Saturday, March 17, 2012

Kabla ya ndoa jiulize, kwa nini umempenda

Uamuzi wa ndoa si wa kujaribu. Unatakiwa kujihakikishia kwamba ni kweli umevutiwa na kila kitu cha mwenzako, kwamba utakuwa naye katika shida na raha. Hayo ndiyo mambo ya kuzingatia.
Nimeshaandika mengi kuhusu sifa za anayetakiwa kuoa au kuolewa, lakini nasogea mbele zaidi na kuangalia sababu za kumpenda mtarajiwa wako katika ndoa.

Zipo sababu za msingi sana ambazo unatakiwa kuwa nazo kabla ya kuingia kwenye ndoa

KWA NINI UJIULIZE
Lazima nifafanue hili kwanza kabla ya kuendelea. Hivi unafikiri ni kwa nini ni lazima kujiuliza sababu za kumpenda mwenzi wako?
Yes! Ni kwa lengo la kujiwekea usalama katika ndoa yako ijayo. Kujiandalia amani na pumziko la kweli. Kwenye mapenzi ya dhati pekee ndipo vinapopatikana vitu nilivyotaja hapo juu.

Kwa maneno mengine kuwa na majibu ya swali linalosomeka kwenye kichwa cha mada hii ni kujihakikishia ndoa bora. Tuendelee kujifunza.

NI MWENZI WA NDOTO ZAKO?
Jambo kubwa kuliko yote ambalo unatakiwa kuliangalia kwa jicho la tatu ni kama mwenzi huyo ni wa ndoto zako. Je, yukoje? Rafiki, siku zote kabla ya kuamua kufanya chochote lazima ujiulize kama ndicho ulichokuwa ukikifikiria.
Hata kwa upande wa mwenzi wako, lazima ujiridhishe, ni kweli ni yule uliyekuwa unamtarajia? Ana sifa unazohitaji? Acha tabia ya kujifariji kwamba utampenda taratibu ndani ya ndoa, hicho kitu hakipo.

Hakuna kujifunza kupenda katika ndoa, lazima ujihakikishie mwenyewe kuwa mwenzi wako ni yule mwenye sifa ulizokuwa ukizitarajia. Hili ni la msingi, maana unaweza kuwa naye siku mbili, ukatamani mwingine nje, kwa nini? Kwa sababu si yule mwenye sifa ulizotarajia.

NI SURA, UMBILE?
Kuna baadhi ya watu utawasikia wakisema: “Mpenzi wangu ananivutia sana, yaani ni mzuri sana. Najua hata nikitoka naye, marafiki zangu watanisifia kwa kuchagua vizuri...”
Hizi ni fikra potofu ndugu zangu. Mapenzi ya kweli hayapo kwenye sura wala umbile la mtu. Vipo vigezo vya muhimu kabisa vya kuzingatia tofauti na uzuri wa sura.

Sura hubadilika ndugu zangu, binadamu wanazeeka, kuna kuugua na matatizo mengine ambayo yanaweza kubadilisha mwonekano ambao ulikuvutia. Je, yakitokea ndiyo utakuwa mwisho wa kumpenda?
Kama leo hii unamuoa kwa sababu umevutiwa na matiti yake madogo, akishazaa na kunyonyesha kisha yakaanguka, ndiyo mwisho wa kumpenda? Umempendea ngozi yake nyororo, akipata ‘aleji’ ya mafuta, ngozi ikaharibika na kuwa na mabakamabaka utakuwa mwisho wenu?

Wewe mwenye mpango wa kuolewa na mwanaume mwenye kigezo cha kifua cha kimapenzi, kesho akifutuka na kuwa na kitambi utamuacha? Rafiki yangu, kiukweli ni kwamba kigezo cha uzuri wa sura na umbile si sahihi kabisa katika kuchagua mwenzi. Vipo vitu vingine muhimu zaidi vya kuangalia.

Kama ulikuwa unaishi katika dunia ya fikra hizo, hama ndugu yangu.

No comments:

Post a Comment