Sunday, March 18, 2012

Hofu iliyopitiliza (Generalized Anxiety Disorder, GAD)

Hofu iliyopitiliza

Utangulizi
Mada hii ina lengo la kuzungumzia tatizo la kuwa na hofu au wasiwasi uliopita kiasi au kwa kitaalamu Generalized anxiety disorder (GAD).
Kwa ajili ya kutofautisha kati ya hofu iliyopitiliza na hofu ya kawaida ambayo yaweza kumkumba mwanadamu yeyote, wakati fulani fulani mwandishi atatumia maneno anxiety au GAD katika kuwasilisha ujumbe wake.

Hofu iliyopitiliza au au anxiety au GAD huambatana na hali ya kuwa na wasiwasi kupita kiasi juu ya maisha ya kila siku pamoja na matukio yake bila hata muhusika kuwa na sababu maalum ya kuwa na hofu hiyo. Kwa maneno mengine ni kuwa, watu wenye anxiety hujihisi hofu kubwa bila ya kuwa na sababu yeyote ya msingi ya kuwafanya wawe hivyo. Mara nyingi watu wenye tatizo hili huwa na tabia ya kuhisi kwamba janga kubwa litawatokea karibuni au maafa yatamkumba katika maisha yake na daima hawaachi kuwa na hofu isiyo na sababu juu ya familia zao, pesa, afya, ajira, masomo au hata biashara zao.

Maisha yao ya kila siku huwa na mchanganyiko wa hofu, wasiwasi na huzuni, kiasi kwamba hatimaye hofu hutawala mawazo ya muhusika kiasi cha kuingilia utendaji wake wa kila siku ikiwemo kazi, masomo, shughuli zake za kijamii, na hata mahusiano na mwenza wake wa ndoa.

Dalili za hofu iliyopitiliza (anxiety) ni nini?
Kama tulivyoona hapo juu kwenye utangulizi, hofu isiyo na kikomo huathiri zaidi uwezo wa mtu katika kufikiri, ingawa baadaye humletea matatizo ya kiafya katika mwili. Hali hii inaweza kuambatana na dalili mbalimbali, siyo tu zile zinazohusu uwezo wa kufikiri na akili bali hata zinazohusiana na utendaji kazi wa mwili.

Baadhi ya dalili hizo ni:
• Kuwa na hisia ya kuwepo kwa janga, kwamba kitu kibaya kitatokea muda wowote, na kwamba hatari kubwa inamnyemelea
• Hali ya hofu kuu
• Hali ya kujihisi kutaka kukimbia, kuondoka mbali na hatari hiyo
• Rangi ya ngozi kuwa ‘nyeupe’ kama mtu aliyeishiwa damu
• Kujihisi ngozi kuwaka moto
• Hali ya koo kubana, kujihisi kama koo limefunga, au umekabwa na kitu kooni
• Hali ya kuchanganyikiwa
• Kujihisi kutengwa na ulimwengu, kupoteza hisia, kupoteza kujitambua nafsi yako mwenyewe
• Kujihisi kama mtu anayeota
• Kizunguzungu, kuhisi kichwa kuwa chepesi, kupepesuka unapotembea
• Kuwa na mvurugano wa hisia
• Hofu ya kurukwa akili
• Hofu ya kupoteza uwezo wa kujithibiti mwenyewe
• Kujihisi kama vile kuna kitu kinachobana kichwani (kama uliyezungushiwa kamba au rubber-band)
• Kujihisi baridi sana au joto sana (ingawa hali ya hewa yaweza kuwa kinyume)
• Kushindwa kujituliza
• Kujihisi kitu kinabana tumboni
• kichefuchefu
• kujihisi ganzi au hali ya kuchomachoma sehemu fulani fulani za mwili
• kuwa na hisia za kupanic
• kuhisi kuziba masikio
• moyo kudunda sana
• Moyo kwenda kasi isivyo kawaida
• Maumivu makali kifuani, shingoni, kwenye bega, kichwani au usoni
• Hali ya kuhisi kukosa hewa au kupumua kwa shida
• Kutokwa na jasho
• Kubanwa na kifua
• Kutetemeka (kunaweza kuonekana waziwazi au kutetemeka kwa ndani bila mtu mwingine kutambua)
• Kuchafuka kwa tumbo
• Kujihisi haja ndogo au kubwa mara kwa mara
• Kutapika
• Uchovu wa mara kwa mara
• Shida ya kupata usingizi au kulala usingizi wa mang’amung’amu

Hofu iliyopitiliza (GAD) husababishwa na nini?
Chanzo halisi cha matatizo ya kuwa na hofu kupita kiasi hakifahamiki. Hata hivyo kuna baadhi ya vitu ambavyo vimegundulika kuwa vinachangia sana kuwepo kwa tatizo hili miongoni mwa watu.

Vitu/mambo hayo ni pamoja na:
Nasaba (genetics): baadhi ya tafiti zimeonesha kuwa nasaba ina nafasi kubwa ya kumfanya mtu wa familia yenye matatizo ya hofu iliyopitiliza naye kuwa na uwezekano mkubwa wa kupata haya. Hii inaamnisha kwamba, hofu iliyopitiliza inaweza kurithiwa miongoni mwa wanafamilia.
Mfumo wa kemikali za ubongo: Kuwepo kwa hofu iliyopitiliza kumehusishwa na kuwepo kwa kiwango kisicho sahihi cha baadhi ya kemikali zinazosaidia kusafirisha taarifa katika ubongo yaani neurotransmitters. Kazi ya kemikali hizi ni kupitisha taarifa na ujumbe mbalimbali kutoka seli moja ya neva mpaka seli nyingine. Iwapo kemikali hizi zitakuwa katika kiwango kisicho sahihi (ama kupungua au kuongezeka) taarifa hazitaweza kusafirishwa kati ya seli za neva na hatimaye hazitaweza kuufikia ubongo inavyotakiwa. Hali hii inaweza kusababisha mabadiliko katika utendaji kazi wa ubongo na hatimaye kusababisha mtu kupatwa na hofu iliyopitiliza.
• Sababu za kimazingira: matukio kama vile ajali, kuumia au matukio yenye msongo mkubwa kama vile kunyanyaswa kwa namna yeyote ile, kufiwa na mtu unayempenda, talaka, kubadilisha kazi au kuachishwa/kufukuzwa kazi, kubadilisha shule au kufukuzwa/kuacha shule nayo pia yanaweza kusababisha kuwa na hali ya hofu iliyopitiliza. Hofu (GAD) pia huwa mbaya zaidi kipindi ambapo muhusika huwa katika hali ya msongo mkubwa wa kimaisha (stress). Aidha matumizi ya vitu vyenye kulevya kama pombe (alcohol), sigara (nicotine) au hata kahawa nayo pia yanaweza kuongeza ukubwa wa tatizo hili. Kadhalika, watu waliokuwa watumiaji wakubwa wa vitu hivyo kisha wakaacha ghafla, nao wapo katika hatari kubwa ya kukumbwa na tatizo hili.

Ukubwa wa tatizo
Bahati mbaya, takwimu za ukubwa wa tatizo nchini Tanzania hazikuweza kupatikana. Hata hivyo, inakadiriwa kuwa takribani watu wazima milioni 4 mpaka 5 huko nchini Marekani hukumbwa na tatizo hili kila mwaka.

Kwa kawaida, wanawake huathiriwa zaidi kuliko wanaume. Aidha hofu iliyopitiliza mara nyingi huanza kipindi cha utoto au utoto kabla ya ujana ingawa pia inaweza kutokea wakati wa utu uzima.

Vipimo na uchunguzi
Iwapo mgonjwa ana dalili za hofu iliyopitiliza, kwanza daktari atataka kufahamu historia yake kwa kumuuliza maswali juu ya maisha yake na dalili zinazomsumbua kabla ya kumfanyia uchunguzi wa mwili mzima ili kufahamu kama hana tatizo jingine la mwili linaweza kumletea dalili kama hizo.

Kuweza kutambua kama mgonjwa ana tatizo hili, daktari atatilia mkazo kwenye ukubwa wa tatizo lenyewe, muda tangu dalili zilipoanza kujitokeza, na iwapo tatizo hili linamfanya mgonjwa kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kila siku.

Iwapo daktari ataweza kubainisha katika historia ya mgonjwa kuwa mgonjwa amekuwa akisumbuliwa na dalili hizi karibu kila siku (au muda mwingi) katika kipindi cha miezi sita, hapo tunaweza kusema kwa hakika kuwa ni kweli mgonjwa ana tatizo la hofu iliyopitiliza (GAD). Dalili hizi pia ni lazima ziingilie na kuathiri mfumo wake wa maisha ya kila siku.

Pamoja na kuwa hakuna kipimo cha kuweza kugundua ugonjwa huu, daktari pia anaweza kuagiza kufanyika kwa vipimo vingine ili kuchunguza iwapo mgonjwa ana tatizo jingine lolote la kiafya.

Matibabu
Iwapo uchunguzi utaonesha mgonjwa hana tatizo lolote la kiafya katika mwili, daktari atampeleka kwa wataalamu wa masuala ya afya ya akili kwa ajili ya matibabu zaidi. Matibabu ya tatizo hili kwa kawaida hujumuisha matumizi ya dawa pamoja na tiba isiyohitaji dawa (au tiba ya kujitambua yaani cognitive-behavioral therapy).
Matumizi ya dawa: kwa watu ambao tatizo hili linaingiliana na maisha yao ya kila siku, matumizi ya dawa yameonekana kusaidia sana kuwafanya warejee katika hali yao ya kawaida. Dawa hizo ambazo pia huitwa tranquilizers husaidia kumtuliza mgonjwa na kumfanya ajihisi kupumzika. Dawa zinazotumika zipo katika jamii ya benzodiazepines nazo hufanya kazi ya kupunguza dalili za GAD kama vile kukaza misuli ya mwili au hali ya mgonjwa kutotulia. Baadhi ya dawa zilizo kwenye jamii hii ni kama vile diazepam (valium) na Ativan. Jamii nyingine ya dawa ni zile za kuondoa msongo wa mawazo (depression) yaani Antidepressants, kama vile Prozac, na Zoloft. Hizi nazo hutumika katika matibabu ya muda mrefu ya watu wenye hofu iliyopitiliza.
• Tiba ya kujitambua (cognitive-behavioral therapy): watu wenye matatizo ya hofu iliyopitiliza wanaweza pia kupatiwa tiba hii ambapo mgonjwa hufundishwa jinsi ya kutambua na kubadili namna anavyofikiri na tabia zinazomfanya awe na hisia za hofu. Aina hii ya tiba husaidia kuzuia kuibuka kwa mawazo ya hofu kwa vile humfanya mgonjwa kuyachunguza na kuziangalia hofu zake katika hali ya uhalisia.

Aidha mbinu mbalimbali za kuutuliza mwili (relaxation) kama vile kuvuta pumzi nyingi ndani kisha kuiachia taratibu nazo pia husaidia kuondoa kukaza kwa misuli kunakoambatana na kuwepo kwa hofu iliyopitiliza.

Pamoja na kwamba baadhi ya watu wenye tatizo hili hawawezi kutibiwa na kupona moja kwa moja kwa kuwa bado huendelea kupatwa na dalili hizi kwa kitambo fulani fulani, wengi wao hupata nafuu ya uhakika iwapo watapata tiba sahihi na wakatilia mkazo unaotakiwa kwenye tiba hiyo.

Kinga
Je kuna kinga dhidi ya tatizo hili?

Hofu iliyopitiliza haina kinga. Hata hivyo kuna baadhi ya mambo ambayo husaidia sana kupunguza makali ya dalili za tatizo hili. Mambo hiyo ni pamoja na:
• Kuacha au kupunguza matumizi ya vyakula au vinywaji kama vile kahawa, chai, cola au chokoleti.
• Kuepuka kutumia dawa zozote zenye vitu vinavyoweza kuchochea kutokea kwa hali bila kupata ushauri wa kitaalamu.
• Kujitahidi kufanya mazoezi ya mwili kila siku
• Kutafuta msaada wa ushauri nasaha pindi unapopatwa na matatizo yenye kuumiza moyo/nafsi, na
• Kujifunza kuthibiti msongo wa mawazo kwa kufanya mazoezi mbalimbali kama vile yoga

No comments:

Post a Comment