 
Wiki iliyopita tulieleza mambo kadhaa ambayo yatasaidia kutuwezesha kuishi kwa mafanikio na furaha zaidi.
Nilikuomba  msomaji utafakari kwa kina dondoo  zile lakini kwa kuwa hazikwisha,  zinaendelea leo katika safu hii na nitazifasiri kwa ufupi sana kama  ifuatavyo:
Acha kuyakuza mambo madogo: Moja ya njia za kufahamu mambo muhimu  ni kujiuliza swali hili;  “Je, jambo hili litakuwa muhimu katika  kipindi cha mwaka mmoja?  Litakuwa muhimu katika miaka mitatu au mitano  ijayo?  Kama jibu ni hapana, basi huna haja ya kuhangaika nalo.
Usifanye jambo kwa kutegemea matarajio ya wengine badala yake  fanya jambo lako kikamilifu na ikiwezekana livuke matarajio yako.  Baada  ya hapo mambo yote yatajinyoosha yenyewe.
 Usikimbilie ufumbuzi  mwepesi  wa matatizo yako: Hivi sasa watu wanakimbilia kupata ufumbuzi  wa haraka wa matatizo yao.  Kwa mfano, watu wanakimbilia kumeza vidonge  vya kupunguza uzito badala ya kufanya mazoezi na kula chakula bora.   Ukweli ni kwamba hakuna maajabu ambayo yanashinda nguvu za mtu kufanya  bidii, kujiwekea malengo na kufanya kazi kwa nguvu.
Usitoe ahadi utakazoshindwa kuzitimiza:  Usitoe ahadi zitakazokushinda.  Timiza unalolifanya kwa kuzidi hata lengo ulilojiwekea.
Usikubali  fikra na hisia zako zikakubana moyoni: Watu hawawezi kumsoma mtu na  kutambua mawazo yake. Hawatafahamu unavyojihisi mpaka uwaeleze.  Hivyo,  waeleze watu wengine shida zako.
Acha kusema jambo kwa kufichaficha: Jambo unalotaka kulisema liseme waziwazi na hakikisha unajieleza kinagaubaga.
Usitake kuzuia mabadiliko: Kwa vyovyote, hali ikiwa nzuri au  mbaya sasa, ni dhahiri baadaye itabadilika.  Hili ni jambo la wazi.   Hivyo kubaliana na mabadiliko na fahamu kwamba mabadiliko huja kutokana  na sababu zake.  Mwanzoni hayawezi kuwa mepesi au ya wazi, lakini  baadaye yatakuwa ya maana.
Usifikiri una haki katika jambo fulani: Hakuna mtu mwenye haki  maalum katika dunia hii.  Sote tuko sawa.  Tunavuta hewa ileile.   Tunapata kile tunachotoa kwa wengine.  Tunapata kile tunachokitokea  jasho.
Usisubiri kufanya jambo hadi dakika ya mwisho: Watu ambao wanashindwa kupanga, hupanga kushindwa.
Usitake  kujionyesha sana: Usitake kujiingiza katika mambo ya watu wengine na  usitake kujionyesha kwa wengine bila sababu ya maana.
Acha uvivu: Ushughulishe mwili wako!  Fanya matembezi marefu ya  kujinyoosha mwili au tenga dakika 30 kwa ajili ya kufanya mazoezi  mbalimbali nyumbani kwako au sehemu wanazofanyia watu mazoezi (Gym).
Usile vyakula ambavyo havina faida mwilini mwako: Fahamu kwamba kile unachokula ndivyo kinaufanya mwili wako uwe ulivyo sasa.
Acha tabia ya kula kama vile ni moja ya burudani: Usile chakula wakati hujisikii kufanya hivyo.Kula wakati ukiwa na njaa tu.
Achana  na tabia za kipumbavu ambazo unajua kabisa ni za kipumbavu: Usisome  huku unaendesha gari.  Usitumie kilevi halafu ukaendesha gari.  Usivute  sigara wakati unaendesha gari na kadhalika.
Achana na watu ambao wanakurudisha nyuma kimaendeleo: Kusema  “hapana” kwa watu sahihi kunakupa muda na nguvu za kusema “ndiyo” katika  mambo ya maana.  Utumie muda wako kuwa na watu wema na makini na ambao  mnafanana mawazo yenu.
Usijitenge: Jichanganye na watu wengine. Kutana na watu wapya, uliza maswali na jitambulishe.
Itaendelea wiki Ijayo.
 
 




 
No comments:
Post a Comment