Saturday, March 17, 2012

Anakupenda lakini anakutesa, mapenzi yapo wapi

Mtu anasema kuwa ana mpenzi wake ambaye wanapendana sana lakini sasa hivi hamuelewi baada ya kuona upendo umepungua.
Ukiangalia kichwa cha habari hapo juu, kina jibu la moja kwa moja lakini ni vigumu mtu kuelewa kwa vile bado hajifahamu katika mapenzi amesimama upande gani.
Unasema wewe na mpenzi wako mnapendana sana, lakini sasa hivi mpenzi wako humuelewi, ukimpigia simu hapokei kama zamani au akipokea, anakuwa na majibu ya mkato tofauti na mwanzo wa mapenzi yenu.
Hili swali naweza kusema limekuwa fasheni katika mapenzi ya sasa, hasa kwa wapenzi waliokuwa pamoja na baadaye kutengana kwa ajili ya kazi au masomo, kwa hawa lazima baada ya muda tatizo hili hutokea.

Kuna nini?
Wengi sehemu hii huwashinda kwa vile huwa na mapenzi ya mdomoni na machoni. Wapenzi wengi huwa na heshima na uaminifu kama wanawaona wapenzi wao kila siku, mtu huogopa kufanya usaliti kwa kuwa mpenzi wake yupo, lakini huyohuyo huwa hana uaminifu anapokuwa peke yake sehemu ya mbali.

Huwa mwepesi kuanzisha uhusiano mpya kwa kuamini ni wa kupita.
Kwa vile wengi hawana mioyo migumu ya uvumilivu, hujikuta wakizama moja kwa moja na kuwasahau waliowaacha nyumbani. Hapo ndipo ule utata unaosumbua huanza. Utasikia nipo bize au simu kutopokelewa kabisa na kwa wengine huwapa wapenzi wao wapya wapokee.
Kwa vile uliye mbali na mpenzi wako hujui mwenzako kazama kwenye penzi jipya, hapo ndipo huanza kuumia moyoni ukiamini kabisa mpenzi wako anakupenda lakini hujui tatizo.
Kama ungekuwa mfuatiliaji mzuri wa makala zangu, ungejua mtu mwenye mapenzi ya kweli yupo vipi. Mwenye mapenzi ya kweli ni tulizo la mawazo ya mpenzi wake, ni mpole na mwenye huruma na mara zote hujiepusha kuwa sehemu ya maumivu yako.

Hivyo, ukiona mpenzi wako haeleweki, unatakiwa kuanza kuizoea hali ile ili kujiandaa kwa penzi jipya, kwa vile ule mche wa mapenzi ulioupanda ndani ya moyo wa mwenzako umesinyaa.
Usipende kujitesa kwa kujitakia, kama umeona kabisa kuna mabadiliko ndani ya penzi ni wakati wa kuchukua uamuzi mgumu ili kunusuru mateso yasiyo na sababu.

Jiepushe kuishi mapenzi ya mazoea kwa kuamini unapendwa wakati unateswa, hakuna upendo wa mateso hata siku moja. Mapenzi ni furaha na wala si karaha. Acha kuusemea moyo wa mwenzako kuwa anakupenda wakati ndiye chanzo cha ugonjwa wako wa moyo.
Kabla ya kuchukua uamuzi mgumu wa kuvunja penzi, msomee mpenzi wako mashtaka na kumueleza ukweli kuwa umechoka kuumia, akikosa utetezi unaoeleweka, una nafasi ya kuvunja penzi.
Kama atakuwa tayari kukiri makosa na kujirudi, unaweza kumpa nafasi nyingine lakini akirudia makosa, achana naye, fungua ukurasa mpya.

No comments:

Post a Comment