Saturday, March 17, 2012

UKIMSALITI MPENZI UTAFAIDI NINI?

KAMA kuna kitu kinachukiwa na wengi katika mapenzi, basi ni usaliti. Ni kilio cha wengi. Vijana kwa wazee, wote hawa hawataki kusalitiwa. Usaliti una maumivu makali. Kiukweli kila mmoja huwa anajisikia vibaya sana anaposalitiwa.

Wengi (hasa wanawaume) baada ya kuwasaliti wapenzi wao huwa na maamuzi mazito sana. Wakati mwingine hufikia uamuzi wa kukatisha uhusiano kwa sababu hiyo. Unadhani ni kwa nini wanachukua uamuzi huo mgumu? Hakuna kingine zaidi ya maumivu.

Leo rafiki yangu, nakwenda kuzungumzia upande wa pili wa maumivu ya usaliti. Unajua kuna watu ambao huumia na kuchukia sana wanaposalitiwa, lakini wao ni wasaliti namba moja. Kwa nini wanafanya hivyo?

Je, kwa kufanya hivyo wanafaidika nini? Hebu nizungumze na wewe rafiki yangu ambaye una tabia hiyo mbaya ya kusaliti, unajisikiaje unaposaliti? Amani? Kuna faida unayoipata kwa kusaliti kwako?

BINADAMU WOTE SAWA
Kuna mambo mengi ambayo mpenzi akifanyiwa na mwenzake lazima ataumia sana. Ingawa kuna mengine yanafichwa au kupasishwa kama sahihi, lakini ukweli unabaki pale pale kwamba yanaumiza.

Kikubwa ambacho unatakiwa kufahamu ni kwamba maumivu hayo yapo sawa kwa kila mmoja. Haijalishi jinsi, umri, kabila wala dini, maumivu ya mapenzi yote yanafanana. Kufanana huko kunasababishwa na mioyo yote kuwa na nyama!
Kwa sababu mioyo yote ina nyama basi unatakiwa kufahamu kwamba, jinsi unavyoumia wewe moyoni mwako, ndivyo mpenzi wako anavyoumia ikiwa utamkwaza kwa namna yoyote.

VIPI UKISALITIWA?
Unajua kabisa una mpenzi, tena inawezekana wakati mwingine mmeshawahi kuzungumza juu ya kuishi pamoja, lakini bila haya wala aibu, unamsaliti! Kwa nini unafanya hivyo? Kama umeona hana thamani tena kwako, kwa nini unazidi kumpotezea muda?
Unafikiri anafurahia sana wewe kuwa na kimada mwingine huko uchochoroni au unadhani atafurahi siku akijua kuwa una mtoto umezaa nje ya ndoa yako? Nafsi yako yenyewe inakusuta, inajua ni kiasi gani unamkosea mpenzi wako lakini unajifanya kichwa ngumu na kuendelea na uchafu wako. Kwa nini hutaki kubadilika?

Hebu jitoe katika nafasi yako, kisha mfanye mpenzi wako ndiyo wewe, halafu fikiria kama yeye ndiyo angekuwa anakusaliti, ungejikiaje? Lazima utaumia! Sasa kama utaumia kwa nini unaendelea kumfanya mwenzako akose raha?

Lazima uwe na moyo wa huruma, akili yako ifanye kazi ipasavyo na kugundua makosa unayoyafanya kisha kufanya mabadiliko ya haraka. Amini jinsi utakavyoumia kwa kufanyiwa mabaya na mwenzako ndivyo mpenzio anavyoumia kwa mabaya unayoyafanya.
Wengi wamekuwa wakiwasaliti wapenzi wao wakiwa hawafikirii siku ya wao kufanyiwa hivyo itakavyokuwa. Hebu vuta picha, unakwenda nyumbani kwa mpenzi wako, unagonga mlango haufunguliwi!

Lakini baadaye unahisi kama ndani kuna watu, hilo linaingia akilini mwako baada ya kuona viatu vya mpenzi wako pamoja na viatu vingine vya jinsi tofauti ya mpenzi wako. Unaamua kusukuma mlango na kuingia ndani, hamadi! Unakuta mpenzio akiwa anafanya mapenzi na patna mwingine...utajisikiaje?
Mapenzi ya kweli hayaambatani na usaliti. Penzi la kweli lina uaminifu wa dhati, kuchukuliana, kupendana, kusaidiana, ukarimu, huruma na mengine mengi ambayo huyafanya mapenzi yazidi kuwa imara kila siku.

HAKUNA MWENYE HAKI YA KUSALITI
Acha kujiwazia mwenyewe, kujiona wewe pekee ndiye mwenye haki ya kuwa salama katika penzi lako. Chunga nafsi yako lakini wakati huo huo ukiangalia kwa jicho la tatu, nafsi ya mwenzako.

Kila mmoja anaumia anapohisi anasalitiwa, hivi unafikiri ni nani, anayependa kushea mapenzi? Nani mwenye haki ya kumsaliti mwenzake? Kimsingi hakuna. Utakuta mwingine simu ya mpenzi wake ikiita yeye anakuwa wa kwanza kuichukua na kutaka kupokea au kusoma sms, lakini subiri sasa simu yake iite; anakuwa mkali huyo! Acha kujifikiria peke yako.

ZINGATIO LA MWISHO
Siamini kama kuna ambacho sijaandika katika vipengele vyote vinne vilivyopita, lakini hapa nakusisitiza ufanye mabadiliko ya haraka ili mwisho wa siku uweze kuishi maisha mapya, mazuri, yenye mapenzi ya kweli huku moyo wako ukiwa huru.

Hutakuwa na hukumu moyoni mwako, maana utakuwa unamtendea haki mpenzi wako. Lakini kama ukiendelea kumsaliti, ujue wazi kwamba utakuwa unajizidishia maumivu katika moyo wako.

No comments:

Post a Comment