Showing posts with label maisha. Show all posts
Showing posts with label maisha. Show all posts

Saturday, March 17, 2012

Jinsi ya kuishi na wafanyakazi wenzako

Kumekuwa na tatizo kubwa kwa baadhi ya watu namna ya kuishi na wafanyakazi wenzao hasa katika ofisi kubwa zinazojumuisha watu wengi.

Kwanza ifahamike kuwa, popote palipo na mkusanyiko wa watu wengi, basi kuna mrundikano wa tabia, mila na desturi tofauti. Yaani kila mtu ametoka katika familia yenye malezi tofauti na ya kwao hivyo katika utofauti wa mambo hayo, ni lazima kutakuwepo na migongano ya hapa na pale kwani kila mmoja ana amini alichojifunza nyumabani kwao.

Hivyo basi, unapokuwa ofisini unakutana na watu wa aina hiyo. Watu ambao mnatofautina mambo mengi ikiwemo uelewa, vipaji na ustaarabu.

Hivi ndivyo unapaswa kuishi na wafanyakazi wenzako:

Soma Mazingira

Unapokuwa ofisini na wafanyakazi wenzako, jitahidi sana kusoma mazingira ili ujue ni mambo gani hayatakiwi na ni yapi yanatakiwa kufanyika na kwa wakati gani. Hii itakusaidia kuepuka baadhi ya migogoro na wafanyakazi wenzako.

Ninaposema kusoma mazingira ninamaanisha kuwa, kuna baadhi ya mazingira ndani ya ofisi ambapo watu hawapendi kuchangia vifaa kama kompyuta na vingine. Sasa unapoingia na utaratibu wako pasipo kusoma na kuyajua mazingira hayo, unajikuta moja kwa moja unavunja taratibu za kiofisi kwa sababu tu hukusoma mazingiara tangu awali.

Tambua udhaifu na uimara wa wafanyakazi wenzako:

Kila binadamu ana udhaifu na uimara wake. Katika mazingira unayofanyia kazi, jitahidi sana kumsoma kila mfanyakazi mwenzako ili ujue ni kwa namna gani utaweza kuishi naye.
Kuna baadhi ya watu hawapendi utani, wengine wanapenda sana utani na wengine huonekana wamenuna hata kama wanafuraha. Hivyo ni lazima kuwasoma mmoja mmoja.

Katika maofisi, utakutana na wafanyakazi ambao ni waongeaji, wengine wakimya, wengine wanapenda kucheka pasipo na sababu ya msingi na kila aina ya tabia ambapo ni lazima kila mtu amjue mwenzake ana kasumba na tabia zipi.

Tumia lugha na maneno ya heshima

Epuka sana tabia ya uropokaji usiozingatia lugha nzuri hasa lugha za mitaani. Vijana wengi sana wanashindwa kutofautisha mazingira ya ofisini na mitaani ambpo utakuta maneno anayoyatumia mitaani ndiyo anajaribu kuyatumia hata katika mazingira ya ofisini kwa wafanyakazi wenzake. Jambo ambalo si sahihi.

Kama unashida na mfanyakazi mwenzako, basi mfuate kwa utaratibu kisha muite kwa jina lake ndipo umueleze shida yako.

Katika hili zingatia maneno ya samahani kabla ya kumueleza shida yako.
Na inapotokea umemkosea mfanyakazi mwenzako kwa namna moja au nyingine, basi ni busara kama utamtaka radhi na kutorudia kosa lile.

Sasa utakuta mtu anashida na mfanyakazi mwenzake lakini jinsi anavyomuita na kumueleza, utadhani anamuamrisha mwanaye.

Epuka sana madeni kwa wafanyakazi wenzako na kama ikitokea umekopa fedha kwa mfanyakazi mwenzako basi jitahidi kurejesha kwa muda muafaka, na tena katika hali ya ustaarabu. Pia jitahidi kutoa misaada kwa wenzako wanapopatwa na matatizo.

Kuna wale wenzangu na mimi ambo wao hupenda kusaidiwa tu lakini siyo kusaidia wenzao! Hii ni hatari sana. Jitahidi kuwa karibu na wafanyakazi wenzako kwa kila hali. Kama ni matatizo basi shirikiana nao.

Nguzo Kuu za Mafanikio Maishani

Katika maisha, hakuna kitu kinachoweza kufanyika kama hakutakuwa na bidii ya utendaji.

Huo ndiyo ukweli, bidii ni kiungo muhimu sana katika kufanikisha jambo lolote kwa mtazamo chanya.

Lakini bidii peke yake inatosha kukamilisha mafanikio maishani? Jibu ni kwamba si kweli kwani pamoja na bidii kuwa kiungo muhimu cha mafanikio, lakini bado kuna vitu vingine muhimu zaidi ili kujipatia maendeleo na mafanikio maishani ambavyo ni Uaminifu, Ukweli na Imani.

Vitu hivi kwa pamoja vinakamilisha nguzo kuu muhimu maishani kwa mtu aliyedhamiria kupata mabadiliko. Katika kila jambo unalofanya, hakikisha kuwa unalifanya kwa bidii huku akili na nguvu zako zikiwa kwa asilimia 95, ukifanya hivyo lazima utapata mafanikio.

Baada ya kuwa na bidii kwa kiwango hicho, jambo linalofuata ni uaminifu wako katika mazingira unayofanyia kazi. Kumbuka kuwa uaminifu haujali kama wewe ni mfanyakazi au mfanyabiashara bali kwa kila eneo unalofanyia kazi hakikisha kuwa unakuwa muaminifu kwa kiwango kikubwa. Uaminifu katika kazi zako lakini pia uaminifu kwenye mali za wengine.

Mathalani bosi wako amekuagiza kufanya jambo linalohitaji fedha nyingi, basi usifanye ujanja wowote kuzidisha kiwango cha kawaida kwani kufanya hivyo si ujanja badala yake ni kujiwekea mazingira magumu sana maishani.

Hivyo uanimifu ni nguzo nyingine muhimu sana katika safari ya kutafuta mafanikio maishani mwako.

Unapokopa fedha au kitu flani kwa mtu, hakikisha unakirejesha kwa muda mliokubaliana, achana na tabia ya kudhulumu vitu ambavyo si halali kwako kwani utafiti wa kisaikolojia unaonesha kuwa, mali zote zinazopatikana kwa njia za mkato au njia ambazo si za uaminifu mara nyingi huwa hazidumu.

Hivyo msomaji wangu, jitahidi sana kuboresha eneo la uaminifu katika mazingira unayojipatia riziki maishani mwako.

Lakini pia, nguzo nyingine ni Ukweli kwani ukitaka kuishi maisha ya amani na yenye furaha basi jitahidi sana kusema ukweli kwa kila sentensi inayotoka kinywani mwako. Katika ofisi ninayofanyia kazi, ninashika nafasi ndogo sana ya uongozi lakini kitu ambacho huwa nasisitiza kwa wafanyakazi wenzangu ni kusema ukweli.

Achana na ahadi ambazo unajua kabisa kwamba huwezi kuzitimiza kwani ukijijengea mazingiara ya uongo katika jamii unayoishi basi utakuwa unafukuza myanya ya mafanikio maana unaweza kuwa na kitu cha muhimu sana kukifanya lakini kwa kuwa umejijengea mazingira ya uongo basi hakuna atakaye kuamini.

Ukiwa msemakweli, hautalaumiwa na mtu na wala hutamlaumu mtu.

Mfano, rafiki yako anakuomba umfanyie jambo flani kwa wakati maalum na wewe unakubali japo unakuwa na uwezo mdogo kufanya hivyo, unafikiri kama muda ukifika na haujafanya kitu hicho ni nini kitafuata? Jibu ni lawama kwani umeahidi kitu ambacho huwezi kukifanya na siku nyingine hawezi kukuamini.

Juu ya hayo yote kuna kitu muhimu zaidi ambacho ni Imani.
Hapa ndipo kwenye kiini kikubwa cha mafanikio maishani kwani hata kama unafanya kazi kwa bidii kiasi gani, ni mkweli kwa kiasi gani lakini kama hauna imani na unachokitaka basi ni vigumu kufanikiwa.

Jinsi "mke wa mtu" Anaweza Kujiepusha na Mazingira Hatarishi

Nini sababu ya kuandika mada hii? Inatokana na kupata swali la mwanamke ambaye aliingia katika gogoro na mumewe kutokana na kukutwa katika mazingira yasiyo salama.

Kutokana na maelezo yake kuna kaka mmoja alikuwa akimtaka kimapenzi japo alijua ni mke wa mtu, alimkatalia lakini kaka yule hakuchoka kumfuatilia.

Siku moja wakati anatoka dukani alikutana na kaka yule na kumsimamisha, baada ya kusimama aliendelea kumwagia sera kwa muda huku yule dada akijitahidi kumkatalia kwa bahati mbaya mumewe aliwaona.

Alimuuliza juu ya yule mwanaume, naye akajitetea kuwa alikuwa akimtongoza lakini alimkatalia, mumewe hakumuelewa na kusema yule ni ‘mtu wake’.

Aliomba msaada wa kuokoa ndoa yake, nimlimpa ushauri uliomsaidia kurudisha amani katika ndoa yake.

Lakini matatizo hayo yamewakuta wanawake wengi kukutwa na wanaume wao sehemu zisizo salama japo hawakuwa tayari kusaliti ndoa zao.

KUSUDI LA MADA HII NI NINI? Nina imani ulisoma mada ya wiki jana kuhusu wivu ambao niliuelezea kwa upana sana, lakini baadhi ya mazingira hayafai kwa mke au mume wa mtu kusimama.

Sawa mtu anakutongoza lakini humtaki mnatumia zaidi ya robo saa kuzungumza na mtu ambaye si sahihi kwako unazungumza nini? Kama umeolewa ukisha jibu ‘nimeolewa’ lakini akazidi kukusumbua mwambie ‘sitaki’, naneno yasiyo chukua hata sekunde mbili.

Unapokuwa ndani ya mamlaka ya mtu unatakiwa kujiheshimu na kuyaepuka mazingira yote yanayoweza kutoa tafsiri mbaya kwa watu wa pembeni.

Umetongozwa mke wa mtu ufanye nini? Kwa vile mke wa mtu huwa hana muhuri, si wote wanaotembea na pete, kama mwanaume amekutongoza na kumueleza kuwa umeolewa na bado anakufuata unachotakiwa kuyafanya ni haya:

Moja, usikubali kusimama atakapo kusimamisha, huwezi kukataa salamu yake ila jiepushe kupokea neno litakalofuata lisilokuwa salama kwako.

Japo wapo wanawake wenye msimamo, lakini baadhi ya maneno ya wanaume kama utakubali kuyasikiliza yana nguvu ya kuivunja ngome ya moyo wako na kufikia hatua ya kumsaliti mumeo.

Pili, Ishi mazingira salama.

Mazingira salama ni yapi? Kujiheshimu, mwanamke anayejiheshimu humuweka mbali na wanaume wakwale tofauti na mwanamke asiyejiheshimu ambao hawana kinga yoyote na kumfanya mwanaume kusema lolote.

Tatu, jiepushe na mazoea ya kuvuka mipaka na wanaume ambayo huwapa nafasi wakwale kuingiza mambo yako.

Nne, unapomweleza mwanaume umeolewa onyesha kweli unaiheshimu ndoa yako na si kusema huku unacheka kuonyesha maneno yako ni ya mdomoni wala si moyoni.

Tano, usimpe nafasi mwanaume anayekutongoza akushambulie kwa maneno na wewe umesimama unamsikiliza lazima atakushinda.

Sita, lazima ujue thamani yako unapokuwa mke wa mtu kwa kuvaa nguo za heshima, kuwa mbali na wanaume wenye mazoea yaliyovuka mipaka kama kuzungumza maneno yaliyokosa staha pia hata kukugusa sehemu nyeti kujifanya wanakutania.

Saba, angalia mazingira ya kusimama na mwanaume na yasizidi dakika mbili labda awe na shida kubwa inayoitaji msaada wako.

Kwa Nini Babu Zetu Hawakufa kwa Ugonjwa wa Saratani

Ni ukweli ulio wazi kuwa magonjwa ya saratani yameibuka miaka michache tu iliyopita na yameshika kasi katika miaka ya hivi karibuni.

Hapo zamani, enzi za mababu zetu zaidi ya miaka 1,000 iliyopita, kulikuwa hakuna magonjwa ya saratani au kansa kama inavyojulikana na wengi.

Ni ukweli ulio dhahiri kuwa vyakula tunavyokula kila siku ndiyo chanzo kikubwa cha magonjwa ya saratani na magonjwa mengine sugu, kama kisukari, shinikizo la damu na magonjwa ya moyo.

Vyakula vya asili havipewi nafasi tena na badala yake kila kitu tunachokula ni ‘refined’ (kimesafishwa) na tunadhani kwa kula vyakula ‘vilivyosafishwa’ ndiyo tunakula vyakula bora.

Mababu zetu hawakuwahi kufa kutokana na magonjwa ya saratani kwa sababu walikuwa wakila vyakula vya asili ‘visivyosafishwa’ vilivyopatikana porini, kama vile matunda, mboga za majani, vyakula vya baharini, wakiwemo samaki, nyama ya porini, wakiwemo ndege kama mbuni na vingine vingi vizuri.

Mlo wa aina hiyo umethibitika kisayansi kuwa ndiyo uliowafanya mababu zetu kuishi kwa miaka mingi na ndiyo hasa unaofaa kuliwa na binadamu wa sasa ikiwa kweli tunapiga vita adui maradhi.

Kwa bahati mbaya sana, milo mingi ya sasa imetawaliwa na sukari kwa wingi na iliyoondolewa virutubisho.

Tukila mikate, tunakula ambayo ngano yake ilishaondolewa viini lishe vyote, tukinywa maziwa tunakunywa yaliyopitia kwenye mitambo na kuondolewa lishe yote, kila kitu tunachokula ni hatarishi, tunaishi kwa kudra ya Mungu pekee.

Kama unahitaji kujiepusha na maradhi sugu, huna budi kujiepusha na ulaji wa sukari na vyakula vinavyotengenezwa kwa sukari nyingi pamoja na kujiepusha na ulaji wa nafaka zilizokobolewa pamoja na vyakula vyake.

Ulaji wako wa sukari hautakiwa kuzidi gramu 25 tu kwa siku.

Ukiweza kuzingatia hayo, kamwe huwezi kusumbuliwa na maradhi kiasi cha kuona ni sehemu ya maisha yako na kwamba kila mtu ni lazima augue.

Pendelea kula vyakula vibichi zaidi kuliko vya kupika, mfano pendelea kula nyanya mbichi kuliko iliyopikwa au karoti mbichi kuliko ya kupika, n.k.

MAZOEZI


Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na jarida la ‘Lancet’, umeonesha kuwa mazoezi ni sehemu muhimu sana ya kuimarisha afya ya mtu na kumuepusha na maradhi.

Imeelezwa kuwa mazoezi ya dakika 15 huongeza umri wa kuishi kwa miaka 3, hata kama uko katika hatari ya kupatwa na ugonjwa wa moyo.

Halikadhalika, wale wasiopenda kufanya mazoezi, wako katika hatari ya kupatwa na maradhi kwa asilimia 17 zaidi ya wanaofanya mazoezi.

Maradhi ya kisukari kwa mfano, yanaelezwa kusababishwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa mazoezi licha ya ulaji wa vyakula vingine vinavyochangia ugonjwa huo.

Hivyo, kila mtu anayejali maisha na afya yake anatakiwa kujiwekea utaratibu wa kufanya mazoezi ya angalau dakika 15 kwa siku kwa njia yoyote anayoweza ili kuujenga na kuupa kinga mwili wake dhidi ya maradhi.

Mazoezi yanachukua asilimia 20 na mlo sahihi unachukua asilimia 80 ya afya yako.

Kanuni za Kuishi na Wanaokuchukia

Maisha ya mwanadamu wakati mwingine yamejaa matukio ambayo mwenyewe hawezi kuyaepuka. Moja kati ya hayo ni mtu kuchukiwa na wenzake na kujikuta katika wakati mgumu iwe kwenye familia na hata kazini.

Mara nyingi uamuzi mwepesi ambao wanaochukiwa huwa wanauchukua ni kujibu mashambulizi huku wengine wakiamua kujiepusha eti kwa kuhama maeneo wanayoishi au kujitenga na wenye chuki.


Njia hizo zinaweza kuwa sahihi lakini si zenye kuleta mafanikio ya kudumu. Ni vema ikafahamika kwamba kujibu mapigo ya chuki hukuza migogoro na jambo baya zaidi ni kwamba maadui huongezeka.


Pengine msomaji wangu ungependa kujua kwa nini maadui huongezeka? Jibu ni kwamba wanaompenda huyo unayemlipiza kisasi wataingilia ugomvi na kufanya kila liwezekanalo wakumalize.


Nimewahi kushuhudia watu wawili kazini wanahitilafiana kwa jambo fulani lakini mwisho kundi la wafanyakazi liliingia kwenye mgogoro, chanzo kikiwa ni kile kile cha watu wawili wa mwanzo.


Kwa nini hali hiyo hutokea? Kwa sababu ya utashi wa kibinadamu na msukumo asili wa kupenda kwani sote tunajua hata wezi hupendana na kuteteana.


Aidha, tunapotazama uamuzi mwingine wa kukimbia maadui zetu tunajikuta tukipata utata wa kimaamuzi kwa sababu hatuwezi kuwakimbia wote kwenye maisha yetu, tukifanya hivyo tutakuwa watu wa kuhamahama kila siku, maana wenye chuki ni wengi na wanaanzia kwenye familia zetu mpaka kazini.


Jambo la msingi la kufanya pale tunapobaini kuwa kuna watu wanaotuchukia mahali popote pale, ni kutumia njia zifuatazo;

KWANZA: Ni kufunua ukweli kuhusu kuchukiwa, yaani tuwaambie wanaotuchukia kuwa hatufurahishwi na chuki, tuwaombe msamaha ikibidi.

PILI: Tujilinde wenyewe kwa kupunguza uhusiano na mwingiliano wa kimatendo na kauli hasa zenye kupingana.

TATU: Tutumie muda mwingi sana kuambatana na wanaotupenda na kupata faraja kwao, lengo ni kuharibu hisia mbaya zitakazokuwepo kwenye akili zetu juu ya wanaotuchukia.

NNE: Tusiachie nafasi za kimaisha wazitawale adui zetu; “mimi sitafanya kazi na fulani acha afanye yeye aone raha.”

“Nitaacha kazi ili tusigombane naye zaidi.” Kamwe tusitoe nafasi za utawala badala yake tuonyeshe wengine kwamba tunatekeleza majukumu yetu ya kimaisha vizuri ingawa tunachukiwa kwenye familia au kazini.

TANO: Tuwashirikishe ndugu/rafiki wenye busara katika kila kwazo ili wasaidie namna ya kufanya. Tusichukue uamuzi wenyewe bila ushauri hasa tunapokuwa na hasira. Tujipe muda wa kutafakari zaidi kila jambo la chuki tunalofanyiwa kabla ya kuamua kufanya chochote.

MUHIMU: Tuepuke kukuza mgogoro kwa kuwajumuisha wengine kwenye ugomvi. Tusikumbatie tatizo na kulikuza kwenye mawazo yetu. Tuwe watu wa kupuuza na kupunguza msongo wa mawazo.

Tusimwambie kila mtu tatizo letu. Tusimame kwenye nguzo ya uvumilivu kwa muda mrefu kabla ya kukata tamaa.

Utafiti:Utazamaji filamu ni tiba ya matatizo

Familia nyingi na hasa watoto wamekuwa wakikatazwa na wazazi wao kuangalia sinema kwa fikra kwamba zinapumbaza na kupoteza muda, jambo ambalo wanasaikolojia wanapingana nalo.

Mwanasaikolojia Dorothy Halla-Poe kutoka Marekani anabainisha kitu tofauti na mtazamo wa wengi kuwa, kazi ya filamu si burudani pekee, bali tafiti zinaonyesha kuwa ni njia yenye mafanikio makubwa katika kujifunza mambo na kutibu baadhi ya matatizo yanayowakabili wanadamu.

Eti, tuamini kwamba sinema zinafundisha na kutatua shida zetu? Jibu ni ndiyo kwa asilimia mia moja, kwani ndani ya filamu uanadamu wetu unakamilishwa kwa kujifunza kupitia kusikia, kuhisi na kutafakari, mambo ambayo yanapatikana ndani ya filamu.

Hakuna ubishi kwamba uchaguzi wa simulizi, visa na tungo zinazopatikana kwenye filamu ndiyo jambo pekee linalohitajika kuzingatiwa, hii ikiwa na maana kwamba kujifunza, kujitibu matatizo yetu kunaanzia kwenye kile tunachotaka kukitazama ndani ya filamu.

Upo ushahidi wa kutosha juu ya watu wenye matatizo ya hisia za kimapenzi kumaliza ugonjwa wao kwa kutazama sinema za ngono huku wengine wakitajwa kujengwa kiimani, ujasiri na uvumilivu kupitia michezo ya kuigiza.

Kwa msingi huo hatuwezi kupuuza utazamaji wa sinema kwani inawezekana kuihamasisha jamii yetu kuwa hodari katika mambo wanayoyaona yakitendwa na waigizaji.

Kupitia filamu tunaweza kuwapatia watoto wetu moyo wa kishujaa mithili ya michezo inayoigizwa na wasanii. “Mimi Rambo” “Basi mimi Schwarzenegger” Naamini tumeshasikia watoto wakijifu kupitia majina hayo ya wacheza filamu.

Hii ina maana kwamba, filamu za waigizaji hao zimesaidia kwa kiwango kikubwa kuwajenga watoto katika ujasiri unaoweza kuwa mfano mmoja tu wenye faida na motisha unaopatika kwenye filamu na hivyo kutia nguvu mada hii kwamba, tunaweza kuwahamasisha vijana wanaochipukia kuwa akina Rais Julius Nyerere, Kwame Nkrumah, Nelson Mandela kwa kuwapatia filamu za viongozi hao na kuzitazama.

Kama hilo halitoshi wanasaikolojia wanaamini kwamba, mtu anaweza kujitibu mwenyewe tatizo la msongo wa mawazo kwa kuangalia filamu zenye ujumbe unaohusiana na tatizo lake na hivyo kujiongezea moyo wa ushindi kupitia waigizaji anaowataza kwenye sinema.

Kwa mfano, mtu anaweza kuwa mgonjwa miaka sita na akawa katika hali ya kutaka tamaa lakini akiletewa filamu inayomuonyesha mtu mwenye ugonjwa kama wake akihangaika na hatimaye kupona hata yeye atafarijika na kuamini kuwa ipo siku atapona kama yule muigizaji na hivyo kupata imani ambayo itamsaidia kuishi.

Ninachotaka kueleza hapa ni kwamba , filamu hutengeza ndoto za maisha, huleta ubunifu na kuamsha hamasa ya kufikia malengo yetu, hivyo si busara kuipuuza tasnia ya uigizaji kwa mtazamo kuwa inawapotezea watu muda wa kutafuta mafanikio.

Jambo muhimu la kuzingatia kama nilivyodokeza hapo mwanzo ni kuwa makini na uchaguzi wa filamu tunazotaka kuziangalia. Maana hakuna ubishi kwenye elimu hii kwamba mtoto akizoezwa kuangalia filamu za kikatili atabadilika na kuiga tabia ya ugomvi, vivyo hivyo wanaopendelea sinema za ngono zitawashawishi kufanya kitendo hicho lakini sinema za kuelemisha ni msaada mkubwa wa kukuza ufahamu wa watu.

Naamini, wazazi wengi wakitumia filamu zinazoonyesha mateso wanayopata watoto wa kike baada ya kupewa mimba wakiwa shuleni na baadaye kutengwa na familia zao wanaweza kufikisha ujumbe wenye nguvu kwa watoto wao wa kike zaidi ya wao kutumia ukali na vitisho.

Ukweli ni kwamba, filamu zina uwezo mkubwa wa kutengeneza hisia kama nilivyosema kuliko maneno ya moja kwa moja, ndiyo maana upo utofauti mkubwa kati ya ujumbe unaotumwa kwa njia ya wimbo na ule unaoweza kutolewa kwa njia ya sinema.

Kama hilo halitoshi, kusahau maneno ni rahisi zaidi kuliko sinema hivyo kutumia njia ya filamu kufundishia kunatajwa kuwa ni njia bora zaidi ya kutolea maelekezo hasa kwa watoto ambao kusahau ni jambo jepesi kwao.

Je ni Kweli Unachukiwa Bure?

“Nashanga mama mdogo ananichukia bure, tena hakuna kosa nililomfanyia lakini hanipendi tu” Je, wewe nawe umekuwa miongoni mwa watu wanaodhani unachukiwa bure?

Achana na hulka hiyo, hebu tambua ubaya wako kwa kuangalia vidokezo vifuatavyo, ambavyo naamini ukivisoma kwa umakini utagundua ni wapi unakosea hadi kufikia hatua ya kuchukiwa katika jamii.

Je, inapotokea umesababisha wenzako wajisikie vibaya huwa unajisikiaje moyoni mwako? Mfano ulikuwa katika mazungumzo ya kawaida na rafiki yako, lakini kwa sababu za kibinadamu akapokea mazungumzo yako vibaya na kufadhaika. Wewe unapotambua kuwa umemuondolea mwenzako furaha huwa unajisikiaje moyoni? Kama huumizwi na tukio hilo tambua kuwa wewe ni mtu mbaya.

Jiulize, katika maisha yako ni mara ngapi umewafanya wengine wafurahi kwa kuwatatulia matatizo yao, kuwasaidia wakati wa shida na kuwavusha kwenye hali ngumu za kimaisha? Au umekuwa mtu wa kusubiri usaidiwe hata kwa vitu unavyoweza kuwasaidia wenzako?

Tangu umeanza kazi umeshawahi kutoa sehemu ya mshahara/pato lako kuwasaidia wazazi na ndugu zako au umekuwa mtu wa kutoa visingizio vya hali ngumu ya maisha licha ya kuwa unafanya anasa mjini? Ikiwa hujawahi kuwasaidia watu kupata furaha, fahamu kuwa unaishi na ubaya kwenye jamii, jiandae kuchukiwa.

Je, unaposikia wenzako wana shida huwa unazichukuliaje?, je ni sehemu ya tatizo lako au hujiweka pembeni na kuwaachia binadamu wenzako wamalize matatizo yao? Ukiwa hivyo hicho ni kipimo kikubwa cha ubaya wako kwenye jamii unayoishi.

Umekuwa ukitumiaje uwezo wako wa mali au hata nguvu za mwili mbele ya wenzako? Je, ni kwa kuonea na kuwakandamiza watu uliowazidi? Ikiwa una tabia hiyo anza kujihesabu kuanzia leo kwamba wewe ni mtu mbaya mbele ya jamii.

Angalia mazungumzo yako, je yamekuwa ni ya kuwatia moyo watu, kuwafariji na kuwaelimisha au umekuwa mtu wa kutoa matamshi ya kudhalilisha, kuudhi na kuwavunjia heshima wenzako? Kama ulimi wako unatoa maneno yenye ‘sumu’ usitegemee kupendwa.

Je, umekuwa mtu wa haki, mwenye kuwatanguliza wenzako? Unaweza kutoa unachokitegemea ili kumsaidia binadamu mwenzio? Ukiwa huwezi kufanya hivyo na umekuwa mtu wa kukumbatia mali zako ujue wewe ni mbaya.
Toka ndani ya moyo wako unafurahia jamii kuwa na umoja au umekuwa mtu unayechochea migawanyiko baina ya watu wanaopendana? Endapo una tabia kama hiyo fahamu kuwa matendo yako ni mabaya.

Ni mara ngapi umezuia hasira zako kwa lengo la kuepusha migogoro? Unaweza kuvumilia kuonewa au umekuwa mtu wa kulipa kisasi kwa kudhamiria kufanya mambo mabaya kwa makusudi licha ya moyo wako kukuonya mara nyingi usifanye hivyo? Kama una tabia hiyo tambua kuwa huo ndiyo ubaya wako kwenye jamii.

Baada ya kupitia dokezo hizo chache, naamini msomaji wangu utakuwa umejifunza kitu na kuanzia leo utahakikisha kuwa unafanya mambo ambayo yanaifurahisha jamii na hivyo kuepukana kabisa na ubaya ambao una madhara makuwa kwenye maisha yako.

Je Ni Kweli Fedha Hununua Furaha

Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha British Columbia (UBC), wanasaidia majibu ya swali hili kulingana na uchunguzi walioufanya na kuuchapisha katika Jarida la ‘Journal Science’ la Machi 21, 2008 kwamba watu wengi hutumia fedha zao kununua furaha.

Inaelezwa katika ripoti zao kwamba watu wengi wanapokuwa na fedha hupenda kuzitumia kwa kununua kadi, zawadi kwa wawapendao, kukusanyika pamoja na marafiki ili kushiriki furaha za pamoja kwa kunywa, kula na kustarehe sehemu mbalimbali.

“Ni ukweli ulio wazi kwamba fedha nyingi hutumika kununua furaha. Tumeona hili katika uchunguzi wetu uliohusisha zaidi ya watu 630 kutoka nchini Marekani ambapo asilimia 87 kati ya tuliowadodosa kuhusu matumizi ya fedha zao walisema wanazitumia kununulia mahitaji na vitu vidogovidodo zikiwemo zawadi na nguo, ” anasema Profesa Elizabeth Dunn mmoja wa watafiti wa UBC.

Utafiti huo wa kitaalamu una maana kubwa katika maisha ya binadamu hasa linapokuja suala la mafanikio. Ukiangalia kwa makini, watu wengi hutumia fedha kuleta furaha katika maisha yao, jambo ambalo ni hatari kimaendeleo.

Uhusiano wa matumizi ya fedha, tabia za mwanadamu na kanuni za mafanikio ni mambo yanayohitaji elimu ili kumfanya mtu atambue hasara za ununuzi wa furaha ambazo anazipata pale anapotoa fedha zake kujipatia vitu anavyovipenda.
Ni mambo yaliyo wazi kwamba, mtu anaponunua pombe au kuandaa pati ya kuzaliwa kwake, hufurahi, lakini kanuni za maendeleo haziko kwenye msingi wa furaha ya kununua kwa siku moja bali matarajio ya furaha.

Katika hali ya kawaida, wengi hawataki kutarajia furaha bali kufurahi kila wanapohitaji. Ili kujua zaidi kuhusu hali hii, ni vema tukajiuliza ni nani aliyepata kujenga nyumba huku akifurahi? Tunasikia kila siku watu wakisema, “Jamaa amekuwa bahili sana, sijui anajenga nyumba?” au “Maisha yangu yamekuwa magumu sana siku hizi namalizia kibanda changu.”

Tafsiri ya kumalizia kibanda ni maisha magumu na ubahili, lakini baada ya nyumba kukamilika kile kinachotajwa kama furaha ya mafanikio hujitokeza na kumfanya mhusika kujua kuwa kipindi cha ubahili kilikuwa ni cha furaha pia, tofauti na mtazamo wa wengi.

Watu huniuliza; kwa nini fedha zangu hazikai, yaani kila nikizipata zinakwisha hivihivi wala sijui hata nimezifanyia nini? Waulizao maswali ya namna hii huwa hawajui kuwa maisha yao wameyaelekeza katika kununua furaha.

Wengi wetu tumekuwa wepesi kutii tamaa kwa kununua mavazi, kwenda saluni, kula vyakula vinono, kufanya starehe na kusahau kufanya mambo ya msingi ya kujijengea uwezo wa kutufikisha kwenye furaha ya muda mrefu yaani kuishi maisha yenye mafanikio makubwa.

Bila shaka kila anayetaka kufanikiwa lazima aache kuwa mteja wa furaha, azuie fedha zake zisitoke kwa lengo la kuufurahisha mwili, kujenga urafiki na watu wengine na kujikweza.

Mtu yeyote akitaka kujua kama anaishi kwa kununua furaha achukue kalamu na karatasi, aorodheshe matumizi yake kwa mwezi atagundua asilimia zaidi ya 85 ya mshahara wake, kama walivyosema watafiti wa UBC, zimetumika kununulia furaha.

Katika orodha hiyo atakuta amewapa ofa watu fulani, alimhonga msichana, alilipia kiingilio cha muziki, alilipa pango kwenye nyumba ya kulala wageni, alinunua pombe, yote hayo ni mambo ya fedha kununua furaha.

Nimalize kwa kusema kwamba, makala haya yanashauri kila mtu awe tayari kuishi kwa kutegemea furaha si kununua furaha kwa sababu ni hasara kufanya hivyo.

Bila shaka wanaotegemea furaha wataweka benki fedha zao ili waanzishie miradi, watanunua mifuko ya simenti, watasomesha watoto wao, watanunua viwanja na kadhalika, mambo ambayo ukiyatazama kwa juujuu utadhani yanapunguza uwezo fulani kwenye maisha lakini kumbe ndiyo mafanikio yenyewe.