Sunday, March 18, 2012

Kukosa Usingizi Husababisha Upungufu wa Homoni ya Testosterone

Kukosa Usingizi
Mnamo mwaka 2007, watafiti nchini Marekani walifanikiwa kutoa ripoti inayojaribu kuhusisha ukosefu wa usingizi na upungufu wa homoni ya testosterone miongoni mwa wanaume watu wazima.

Kwa kawaida kiwango cha homoni ya testosterone hupungua kadiri mwanaume anavyozidi kuwa mtu mzima, na kwa baadhi ya wanaume, kupungua huku kwa testosterone huweza kusababisha ulegevu wa mwili, kukosa hamu ya ngono na hata kuvunjika mifupa ya mwili.

Watafiti wanasema kuwa, wapo baadhi ya wanaume walio kwenye miaka 80 bado huweza kuwa na kiwango cha juu cha testosterone sawa na kile kinachopatikana kwa wanaume vijana. Hata hivyo sababu kubwa inayofanya kuwepo na utofauti katika viwango vya testosterone miongoni mwa rika hizo mbili bado hazieleweki sawasawa, ingawa watafiti wanasema kuwa ukosefu wa usingizi miongoni mwa watu wazima na wazee unaweza kuwa chanzo kimojawapo cha kuwepo kwa hali hiyo.

"Matokeo ya utafiti wetu yanaongeza uwezekano kuwa wanaume watu wazima na wazee ambao hupata muda mfupi sana wa kulala nyakati za usiku huwa na kiwango kidogo sana cha homoni ya testosterone wakati wa asubuhi," anasema mtafiti Plamen Penev, wa kutoka Chuo Kikuu cha Chicago, nchini Marekani.

Wakati wa utafiti, wataalamu waliofanya uchunguzi huo walipima kiwango cha homoni ya testosterone katika damu kila asubuhi cha wanaume watu wazima wenye umri kati ya miaka 64 na 74 waliojitolea kushiriki kwenye utafiti huo. Aidha, mtindo wao wa kulala pamoja na kupata usingizi pia vilichunguzwa kila siku kwa muda wa wiki nzima.

Matokeo ya uchunguzi huo yalionesha kuwa kiasi cha usingizi walicholala kilikuwa na uhusiano wa karibu sana na kiwango cha testosterone katika damu wakati wa asubuhi. Wale waliopata usingizi mzuri na kwa muda mrefu (walau saa nane) walikuwa na kiwango kikubwa cha testosterone wakati wale waliopata usingizi wa kubabaisha (saa nne) walikutwa na kiwango cha chini cha homoni hiyo. Wastani wa muda wa kulala ulikuwa masaa sita.

"Pamoja na kwamba matokeo ya utafiti huu yanaonesha kuwa urefu wa muda wa kulala wa mtu waweza kuwa kiashiria cha mabadiliko ya homoni katika mwili yanayohusiana na umri, matokeo ya utafiti huu yanatoa tu picha ya nini kinachotokea mwilini kama mtu asipopata usingizi wa kutosha. Hata hivyo, tafiti zaidi zinahitajika ili kuthibitisha umuhimu wa uhusiano kati ya usingizi na mabadiliko ya homoni katika mwili," anasema Dr. Penev.

Wataalamu wa masuala ya afya ya usingizi wanashauri watu wazima kupata wastani wa angalau saa saba mpaka nane za kulala kila usiku ili kuwa na afya bora. Ripoti kamili ya matokeo ya utafiti huu inapatikana katika toleo la mwezi April, 2007 la jarida la afya la Sleep.

No comments:

Post a Comment