Saturday, March 17, 2012

Mbinu za kumwacha mpenzi wako bila ya kumuumiza

Katika ulimwengu wa mapenzi, kila siku watu wanaingia kwenye uhusiano lakini elewa kwamba siku ambayo wewe unamzimikia mtu flani siku hiyo hiyo wapo wanaozinguana na kuachana.
Si kwa wapenzi tu, hata kwenye ndoa wapo ambao leo hii ndiyo wanaoana lakini leo hii hii kuna wanaopeana talaka. Iko hivyo na kwa maana hiyo suala la kupendana lipo lakini la kuachana nalo halikwepeki.
Ndiyo maana ukijaribu kufuatilia hata wewe unayesoma makala haya yawezekana mpaka umefikia hatua uliyonayo umeshaacha au kuachwa.
Hilo ndilo limenifanya niandike mada hii. Je, unajua mbinu sahihi za kumuacha mtu ambaye mlikuwa mkiambiana I love you, I love you too? Kama jibu ni hapana, leo nitakupa shule inayoweza kukuongoza katika hilo.
Lakini kabla ya kulizungumzia hilo niseme tu kwamba miongoni mwa vitu nisivyovipenda katika maisha yangu ni kusikia flani na flani waliokuwa wanapendana sana hadi kuwa gumzo mtaani wameachana.
Inaniuma kwa sababu najua ivavyouma. Mara nyingi anayeachwa anaumia zaidi hasa akiwa hajajiandaa na ndiyo maana wataalamu wa masuala ya mapenzi wamejaribu kuanisha mbinu ambazo unaweza kuzitumia katika zoezi zima la kumuacha mpenzi au mume/mke wako hasa pale zinapokuwepo sababu za msingi zinazoweza kukubalika.

1. Hakikisha umedhamiria
Unatakiwa uwe umejiandaa kumkosa katika maisha yako. Jadiliana na akili pamoja na moyo wako kama kweli vimeridhika na uamuzi unaotaka kuchukua. Jiulize ni kweli amekukosea kiasi kwamba huwezi kuendelea kuwa naye?

2. Usiwe mwenye hasira
Unapotaka kumuacha mpenzi, mume au mke wako kwa sababu maalum, hakikisha huna hasira.Tulia ili hata pale utakapokuwa hauko naye usije ukajuta na kudhani hukuchukua uamuzi sahihi.

3. Muda na siku sahihi
Wataalamu wa mapenzi wanasema kuwa, muda wa asubuhi siyo mzuri kumuacha mpenzi wako kwani utampa wakati mgumu siku nzima lakini pia kwa wapenzi wanaofanya kazi siku za katikati ya wiki siyo siku nzuri.
Siku ya Ijumaa jioni inapendekezwa kuwa siku nzuri ya kumuacha mpenzi wako kwa maelezo kwamba ataitumia wikiendi kujiliwaza na hata inapofika Jumatatu, anakuwa amepoa tayari kwa kuendelea na majukumu yake.

Kama nilivyosema awali, kila siku watu wanaingia kwenye uhusiano mpya lakini pia wengine wanaachana. Sababu za kuachana kwa wapenzi zinatofautiana ila kikubwa ni kwamba unapoachana na mtu ambaye mlikuwa ‘mwili mmoja’ hutakiwi kumgeuza adui yako kwa asilimia zote, hata kama kakukosea vipi.
Kwa mfano, yawezekana ulitokea kumpenda na kuhisi angeweza kuwa wako wa maisha lakini kadiri siku zinavyokwenda unabaini si mtu sahihi kwako. Katika mazingira hayo suala la kumuacha haliepukiki ila cha kujiuliza ni kwamba utamuachaje?

Je, itakuwa ni sahihi kumuambia laivu kwamba mimi na wewe basi? Inawezekana ukafanya hivyo ila wataalam wa mapenzi hawashauri kwani wanajua madhara ya kutumia mbinu kama hiyo na ndiyo maana wakashauri kutumia njia ambazo zinaweza kusaidia ukamuacha lakini bila kumuumiza na maisha yakaendelea kuwepo.

Jitoe taratibu
Chukulia kwamba umekuwa naye kwa muda mrefu kidogo ukiwa na malengo ya kuingia naye kwenye ndoa lakini katika utafiti wako ukabaini hakufai, unashauriwa kujitoa kwake kimyakimya. Unachotakiwa katika mbinu hii ni kupunguza kumtendea mambo ya kiupendo.
Kwa mfano, unaweza kupunguza kuonana naye, kumpigia simu, kumtumia sms na hata kumsaidia kifedha kama ulikuwa ukifanya hivyo. Kwa kufanya hayo ni lazima ataanza kuona tofauti na kuhisi penzi linaelekea ukingoni.
Aidha, kwa kumfanyia hivyo ni lazima atahoji juu ya mabadiliko hayo. Wewe hutakiwi kutoa maelezo yoyote zaidi ya kuendelea kuyeyusha bila kumwambia wazi kwamba umemtoa moyoni mwako.
Kama huyo mpenzi wako ni mwelewa atagundua kuwa, ndiyo unamuacha kimtindo na yeye ataanza kujiandaa kukukosa, hata pale utakapokata mawasiliano moja kwa moja atakuwa ameshajua kuwa umemuacha hata bila kumueleza.
Ukigundua ameshafahamu kuwa umemuacha, hapo unaweza kumwambia kwa kifupi kwamba umeamua bora kila mmoja aendelee na maisha yake. Kisaikolojia utakuwa hujamuumiza sana lakini tayari utakuwa umemuacha.

Maneno ya busara
Unaweza kumuacha mpenzi wako kwa kutumia lugha ambayo yeye mwenyewe atahisi hukuwa na jinsi, ilikuwa ni lazima umuache. Mfano: ‘Ashura, kusema ukweli nilikupenda sana na mpaka sasa naamini wewe ni mwanamke wa maisha yangu, sikuamini kama yupo mwanamke mwingine wa kunipa furaha kama wewe lakini kwa hili lililotokea sina jinsi, inabidi nikuache. Utaendelea kuwa rafiki yangu na kama ni kukusaidia nitakusaidia kama rafiki na si mpenzi.”
Hayo ni maneno ambayo mwanaume anamwambia mpenzi wake akimaanisha anamuacha lakini ukiyachunguza utabaini hayachomi sana kwa kuwa anayeachwa bado anapewa nafasi nyingine ya urafiki wa karibu na si mapenzi tena.
Mimi nikushauri tu kwamba, hakikisha unapotaka kuachana na mtu ambaye mmekuwa pamoja kwa muda mrefu unakuwa makini. Hata kama amekukosea vipi lakini busara itumike hasa kwa kuzingatia yale mazuri ambayo aliwahi kukufanyia huko nyuma.

No comments:

Post a Comment