Saturday, March 17, 2012

Dhana hizi zinawaharibia wanawake kimapenzi

KUNA msemo kuwa: “Wanawake, mwalimu wao ni kipofu.” Mimi siuamini kwa maana umekaa kiukandamizaji zaidi. Haujengi heshima kwa mtu wa jinsi ya kike tangu analizaliwa mpaka anapoingia kaburini. Binafsi naamini wapo wenye uelewa mkubwa lakini wanashambuliwa na mapokeo ya samaki mmoja akioza.

Ni msemo ambao ukiingia kwenye vichwa vya watu unaweza kuwafanya wanaume wawadharau hata mama zao. Mama anatoa mafundisho lakini kijana anasikiliza, linaingilia sikio la kwanza na kutokea la pili. Kichwani anajiongeza: “Aah, hawa si mwalimu wao kipofu?”

Msemo huo unamaanisha kuwa wanawake huwa hawajui waendako. Kwamba njia ya kupita walifundishwa na mwalimu mwenye ulemavu wa macho. Siupendi kwa sababu siyo tu hauna ladha nzuri kwa mwanamke bali pia kwa mtu mwenye ulemavu husika. Unadhalilisha kupita kiasi.

Tangu nikiwa na umri mdogo, nilipenda sana kusikiliza busara za watu walionizidi umri. Niliamini wananijenga na kweli walifanya hivyo. Mtazamo huo, ulinifanya nijue mengi nikiwa na umri mdogo. Hata haya ninayoandika na kushauri, yanatokana na elimu niliyopata kwenye kada tofauti.

Wakati huo sijui ndani ya mwanamke kuna nini, mtu mmoja aliniambia: “Mdogo wangu Luqman, napenda unavyopenda kukaa na sisi wakubwa. Unaweza kuwa na busara katika maisha yako lakini usipokuwa mwangalifu, mwanamke anaweza kukufanya uonekane mwendawazimu mtaani.

“Siku ukiwa na mwanamke, jaribu sana kuwa mwangalifu. Unaweza kumpa kila atakacho lakini mwisho akakuuguza uendawazimu. Ukatembea barabarani unazungumza peke yako kama kichaa au ukiwa nyumbani ukashinda unabwabwaja maneno yasiyoeleweka mpaka majirani wakakuona mwendawazimu.

“Mkeo anaweza kutoka nyumbani anakwenda kumtembelea shangazi yake, kwa kumthamini na kwa sababu huna gari, ukampa fedha ya kukodi teksi. Akitoka njiani, anakutana na dereva teksi anampa lifti. Huwezi kuamini, huyo aliyempa lifti ndiye atamuona bora, mwenye roho nzuri kuliko wewe uliyempa fedha ya kuchukua teksi.

“Matokeo yake ni kwamba akishamuona ni mkarimu sana, anakuwa mnyenyekevu hata kwenye maeneo mengine. Mwisho wanakuwa wapenzi. Hiyo ndiyo tabia ya mwanamke, atasahau mema yako, hatajali watoto mnaolea.” Huyo mtu aliyeniambia maneno hayo anaitwa Jaffari, ni mtu mzima hivi sasa. Enzi hizo nilikuwa nasoma sekondari Mwanza.

Ukweli upo wapi? Ninachoweza kueleza ni kwamba wapo wanawake waungwana mno hapa duniani. Wanadumisha mapenzi ya dhati bila kusaliti licha ya kukumbana na vishawishi kemkem. Wanajua thamani ya wapenzi wao pamoja na changamoto zinazoweza kuwakabili katika maisha.

Hata hivyo, kuna aina ya wanawake ambao Jaffari alikutana nao ndiyo maana akasema hivyo. Isingekuwa rahisi kutoa maneno hayo pasipo kuona kitu. Inawezekana alitendwa na mkewe au alishuhudia kitu kwa rafiki yake, hivyo kumpa tafsiri aliyojijengea kuhusu wanawake.

Tukishika moja kuwa kuna kitu alijionea, basi ni vema kuwazungumzia wanawake ambao walimfanya akawa na mtazamo huo. Hao ndiyo wanaowaharibia wengine mpaka wanakosa thamani. Mtu anatendwa na mkewe lakini lawama anazielekeza kwa wanawake wote kwamba eti ndivyo walivyo!

Jambo ambalo mtu hapendi afanyiwe, basi asianze kumfanyia mwenzake.

Heshima, woga na ‘breki’ katika kauli, vinapaswa kuzingatiwa. Kusaliti maana yake umekosa woga, heshima na busara ya kimapenzi na maisha kwa jumla.

Hekima ni ipi? Kuendelea kuwa na mwenzi ambaye hana heshima juu yako, hakuhofii kwa chochote, wala busara ya maisha haimuongozi kutenda yaliyo mema kwa ajili ya ustawi wa familia yenu. Bila shaka, hekima inafaa kukuongoza kuchukua uamuzi kwa ajili ya furaha na amani ya kudumu baadaye.

Nitoe hoja kuwa hata wanaume wapo wenye matatizo mtindo mmoja, kwa hiyo na wanawake wapo wenye hulka tofauti.

Kama huyo wako ni pasua kichwa, basi wapo waliojaliwa utulivu, heshima, hekima na maarifa ya kudumisha uhusiano. Ikiwa huyo anakunyima furaha, angalia kama unaweza kujivua gamba, kwani wapo wanawake wema.

Mungu hajaumba mtu akamfanya kuwa mbaya kwa asilimia 100, Shetani ndiye anayeharibu vichwa vya watu na kuwafanya wawe na akili zisizofaa. Hata katika jamii ya Wasamaria, alipatikana mmoja aliye mwema ndiyo maana akaitwa Msamaria mwema.

Hivyo basi, wasisemwe vibaya wanawake wote kwa ajili ya makosa ya wachache.

Hata hivyo, hao wachache wanapaswa kubadilika ili wawape heshima wenzao.

Tamaa haifai kwa namna yoyote.

Binafsi nawaheshimu wanawake kwa maana ndiyo waliotufanya tustarehe kwenye matumbo yao kwa miezi tisa, wanawezesha tuitwe akina baba na kadhalika.

Mambo hayo makuu, hayapingiki ndani ya kila mwanaume isipokuwa Adam.

Pamoja na hivyo, zipo dhana nyingine nyingi ambazo zinafanya wanawake wasemwe vibaya. Twende kwa mifano.

Hivi karibuni, niliitwa nimshauri kijana mmoja ambaye kwa hakika alikuwa amechanganyikiwa kabisa.
Alichanganywa na mapenzi.

Mwanamke ambaye aliamini ndiye wa maisha yake, alimuacha katika mazingira ambayo hakuyategemea.

Alikuwa anamhudumia kwa kila kitu lakini akapigwa kibuti kwa SMS.

Kijana huyo anaitwa Mully, akiwa kazini kwake, akaona SMS iliyotoka kwa mtu ‘aliyemsevu’ kwa jina la My Dream.

Kama ujuavyo tena mapenzi, kijana akafungua haraka, akitegemea atapata maneno matamu kutoka kwa mwenzi wake lakini alichokutana nacho ni hiki: “Kuanzia leo, mimi na wewe basi.

Nimepata mchumba nataka kuolewa.”

Mully aliposoma maneno hayo akapagawa, akaamua kupiga simu ya mpenzi wake lakini hakupokea.

Akaamua kumuuliza kwa SMS: “Baby upo serious au unatania?” Haikupita hata dakika moja, majibu yakarudi: “Nipo serious kabisa, tena kuanzia leo usiniite baby na usinijue kwa lolote.”

Meseji hiyo ikamchanganya akili kijana, akaondoka kazini kwake bila hata kuwaaga wenzake.

Yule mpenzi wake anaitwa Janette, ni mtumishi wa ndani kwenye nyumba ya ofisa wa benki Masaki, Dar. Kijana akaondoka kazini kwake Mwenge hadi kazini kwa mkewe. Akili siyo zake.
Itaendelea wiki ijayo





Tunaendelea kuchambua kuhusu dhana ambazo zinawaharibia wanawake kimapenzi. Katika kuhakikisha somo linaeleweka sawia, mwishoni mwa makala ya wiki iliyopita, nilieleza mfano huu:

Hivi karibuni, niliitwa nimshauri kijana mmoja ambaye kwa hakika alikuwa amechanganyikiwa kabisa.

Alichanganywa na mapenzi. Mwanamke ambaye aliamini ndiye wa maisha yake, alimuacha katika mazingira ambayo hakuyategemea. Alikuwa anamhudumia kwa kila kitu lakini akapigwa kibuti kwa SMS.

Kijana huyo anaitwa Mully, akiwa kazini kwake, akaona SMS iliyotoka kwa mtu ‘aliyemsevu’ kwa jina la My Dream. Kama ujuavyo tena mapenzi, kijana akafungua haraka, akitegemea atapata maneno matamu kutoka kwa mwenzi wake lakini alichokutana nacho ni hiki: “Kuanzia leo, mimi na wewe basi. Nimepata mchumba nataka kuolewa.”
Mully aliposoma maneno hayo akapagawa, akaamua kupiga simu ya mpenzi wake lakini hakupokea. Akaamua kumuuliza kwa SMS: “Baby upo serious au unatania?” Haikupita hata dakika moja, majibu yakarudi: “Nipo serious kabisa, tena kuanzia leo usiniite baby na usinijue kwa lolote.”
Meseji hiyo ikamchanganya akili kijana, akaondoka kazini kwake bila hata kuwaaga wenzake. Yule mpenzi wake anaitwa Janette, ni mtumishi wa ndani kwenye nyumba ya ofisa wa benki Masaki, Dar. Kijana akaondoka kazini kwake Mwenge hadi kazini kwa mkewe. Akili siyo zake.
Alipofika, akagonga geti halikufunguliwa, kwa hiyo akapanga matofali getini akakaa. Baadaye Janette akatoka, alikuwa anakwenda dukani, akakutana uso kwa uso na Mully. Yakaanza maneno, baby nimekukosea nini? … sikutaki… baby niambie kosa langu… nimesema sikutaki...
Mtoto wa kike akaona ubishi unampotezea muda, akaingia ndani, akatoka nje na beseni la maji machafu, akamwagia Mully. Kijana wa watu akaloa chapachapa. Janette akarudi ndani, akapiga simu kwa bosi wake, punde polisi wakafika na kumzoa, eti ni mwizi.
Kaka yake Mully akaenda kumuwekea dhamana Oysterbay Polisi. Kuanzia hapo kijana akawa chini, akawa anazungumza hovyo, kazi akawa hafanyi. Kijana akasema: “Mbona mimi ningemuoa tu, sina shida.” Kijana akawa hali, haogi, kazi hafanyi. Akili zikamruka.
Nilijitahidi kumpa ushauri unaofaa kwa vipindi vitatu ndani ya siku tatu mfululizo, baada ya kuona anapata nafuu, nilishauri apelekwe eneo ambalo atabadili mazingira. Alipelekwa nyumbani kwao Singida. Wiki iliyopita, alirudi Dar akiwa mpya kabisa. Anatazama mbele na hamfikirii tena yule mwanamke.
Hata kazi anaendelea vizuri. Machungu ya kuachwa na Janette yamebaki historia. Vema amekaa sawa lakini kitu ambacho kipo wazi ni kuwa Mully alimpenda sana mpenzi wake na aliamini ndiye mwanamke wa maisha. Hali hiyo ndiyo ilimfanya ashindwe kupokea matokeo ya kuachwa.
Alishawekeza mambo mengi kwa Janette hususan rasilimali. Mully aliniambia kuwa kwa siku alikuwa anampa Janette kuanzia shilingi 15,000 mpaka 20,000. Alikuwa anamnunulia mavazi ya kisasa, kiasi kwamba ukimuona, usingeweza kudhani ni mfanyakazi wa ndani.
Baadaye ikaja kubainika kuwa kumbe Janette alipata kiburi cha kuachana na Mully kwa sababu ya bosi wake. Kwamba yule ofisa wa benki baada ya kumuona mfanyakazi wake anameremeta, akaamua kujiweka, binti naye badala ya kufikiria kuwa ni mume wa mtu akakubali.
Wameendelea kuwa na uhusiano lakini za mwizi ni 40, mke akashtukia kuwa anaibiwa mumewe ndani ya nyumba yake. Akamtimua kazi Janette na kipigo juu. Yule jamaa wala hakumtetea ndiyo kwanza akashiriki kusaidia kumtimua. Binti aende wapi? Kazini ameshaharibu, kwa Mully nako alishalikoroga.

No comments:

Post a Comment