Saturday, March 17, 2012

Usiwe Kipofu wa Mapenzi

Kila kiumbe kina utashi wa kupenda kwa vile upendo ndiyo tuliohimizwa sisi wanadamu, lakini ukizidi unakuwa ugonjwa ambao huenda usipate dawa.
Naleta maada hii baada ya kupata swali kutoka kwa dada yangu mmoja ambaye alitokea kumpenda kaka mmoja hadi kufikia kushindwa hata kuzungumza pale anapomuona.
Amejikuta akishindwa kujiamini kujieleza kwa yule kaka na kuona hawezi kuzungumza chochote kitakachoeleweka kwa vile amepoteza kujiamini kutokana na kumpenda kupita kiasi.
Kupenda bila kujielewa ni sawa na wendawazimu, hata unapokuwa ndani ya penzi hilo lililokutia wendawazimu, unapoteza kujiamini kwa kuogopa kulipoteza penzi ulilolitafuta kwa muda mrefu.
Nimekuwa nikielezea kujiamini kwa mwanadamu mbele ya mapenzi na kutojishusha thamani hata kama umempenda mtu kupindukia. Kupenda ni haki yako ya msingi lakini usiwe mtumwa wa mapenzi kwa kushindwa kujitambua wewe ni nani na kwa nini upo pale.
Kupenda sawa, lakini ukizidisha inakuwa sumu inayokutafuna taratibu kwa vile huna maamuzi yoyote ya moyo wako kwa kuogopa kumuudhi umpendaye. Hii si kwa wanawake bali kwa watu wote.
Wapo wanaofanyiwa vituko vya makusudi na wapenzi wao kwa vile tu wanatambua wanapendwa na kukaa kimya kiasi cha kuwashangaza watu.
Kwa vile hujiamini na mapenzi ndiyo yaliyochukua nafasi kubwa kwako na kuziba mishipa ya ufahamu na kuamini hakuna mpenzi mzuri kama uliyenaye na kuona kumpata kwako ni bahati, unakuwa huna maamuzi, kila utakaloambiwa unaona sawa, liwe zuri au baya.
Hapa kidogo napenda mnisikilize kwa makini, kila kiumbe kina haki ya kupenda, lakini lazima ujue unayempenda kama kweli ana mapenzi ya dhati kwako. Kwa vile unampenda unajitoa kwake kama kafara ya mapenzi na kuwa tayari kufanyiwa chochote lakini usiachwe.
Tumeshuhudia wanawake kwa wanaume wakiteseka ndani ya mapenzi yao kwa penzi la upande mmoja, unayalazimisha mapenzi kwa vile tu unampenda na kuona hakuna kiumbe chochote mbele yako. Acha kuwa kipofu wa mapenzi, siku zote mbegu ya upendo huota katika moyo wenye rutuba ya upendo.
Usihadaike na rangi tamu ya chai sukari, matendo mema ndiyo yanayojenga upendo ndani ya nyumba. Usiitupe ovyo mbegu yako kwa vile tu umetokea kumpenda na kwamba kila ukimuona unachanganyikiwa.
Je, unajua historia yake? Ana mapenzi ya kweli kwako? Jiepushe kuutoa mwili wako ovyo kwa vile umependa tu bila kujua mwenzako naye anakupenda.
Hata unayempenda ukimpata basi usikubali kuwa mtumwa wa mapenzi, kwa penzi kukuongoza wewe na si wewe kuliongoza penzi. Siku zote wewe ndiye uliongoze penzi na kutoa maamuzi pale litakapokwenda kinyume.
Hii itakufanya uonekane mwenye msimamo na si mtu wa kuburuzwa.

No comments:

Post a Comment