Showing posts with label mwanafunzi. Show all posts
Showing posts with label mwanafunzi. Show all posts

Thursday, March 15, 2012

Wazazi na Mafanikio ya Kimasomo

Uchunguzi wa kitaalamu uliofanywa na baadhi ya mashirika yanayojihusisha na malezi ya watoto ulimwenguni akiwemo Daktari Janet Gonzalez Mena wa Marekani umebaini kuwa wazazi ndiyo mwanzo hasa wa mafanikio ya watoto wao na kwamba wengi kati ya vijana wanaoshindwa katika maisha kushindwa kwao kunaanzia ndani ya familia zao.

Malezi ya wazazi kwa tafsiri sahihi ndiyo yanayomkuza mtoto na kumtambulisha katika jamii kwamba yeye ni nani? Tunawapata watu wa kabila la Wanyamwezi, Wayao, Wamakua, Wamakonde kwa sababu wamezaliwa na kulelewa na wazazi wa makabila hayo.

Pamoja na yote, kuzaa peke yake yakusimamii tabia ya mtoto, bali kulea. Waswahili husema: “mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.” Kwa bahati mbaya wazazi wengi wamekuwa hawaelewi kuwa wao ndiyo wenye jukumu la kumtayarisha mtoto awe mwema na mwenye uwezo wa kufikiri.

Hali hii inatokana na kutokuwepo kwa elimu inayotoa somo la jinsi ya kuwalea watoto bila kuwaharibia ufahamu na kuwadumaza katika uelewa wa mambo.

Jambo la kusikitisha ni kwamba, wazazi ambao ndiyo wenye uchungu na watoto wametajwa kuwa chanzo cha watoto kushindwa kukabiliana na changamoto za kimaisha pamoja na masomo.

Ukichunguza kwa makini watoto wengi wanaokuwa mbumbumbu darasani (nazungumzia wale wasiokuwa na kasoro za kibaiolojia) ni wale ambao wazazi wao hawakuzingatia mambo yafuatayo katika kuwalea tangu walipokuwa wadogo hadi kukua kwao.

HUDUMA BORA

Wazazi wengi hasa wa dunia ya tatu wanakabiliwa na tatizo la uzazi holela, usiozingatia uwezo wa kulea na kuwapatoa huduma muhimu kwa watoto. Mfano lishe bora, mavazi na malazi. Wanasayansi wanasema chakula bora ndicho kinachoweza kuimarisha ukuaji wa viungo vya mtoto na kuufanya ubongo uwe katika hali nzuri ya kumudu kutafsiri mambo.

Hivyo ni jukumu la mzazi anayetaka mtoto wake awe na uelewa mzuri darasani ahakikishe kuwa anampatia mwanae chakula bora kitakachomjenga afya na kumuwezesha kuwa na mwili wenye nguvu ya kukabili magonjwa ya kitoto. Lakini sambamba na hilo mzazi anatakiwa kusimamia afya ya mwanae kwa kumpeleka hospitalini mara kwa mara kutibiwa na kushauriwa.

UTAMBUZI WA KIPAJI

Jambo la pili ambalo ni muhimu kwa mzazi ni kutambua mapema kipaji ha mtoto na kumuongoza sawa na kipaji chake. Ingawa shule nyingi nchini (Tanzania) hazitoi elimu ya ngazi ya chini lakini baba na mama bado wanawajibika kujua ni elimu ya kiwango gani kutoka shule gani itamfaa mtoto wao.

Inashauri kwa mzazi kumtambua mwanae ana uelewa gani, ili ajue namna ya kumsaidia ili afikie kiwango bora cha uelewa. Kwa mfano mtoto akiwa na uelewa wa chini anatakiwa kupelekwe kwa waalimu wazuri wenye uwezo wa kumsaidia anaposhindwa, haifai mtoto wa aina hii kupelekwa shule za ilimradi na kudhani huko atasoma na kuelewa.

Mwanafunzi na Mazingira ya Shule

Kikwazo kingine cha mwanafunzi kushindwa kimasomo ni kuzoea mazingira ya shule ambayo ameandikishwa au amefaulu kujiunga nayo. Kama wengi wetu tunavyofahamu, watoto wengi hulelewa na wazazi wao na kushinda kutwa nzima wakideka na kubembelezwa, huku wakiwa na uangalizi wa karibu kutoka kwa ndugu wanaowafahamu.

Sasa unapokuja muda wa mtoto aliyelelewa hivyo kuandikishwa shule na kushinda na watu ambao hakuwazoea, anaweza kuathirika kisaikolojia kwa kushindwa kujiamini na wakati mwingine kukinai mapema masomo. Wasi wasi wa kupigwa na wenzake ambao ni watukutu unaweza kumfanya mwanafunzi akaanza kutoroka shule au kutozingatia masomo kwa kiwango stahili.

Wataalamu wanaliorodhesha suala la mtoto kuanza shule kama tatizo linaloweza kuleta mfadhaiko wa akili na kuharibu ufahamu wa mwanafunzi. Inatajwa kuwa asilimia 26% ya wanafunzi hukumbwa na hofu pale wanapoambiwa kuwa wanakwenda masomoni mbali na wazazi wao. Kwa maana hivyo ni vema mwanafunzi akafundishwa namna ya kukabili tatizo hili.

MWANAFUNZI SHULE ZA MSINGI

Kwa kuwa watoto wengi wanaoanzishwa shule ya msingi huwa na umri mdogo wa kati ya miaka sita na saba, umri ambao ufahamu wao ni mdogo ni wajibu wa mzazi kuhakikisha kuwa anapomwandikisha mwanae kuanza masomo ya darasa la kwanza amfanyie yafuatayo:

KWANZA: Ahakikishe anamwandaa vya kutosha kukabili mazingira mapya ya maisha ya shule, inashauriwa kuwa mtoto anayekaribia kufikia umri wa kwenda shule ni vema akatengwa kimalazi na wazazi wake. Hii itamuongezea ujasiri wa kukabiliana na mambo madogo madogo akiwa peke yake.

PILI: Mtoto anapopelekwa shule asiachwe bila ulinzi wa mtu anayeweza kumtegemea katika matukio ya kumuogopesha. Ni wajibu wa mzazi kumkabidhisha mwanae kwa mwalimu au mwanafunzi mwingine anayemfahamu ili amtie imani wakati anapofadhaishwa na wakati mwingine kumlinda anapoonewa.

TATU: Mzazi amuwezeshe mtoto wake katika mahitaji ya msingi kwa mfano mavazi safi, madaftari, pesa za matumizi, vyote hivi ni kumuondolea hali ya kujiona duni hasa pale anapokutana na wenzake ambao wanamzidi katika hayo niliyotaja na mengineyo.

NNE: Ni wajibu wa mzazi kufuatilia malalamiko ya mwanae atakayoleta pindi atokapo shule na kumuongoza. Ikiwa anapigwa na wenzake ni vema mzazi akampeleka mwanae shule na kuzungumza na waalimu namna watakavyosaidiana nao kumlea na wakati huo huo kumuonyesha mtoto kimbilio lake pindi atakapokuwa shuleni. “MWANANGU UKIPIGWA NA MTU MWAMBIE MWALIMU HUYU ATAWACHAPA WANAOKUPIGA.”

TANO: Lazima mzazi amtie moyo mwanae kwa kumpatia zawadi kila anaporudi kutoka shule na amsifie kwa kazi zake “Kwa sababu leo umeamka mwenyewe nakuzawadia pipi kumi na kesho ukiwahi nitakununulia juisi”

Umuhimu wa Utii na Uaminifu kwa Mwanafunzi

Nguzo imara ya mwanafunzi yeyote anayetaka kufanikiwa katika masomo yake ni kuwa mfuasi wa UTII na UAMINIFU mahali popote na kwa mtu yeyote. Nakumbuka wakati nikiwa shule ya sekondari nilikiuka sana mambo haya muhimu, nilikuwa mtu wa vurugu na mwanzilishi wa migomo.

Wakati huo sikuona kama nilikuwa nafanya makosa, mara zote nilijitazama kama shujaa kwa vile jamii, walimu na wanafunzi wenzangu walikuwa wakiniogopa. Kifupi nilikuwa na akili darasani lakini matokeo ya mwisho yalipotoka yalinishangaza kwani nilifeli.

Kushindwa huko kulinirudisha kwenye mikono ya wazazi ambao tayari nao nilikuwa nimewachosha kwa tabia zangu. Toka hapo hakuna mjomba wala shangazi aliyejitokeza kunisaidia kimasomo kwa kuwa sikuwa mtu wa kuaminiwa. Nilikaa nyumbani kama mtu muhuni kwa miaka mitano hadi nilipokubali kubadili tabia yangu.

Nilifikia uamuzi huo kwa sababu nilinusurika kufungwa jela baada ya kushiriki katika ugomvi ulioleta harufu ya mauaji ya kijana mmoja tuliyekuwa tukigombana naye. Nililazimika kutoroka na kukaa uhamishoni kwa miaka kadhaa. Baadaye nilikutana na maisha magumu ambayo siwezi kuyasahau.

Nakumbuka wakati huo wa dhiki nilijutia utundu nilioufanya shule kwa kuchezea elimu na kujikita katika mambo ya kihuni ambayo hayakunisaidia. Mwezi wa nane mwaka 1998 nilikubali kubadilika na kuanza kujifunza upya maisha ya utii na uaminifu chini ya uongozi wa walimu wa dini yangu ya kikristo.

Mafundisho ya kidini yalinisaidia kuacha ulevi na uvutaji wa sigara. Marekebisho hayo ya tabia yalinijenga zaidi upande wa rafiki zangu niliokuwa nasali nao, lakini ndugu walikuwa bado wananitilia shaka. Rafiki zangu hawakupata shida tena kunituma kusimamia ujenzi wa nyumba zao na miradi yao na mara nyingine niligeuka kuwa ‘benki’ nikawa natunza pesa za watu.

Simulizi ni ndefu lakini mwisho wa yote uaminifu wangu huo ndiyo uliomsukuma mmoja kati ya rafiki zangu kujitolea kunisomesha masomo ya jioni ili nirudie masomo niliyofeli nilipopata nafasi hiyo sikuichezea kwani tayari nilikuwa nimeonja machungu ya ujinga. Nilijituma kusoma kwa malengo na kufanikiwa kusahihisha cheti changu.

Nilipomaliza nilichagua fani ya uandishi wa habari, ambapo alitokea mama mmoja niliyemheshimu na kumtii akanisaidia tena kunisomesha. Kifupi maisha yangu yalikuwa ya kubebwa na watu niliowaonesha uaminifu na utii wangu.

Hawa ni rafiki zangu wa hapa nchini achilia mbali Dr ………………… kutoka chuo cha American Psychology ambaye alijitolea kunifundisha masomo ya Saikolojia elimu ambayo ilinifumbua macho na kuniwezesha kuwa hivi nilivyo sasa.

Huu ni ushuhuda wangu kwa ufupi, ambao nimeutoa kwa lengo la kuwafundisha kwa vitendo nguvu ya uaminifu na utii katika maisha ya kila siku ya mwanadamu na hasa kwa wanafunzi ambao safari ya kupata elimu inahitaji ushirikiano wa watu wanaoishi nao nyumbani na shuleni.

Wanafunzi wengi wameshindwa kufanikiwa kwa sababu ya kutokuwa waaminifu na watii kama nilivyoeleza huko nyuma, jambo ambalo limewafanya watengwe na jamii mithili ya yale yaliyonitokea mimi.

Ifahamike kuwa mwanafunzi hawezi kupata msaada wa kutosha kwa wazazi, walimu na ndugu zake kama atakuwa akipewa ada anaitumia vibaya, akiwa na kashfa za ngono, wizi, uvutaji bangi na utumiaji wa dawa za kulevya na kuonesha ukorofi.