Sunday, March 18, 2012

Dawa za Usingizi Chanzo cha Saratani na Kifo

Dawa za Usingizi
Utafiti uliofanywa nchini Marekani hivi karibuni umetoa matokeo ya kushangaza kwa kusema ya kwamba matumizi ya dawa za usingizi huongeza hatari ya kupata saratani pamoja na mtu kufa mapema. Utafiti huo umesema wale wanaotumia dozi kubwa ya dawa ya usingizi wako kwenye hatari ya kupata magonjwa ya saratani.
Utafiti huo ambao ulifanywa na watafiti wa kitengo cha usingizi katika kituo cha Jackson Hole Centre for Preventive Medicine in Wyoming and the Scripps Clinic Viterbi Family Sleep Centre kilichopo jijini California nchini Marekani ili kuangalia hatima ya watu wanaotumia dawa za usingizi aina ya benzodiazepines kama temazepam, diazepam (valium), dawa mpya aina ya zolpidem, zopiclone, zaleplon, dawa za jamii ya barbiturates na zile zinazotumiwa kutibu mcharuko mwili (allergy) na ambazo huleta usingizi.
Matokeo ya utafiti huo yanasema wale wanaotumia dawa za usingizi (Hypnotics) walizoandikiwa na Daktari wako kwenye hatari ya 4.6 kufa ndani ya miaka 2 na nusu ukilinganisha na watu ambao hawatumii dawa za usingizi. Wale ambao wanatumia dozi ndogo ya dawa za usingizi yaani wanaotumia wastani wa vidonge 4-18 kwa mwaka wako kwenye hatari ya mara 3.6 zaidi kufa kulinganisha na wale ambao hawatumii dawa za usingizi.
Wale wanaotumia dozi kubwa yaani vidonge 18-132 kwa mwaka wako kwenye hatari kubwa ya mara 4.4 zaidi kufa, na wale wanaotumia zaidi ya vidonge 132 kwa mwaka wako kwenye hatari ya mara 5.3 zaidi kufa kulinganisha na wale ambao hawatumii dawa za usingizi. Asilimia 93 ya wale walioshiriki katika utafiti huu walikuwa ni wale wanaotumia dozi kubwa ya dawa za usingizi. Pia wale wanaotumia dozi kubwa ya dawa hizi wako kwenye hatari ya asilimia 35 kupata saratani kubwa. Kwa wale wanaotumia dawa aina ya zolpidem wako kwenye hatari ya mara 5.7 kufa huku wale wanaotumia dawa aina ya temazepam wako kwenye hatari ya mara 6.7 kufa kulinganisha na wale wasiotumia dawa za usingizi.
Utafiti huo umesema wale walio kwenye hatari ya madhara haya ya dawa za usingizi ni wale walio katika umri wa miaka 18-55 ingawa sababu halisi haikuelezwa katika matokeo ya utafiti huo. Wagonjwa 10,500 wanaotumia dawa za usingizi walishiriki katika utafiti huo wakilinganishwa na watu 23,500 ambao hawatumii dawa za usingizi walioshiriki katika utafiti huo.
Watafiti hao walisema tiba ya kutotumia dawa yaani ya tiba ya utambuzi wa tabia (cognitive behavior therapy) inaweza kuwa na manufaa zaidi kuliko matumizi ya dawa za usingizi na hata matumizi ya dawa za usingizi kwa muda mfupi yanapaswa kuangaliwa kwa makini. Watafiti hao wakiandika katika jarida la British Medical Journal walisema “Faida chache zinazopatikana kutokana na matumizi ya dawa za usingizi ambazo zilitafitiwa kwa kina na makundi ambayo hayana maslahi yoyote na dawa hizi haziwezi kuhalalisha madhara yatokanayo na matumizi ya dawa hizi za usingizi”.
Matokeo ya utafiti huu ni changamoto kubwa katika fani ya afya hasa ukizingatia ya kwamba watu wengi hutumia dawa za usingizi kutokana na kupatikana kiurahisi katika maduka mbalimbali ya dawa katika Afrika Mashariki. Pia ni changamoto kubwa sana kutokana na dawa hizi kutumika wakati wa upasuaji, kutibu magonjwa ya akili, kutibu mcharuko mwili, msongo wa mawazo na hata kwa wazee.
Kulingana na matokeo haya ni vizuri kuangalia upya matumizi ya dawa za usingizi na utafiti zaidi unahitajika kufanyika kabla ya kutoa msimamo kuhusu matumizi ya dawa za usingizi.

No comments:

Post a Comment