi vipi, utakuwa unakwenda bora siku zisogee na mwishowe utajikuta ukiingia kwenye majuto. Kwa nini uingie kwenye majuto wakati unaweza kujipanga na kufanya kesho yako iwe bora zaidi?
Ndugu zangu, ninapozungumzia kuhusu hisia nina maana kubwa sana. Kwanza, fahamu kuwa hisia na mapenzi ni vitu viwili tofauti kabisa, ingawa ili uwe na hisia lazima pia uwe na mapenzi.

Kwa maneno mengine, mtu mwenye mapenzi ya dhati ni rahisi zaidi kuongozwa na hisia kuliko mwenye hisia kupanda mbegu ya mapenzi ndani ya moyo wake. Hisia katika mapenzi, tunaitafsiri kama ile hali ya kuingiwa na mapenzi ndani ya moyo kupitiliza, pia kuzama katika penzi kiasi cha kuwa mpofu wa kutoweza kuona mbadala wake.

Mtu mwenye hisia kali za mapenzi kwa mwenzi wake, huwa haamini kama kuna mwingine ambaye anaweza kuwa kama mpenzi wake, hali hii inasababisha kufunika makosa au matatizo yatakayotokea katika uhusiano wao hata kama ni makubwa.
Akibahatika kugundua, basi uulizaji wake unakuwa si wa kujiamini sana, lakini pia ni mwepesi wa kuyumbishwa au hata kuomba msamaha kwa kosa ambalo ni la mpenzi wake. Huyu tunamwita anayeongozwa na hisia.

Mtu mwenye hisia zaidi kuliko mapenzi, yupo tayari kuishi maisha ya kubahatisha bila kuwa na mipango ya mbele, lakini awe na mpenzi wake. Huu ni ulimbukeni wa hali ya hali juu. Rafiki zangu, kifungo si lazima upelekwe gerezani, hata wewe unaweza kujiingiza katika kifungo cha mapenzi.

Usikubali kuendelea kuwa katika mapenzi na mtu ambaye unajua wazi ana kasoro kibao, kwa sababu eti unampenda! Hata kama unampenda kwa kiwango gani, lakini ndiyo hivyo si mwaminifu, mkorofi, hana heshima; Utaendeleaje na mpenzi wa aina hii?

Lakini katika yote hayo, tatizo kubwa zaidi ambalo ni la hatari, ni ile hali ya kuwa na mwenzi ambaye si mwaminifu. Kutokana na kigezo chako cha kuangalia jinsi hisia zako zinavyokuongoza, wakati mwingine unaweza kusalitiwa lakini usijue au unajua lakini unaamua kuacha kwa kuhofia kumpoteza. Huu ni ulimbukeni rafiki zangu.

Katika suala la usaliti ni vizuri kuwa makini katika kufanya uchunguzi kwanza kabla ya kufanya maamuzi. Mathalani mpenzi wako amekuja, anaonekana amechoka-choka, hana furaha na uso mng’avu kabisa!
Tabasamu lake halipo na kwa kumwangalia tu usoni unagundua kwamba ana alama ya busu kwenye shavu lake! Wakati mwingine ananukia manukato ambayo siyo aliyoyatumia asubuhi.

Au anaweza kuja na furaha kupitiliza, uchangamfu kupitiliza, kukukumbatia kwa muda mrefu zaidi kuliko kawaida ambavyo mmezoeana n.k.
Hizi ni dalili za wazi kabisa, katika hali kama hiyo lazima uwe na mashaka na inawezekana akawa ametoka kwa mtu mwingine. Alama ya busu shavuni mwake, haina haja ya kuwa na maswali mengi maana tayari jibu utakuwa nalo.

No comments:

Post a Comment