Sunday, March 18, 2012

Saratani ya tezi ya thyroid (Thyroid cancer)


Hii ni aina ya saratani inayokumba tezi ya thyroid. Ikumbukwe kuwa tezi ya thyroid ipo sehemu ya mbele ya shingo ya mwanadamu ikiwa na sehemu mbili (lobes) moja kila upande wa shingo.

Visababishi na ukubwa tatizo
Saratani ya thyroid huwapata watu wa umri mbalimbali, kuanzia watoto mpaka watu wazima. Watu waliowahi kupigwa mionzi sehemu ya mbele ya shingo wapo katika hatari kubwa ya kupata aina hii ya saratani. Kadhalika watu wazima ambao waliwahi kupigwa mionzi kipindi cha utotoni nao pia wana hatari kubwa zaidi ya kupata saratani ya thyroid hata kama hawakuwahi kupata tatizo hilo wakati wanakua.

Tiba ya mionzi maeneo ya shingoni ilikuwa ikitumika sana zamani kwenye miaka ya 50 mpaka 60 kwa ajili ya matibabu ya uvimbe wa tezi ya thymus, mafindofindo (tonsils), au baadhi ya magonjwa ya ngozi. Hata hivyo ni nadra sana kwa tiba hii kutumika katika zama hizi.

Vihatarishi vingine vya saratani ya tezi ya thyroid ni pamoja na kuwepo kwa historia ya tatizo hili miongoni mwa wanafamilia na kuwa na goita iliyodumu muda mrefu bila kutibiwa.

Aina za saratani ya tezi ya thyroid
Kulingana na aina ya seli zinazounda tezi ya thyroid zinazoshambuliwa, saratani ya thyroid inaweza kugawanywa katika aina zifuatazo:
• Aina inayojulikana kitaalamu kama papillary carcinoma. Hii ni aina maarufu zaidi miongoni mwa watu wenye saratani ya tezi ya thyroid. Kwa kawaida, aina hii huwapata zaidi wanawake walio katika umri wa kuzaa. Aina hii husambaa taratibu sana na haina madhara sana kwa mgonjwa ikilinganishwa na aina nyingine za saratani ya tezi ya thyroid.
• Aina nyingine ni ile inayofahamika kwa jina la follicular carcinoma. Aina hii hutokea katika asilimia karibu 10 ya watu wanaopata saratani ya thyroid. Follicular carncinoma huwa na tabia ya kupotea lakini pia huwa na uwezo wa kumrudia mgonjwa na kisha kusambaa kwa kasi.
• Aina ya tatu ni ile inayojulikana kama anaplastic carcinoma. Aina hii, japokuwa ni nadra sana kuonekana miongoni mwa wagonjwa wenye saratani ya thyroid, ndiyo aina ya hatari zaidi miongoni mwa aina zote za saratani ya thyroid. Anaplastic carcinoma husambaa kwa kasi kubwa na haiwezi kutibika kwa kutumia tiba ya madini ya nuklia ya Iodine.
• Aina nyingine huitwa medullary carcinoma. Hii ni aina ya saratani ya thyroid ambayo hutokea katika seli ambazo si za tezi ya thyroid lakini zipo ndani ya tezi hiyo (kuna baadhi ya seli ambazo si za tezi ya thyroid lakini zinapatikana na kuishi ndani ya tezi ya thyroid, mfano wa mgeni anayeishi katika nyumba isiyo yake). Aina hii huwapata zaidi wanafamilia na watafiti wameihusisha na mabadiliko ya kinasaba (genetic mutations), na kwa ujumla matibabu yake hutofautiana sana na yale ya aina nyingine za saratani ya thyroid.

Dalili
Dalili hutofautiana kulingana na aina ya saratani, ingawa kiujumla zaweza kujumuisha:
• kikohozi
• Shida wakati wa kumeza chakula, vinywaji hata mate
• Kuvimba kwa tezi ya thyroid
• Mabadiliko katika sauti, sauti kufifia au kuwa ya mikwaruzo
• Uvimbe kwenye shingo
• Tezi ya thyroid kuwa na nundu au vinundu

Vipimo na uchunguzi
Mgonjwa anayehisiwa kuwa na saratani ya thyroid hufanyiwa uchunguzi wa mwili kabla ya kufanyiwa vipimo kadhaa ili kujiridhisha kuwa ni kweli ana tatizo la saratani ya thyroid. Uchunguzi wa mwili unaweza kuonesha uwepo wa nundu au uvimbe katika thyroid na/ kuvimba kwa tezi za mitoki katika shingo.

Vipimo ni pamoja na:
• Ultrasound ya tezi ya thyroid
• Kukata sehemu ya thyroid na kukichunguza kimaabara (thyroid biopsy)
• Picha ya utendaji kazi wa tezi ya thyroid (thyroid scan)
• Uchunguzi wa sehemu ya ndani ya koo (laryngoscopy)
• Kupima damu ili kuchunguza kiwango cha homoni ya calcitonin. Iwapo kiwango kitakuwa juu kuliko kawaida, hii yaweza kuashiria uwepo wa medullary carcinoma.
• Kupima damu ili kuchunguza kiwango cha viasili vya thyroglobulin ambavyo vywaweza kuashiria uwepo wa saratani aina ya papillary carcinoma au follicular carcinoma.
• Kupima damu ili kuchunguza kiwango cha homoni za thyroid za T3, T4 na TSH.

Matibabu
Matibabu hutegemea sana aina ya saratani, ingawa upasuaji wa tezi ya thyroid ndiyo aina ya tiba inayoongoza. Wakati wa upasuji, kwa kawaida tezi yote huondolewa, na iwapo daktari atahisi kuwa hata tezi za mitoki zilizo karibu na thyroid nazo pia zimeathirika pia huondolewa.

Aidha mgonjwa anaweza pia kupatiwa tiba ya mionzi ambayo hutolewa kwa njia ya kupigwa mionzi ya moja kwa moja (external beam radiation) au kwa kutumia (kunywa) vidonge vya madini ya Iodine vyenye nguvu ya nyuklia yaani radioactive iodine. Njia hii inaweza kufanyika ikiambatana pia na upasuaji au bila upasuaji.

Baada ya matibabu, mgonjwa anapaswa kuendelea kutumia dawa maalum za kumrejeshea homoni za thyroid ili kurudisha kile alichopoteza baada ya kuondolewa kwa tezi. Kwa kawaida dozi inayotolewa huwa kubwa kuliko ile inayohitajika mwilini ili kusaidia saratani isijirudie tena.

Iwapo upasuaji au mionzi haujasaidia kuondoa kansa, na kwamba saratani inaendelea kusamabaa sehemu nyingine za mwili, mgonjwa anaweza kuanishiwa dawa za kutibu saratani (chemotherapy) ingawa nayo inaweza ikawa na manufaa kwa baadhi ya wagonjwa tu na si wagonjwa wote.

Nini cha kutarajia
Saratani aina ya Anaplastic carcinoma ina matokeo mabaya zaidi kuliko aina zote zilizobaki, na mara nyingi mgonjwa hufariki hata baada ya matibabu ya uhakika ya muda mrefu. Follicular carcinomas pamoja na kuwa na tabia ya kusambaa kwa kasi kwenye maeneo mengine ya mwili huwa na matokeo mazuri ikitibiwa. Matokeo ya wagonjwa wenye aina ya medullary carcinoma yanatofautiana kati ya mgonjwa na mgonjwa, ambapo wanawake wenye umri chini ya miaka 40 wameonekana kuwa na matokeo mazuri zaidi baada ya tiba kuliko walio na zaidi ya umri huo. Aidha wagonjwa wengi wenye Papillary carcinomas hupona kabisa na kuendelea na maisha yao ya kawaida.

Jambo la kukumbuka ni kuwa, mara baada ya tiba, mgonjwa anapaswa kuendelea kutumia vidonge vya kurejesha homoni za thyroid kila siku za maisha yake.

Madhara ya saratani ya thyroid
Madhara ya saratani ya thyroid ni pamoja na madhara katika sanduku la sauti kabla ya upasuaji, na sauti ya mikwaruzo baada ya upasuaji, kupungua kwa kiwango cha madini ya calcium mwilini iwapo tezi ya parathyroid ambayo ipo juu kidogo ya thyroid itaodolewa kwa bahati mbaya wakati wa upasuaji, na kusambaa kwa kansa katika sehemu nyingine za mwili kama vile mifupa, au mapafu.

Kinga
Mpaka sasa hakuna kinga rasmi ya ugonjwa huu. Hata hivyo, ni vizuri jamii ikawa makini na mionzi isiyohitajika sehemu za mbele ya shingo. Aidha wale wenye historia ya tatizo hili katika familia zao ni vema wakamuona daktari kwa ajili ya uchunguzi kabla tatizo halijajitokeza, au kuwa kubwa.

No comments:

Post a Comment