Sunday, March 18, 2012

Heri upweke kuliko mpenzi asiyejua maana III

KATIKA somo lililopita kama nilivyogusia ushauri wa Brandon King na makala yake ya “Be aware with ones heart” nilieleza kuwa ni kosa kubwa kumuona mwenzi wako ana thamani ndogo na wakati huo huo ukawa unatoa kipaumbele kwa watu wa pembeni.

Tafsiri inayotawala katika uhusiano ni kuwa kundi linalosumbua mno na kuonekana ni sugu kwa tabia ya namna hii ni lile ambalo linawahusisha memba wanaoingia kwenye uhusiano wa kimapenzi pasipo imani kamili.
Wanajaribu na hawana ufahamu kwamba moyo haufanyiwi majaribio.
Hii ndiyo sababu ya kusisitiza kuwa ikiwa hujaamua kupenda basi kaa mbali.

Kuna mengi unayoweza kumsababishia mwenzako, ukampotezea muda huku ukimjengea imani upo naye lakini mwisho anakuja kujikuta anauguza dondo la moyo.
Sikitiko la mahaba linashinda msiba!
Hujaumia subiri usimuliwe.

Moyo unapouma kwa sababu ya mapenzi hakuna kitu cha kupoza. Unaweza kunywa pombe na usilewe, ukabugia dawa za usingizi na usilale.
Kifua kinajaa na kwa sababu inaathiri mfumo wa upumuaji na mapafu nayo huingia katika maumivu.
Sikitiko la mahaba ni hatari, likikufika utapungua uzito kwa kasi bila maelezo ya ziada.

Chakula hakiwezi kupita na macho yanaweza kujaa machozi ilhali unatamani kujizuia. Binadamu tumetofautiana, wapo wanaotamani kupendwa lakini wengine wanawacheza shere wanaowapenda.
Dawa kuu ni kujihadhari na watu wasio na mapenzi ya dhati.

Kuwaepuka kadiri inavyowezekana.

Ni mzuri na anakuvutia lakini heri umuone kwa mbali kwa sababu ukimjaza moyoni atakusumbua.
Atakutoa machozi katika eneo ambalo ulihitaji kufurahi.
Maumivu yako hata yajali kwa sababu hana hisia na wewe.

Atakusaliti bila woga kwa maana hana hofu yoyote juu yako.
Itakuwa ngumu kumuacha, vilevile utaona uamuzi wowote wa kutengana naye ni mateso makubwa kwamba heri uumie ukiwa naye kuliko kuachana.

Usijidanganye ndugu yangu, wewe ni binadamu uliyekamilika, kwa hiyo usitarajie mtu wa pili au wa tatu anaweza kusikia kile kinachokuuma moyoni.

Mateso yaliyopo ndani yako unayajua mwenyewe, kwa hiyo unatakiwa kuwa wa kwanza kujihurumia na kuchukua uamuzi wa kujiokoa na mateso.

Kuna kitu kimoja ambacho unatakiwa kukifahamu; Binadamu ni wa ajabu sana, watayajua yako ya siri na kile ambacho mwenzi wako anakifanya pembeni, lakini hawakwambii badala yake wataketi pembeni kuzungumza. “Aah yule wa ajabu, anadhani kapata mpenzi kumbe kapatikana!”

Wengine utakaa nao meza moja kushauriana mambo mbalimbali, lakini anayekwambia umvumilie mwenzi wako licha ya vitimbi anavyokufanyia, ndiyo huyo huyo akikaa pembeni na watu anawaambia kwa mtindo wa kukucheka kwamba unamng’ang’ania mpenzi bomu.

Lingine ni kuwa unapokuwa na mpenzi ambaye hakuheshimu, thamani yako katika jamii inashuka.
Kukuheshimu si mpaka akutukane, bali vitendo vyake. Kutoka na wapenzi wengine, kujenga mazoea na watu wa jinsia nyingine kiasi kwamba mpaka anahusishwa kwamba ni wapenzi wake.

Mathalan, mpenzi wako anakuwa na urafiki na watu mpaka anafikiriwa anatembea nao.
Hii ni tabia mbaya na haikubaliki, ingawa wapo wazuri wa kutetea. Watasema, sisi ni washkaji ila fahamu mapenzi yenu yanazikutanisha familia mbili. Una ndugu, marafiki, wazazi.

Inakuaje mpenzi wako anahisiwa anatoka na mwanamke mwingine na taarifa zinafika mpaka kwa wazazi wako? Watajua mkwe wao ni kicheche na hilo litakugharimu kwa kiasi kikubwa.

Unatakiwa kulinda thamani, heshima na utu wako, kwa hiyo achana na mtu asiyejua maana!
Unaweza kuona leo inakuuma kwa sababu unaepukana na mtu ambaye unampenda lakini hiyo ni nafuu kwako kesho.
Amini kwamba mwisho wa mateso hayo ya moyo ni furaha kubwa, mwisho utajiuliza:

Ni kipi kilichokuwa kinakufanya uumie kwa muda wote? Upo huru sasa!
Mapenzi maana yake utulivu wa moyo, yaani wewe na mtu wako spesho muogelee katika dimbwi maalum, ninyi wote mkiwa na amani.

Mkishirikiana katika hali zote. Inakuwa hakuna anayewaza la kwake peke yake isipokuwa kwa ajili yenu.
Ukilia anakuwa wa kwanza kukubembeleza, anapogundua amekuudhi ni mwepesi kukuomba msamaha.
Anasoma mabadiliko yako na kukuuliza kile kinachokusumbua.
Anaficha siri zako, anazungumza lugha tamu na hisia zake zote zipo kwako. Kwa wengine haoni hatamani.

USITHUBUTU KULAZIMISHA PENZI

Yamewafika wengi na wameumia, kwa hiyo ni vizuri kuwa makini.
Utauguza donda la moyo lisiloweza kutibika, utakonda wenzako watakucheka, atakugeuza punda afanye anachokitaka.
Ni kazi bure kumpenda mtu asiyekupenda.
Pamoja na maumivu unayoweza kuyapata lakini kuna vitu hivi lazima vikukute kwa huyo mwenzi wako wa kulazimisha.

ATAKUTESA KWA UBINAFSI WAKE

Hana mapenzi ya kweli na wewe, kwa hiyo si kila wakati atakufikiria.
Kama hamjawa kwenye ndoa itakusumbua kwa sababu ni ngumu kufikiria kwa ajili yenu, isipokuwa atawaza kwa matilaba yake. Kama kuoana, utalazimisha wewe lakini yeye hatokuwa na habari.

Mkiwa kwenye ndoa, hatojisikia fahari kutoka na wewe atalazimisha maisha ya kila mmoja kuwa huru kufanya mambo yake.
Nguo atanunua za kwake na hata siku moja hutoona amekununulia. Wewe utafanya mengi kwa ajili yake lakini yeye atabaki na ubinafsi wake.
Atakutesa, pasha moto ubongo!

AKIONA WENGINE ATAHISI NI WAZURI ZAIDI YAKO!

Mtu huishi kwa fikra zake, kwa hiyo kwa sababu hakupendi kwa moyo wake wote inakuwa ngumu kukukubali, hivyo anapokutana na watu wengine barabarani atadhani ni wazuri kuliko wewe. Atababaika hata mbele yako.

Unahitaji heshima ya kiwango bora na kwa kawaida mpenzi wako anapaswa kukuona wewe ni mtu namba moja.
Kama hakupi nafasi hiyo maana yake anapenda nusunusu au hapendi kabisa.
Usikaribishe mateso, fikiria kesho, chukua uamuzi leo.

HASIFU MUONEKANO WAKO, ANA LAKE KICHWANI!
Hujiulizi, kila siku anakuona na hakusifii! Ni wazi kuwa hata kama wewe ni mzuri kiasi gani, unavaa na kupendeza kwa namna bora kabisa lakini mwenzi wako hawezi kukupa pongezi kwa sababu ana lake kichwani.

Ukiona hilo ujue kwamba yupo mtu ambaye anamsifu kwa sababu ndiye anayemkubali, na wewe utasifiwa na wengine.
Inauma mwenzi wako kukuacha nyumbani na kwenda kumwaga sifa pembeni, wakati na wewe unazihitaji.
Una thamani kubwa, pigania utulivu wa moyo wako!

No comments:

Post a Comment