 
JE, uhuru unaweza kukufanya uwe mwenye furaha?  Uhuru  unaweza kutupa furaha ya kweli maishani?  Jibu la maswali haya ni ndiyo  na hapana.  
Ni vyema kufahamu kwamba furaha inayoambatana na  uhuru  inategemea na aina ya uhuru ambao unao.  Unaweza kuwa huru katika  sura mbili tofauti.  Ukiwa huru  kwa kuachana na dhambi na uovu,  unaweza kuwa na furaha ya kweli.  Lakini ukiwa na uhuru ambao hautokani  na misingi ya uadilifu na wema, basi utakuwa katika mateso.  
Jambo  hili lina sehemu mbili ambazo zinaweza kumfanya mtu akawa mtumwa.Ukiwa  mtumwa wa dhambi na uovu, utajikuta katika mateso, vilevile ukiwa mtumwa  wa kutimiza matendo ya wema na ukarimu, utajikuta katika furaha ya  kweli.
HAKUNA UHURU KAMILI
Jambo muhimu la kufahamu ni kwamba,  katika hali halisi, hakuna uhuru kamili au utumwa kamili kwa binadamu.   Siku zote tunapojiona tuko huru tufahamu wazi kwamba wakati huohuo  tunakuwa watumwa. 
Tofauti inategemea ni nani tunayemtumikia  na  nani ambaye hatumtumikii.  Ukweli ni kwamba huwezi kuwa huru kwa kila  kitu, kwani iwapo utakuwa huru kabisa, basi utajikuta umekuwa mtumwa wa  kutokuwa na kitu chochote. 
Hali ya kutokuwa na kitu chochote  itakutupa katika mateso makubwa.  Iwapo utahitaji uhuru kamili, basi  utakuwa unataka kitu ambacho hakipo yaani hali ambayo haiwezi kuwepo au  kupatikana.
HALI ITAKAYOKUFANYA UWE NA FURAHA
Uhuru  utakaokufanya uwe na furaha ni uhuru wa kuachana na dhambi na maovu.   Huu ni uhuru unaokutenganisha na chuki, fahari, wivu na maovu mengine. 
Huu  ni uhuru ambao utakupa amani na dhamira njema ya moyo.  Kwa upande wa  pili, utumwa unaweza pia kukufanya ukawa na furaha. Huu ni utumwa ambao  utakufungamanisha na wema, upendo, uvumilivu na maadili mengine katika  jamii. 
Iwapo dhamira yako itaweka mbele kuheshimu vitendo vyema katika  jamii, basi utakuwa umejiweka katika nafasi njema na yenye kukuletea  furaha.
UHURU UTAKAOKULETEA HUZUNI
Uhuru ambao unaweza  kukufanya uwe na masikitiko ni uhuru wa kutokuwepo kwa upendo, amani,  ukarimu na mambo mengine ya kiadilifu.   Hebu fikiria, iwapo utajitenga  na vitu hivyo muhimu, unaweza kweli kuwa na furaha?
“Mimi sioni  sababu ya kujitesa, bora niwe huru kwa kuishi peke yangu, kwani napata  nini kwa kujipendekeza kwao zaidi ya kupoteza muda wangu na mali zangu.”  Kauli hii ni ya kutafuta uhuru utakaokuletea huzuni baadaye.
NI NANI KIONGOZI WAKO?
Furaha  yako ni kazi inayofanywa na pande mbili, yaani wewe na kiongozi au  bwana wako.  Ufahamu kwamba siku zote una mkuu wako anayekuongoza.   Iwapo utakuwa umejitenga na maovu na ukawa mtu wa kutenda wema, basi  wema au uadilifu ndiye bwana wako.  
Iwapo utakuwa umeachana na  matendo mema na ukawa mtumwa wa maovu,  fahamu kabisa kwamba uovu ndiye  kiongozi wako. Na iwapo utakuwa umetengana na  wema na maovu, je bwana  wako ni nani?  Bila shaka anaweza kuwa ni wewe mwenyewe.
Ukiamini  hivyo utakuwa unakumbatia kiini macho.  Hii ni kwa sababu tukiwa  tunaendelea kuishi, hatuwezi kuachana kabisa na mema na maovu. Mambo  hayo mawili siku zote yatakuwa yanatuandama katika safari ya maisha yetu  kwa kuyapenda au kuyachukia, kila mara yakitupa changamoto ya kuchagua  upande tunaotaka kuutumikia.
TUNATAKIWA KUCHAGUA 
Tunatakiwa  tuchague aina ya uhuru tunaoutaka.  Tunatakiwa tumchague bwana au  kiongozi ambaye anaweza kutupa furaha ya kweli. Ni lazima tuchague  upande wa kuutumikia.
Je, unataka kutumikia uovu au unataka kutumikia uadilifu? Au, je, unataka kujitumikia wewe na masilahi yako tu? 
UPANDE MUHIMU WA KUUTUMIKIA
Inawezekana  wapo watu kwenye jamii tunazoishi ambao wanatafuta uhuru kwa kujitoa  kwenye matendo mema, yaani wanaona ni utumwa kuwasaidia wenzao na hivyo  kuamua kutafuta uhuru kwa kujitenga au wanatafuta unafuu wa kupumzika  katika majukumu ya kuwafanya binadamu wenzao wafurahie maisha.
Jambo  hili si jema, kwani upande sahihi uletao furaha ya kweli ni kuwa huru  mbali na matendo maovu. Asiwepo mtu miongoni mwetu ambaye atataka uhuru  kwa kujitenga na mema eti kwa sababu wema unamtumikisha kwa kumchukulia  muda na fedha zake.
 
 




 
No comments:
Post a Comment