 
HAKIKA Mungu ni mwema kwa kila kitu anachonitendea maishani mwangu. Ni wengi walitamani sana kuuona mwaka huu mpya lakini kwa neema na fadhila zake wametangulia mbele ya haki. Jina lake lihimidiwe.
Baada ya kusema hayo, ngoja tuingie moja kwa moja kwenye mada  yetu ya leo inayotufungulia mwaka ambayo naamini itabadilisha kabisa  maisha yako. Na ndiyo sera ya kona hii ya Jitambue.
Safari ya maisha ni ndefu, ina kila aina ya adha, mabonde,  miteremko, miinuko na milima mingi. Hakika ni safari inayohitaji ujasiri  mkubwa kuikabili. Ni wale waliodhamiria kwa dhati tu ndiyo huikamilisha  safari hii! Wengi wetu huishia njiani kwa kukata tamaa.
Kama ilivyo kwa safari yoyote ambayo ni ndefu, hivyo ndivyo  ilivyo hata safari ya maisha nayo inachosha sana. Iwe kwa gari, ndege,  meli n.k ni lazima uchoke.
Yawezekana kabisa unayesoma makala haya tayari safari ya maisha  yenye mafanikio imeshakuchosha kutokana na urefu au ugumu wake. Umekata  tamaa kabisa na kuacha mambo yaende kama yalivyo. Huna njia nyingine   ambayo unaweza kuitumia yaani huna usafiri mwingine, umeanguka na  unadhani huwezi kunyanyuka tena. Maisha yako yamejaa machozi, simanzi,  maumivu, majuto, tabu, mihangaiko, hofu, mashaka, upweke, simanzi,  huzuni, manung’uniko nk.
Umejaribu kufanya mambo mbalimbali kwa miaka mingi  lakini  hakuna chochote ulichoambulia zaidi ya kubaki palepale. Kuchekwa,  kukatishwa tamaa, kuzomewa, kubezwa, kusimangwa, kuseng’enywa na  kudharaulika imekuwa sehemu ya maisha yako kila kukicha.
Ndugu nyangu, hata kama giza nene la ufukara na umasikini  limetanda maishani mwako, huoni mbele, nyuma, kulia, kushoto na  kwingineko na umezama kwenye lindi la umasikini, leo nataka kuzungumza  na nafsi yako, nataka kupandikiza mbegu tofauti kabisa akilini na moyoni  mwako. MBEGU YA USHINDI! Mbegu ambayo italeta mwanga na matumaini mapya  kabisa maishani. Kabla ya kuendelea na makala yangu yangu hebu ngoja  nikukumbushe kitu kimoja muhimu kuwa WEWE NI MBARIKIWA, WEWE NI TAJIRI  MKUBWA NA LAZIMA UFANIKIWE. Muda wa Baraka zako ulikuwa  haujafika,  wakati umewadia.
AMKA NA USIMAME
Msomaji, katika maisha  haya ya mafanikio, kuna siri kubwa mno ambayo imejificha nyuma ya pazia,  ni hazina ambayo wengi wetu tumefichwa, leo naweka wazi kila kitu.
MPAKA KIELEWEKE
 Kila binadamu aliyezaliwa hapa chini ya jua, ameumbwa na Mungu kwa  makusudi maalum, ana umuhimu mkubwa mno. Mungu hakukuumba kwa bahati  mbaya maana hata hayo majani, miti na viumbe vingine vimeumbwa kwa  sababu maalum sembuse wewe binadamu unayefanana naye kwa kila kitu.  Tuliza akili nikupe dawa na njia bora za maisha.
Siri kubwa ambayo nataka kuiweka wazi hapa ni kuwa siku zote   maishani hakuna kitu kizuri ambacho huja kwa urahisi. Hakuna mafanikio  pasipo maumivu. Ni lazima utoke jasho. Watu wengi husahau kuwa siku zote  kabla Mungu hajakupa matunda ya duniani ni lazima akuonjeshe joto la  jiwe kwanza, ni lazima ujutie, ukifanikiwa kwa urahisi bila kuhangaika  mara nyingi mafanikio hayo huwa hayadumu. Kwa ndugu zangu Wakristo ngoja  niwakumbushe mifano miwili kutoka kwenye Biblia.
Baba yetu Ibrahimu ndiye anafahamika kwa jina la Baba wa Imani.  Lakini jina hili hakulipata kirahisi, kuna kitu cha hatari sana  alikifanya, alijitolea.  Mungu alitaka kumjaribu kabla ya kumpa Baraka  za kuwa na uzao imara. Alimwambia amtoe mwanaye (Isaka) kama sadaka ya  kuteketeza.
 Kwa wazazi mtakuwa mnaelewa namaanisha nini. Yaani mwanao wa  damu halafu umtoe kwa kumchinja kwa mkono wako mwenyewe. Inatisha na  yataka moyo. Lakini Ibrahim alikuwa tayari.
Alimchukuwa Isaka hadi porini lakini Mungu akamzuia kufanya hivyo ndipo akapewa jina la Baba wa Imani.
 Aidha, katika nchi ya Usi kulikuwa na babu yetu Ayubu ambaye ukisoma  mateso yake ni lazima utokwe na machozi, huyu aliteseka hadi akailaani  siku aliyozaliwa.
 
 




 
No comments:
Post a Comment