Tuesday, June 16, 2009

Yote Kuhusu Ubakaji

Ubakaji
eyes
Kwa nini? Kwa nini?

Watu wengi hufikiria kwamba ubakaji ni uhalifu unaotekelezwa tu na watu ambao kamwe hatuna ufahamu nao maishani - wanaovizia watu vichochorini kwa lengo la kuwadhulumu kwa njia hiyo.

Ukweli ni kwamba si wabakaji wote ni watu wa aina hiyo. Uchunguzi unaonyesha kuwa mara nyingi ubakaji hutekelezwa na watu tunaowajua, yaani wanawake wanaobakwa, mara nyingi hubakwa na watu ambao wamewahi kukutna nao, wanawajua vyema, huenda pia ni watu wanaowaamini au hata kuwa ni wapenzi wao.

Kwa hivyo hali yoyote ile, ambayo mtu anamlazimisha mwengine, kwa vitisho, nguvu au vyenginevyo, kufanya nae ngono huwa ni ubakaji.

Tahadhari na Madawa na pombe inayotumiwa na wabakaji kumpoteza fahamu yule wanaokusudia kumbaka!

Wakati wengine wabakaji hutumia madawa ya kulevya kumpoteza fahamu yule wanaedhamiria kumbaka. Madawa kama vile rohypnol, GHB au ketamine na hata pombe hutumiwa katika ubakaji pia kumfanya mwenye kubakwa asiweze kujitetea kwa njia yoyote.

Madawa hayo yanaweza kutiwa ndani ya kinywaji cha mtu anayenuiwa kubakwa. Madawa hayo yanaweza kuwa yasiyo na rangi yoyote, yasiyo na ladha wala kunukia. Lakini kuna mambo fulani unayoweza kuyafanya ili kuepuka visa kama hivi.

  • Kumbuka kama wewe unatumia pombe kujistarehesha , kuchunguza ni kiasi gani unachokunywa – pombe inaweza kutumiwa katika visa vya ubakaji
  • Tahadhari! Usiamini sana uwezo wa mwili wako wa kuhimili pombe... Kama unajisikia huko katika hali ya kawaida, kuchafukwa na moyo, kujikuta unalewa haraka baada ya kunywa kidogo tu, jaribu uende mahali utakapojisikia uko salama
  • Kama una marafiki unaowaamini, waeleze wasiwasi wako. Wasihi wakusindikize hadi nyumbani au kama hali yako ni mbaya, wakupeleke kwenye kliniki ya matibabu
  • Wasihi wakae na wewe mpaka dawa iishe mwilini
  • Kama umeandamana na mtu usiyemjua vyema, nenda kwa mwenye kilabu au meneja uwaombe usaidizi.
  • Subiri ndani ya ofisi huku wakiwapigia simu jamaa zako, wazazi wako, rafiki ama taxi ya kukupeleka nyumbani salama.
  • Usimruhusu mtu usiyemjua akusaidie, huenda ndiye aliyekutilia dawa ndani ya kinywaji chako.

Waathiriwa wa ubakaji mara nyingi hujilaumu wenyewe

akijuta kwanini alijiweka katika hatari ya kubakwa, kwanini alikubali kinywaji kilichomfanya kupoteza fahamu, kwanini hakuwa mwangalifu zaidi, kwanini aliiwaamini watu ambao kumbe ni walaghai, wahalifu, wabakaji ... kwanini kisa hicho kimemtokea yeye ... kwanini, kwanini, kwanini ...nk.

Pia huwa kuna wasiwasi kuwa alotekeleza kitendo hicho anaweza kukifanya tena! Wasiwasi mwengine ni kama anahisi vyombo vya usalama visimpe usaidizi wa kutosha, huenda watu wasimwamini hasa ikiwa alombaka ni mtu alowahi kuwa na uhusiano nae wa kimapenzi.

Kujuta kutakuwepo lakini ni vyema kutafakhari zaidi hatua za kukabiliana na kisa hicho.



Ubakaji wa mume kwa mume

Mbali na madhara ya kiafya, kubakwa kwa wanaume kunachukuliwa kuwa kitendo cha kufedhehesha zaidi kwani wengi huamini kuwa ni wanawake tu wanaoe weza kubakwa.

Kutokana na mtazamo huo mwanamume waliobakwa, ni vigumu zaidi kwao kukabiliana na hali hiyo. Ndio sababu vingi ya visa vya ubakaji wa wanaume haviripitiwi!

Sababu nyengine zinazomfanya mwanamme kuona ugumu zaidi kukabiliana na kisa cha kubakwa ni kama zifuatazo.
Kuuhisi kuwa uanaume wake umepungua
Na kama ni msenge, watu huenda wakaona anastahili kufanyiwa hivyo, au aliyataka mwenyewe.

  • Hofu kwamba kama mbakaji walifanikiwa kumshambulia mara moja, huenda anaweza tena kumbaka.
  • Kuhisi kuwa hataaminiwa wakitoa habari kwa polisi, hasa kama alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mbakaji hapo awali.
  • Wakati wa kubakwa wanaume wengine hutoa manii , sio kwamba wanafurahia kitendo hicho bali ni kwa sababu ya hofu na uoga…. Lakini wengine hutafsiri vibaya hali hiyo.
  • Pia ni mashirika machache sana yanayoshughulikia visa vya dhuluma dhidi ya wanaume ukilinganisha na yale yanayoshughulikia visa vya dhulma dhidi ya wanawake.



Kukabiliana na kisa cha ubakaji

Kama yakikufika

  • Usioge ama kubadilisha nguo, kwani kufanya hivyo huenda ukaharibu ushahidi muhimu
  • Tafuta usaidizi – mweleze mtu mnaeaminiana.
  • Mwone daktari – Ni vyema kama daktari atakufanyia uchunguzi ndani ya muda wa masaa 48 tangu kisa cha kubakwa – Daktari pia ataweza kuhifadhi ushahidi unaweza kupelekea kukamatwa kwa mbakaji.
  • Daktari au wataalam katika kliniki ya GUM (Genito-Urinary Medicine) – wanaweza kukufanyia uchunguzi na kuchukua hatua za haraka za kukukinga dhidi ya maaambukizo ya majonjwa ya zinaa ikiwemo virusi vya HIV.
  • Ni vyema kupiga ripoti kwa polisi haraka iwezekanavyo, maelezo na uchunguzi wa mapema utasaidia katika harakati za kumsaka huyo mbakaji.
  • Polisi pia wataangalia kama unahitaji matibabu, na kukufanyia mipango ya kwenda hospitali.

Kama unafikiria ubakaji huo ulishirikisha madawa ya kulevya basi unapaswa:

  • Kuweka ushahidi huo, hata kama itamaanisha kuhifadhi mkojo kwenye chombo kama kichupa au hata kwenye kikombe. Kumbuka athari za madawa ya kulevya humalizika haraka ndani ya mwili kuliko ndani ya chombo nje ya mwili.
  • Upeleke ushahidi huo ukafanyiwe uchunguzi haraka iwezekanavyo, kwani baadhi ya madawa hupoteza nguvu baada ya masaa sita.
  • Muhimu zaidi- Jaribu usibabaike, elekeza juhudi zako zaidi kuhakikisha unapata usaidizi wa kimatibabu na kisheria ili kumnasa mbakaji.

Kutoa habari kuhusu ubakaji

  • Utahitajika kuandika taarifa (Statement) kwa polisi hivyo basi huenda ukahitajika kujibu maswali mengi kwa undani.
  • Chukua nguo za kubadilisha, polisi huenda wakataka kuchukua nguo ulizokuwa umevaa kama ushahidi.
  • Chukua mda ili kukumbuka vyema matukio yalofanyika wakati wa ubakaji –lakini unaweza kuomba kupumzika iwapo unashindwa kutoa maelezo kwa sababu ya hisia za machungu ulonazo au kwa jambo lengine lolote - kumbuka unaweza kuondoka kituo cha polisi wakati wowote.
  • Utakapo maliza, isome tena kwa makini taarifa yako kuhakikisha ni sahihi kwa vile itatumiwa mahakamani.
  • Andika kila kitu unachokumbuka, ikiwa ni pamoja na tarehe, mahala, watu, kile walichosema na kuvalia, hata kama inaonekana kutohusiana kabisa na kisa hicho.Endelea kuandika kadri unavyaoendelea kukumbuka.

Usiogope kuomba usaidizi. Daktari wako anaweza kukupeleka kwa mshauri ambaye anashughulikia na visa vya ubakaji, na kuna mashirika mengi yanayoweza kusaidia.

Unaweza kumsaidia vipi mtu aliyebakwa?

  • Mfariji na msikilize kwa makini anayokwambia, mhakikishie kuwa unamwamini nae anaweza kukuamini
  • Usimlaumu kwa yale yaliyotokea – lawama zinamstahiki yule mbakaji na wala si kwa yule alobakwa!
  • Mpe mda – na mjulishe ya kwamba wakati wowote anapokuhitaji kuzungumza nawe, utakuwepo.
  • Kuwa mstahamilizu na mkakamavu- Kwani huenda ukasikia maneno yatakayokubughudhi na kukutia machungu.
  • Mpe mda, akihisi kulia mwache alie, – kwani kurundika machungu moyoni kunaweza kuwa na athari mbaya zaidi.
  • Kumbuka watu hukabiliana na visa vya fedheha kwa namna tofauti. Wengine hukataa kupiga ripoti polisi na wanahitaji ushawishi mkubwa! Lolote atakaloamua heshimu uamuzi wake.
  • Huenda ukahisi usaidizi wako ni mchache mno, lakini huenda usaidizi wako ukamsaidia kwa kiasi kikubwa yule aliyebakwa.

No comments:

Post a Comment